Zanzinet Forum
Where Zanzibaris Meet

Zanzinet History


Ukumbi wa ZANZINET ulianzishwa rasmi mwezi wa Agosti, mwaka 1994. Kwa bahati mbaya jitihada hazikuweza kufanikiwa kufahamu siku hasa ukumbi huo ulipoanzishwa rasmi, kwa sababu kulikuwa na majaribio kadhaa katika mwezi huo.

Ilitokezea kwamba Kassim Abdulrahman Abdullah, aliyekuwa chuo kikuu cha Queen's, kilichoko, Kingston, Canada, akisomea shahada ya udaktari wa falsafa (Ph.D), katika fani ya Biomechanics, na Hassan Omar Ali, aliyekuwa chuo kikuu cha Ottawa, Canada, akisomea shahada ya udaktari wa falsafa (Ph.D), katika fani ya uhandisi-umeme (electrical engineering), wote walikuwa wajumbe wa ukumbi uliokuwa ukiitwa WANANET. Ukumbi wa WANANET, ambao baadaye ulibadilishwa jina na kuitwa TANZANET, ulikuwa ni ukumbi uliowakusanya Watanzania wa sehemu mbali mbali za dunia, kujadili na kupashana habari zinazohusu Tanzania kwa kupitia njia ya Internet. Ukumbi huo ulianzishwa tarehe 17 Julai 1992 ingawa haukupata nguvu mpaka katikati ya mwaka 1993.

Ukumbi wa TANZANET ulikuwa ukiendeshwa kwa kutumia anuani kadhaa za e-mail. Moja kati ya anuani hizo ilikuwa ni hassan@aix1.uottawa.ca ambayo kwa kweli ilikuwa moja kati ya anuani binafsi za Hassan Omar Ali, alizopatiwa chuo kikuu cha Ottawa. Kwa ujumla alikuwa na anuani zisizopungua tatu kwenye kompyuta mbali mbali za chuoni hapo ambazo alikuwa na uwezo wa kuzitumia. Aliamua kuitumia anuani yake hiyo iliyokuwa kwenye kompyuta inayotumia operating system ya UNIX, kama anuani ya akiba ya kuendeshea ukumbi wa WANANET.

Ukiwa na akaunti kwenye kompyuta inayotumia UNIX, ujumbe wowote wa e-mail unaotumwa kuja kwenye anuani ya e-mail ya akaunti hiyo,

utasambazwa kwenda kwenye anuani zozote zile ulizoziorodhesha kwenye faili lenye jina .forward linalowekwa kwenye akaunti hiyo. Mbinu hiyo ndiyo aliyoitumia Hassan Omar Ali tarahe 21 Machi 1994 kutengeneza anuani ya akiba ya WANANET inayotumia anuani ya akaunti yake. Alichokifanya,ni kuandika orodha ya anuani za wajumbe wote wa WANANET kwenye faili lenye jina .forward kwenye akaunti yake hiyo.

Siku moja, katika mwezi wa Agosti 1994, Kassim Abdulrahman Abdullah, kwa kuwa na yeye alikuwa na akaunti kwenye kompyuta kadhaa chuoni pao, alimshauri Hassan Omar Ali, kuona kama ingewezekana kutumia mbinu aliyoitumia yeye ili kuwezesha kuwa na anuani ya kutumika kwa ajili ya ukumbi wa ZANZINET, wa kuwajumuisha Wazanzibari duniani kote. Hilo halikuwa na tabu kulifanya, na mara moja ZANZINET ikaanzishwa na kuwa na anuani rasmi kassim@me.queensu.ca. Kassim Abdulrahman Abdullah akawa ndiye mratibu wa kwanza wa ukumbi wa ZANZINET.

Wajumbe wa kwanza wa ZANZINET wote walikuwa ni Wazanzibari waliokuwa masomoni Canada. Orodha kamili ya wajumbe hao (ambao walikuwa sita) na anuani zao ni kama ifuatavyo:

  • abdullak@qucdn.queensu.ca <Kassim Abdulrahman Abdullah>
  • ali@trix.genie.uottawa.ca <Hassan Omar Ali>
  • cantwell_group@dept.chem.ualberta.ca <Yusuf Muombwa>
  • haji@ac.dal.ca <Ahmed Mohammed Haji>
  • hkhemed@acs.ucalgary.ca <Hemed Khalfan Hemed>
  • mozzad@civil.lan.mcgill.ca <Mozza Amin Said>

