Author : Dr. Y. Salim
    Date: Sat, 05 Feb 2000
Subject: KATIBA SI MSAHAFU

Wa-Bara wanakemea
Hivi karibuni maoni tofauti yenye kuunga mkono au kupinga urekibishaji  wa 
Katiba ya Serikali ya Zanzibar yamesikika. Kauli kali kali zimetolewa 
kushambulia matayarisho hayo ya ubadilishaji wa Katiba ya Zanzibar. Watu 
wanaotambulika na kuheshimika kama akina Jaji  Warioba wamesikika wakitoa 
maoni yao dhidi ya mpango huo na hadi kuufananisha na usultani. Wataalamu 
wengine wameuita udikteta na un´gan´ganiaji wa madaraka. Ndugu zetu wa
Bara 
wamechukua jitihada kubwa kuweka maoni yao wazi na yasikike pembe zote. La 
muhimu zaidi mara hii Wana-CCM wa Bara nao wamejitokeza hadharani na 
kusambaza barua walizomuandikia Dr. Salmin Amur Juma (SAJ), Rais wa
Zanzibar.

Moyo, Diria na Ali Ameir
Kwa upande wa Zanzibar akina wanasiasa wakongwe kama vile Hassan Nassor
Moyo kaweka mawazo yake dhidi ya mapendekezo hayo bayana kabisa. Ingawaje,
Moyo 
kwa muda mrefu sasa haishi tena Zanzibar na ni siri ya wazi kwamba Moyo na 
Dr. SAJ ni paka na chui. Nyuma ya mgongo wa Hassan Nassor Moyo kuna akina 
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Ali Ameir na   Balozi Hassan Diria,
kwa upande wa wale wana-CCM wa Kizanzibari walioko Bara. Kwa pamoja hawa
wamekuwa 
wakipanga mikakati ya siri ya kumpindua Dr. SAJ. Aliyeweza kujitokeza kati 
yao kuonekena na kusikikana hadharani ni Moyo, yeye hana cha kuogopa tena, 
tonge yake imekwisha salimika na hamtegemei Dr. SAJ kwa njia yoyote.
Balozi  Diria ameonyesha hamu na shauku yake kubwa ya kutaka kuwania au
kugombania 
cheo cha Urais wa Zanzibar, lakini baada ya kuona kwamba Dr. SAJ bado 
anakitaka kiti chake ikabidi Mtukufu Balozi Diria arudi nyuma kidogo na 
kuingia mvunguni. Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya ndani yeye amejigeuza 
muitikiaji dhikiri angurumae ndani kwa ndani bila ya nini anachokiitikia 
kujulikana. Ukoko wa CCM-ZNZ wanamjua vizuri msimamo wake na kujua kwamba 
siku atakayo anguka Kingi, yeye ndiye atakae kuwa wa mwanzo kusema "the
King is dead, long live the King", na atahakikisha kwamba Kingi
anapoanguka 
atajiweka mbali sana ili shina na matawi yasije muangukia.

Dr. Omar apiga mbizi
Oktoba inakaribia, wengine wameona uchaguzi unapiga hodi, kama kampeni
sija 
fanya sasa basi naweza kuchelewa kibweni au kwa maneno ya leo kuchelewa 
n´gambo ya pili. Kwa kiwango fulani Dr. SAJ ameweza, akin´gan´gania mpini
na kuachia wenziwe washike pakali, kwa siku zote kutimua timua mambo
Zanzibar na 
kwa kiwango fulani kuweza kuwaziba midomo maadui zake. Kwa upande wa CUF, 
amewatia ndani viongozi wake na kufanya harakati za CUF kwa kiwango
kikubwa 
kushughulikia kesi ya "uhyena" na kupoteza lengo la kampeni za uchaguzi na 
ujenzi wa maendeleo ya nchi kwa jumla.  Lakini mashine ya Dr. SAJ 
haikuwashughulisha wana-CUF tu, bali mitambo iliwakumba hata wale viongozi
wa 
Zanzibar ambao walikuwa na ndoto ya kuuchuchumilia Urais wa Zanzibar. Hali 
hii ilimlazimisha mtu kama Makamu wa Rais Dr. Omar Ali Juma (Dr. OAJ)
kufanya 
kampeni ya kupiga mbizi bila ya kuthubutu kuibuka. Kwa hivyo kampeni yake 
ikawa inadunga vile vikundu fulani vya jamii ambavyo, yeye mwenyewe, Dr.
OAJ, 
alijuwa kwamba siri yake hawataifichua. Katika kampeni hii fedha nyingi 
zimemtoka Dr. OAJ katika kulishia-lishia, hasa kwa watu binafsi ambao kwa 
mfano walifikwa na maafa, kama vile kufiwa au wale waliokuwa wamekabiliwa
na matumizi makubwa kama vile harusi n.k. 

