Author :Dr. Omar Khatib
    Date:Sun, 19 Dec 99
Subject: UGONJWA WA KISUKARI
_____________________________________________________
     
Assalaam Aleykum wanazanzinet,

Nitazungumzia somo la hapo juu yaani KISUKARI (DIABETES)
MAELEZO:
Mwezi huu wa Ramadhani unaambatana na ulaji wa vyakula vingi na vya mchanganyiko. Vyakula vingi hivyo vimo katika aina tatu zijulikanazo kama:
UWANGA (Starch au Carbohydrates)
MAFUTA (Oils au Lipides)
Mchanganyiko wa Vitamini na madini (Vitamins na Trace Minerals)

Kila kimoja katika hivi kina kazi yake. Uwanga ndio unaleta nguvu (energy) ya kufanya kazi katika kila sehemu au kijisehemu cha miili yetu. Asilimia kubwa ya vyakula ni uwanga (carbohydrates). Mafuta nayo pia inapohitajika hutumiwa kutoa nguvu lakini zaidi ndiyo inyotuletea shaham ndani ya miili yetu. Vitamini na madini huleta uzima wetu kwani japo mahitaji ya yake ni madogo lakini yanahitajika katika ujenzi na ulinzi wa miili. Katika mwezi huu ni vigumu kuapata uiano wa vyakula hivi (balance diet) na haitegemewi kama watu kweli wangeweza kusikia kufanya hivyo baada ya funga ya siku nzima na matamanio yake. Hata hivyo basi ni vyema kuelewa nini kinatookea baada ya mlo wa futari.

MTAFUNO WA CHAKULA (DIGESTION)
Baada ya kwisha kula na chakula kuingia ndani ya matumbo inafuata mtafuno. Huu ni tafauti na ule wa ng'ombe ambae hukitoa chakula matumboni na kukileta mdomoni na kukitafuna tena. Sisi binaadamu hatuna uwezo huo. Tumbo linatufanyia kazi yote hapo. Mtafuno unaotokea katika tumbo na ndani ya machango husababisha chakula kusagwa na kuvunjwa vunjwa na kupatikana sukari aina ya GLUCOSE. Hii ni aina safi ya sukari ambayo inaweza kutumiwa na sehemu zote za mwili. Sasa sukari hiyo husafirishwa na damu kwenda katika kila sehemu ya mwili. Kama muelewavyo hakuna sehemu ya mwili ambapo damu haiifikii. Kama nilivyoeleza hapo juu sukari ndio chanzo cha mwili kupata nguvu lakini kupatikana nguvu kunahitaji sukari itoke kwenye damu na iingie kwenye misuli au chembe za mwili (body-cells) na huko sukari ivunjwe kwa kutumia hewa ya OXYGEN iliipatikane nguvu.Sukari hutoolewa kwenye damu kwenda huko kwenye misuli na chembe za mwili kwa kutumia chemikali ya INSULIN inayotemwa katika machango na BANDAMA (PANCREASE.) Sasa kwa wenzetu wenye kuuguwa maradhi ya KISUKARI hapa ndipo panapoleta mushkeli wote wanapo kula vyakula vyenye sukari. Insulin inayotoka kwenye bandama (Pancreas) zao huwa ama haitoshi kuitoa sukari yote kwenye damu na kuipeleka huko au huwa haipo kabisa.
Nini kitaokea mtu anapokuwa na maradhi hayo?

DALILI ZA KISUKARI
YAKUMBUKE MAMBO MATATU YAFUATAYO:
- Wingi wa kukojoa kojoa;
- Wingi wa kiu
- Wingi wa njaa
Haya ni mambo ambayo katika Ramadhani ni ya kawaida kwa kiasi fulani lakini jiangalie na jipeleleze na ukiwa na wasi wasi basi muone daktari umueleze na akufanyie uchunguzi.

AINA ZA KISUKARI
KUNA AINA MBILI MUHIMU ZA KISUKARI nazo ni:
AINA 1 = KISUKARI Kinacho tegemea INSULIN PEKEE yaani lazima kupata INSULIN
AINA 2 = KISUKARI Kisicho tegemea INSULIN yaani inaweza kutumiwa vidonge badala ya INSULIN

NANI ANAWEZA KUPATA KISUKARI?
WAFUATAO WANAWEZA KUPATA MARADHI YA kisukari:
- Mtu mnene mno (overweight);
- Mtu anaezidi umri wa miaka 40;
- Mtu mwenyekuhusiana na mwenye KISUKARI (nakusudia mtu ambaye ana jamaa wenye maradhi hayo ndani ya ukoo wake);
- Mwanamke mjamzito mwenye toto nene(large baby).
Naomba tufahamu kwamba hizi ni dalili zinazo ashiria uwezekano wakupata maradhi (risk factors). Ukiwa na hayo basi ni vyema ukajiangalia na ikiwezekana kufanya uchunguzi wa kuhakikisha hali yako ikoje.

JEE KUNA MATIBABU (CURE) YA KISUKARI?
JAWABU NI KWAMBA KWA SASA HAKUNA MATIBABU HAYO ILIOPO NI TIBA YA KUMPUNGUZIA MGONJWA MASHAKILI YA MARADHI HAYO.
Kwa mgonjwa wa AINA 1 atahitaji kupata tiba ya Insulin, achunguzwe damu yake kila mara, ale vyakula vya kisiha ambavyo havina sukari nyingi (ngano nzima, mtama, uwele, maharagwe, kunde, nk.) na ajishughulishe na uzoefu wa mazoezi ya mwili. Kwa mgonjwa wa AINA 2 atahitaji vidonge vya matibabu, chakula chenye siha kama mwenziwe mwenye AINA 1 na pia afanye mazoezi. Nae pia anahitaji kuchunguza damu yake hasa pale anaposhindwa na ulafi wa kubwagia utamu. Tukumbuke kwamba maradhi yo yote yale yanahitaji kugunduliwa mapema kabla ya kuathiri kiwili wili ili maisha yawe ya raha zaidi bila matatizo makubwa ya kiafya.

Tukumbuke duniani leo kuna watu zaidi ya milioni 140 wana KISUKARI idadi huenda ikaongezeka kufikia milioni 300 mwaka 2025. Tujitahidi tusiwekatika hao wataoiongezea hisabu ya maradhi haya. Tuhakikishe UZIMA wetu.

Wenu,
Dr. Omar.

 

Maintained by rai@ee.bilkent.edu.tr