ZANZINET iliendelea, kwa muda wa kama mwezi mmoja hivi, kutumia anuani kassim@me.queensu.ca ambayo ilikuwa ni anuani ya akaunti ya Kassim Abdulrahman Abdullah iliyokuwa kwenye kompyuta yenye jina mech01. Anuani hiyo ilibidi ibadilike kutokana na tatizo alilolielezea Kassim Abdulrahman Abdullah kwenye ujumbe uliopo hapa chini aliompelekea Hassan Omar Ali:

------------------------------------------------------

Date: Fri, 23 Sep 1994 14:53:01 -0400 (EDT)

From: Kassim Abdullah <kassim@me.QueensU.CA>

To: ali@trix.genie.uottawa.ca

Cc: abdullak@qucdn.queensu.ca

Subject: TRY CONN

Hassan,

Assalaamu alaykum. Hapa ME wameweka mitambo mipya (new server) ambayo inaitwa CONN. Lakini wameunganisha kila kitu katika mech01 na hii server. Hivyo, kama ukituma ujumbe kupitia conn ni sawa kama umetuma kwa mech01. Pia, hapa ME wameanzisha utaratibu wa kuwasiliana kwa kompyuta badala ya kubandika matangazo ukutani. Kwa maana hii, katika siku zijazo itabidi ZANZINET niihamishe na kuipeleka mahala pengine, ikiwezekana kule jeff-lab. Maana bila ya kufanya hivyo, itakuwa kero kwa nyote huko kupokea barua zisizowahusu. Nitajaribu kwenda kuwaona wanaohusika kule jeff-lab, ili kutatua lile tatizo la forwarding ikiwezekana.

Kassim.

-------------------------------------------------------

Kuanzia siku hiyo, tarehe 23 Septemba 1994, ZANZINET ikahamishwa kutoka kwenye kompyuta yenye jina mech01, na kuhamia kwenye kompyuta yenye jina qlink, iliyo kwenye idara ya uhandisi-mekanika (mechanical engineering), ya chuo kikuu cha Queen's, Kingston, Canada. Kwenye kompyuta yenye jina qlink, Kassim Abdulrahman Abdullah alikuwa na akaunti yenye jina 3kaa2. Kutokana na hivyo, anuani mpya ya ZANZINET ikawa 3kaa2@qlink.queensu.ca.

Hapa chini ni barua aliyoituma mratibu wa kwanza wa ZANZINET, Kassim Abdulrahman Abdullah, kama mwezi mmoja hivi tangu ukumbi uanzishwe:

======================

Date: Sun, 25 Sep 94 22:43:47 EDT

From: ABDULLAK@QUCDN.QueensU.CA

To: 3kaa2@qlink.queensu.ca

Subject: Wanachama wapya... Karibuni..

Ndugu wapenzi,

Nataraji barua hii muipate mkiwa katika hali ya afya na furaha.

Kwa kweli ulimwengu wa mawasiliano unakuwa kwa kasi sana na hatua iliyofikiwa inatuwezesha kuwasiliana na watu wa sehemu mbali mbali za dunia kwa wakati mmoja. Hii ni neema kubwa sana. Kutokana na kupanuka huku kwa mawasiliano hasa kwa njia hii ya e-mail, kumesababisha kuzuka kwa makundi kadhaa ya mijadala na kupashana habari ambayo yanajumuisha watu wa kila fani na mielekeo taofauti ya kimawazo. Kuna maelfu ya makundi kama haya yaliyozagaa duniani kote.

Na sisi Wazanzibari tulioko huku tuliona ni jambo zuri kuwa na njia ya kuwasiliana na kubadilishana mawazo na habari nyenginezo za masuala yanayotuhusu na yanayohusu nchi yetu ya Zanzibar. Kwa hivyo tulikubaliana suala la kuanzisha kiji-network ambacho kitajumuisha Wazanzibari tu kwa nia njema kabisa ya kupashana habari na kujadiliana masuala mbali mbali yanayohusu Wazanzibari. Kuna masuala chungu mzima ambayo ni mahsusi kwa Zanzibar yanayopaswa kuzungumziwa na kujadiliwa. Network hii itatoa fursa hiyo.

Ni imani yangu kuwa wajumbe wote wa network hii, wapya na wazamani, tutaitumia fursa hii ipasavyo ili kufanikisha malengo hayo.