Dr. Omar mtoto wa Butiama
Dr. OAJ si mwana siasa lakini ni mtu Wazanzibari wanaeweza kumwita 
juttarr.Yaani mjanja, rogi bila ya watu kuweza kuchukizwa na urogi wa aina 
hiyo, lakini tatizo ni kwamba Dr.OAJ, alivuka mipaka kwa wale wanaoujua  
uchungu wa wana-AfroShirazi wakitoneshwa. Pale alipoingilia kati kuhusu 
kutiwa sahihi suala la "Muwafaka", na hadharani kuja kuwafunza na
kuwaadhiri Wana-Afro wenziwe. Kwa hilo hawakuweza kumsamehe wala hakuweza
kusamehewa 
pale alipouweka Muungano mbele ya Zanzibar. Na ndio maana pale alipokwenda 
Bara kushika cheo cha Umakamu wa Rais,  wenziwe walipumua na kusema muache 
atoke na kutokomea.
Zaidi ya hayo kilichowachukiza Wazanzibari kwa jumla na sio CCM-ZNZ tu ni 
pale alipopendekezwa na Nyerere kuwa ndio mrithi wa Salmini Zanzibar.
Suala 
muhimu halikuwa kuwa atawekwa kwenye kiti cha Dr. SAJ au la. Suala muhimu 
likiwa ni kwa nini Nyerere alimchagua yeye awe mtawala wa Zanzibar, kwa
nini  
awe yeye? Na kwa nini hasa Nyerere awachagulie Wazanzibari nani awaongoze
au awe Rais wao. 

Madhambi ya Nyerere
Hali hii ilitokana  na sababu mbili muhimu, moja ikiwa pale Nyerere 
alipoilazimisha Zanzibar, eti kwa kipengee cha kuvunja  Katiba ya
Muungano, 
kujitoa katika Jumuiya ya Waislaam wa Ulimwengu. Hapa  Wazanzibari
walihisi 
kwamba, Katiba ni Nyerere na Nyerere ni Katiba. Sababu nyengine muhimu
ambayo 
imekuwa ikitokota ndani kwa ndani katika nyoyo za Wazanzibari ni pale 
walipoanza kutambua kwa uwazi zaidi kwamba Nyerere alijishirikisha kwa 
kiwango kikubwa sana kuwanyima Waislaam wa Tanganyika haki sawa. Hili 
lilikuwa ni pigo kubwa mno kwa Wazanzibari kutambua, hasa kwa wale
waliokuwa wakimpenda Nyerere, wawe ni wapinzani au wana-CCM, kwa sababu
karibu 
Wazanzibari wote ni waislaam. Kwa hivi sasa, kwa sababu ya vitimbi vya 
Nyerere  Wazanzibari wengi zaidi wanauona Muungano, sawa na U-Nyerere
yaani 
upikaji majungu dhidi ya uislaam. Vile vile ilipodhihirika kwamba Rais
Mkapa kwa kutumia Uhariri wake wa Magazeti wakati huo, alikuwa ni upondo
wa kidau 
cha Nyerere, ikawa sasa Mkapa nae hapendezi Zanzibar. 

