CUF's Press Release (Dec 05, 2004)
Ujumbe kwa Wananchi
Taarifa ya CUF No. 005 5 Disemba, 2004
YANAYOENDELEA KATIKA MKOA WA KUSINI, PEMBA
Sote tu mashahidi wa kile kinachoendelea sasa katika Mkoa wa Kusini, Pemba, ambako Uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura umeanza na unaendelea. Kupitia taarifa za uhakika kutoka kwa wenzetu walioko huko na baadaye kuthibitishwa na vyombo huru vya habari, kuna uharamia wa kisiasa unaofanywa na askari wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (Janjawid) kwa nia ya kuharibu zoezi zima la uandikishaji huo na hatimaye Uchaguzi Mkuu wa 2005.
Uharamia huo una lengo la kuuchafua na kuuviza mchakato wa kidemokrasia ambao nchi yetu uliridhia kuingia tangu kurudishwa kwa mfumo vyama vingi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Nyuma ya matendo hayo ya kiharamia, kuna mkono wa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi wa SMZ na Suleiman Othman Nyanga, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais (VK). Lakini huu si uharamia unaoweza kupangwa na wawili hawa tu. Hali ilivyo, pana kila dalili kwamba hizi ni njama za muda mrefu za CCM Zanzibar kwa kushirikiana na SMZ.
Siku nyingi kabla ya zoezi hili kuanza, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Mkanyageni, Mhe. Haji Faki Shaali, alimuandikia, kwanza, Rais Benjamin Mkapa na kisha Tume ya Pamoja ya Usimamizi wa Muwafaka, kuwaeleza matayarisho yaliyokuwa yanafanywa na SMZ kwa kupeleka vijana wake katika makambi yaliyo katika jimbo hilo.
Barua kama hiyo pia iliwahi kuandikwa na Katibu wa CUF wa wilaya ya Mkoani, Mhe. Tahir Aweis Mohammed, kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Barua zote hizo ziliwataka walengwa kuingilia kati uhalifu huo wa kisiasa uliokuwa ukifanywa na SMZ ili kuinusuru hali kabla haijakuwa mbaya. (Barua hizo zimo kwa ukamilifu katika Ujumbe Na. 001 na 004).
Barua hizo, pamoja na miito mingine iliyokuwa ikitolewa na Chama chetu mara kwa mara kabla ya Uandikishaji huu kuanza, haikujibiwa na walengwa na, badala yake, pakaonekana jitihada za makusudi zilizoongozwa na Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi wa SMZ, na Suleiman Othman Nyanga, Waziri wa Nchi afisi ya Rais (VK) kuhakikisha kuwa maafa yanatokea.
MATUKIO YA UHARAMIA WA KISIASA YANAYOFANYWA NA SMZ
1. Siku ya mwanzo ya Uandikishaji, tarehe 29 Novemba 2004, askari wa Vikosi vya SMZ wakiwa na silaha walivivamia vituo vya Chokocho na Ngombeni na kulazimisha waandikishwe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, huku wakiwa hawana sifa za kuandikishwa. Moja ya sifa zinazowastahikia kuweza kuandikishwa wakiwa kama wafanyakazi wa SMZ ni kuwa na barua za uhamisho. Askari hawa hawakuwa na barua hizo.
2. Siku ya tarehe 30, Novemba, 2004 ikiwa ni siku ya pili ya uandikishaji, Sheha wa Shehia ya Kiwani na mwanawe walikivamia kituo cha uandikishaji cha Kendwa na kukimwagia petroli na hatimaye kukipiga moto kwa madai kwamba hawawatambui watu walioandikishwa katika daftari hilo. Katika siku ya pili magazeti yaliripoti kuwa hilo lilikuwa ni bomu la petroli.
Siku hiyo hiyo, gari ZNZ 35805 la mbunge wa Pandani (CUF), lilishambuliwa na kuharibiwa vibaya. Hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na tukio hilo, hata baada ya kuriporiwa kituo cha polisi cha Mkoani na kwamba ilifahamika hapo hapo aliyelishambulia gari hilo.
3. Siku ya tarehe 1 Disemba 2004, askari wa KMKM (Janjawid) waliwapiga risasi watu watatu katika kituo cha uandikishaji cha Ngombeni. Wakamuua mmoja, kijana Juma Omar Juma mwenye umri wa miaka 16, na kuwajeruhi wawili: Bakar Ali Bakar na Shaib Ali Abeid. Hiyo ilikuwa ni katika jitihada zao za kulazimisha waandikishwe.
Usiku wake, kiasi ya saa 2:30, askari wa JKU (Janjawid) walikivamia na kukiteka kituo cha uandikishaji cha Chokocho. Usiku huo huo, mnamo saa 6:00, askari wengine wa Vikosi vya SMZ waliletwa katika kituo hicho na kujipanga foleni kabisa ili asubuhi watu watakapokwenda wakute wao wapo tayari wameshakuwepo. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa.
4. Siku ya tarehe 2, Disemba 2004, kituo hicho cha Chokocho kilikuwa hakiandikishi mtu yeyote isipokuwa Janjawid hao tu. Wala hapakuwa na hata wakala mmoja wa Chama chetu. Hata kama kwa sasa kituo hicho kimefungwa, lakini tayari Janjawid wameshaandikishwa katika Daftari kupitia kituo hicho, kinyume na matakwa ya sheria za Uchaguzi.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA CHAMA CHA WANANCHI (CUF)
Kwa ujumla hali ya kisiasa nchini ni tete katika wakati huu ambao maafa haya yanaendelea kutokea. Chama cha Wananchi (CUF) ni chama cha siasa kinachoamini juu ya ufuatwaji wa sheria na taratibu na kinacholenga katika utawala wa sheria na wa kidemokrasia unaojali haki za binaadamu.