Pia, natoa ombi kwa ye yote yule kuitangaza net hii kwa anaowafahamu popote pale walipo ili wapate kujiunga nasi katika ukumbi huu. Kwa watakaopenda kujiunga watume maombi kwa anwani ifuatayo: 3kaa2@qlink.queensu.ca. Vile vile kwa anayetaka kupeleka ujumbe kwa Wanaukumbi wote atumie anwani hiyo hiyo.

Karibuni wajumbe wapya na twataraji kusikia mengi kutoka kwenu.

Orodha ya wanachama wote sasa ni hii:

  • 055975@acadvm1.uottawa.ca <Hassan O. Ali>
  • abdullak@qucdn.queensu.ca <Kassim A. Abdullah>
  • ali@trix.genie.uottawa.ca <Hassan O. Ali>
  • atalha@engr.mun.ca <Talha Masoud Ali>
  • cantwell_group@dept.chem.ualberta.ca <Yusuf Muombwa>
  • haji@ac.dal.ca <Ahmed M. Haji>
  • hkhemed@acs.ucalgary.ca <Hemed K. Hemed>
  • mozzad@civil.lan.mcgill.ca <Mozza A. Diwani>
  • o947@unb.ca <Ali Alawi Ali>

Nawatakia nyote kila la kheri na kazi njema.

Kassim.

==============================================================

Ilifahamika kuwa anuani ya ZANZINET, 3kaa2@qlink.queensu.ca, ingesita kufanyakazi baada ya Kassim Abdulrahman Abdullah kumaliza masomo yake. Hii ni kwa sababu, akaunti zote za mwanafunzi hufutwa na zikawa hazitumiki tena mara tu anapomaliza masomo yake. Kutokana na ukweli huo, ikaonekana ipo haja ya ZANZINET kuwa na anuani ya akiba ya kuweza kutumika mara tu anuani 3kaa2@qlink.queensu.ca itakaposita kufanyakazi kwa sababu yoyote ile, iwe kwa Kassim kumaliza masomo au kwa kompyuta ya qlink kuharibika.

Hassan Omar Ali alichukua jukumu la kupatikana anuani nyengine ya ZANZINET, na mnamo tarehe 3 Machi 1997, ZANZINET ilipata anuani mpya na ya ziada, zanzinet@glcom.com. Anuani hiyo iliendeshwa kwenye kompyuta ya Hassan Omar Ali inayotumia operating system ya Linux, iliyo nyumbani kwake, Ottawa, Canada.

Hassan Omar Ali, anamiliki GLCOM.COM, ambalo ni jina lililosajiliwa rasmi na linalotambulika kwenye mawasiliano ya Internet (yaani Internet domain name). Kompyuta iliyo nyumbani kwake ndiyo inayohudumia domain name hiyo ya GLCOM.COM. Internet service provider (ISP), aliyekuwa anamtumia Hassan Omar Ali ni kampuni iliyo Ottawa, Canada inayoitwa Synapse. ISP huyo alimpatia akaunti ya aina ya UUCP (Unix-to-Unix Copy Protocol), iliyomuwezesha kupokea barua zote zinazotumwa kwenda kwenye akaunti mbali mbali zilizo kwenye domain name yake, GLCOM.COM. Kutokana na uwezo huo, aliweza kupokea barua za e-mail moja kwa moja kwenye kompyuta yake ya nyumbani kwa kutumia anuani yake hassan@glcom.com. Aliweza pia kufungua akaunti nyengine kadhaa kwenye kompyuta yake ambazo nazo ziliweza kupokea barua za e-mail.

Kwenye kompyuta inayotumia Linux, au kompyuta yoyote ile inayotumia UNIX, unaweza kutengeneza kitu kinachoitwa "alias", yaani jina jengine ambalo linaweza kupokea na kusambaza barua za e-mail kwenda kwenye anuani mbali mbali zinazowakilishwa na "alias" hiyo. Aliases hizo zinawekwa kwenye faili lenye jina /etc/aliases. Njia hiyo ndiyo aliyoitumia Hassan Omar Ali kuipatia ZANZINET anuani zanzinet@glcom.com. Alichokifanya ni kuweka kwenye faili /etc/aliases lililo kwenye kompyuta yake, mstari ufuatao:

zanzinet: :include:/home/request/zanzinet-list

Na kwenye faili /home/request/zanzinet-list, akaweka anuani zote za wajumbe wa ZANZINET, kila anuani na mstari wake. Kwa namna hiyo, barua zote zilizopelekwa kwenye anuani zanzinet@glcom.com ziliweza kusambazwa kwenda kwenye anuani za wajumbe wa ZANZINET zilizo kwenye faili /home/request/zanzinet-list. Kuanzia hapo Hassan Omar Ali akachukua nafasi ya kuwa mratibu wa pili wa ZANZINET.