CCM-ZNZ walioko Bara
Kwa hivyo kumkumbatia Nyerere na sasa Mkapa kumemuweka Dr. OAJ pahala
pabaya katika nyoyo za Wazanzibari, ingawa inawezekana angelikuwa mgombea
bora wa 
CCM-Zanzibar. Ujuttarr na ulaghai wake Dr. OAJ ungeliweza kumpeleka mbali 
kama bahati ingelikuwa upande wake. Lakini tatizo liliopo ni kwamba nae
hivi karibuni kajitia katika kundi la wana-CCM wanaombwekea Dr. SAJ.  Kuna
wale 
walio karibu na hatamu za utawala wanao amini kwamba Dr. Omar
asingethubutu 
kusema alivyosema kama Mkapa hakumbonyeza.. Inamkinika asemayo Dr. Omar 
yakawa ni ya kweli, na yale wanaosema akina Moyo, Diria, Ali Ameir yakawa 
nayo ni sahihi, lakini Wazanzibari wanauliza, jee, haki za kibinaadam na
za 
kidemokrasia ya Zanzibar zinajulikana na kutambulika pale tu wanapowania
nofu 
la Urais wa Zanzibar? Zaidi kuna uhakika gani kwamba hao wanaoshutumu leo 
wasingelifanya kama hayo au akhasi ya hayo kama wao wangelikuwa na hatamu
za utawala. Kama kweli hawa wana uchungu na Wazanzibari kwa nini sauti zao 
hazijasikikika zikiitetea Zanzibar kabla ya hapa? Ali Ameir akiwa ni
Waziri 
wa usalama mwenye uchungu na Wazanzibari, mwenye uchungu na haki za
binaadam na demokrasia, kwa nini akawa amrisha askari polisi na FFU kwenda
kuwapiga 
raia marungu, isitoshe akazidi kupeleka askari kutoka Bara kwenda
kuangamiza raia wasio na silaha wala hatia. Kwani adui wa Ali ameir ni
nani? Ni Salmini na katiba yake au ni wavunja haki za binaadamu na waponda
ponda demokrasia?
Kwa hivyo ikiwa Katiba itabadilishwa isibadilishwe, kwa maslahi ya hawa 
waliotajwa hapo juu, wao wasiwe na tamaa yoyote. Afadhali wanyamaza kimya 
kuwaiga akina Amani Karume ambao wanaweza kuwa na uwezekano wa kumuangusha 
Salmini kuliko wale waliokuwa Mrima.

Haki za binaadam hazikuvunjwa leo tu
Tukiwawacha viongozi wa CCM wa Kizanzibari walio kuwa Bara, kuna wale
Wabunge 
waliomuandikia Dr. SAJ wakitarajia kumbadilisha mawazo Raisi wa Zanzibar. 
Mhesh. Jaji Warioba ni mmoja kati ya wa mwanzo kujitokeza hadharani na 
kupinga azma na njama za Dr. SAJ na kutosita kufananisha hatua hiyo kuwa
sawa 
na usultani. Maneno mazito kutoka kwa Mtanzania Mzito. Lakini basi, hivyo 
kweli katika historia yetu ya karibuni hatuja wahi kuona utawala
uliofanana 
au kupitilia huo tuitao usulatani Tanzania?  Ikiwa usultani una maana ya 
utawala wa mabavu, udikteta, utawala wa kuamua mambo kibinfasi, ulio
pungufu kidemokrasia na ulio na sifa za uvunjaji wa haki za kibinaadaam
basi usultani 
Tanzania haujamalizika januari 1964, kwani watu wakitiwa ndani bila ya 
kupelekwa mahakamani, watu wakiteswa vizuizini na wengine hata kupoteza 
maisha yao. Tanzania bado haijayakemea maovu hayo hadharani, maovu ambayo 
yakitokea Bara na Zanzibar. Wanasheria wasifika bado hawajaweza kujitokeza 
kwa uwazi kulaani kubaguliwa kwa Waislaam katika Tanganyika tokea
kupatikana uhuru wa Tanganyika. Hali hiyo ya kuyakemea mabaguzi kama hayo
yanahitaji 
ujabari na imani safi ya kumtetea yoyote yule anaekandamizwa bila ya
kujali 
imani ya kidini, kisiasa, kikabila au kirangi. Baadhi yetu bado tunasubiri 
kulaaniwa kwa kitendo cha CCM cha kumvua Alhaji Jumbe Urais wa Zanzibar na 
bado tunasubiri kulaaniwa kwa kitendo cha kuwafukuza akina Seif Shariff 
kutoka katika CCM. Viongozi wa CCM wawache mtindo wa kumlaumu na kulaani 
maovu ya Dr. SAJ na wakati huo huo kuyanyamazia maovu ya Nyerere. 