Tunaamini kuwa bila ya kuwepo kwa utawala wa sheria na kidemokrasia unaojali haki za binaadamu, amani ya nchi hupotea na hakuwezi kuwepo kwa maendeleo yoyote kwa watu wake.
Kwa msingi huo, Chama chetu tangu kabla hali haijaharibika hivi, na hadi sasa, kimekuwa kikichukuwa jitihada za makusudi kabisa kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa, haki za binaadamu zinaheshimiwa na hivyo maafa yanaepukwa.
a. Chama chetu kimewasiliana na kushirikiana na wawakilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu, ambacho kinajishughulisha na haki za waathirika wa matukio ya kisiasa (wakiwemo waliowekwa ndani au kufungwa kisiasa). Huko ni kuupa tahadhari ulimwengu juu ya kile kinachoendelea hapa kwetu hivi sasa pamoja na kuwasaidia watu wetu ambao hivi sasa wako ndani kwa kuhusishwa na matukio hayo.
b. Siku ya tarehe 2 Disemba 2004, Katibu Mkuu wa CUF alizungumza na waandishi wa habari huko Dar-es-Salaam ili kuwasilisha msimamo wa Chama kuhusiana na yale yanayoendelea kutokea huko Kusini, Pemba.
c. Tume ya Uchaguzi ya CUF ikiongozwa na Mkurugenzi wake wa Mipango na Uchaguzi, Mhe. Hamad Masoud Hamad, imeonana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini, Waziri wa Mambo ya Ndani, na watendaji wa Tume ya Uchaguzi kuzungumza na kuwasilisha msimamo wa Chama chetu kwao.
TAMKO LETU
Kwa kuwa CUF ni chama cha siasa kinachowajibika na chenye kuchukuwa dhamana yake kutokana na nafasi yake kiliyonayo katika nchi, tunawasilisha mbele yenu msimamo wa Chama chetu kama hivi ifuatavyo:
1. Kutokana na kuwepo kwa taarifa za uhakika kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar aliitwa peke yake bila ya kufuatana na Makamishna wenzake wa Tume ya uchaguzi na Waziri Kiongozi wa SMZ huko Ikulu ya Mkoani tarehe 2 Disemba 2004, na kufanya naye mazungumzo kwa muda wa karibu masaa manne, tunalaani kujiingiza kati kwa Shamsi Vuai Nahodha katika kazi za Tume ya Uchaguzi na hivyo kuifanya isiwe huru.
Kwa kiwango hicho hicho, tunalaani udhaifu wa Mwenyekiti Masauni Yussuf Masanuni kwa kujidhalilisha kwake kupita kiasi mbele ya Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha. Kama mwenyekiti huru wa tume huru ya Uchaguzi, ilikuwa ni juu wa Shamsi Vuai Nahodha kumfuata na sio yeye Masauni kufuata. Kumfuata kwake Ikulu kunazua kila shaka kwamba amekwenda kuchukuwa amri.
Kwa hivyo, tunamtaka Mwenyekiti Masauni avieleze vyama vya siasa kwa ukweli na uwazi ni maneno gani aliyozungumza yeye na Shamsi Vuai Nahodha, bila ya kuficha jambo lolote.
Vyenginevyo, tutachukulia kwamba taarifa ya Shamsi Vuai Nahodha ya tarehe 04 Disemba 2004, kwamba serikali itaufuta uandikishaji endapo hali itazidi kuchafuka Pemba, ndiyo msimamo wa mazungumzo yao na kwamba kumbe walikuwa na matayarisho ya muda mrefu ya kufanya hivyo. Na hilo, Chama cha Wananchi (CUF) hakitalikubali.
2. Tumepokea pia taarifa za uhakika kwamba askari hawa wa Janjawid (Vikosi vya SMZ) wanakwenda katika vituo vya kujiandikisha wakiwa na silaha. Lengo lao ni kuwatisha raia na kufanya mashambulizi na mauaji kama ambavyo wamekwishaanza kuonesha mfano.
Kwanza, ni kinyume na sheria za Uchaguzi kwa wao kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika maeneo hayo ikiwa hawakutimiza masharti. Pili, hata kwa hao waliotimiza masharti (kama wamo) ni kinyume cha sheria kwenda katika kituo cha uandikishaji na silaha yoyote ile.
Kwa hivyo, tunawataka wale askari wote wa Vikosi vya SMZ (na yeyote mwengine ambaye kisheria hastahiki kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoa wa Kusini Pemba) asijiandikishe. Kufanya hivyo mbali ya kuwa ni kwenda kinyume na sheria, lakini pia ni kuwa chanzo cha maafa makubwa yanayoweza kutokea kutokana na kitendo hicho, kama ambavyo imeshadhihirika.
3. Kama tulivyokwishonesha kwamba kampeni hii ya uharamia wa kisiasa imekuwa ikiendeshwa na kusimamiwa moja kwa moja na Waziri Kiongozi wa SMZ na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais (VK).
Hapa tunarudia kauli yetu kwamba mikono ya wawili hawa imeroa damu za wahanga wa matukio ya umwagaji damu yanayofanywa na askari wa Vikosi vya SMZ huko Mkoa wa Kusini, Pemba. Kwa hiyo, tunarudia tena msimamo wetu wa kuwataka wawili hawa wajiuzulu mara moja!
Na kwa mara nyengine tena, tunaitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ikatae kuyumbishwa na wachafuzi wa demokrasia na iendelee na ratiba yake ya Uandikishaji wa Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu kama ilivyokuwa imeahidi.
HAKI SAWA KWA WOTE
Kurugenzi ya Habari na Uenezi wa Sera, CUF