Chini ya uratibu wa Hassan Omar Ali, ZANZINET iliwezeshwa kufanyakazi kwa njia za "automatic", yaani njia ambazo kila mjumbe aliweza kujiingiza (subscribe), au kujitoa (unsubscribe), yeye mwenyewe. Hassan pia aliweka huduma nyingine za automatic, kama za kumuwezesha mjumbe kutafuta kwenye kumbukumbu za barua zilizotumwa ZANZINET, barua zote zilizozungumzia suala fulani. Aliwezesha pia kupatikana huduma ya "anonymous" iliyomuwezesha mjumbe kutuma ujumbe ZANZINET bila ya anuani yake kuonekana kwenye ujumbe huo. Hii ilikuwa ni kuwapa fursa wale wajumbe ambao walipenda kuchangia kwenye mijadala mbali mbali lakini kutokana na sababu mbali mbali, hawakupenda kutambulika kuwa ni wao waliotuma barua hizo.

Tarehe 12 Septemba 1997, Hassan Omar Ali alisajili kwa gharama zake, (jumla ya US$85), domain name ZANZINET.ORG. Domain name hiyo aliikabidhi rasmi kwa ukumbi wa ZANZINET na ikawa mali ya ZANZINET. Aliwezesha pia kwa kutumia kompyuta yake ya nyumbani, kuifanya ZANZINET iweze pia kutumia anuani zanzinet@zanzinet.org.

Kama ilivyoelezwa kabla, uendeshaji wa ZANZINET kwa kutumia anuani zanzinet@glcom.com na zanzinet@zanzinet.org uliendeshwa kwa kutumia kompyuta na akaunti ya UUCP ya Hassan Omar Ali. Akaunti hiyo ilihitaji kulipiwa CAN$30 kila mwezi, na domain name GLCOM.COM na ZANZINET.ORG zilihitaji kulipiwa kila moja, US$35 kila mwaka. Dr. Yussuf S. Salim, aliyeko Denmark, alitoa wazo kuwa "abebwae hujikaza", yaani kwamba ingekuwa bora kuwasaidia wanaoendesha ZANZINET kwa kuwapa pesa kidogo za kulipia gharama za uendeshaji wa ukumbi huo. Akapendekeza kwa ajili hiyo, kuwa wajumbe watoe michango ya hiari ya US$20 kwa mwaka au kima chochote kile mtu anachokiweza. Michango hiyo ikapendekezwa ipelekwe kwa Kassim Abdulrahman Abdullah ambaye aliteuliwa rasmi kuwa mshika fedha wa ZANZINET.

Fedha zilichangwa kwa mafanikio makubwa, na ni kutokana na mafanikio hayo ndipo Hassan Omar Ali akapendekeza kuwa ni vizuri zaidi kwa domain name ya ZANZINET, yaani ZANZINET.ORG, kuwa na makaazi yake yenyewe ya kudumu. Wajumbe wa ZANZINET walilikubali wazo hilo.

Kampuni iliyokubali kuipatia makaazi domain name hiyo (domain name server), ni kampuni inayoitwa American Data Technology, Inc. (ADTI), iliyo Research Triangle Park, North Carolina, USA. Ali Alawi Ali, aliyekuwa masomoni chuo kikuu cha New Brunswick, Canada, alishirikiana na Hassan Omar Ali kutafuta kampuni ya kuipatia makaazi domain name ya ZANZINET na baada ya kuangalia makampuni kadhaa, waliridhika na huduma za ADTI. Fedha zilizochangwa zilitumika kuwalipa ADTI US$29 kila mwezi. Kwa mwaka wa mwanzo, yaani kati ya Julai 1998 na Julai 1999, ZANZINET ililipa jumla ya US$319 (mwezi mmoja bure), na kwa mwaka wa pili, kati ya Julai 1999 na Julai 2000, ZANZINET ilitakiwa kulipa jumla ya US$290 (miezi miwili bure).