Kosa la Salmini ni kutikisa kibiriti
Mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar tumekuwa nao tokea oktoba 1995, jumia ya 
madola imekuwa ikienda mbio kujaribu kusuluhisha, lakini ni CCM hii hii 
ambayo ikijaribu kukokota miguu kama wenye magonjwa ya matende ya miguu
ili 
kuchelewesha mapatano. Muwafaka umetiwa sahihi kijanja janja na hata hivyo 
huajatekelezwa hadi leo. Wafadhili nao wamekuwa wakijaribu kujishughulisha
na 
matatizo ya Zanzibar na kufikia hadi ya kuizuiliya Zanzibar misaada.
Viongozi 
wa CUF wamekuwa kizuizini kwa sasa zaidi ya miaka miwili. Mtiririko wa
mambo yote haya yametokea na viongozi wa CCM wa Bara, Wataalam wa Sheria
wa Bara na 
Warioba wameyanyamazia. Leo, kwa sababu, Salmini anataka kubadilisha
Katiba 
waheshimiwa wote hao wamekuja juu na kumkemea Salmini, na yote nini
sababu? 
Hakuna jengine isipokuwa kwa sababu Salmini ameparaganya mipango ya
Watawala wa Dodoma ambao walikuwa wameshawapangia Wazanzibari nani
awatawalie. Hasira za CCM-Bara sio kwamba Salmini anabadilisha Katiba, au
si kwamba Zanzibar 
kuna mgogoro wa kisiasa au sio kwamba viongozi wa CUF wanaadhibiwa kwa
sababu 
ya maoni na msimamo wao wa kisiasa, wala sio kwamba Wazanzibari wasio
hatia 
wamepigwa marungu bure siku ya kesi ya "uhyena". La, kosa ni kwamba
Salmini 
kaamua kuwatikisia kibiriti na kuonyesha kwamba yeye anajitambua kwamba ni 
Raisi wa Zanzibar na Zanzibar ni Dola, Nchi na Taifa kamili lisilokubali 
kuendeshwa kutoka Dodoma. Salmini kawaweza kwa kuwa hawawezi kumtimua kama 
alivyotimuliwa Jumbe na Seif Shariff kwani yeye yutayari kuifufua ASP.

Katiba si mshahafu - Mkapa hashindi 2000
Katiba si msahafu, inaweza kubadilishwa, pale wakati na mahitaji yanapo 
lazimu. Kwa Katiba ya Zanzibar ni Wazanzibari ndio wenye haki pekee ya 
kuibadilisha au kuirekibisha Katiba yao. Watanganyika, majirani wengine au 
watu wengine wa nje wanaweza kutoa maoni yao lakini hawana haki ya
kushiriki au kushirikishwa katika uundaji, ubadilishaji au urekibishajiwa
Katiba ya 
Zanzibar. Ni Wazanzibari ndio ambao wataamua kuwa urekibishaji maalum au 
unaohusika wa Katiba ni wenye lengo la kibinafsi au wenye maslahi na umma. 
Katiba ya Zanzibar ni Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Muungano ni Katiba
ya 
Muungano, hili lazima wabunge wa Bara walitambue na kuliheshimu. Wabunge
wa 
CCM, Wanasheria na Watawala wa Bara hawawezi kulinyamazia kimya suala la 
kurekibisha Katiba ya Muungano, kitendo ambacho kina lengo la
kumhakikishia 
Mkapa ushindi na kwa wakati huo huo kuzidi kumpa madaraka ya kuweza 
kukandamiza upinzani. Utafiti tofauti ukiwemo za CCM-Bara umeonyesha wazi 
kwamba katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa Rais wa Muungano, Mkapa 
atashinda kwa kiwango kidogo sana, yaani baina ya asilimia tano hadi saba 
(5-7%), wakati katika raundi ya pili ya uchaguzi wa Rias wa Tanzania Mkapa 
atashindwa vibaya sana kwa vile upinzani utakuwa na mtetezi mmoja tu. Kwa 
hivyo inatufanya wengine tuamini kwamba, kama inavyosemekana, lengo la 
kubadilisha Katiba Zanzibar na Bara halina tofauti, yote ni kwa madhumuni
ya kumuendeleza Rais anaetawala abaki madarakani. Sasa kwa nini Mkapa
aruhusiwe na Salmini apingwe ? Tukiliwachilia mbali hilo na
kujishughulisha na siasa za 
ndani za CCM-Bara, imedhihirika wazi kwamba pindi pakiwa na upigaji kura
huru 
Mkapa hawezi kukubaliwa kusimamia Urais na wajumbe wenzake wa Bara na ndio 
maana akawa amejaa tele katika mfuko wa Salmini, siku mfuko huo 
utakapotoboka, ole wake Mkapa. Haifiki miezi sita tokea Mkapa kushindwa 
katika uchaguzi wa ndani ya Chama na kubidi kulishia mapesa chungu nzima
na 
kutumia vitisho ili wajumbe wamuungwe mkono, donda la Mkapa bado
halijapona 
na linauma bado.