Kufuatilia hatua za kuipeleka ZANZINET kwenye makaazi mapya na ya kudumu, iliundwa kamati ya kujitolewa iliyopewa jina ZANZINET Technical Task Force (ZTTF), iliyokuwa na wajumbe wafuatao:

  • Hassan O. Ali
  • Kassim A. Abdullah
  • Ali Alawi Ali
  • Idris Rai
  • Yusuf Muombwa
  • Hamoud Al-Kindy
  • Ali Nassor Sultan

Wajumbe hao walikabidhiwa majukumu kadhaa, na wakawasiliana kwa kutumia "alias" iliyotengenezwa na Hassan Omar Ali, kwenye kompyuta yake - alias hiyo ilikuwa na anuani zanzinet-admin@glcom.com. Wajumbe hao wote walijuilishwa rasmi jinsi ya kuingia kwenye akaunti ya ZANZINET iliyo kwenye kompyuta ya ADTI, na kufanya marekebisho mbali mbali.

Majukumu waliyopewa wajumbe wa ZTTF ni kama ifuatavyo:

  • Utayarishwaji wa ukumbi wa ZANZINET [Hassan O. Ali, Ali Alawi Ali]
  • Uratibu wa ukumbi wa ZANZINET [Ali Alawi Ali]
  • Utayarishwaji wa awali wa web page ya ZANZINET [Idris Rai, Kassim A. Abdullah]
  • Utayarishwaji wa awali wa web page ya Zanzibar [Yusuf Muombwa, Kassim A. Abdullah]
  • Uratibu wa web page ya ZANZINET [Idris Rai]
  • Uratibu wa web page ya Zanzibar [Yusuf Muombwa]
  • Utayarishwaji wa kumbi nyengine zinazohusiana na ZANZINET au Zanzibar [Hamoud Al-Kindy, Hassan O. Ali, Ali Alawi]
  • Uratibu wa huduma maalum za ZANZINET [Hamoud Al-Kindy]
  • Kupanga na kusimamia upatikanaji wa habari za kila siku za Zanzibar na Tanzania [Ali Sultan, Kassim A. Abdullah]

Domain name ya ZANZINET ilihamia rasmi kwenye kompyuta ya American Data Technology, iliyo North Carolina, tarehe 8 Julai 1998, na ukumbi wa ZANZINET ukaanza kufanyakazi rasmi tarehe 17 Julai 1998, kwa kutumia anuani zanzinet@zanzinet.org. Programu iliyotumika kuendeshea ukumbi huo ilikuwa ni BeroList. Ali Alawi Ali na Hassan Omar Ali walifikia kuichagua BeroList baada ya kutafakari mambo kadhaa ikiwemo hali halisi ya utendaji kazi wa akaunti iliyopatiwa ZANZINET na ADTI.

BeroList, ingawa ilikuwa na sifa kadhaa, ikiwemo ya kuwezesha barua zinazotumwa ZANZINET kuweza kusomwa na wanachama kwa njia ya web kwa kutumia anuani : http://www.zanzinet.org/m_archive.html au bonyeza hapa , ilikuwa na tatizo moja kubwa: baadhi ya wakati barua zilipelekwa kwa wajumbe kwa namna ya kurudiarudia mara kadhaa (infinite loop) na kusababisha udhia mkubwa kwa wajumbe. Kutokana na sababu hiyo, ikaamuliwa kutumiwa programu nyengine inayoitwa MReply.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, ZANZINET ilianza na wajumbe wachache tu wote kutoka Canada lakini mpaka kufikia June 7, 1997 ilikuwa na jumla ya wajumbe zaidi ya 70 kutoka nchi zaidi ya 20 duniani kote zikiwemo Canada, USA, UK, Norway, Sweden, Japan, Oman, Turkey, Kenya, Indonesia, Denmark, Malaysia, Poland, Belgium, Germany, Russia, France, South Africa, Netherlands, na Zanzibar. Mpaka kufikia tarehe 7 Julai 1999, ZANZINET ilikuwa na wajumbe 317 waliosambaa duniani kote. Idadi ya wajumbe wa ZANINET ilizidi sana mwaka 2000-2001 mpaka kuzidi 900 mwishoni mwa mwaka 2001.

Ongezeko kubwa la wajumbe lilisababisha kujitokeza udhaifu mkubwa wa programu ya MReply iliyokuwa ikitumika. MReply iliweza kusambaza barua kwa wajumbe kwa kasi ndogo sana. Ilichukua masaa kadhaa kwa kila ujumbe kusambazwa kwa wajumbe wote. Kutokana na sababu hiyo, Hassan Omar Ali akapendekeza kutumiwa programu nyengine ya kuendeshea kumbi za mawasiliano ya e-mail, inayoitwa Listar (pia inaitwa Ecartis). Listar ilianza kufanyakazi rasmi kuendeshea ukumbi wa ZANZINET, tarehe 13 Juni 1999. Sifa kubwa ya Listar ni uwezo wake wa kusambaza barua kwa kasi kubwa sana. Na sifa nyengine ni kuwa ni programu ya bure, yaani haiuzwi, inapatikana bure kutoka kwenye Internet: http://www.listar.org/ Mpaka mwezi wa Novemba 2001 ukumbi wa ZANZINET ulikuwa unaendeshwa kwa kutumia Listar. Baada ya hapo programu nyengine inayoitwa Mailman ilianza kutumika baada ya Listar kuonesha khitilafu kubwa namna inavyozishughulikia baadhi ya barua na kusababisha usumbufu mkubwa kwenye mitambo. Mailman ina sifa ya kuweza kumpa kila mjumbe na wahudumu uwezo wa kupata huduma kwa njia ya mtandao (web).

Pamoja na ukumbi wa ZANZINET ambao ni kwa ajili ya Wazanzibari tu, zipo pia kumbi za wazi (open forums) zinazopatikana kwenye web site ya ZANZINET. Wakati wa kuandikwa historia hii, zipo kumbi mbili za wazi: Zanzibar Open Forum na Zanzibar Technology Forum, ambazo mtu yeyote yule anaweza kushiriki na kusoma yanayoandikwa kwenye kumbi hizo. Kumbi hizo zinafikiwa kupitia anuani http://www.zanzinet.org/zanzinet.html. Katika mwenzi wa Aprili 2004, ukumbi mpya wa habari za kimataifa ulianziswha, ambapo wanaopenda kupokea habari kama hizo wanaweza kujisajili kwa kupeleka maombi yao kwa anwani ya wahudumu wa Zanzinet.

Tangu ukumbi wa ZANZINET uanzishwe, Agosti 1994, umepata kuwa na wajumbe wa rika na hadhi mbali mbali. Kati ya hao ni wanasiasa kama Juma Duni Haji na Fatma Maghimbi wa chama cha CUF; mabalozi kama Mohammed Mwinyi Mzale, Dr. Abdulkadir Shareef, wasomi kama Profesa Abdul Sheriff, na wengineo kadhaa waliosomea fani mbali mbali. Pia wajumbe wa ZANZINET wengi ni wanafunzi na watu wa kawaida wanaoshiriki kikamilifu katika mijadala mbali mbali inayohusu jamii ya Zanzibar.

Moja katika michango muhimu ya ukumbi wa ZANZINET ni waraka ulioandikwa na wajumbe wa ZANZINET, chini ya uratibu wa Mohammed Ali Bakari (aliyekuwa masomoni chuo kikuu cha Hamburg, Ujerumani), na Dr. Yussuf S. Salim, kuhusiana na "White Paper" iliyotolewa na serikali ya Tanzania, kuhusiana na urekebishwaji wa Katiba ya serikali ya Muungano wa Tanzania. Waraka huo ulitolewa tarehe 20 Februari 1999, na kufafanua kwa undani khatima na matakwa ya Wazanzibari kuhusiana na Muungano wa Tanzania.

Kitu chengine muhimu ni kuwa ukumbi wa ZANZINET unatumika kuwakusanya pamoja Wazanzibari wenye misimamo tafauti na kuwapa nafasi ya kujadiliana misimamo hiyo kwa njia za kistaarabu. Hii imesaidia sana kujenga hali ya maelewano kati ya wajumbe wenye misimamo tafauti.

Mbali na mijadala ya kisiasa, Zanzinet imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia mambo mbali mbali yanayowahusu wazanzibari. Kuna wakati wajumbe wa ukumbi huu walishirikiana, chini ya uratibu wa Sheikh Mohamed Baucha, kukusanya mchango kwa ajili ya balaa la ugonjwa wa kipindupindu lililotokea Zanzibar katika mwaka 2002 na 2003. Michango pia imewahi kufanywa kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi walioko masomoni katika nchi za Ulaya ya Mashariki. Mchango mwengine ni ule wa kumsaidia mwanariadha wa Zanzibar aliyetaka kushiriki kwenye mashindano yaliyofanyika Afrika ya Kusini. Haya yote yamewezekana kwa ushirikiano madhubuti walionao wanachama wa ukumbi huu.

Mungu idumishe ZANZINET. Amin.

Hassan Omar Ali,
Ottawa, Canada,
Imehaririwa tena: August 06, 2004.

 

 

About Zanzinet | Site Map | Contact Us | ©2004 Zanzinet