Kamati Kuu ya CCM
Katika hotuba ya sherehe za Mapinduzi za mwaka huu, 2000, Dr.Salmini
alifoka bila ya kuchokozwa na kutishia kwamba yoyote yule atakaeleta fujo
au vurugu 
basi atapambana na kali ya dola, na hakuta kuwa na  huruma. Kwa wakati huo 
hakukuwa na sababu yoyote kwa Dr. SAJ kusema hivyo kwani Wazanzibari
walikuwa 
wanaendelea kama tabia yao ya desturi kuwa ni wavumilivu na kuwa wa pole.
Na CUF kuendelea na msemo wao kuwa " wako tayari kuinunua amani kwa bei
yoyote" na ndio maana ingawa viongozi wao wametiwa vizuizini kwa zaidi ya
miaka 
miwili, wafuasi wa CUF hawakufanya fujo au ghasia yoyote. Kwani Dr. SAJ 
alipokuwa akitoa onyo hilo Wabunge wa CCM-Bara walikuwa wapi ? Kwani
hotuba 
hiyo ilitolewa kwa kichina au kiswahili ? Hivyo kweli hawakufahamu Dr. SAJ 
alikuwa ana jaribu kusema nini kwa matamshi hayo ambayo hayajashokozwa au 
kusababishwa na chokochoko yoyote? Hivyo ilikuwa hawajui kama Dr.SAJ
alikuwa anajitayarisha ikibidi kutumilia kipengee cha Katiba pale ambapo
upinzani 
ungechokozwa na kuchokozeka na kuanza kuingia katika ghasia ? Hivyo
hawajui 
kwamba Rais wa Zanzibar anaweza kutumia kipengele cha vita katika Katiba
ya 
Zanzibar na kuendelea Uraisi wake na kuzuia uchaguzi ? Hivyo hawazijui
zile 
mbinu tofauti zilizotayarishwa, kama moja haikufaa kutumika nyengine,  ili 
mradi Katiba ipigwe chenga? Mbinu hizi zote zimeshafika katika Kamati Kuu
ya CCM na zimepelekwa kwa muda mrefu. Sasa ikiwa hali ni hiyo kwa nini
Wabunge 
wa Bara wakasubiri muda wote huo na ndio kwanza leo kujitokeza ati
kuwaombea viongozi wa CUF waachiwe na ati Katiba isibadilishwe. Siku zote
hizo walikuwa 
wapi? 

Wazanzibari wote waamue
Kama ilivyo Katiba ya Bara si Msahafu basi Katiba ya Zanzibar nayo si 
Msahafu. Mabadiliko na marekibisho ni mambo ya lazima na yanayo wahusu 
Wazanzibari pekee. Lakini urekibishaji wa Katiba utakikanao ni ule utakao 
kuwa wa haki na wa halali na wa kuondosha vipengere vyote vilivyo dhidi na 
maslahi ya Wazanzibari. CCM-ZNZ wametuambiya kwamba ni wananchi, yaani 
Wazanzibari ndio wanao yataka mabadiliko hayo, kwa hivyo wengi wape. Ikiwa
ni 
Wazanzibari wote, yaani CCM-ZNZ na Upinzani pamoja wanataka hivyo, basi 
wananchi lazima wapewe haki hizo za kujiamulia Katiba yenye mfumo gani 
wanaitaka, na Wazanzibari wote washiriki kikamilifu bila ya uoga, vitisho
na bila ya mapendeleo yoyote na maamuzi hayo kusimamiwa na wale wasio
fungamana na upande wowote. Wazanzibari wooote wapewe haki ya kutoa maoni
yao huru 
kuhusu kipengele cha kumzidishia muda zaidi ya vipindi viwili Rais wa 
Zanzibar. Wazanzibari wapewe haki ya kuamua kuwa Rais awe au asiwe anateua 
Tume ya Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi. Kuteua Mhakimu au kutoteua.
Awe 
na nguvu zaidi au asiwenazo. Aweze kushitakiwa au asiweze.  Wazanzibari 
wapewe haki ya kuondosha vipengere vinavyowanyanganya haki za Kidola, za
kuwa 
na Nchi na Taifa huru. Wazanzibari wapewe haki ya kurekibisha Katiba ya 
Muungano kwa yale yenye faida au hasara ya Zanzibar na kuirejesha Katiba
ya 
Muungano ili ihudumie yale mambo kumi na moja tu (11) yaliokubaliwa katika 
Katiba Mama ya Muungano, wakati  ikirejeshea Zanzibar haki zake za kuwa na 
Rais Kamili, Bendera , Wimbo wa taifa, Nembo  na Katiba huru ya Zanzibar. 
Haya yanaweza kupitishwa kihalali pekee kwa kutumia njia ya  kura ya maoni 
itakayo simamiwa na wasimamizi huru..

Wasalaam

Dr. Yussuf S. Salim.