Author : Mohammed Ali Bakari
    Date: Fri, 17 Feb 2000
Subject: ISLAM AND DEMOCRACY

Mada hii ni mojawapo ya mada nyeti sana katika siasa za Zanzibar. Hivyo
pamoja na kwamba mimi si mweledi wa masuala yanayohusiana na dini
nashawishika kuchangia hoja hiyo. Kwa uouni wangu maelezo ya Sk
Muhammad, majibu yake kwa Dr Amour naona yako katika mstari kabisa. Ila
kuyangezea chumvi na viungwa pengine inaweza kusaidia kupata ufahamu
zaidi. Ikitokezea kuwachanganya watu zaidi basi natanguliza kuomba
radhi. Na ikitokezea kukufuru basi nasema Astaghafir llah.

Katika maelezo yangu sitaanza na kufafanua maana na tofauti ya secular
politics na non-secular politics au kwa maneno mengine, ‘man-made
politics’ and ‘God-determined politics or divine politics. Tayari
zimeshatumwa makala kadhaa kwenye ukumbi huu kuelezea nini maana ya
secular politics. Na mara kadhaa Dr Amour amekuwa anaongoza mijadala ya
kuelezea umuhimu wa kufuata mfumo wa kisiasa wa kiislamu badala ya
secularism. Na katika kutetea hoja zake hata watu wanapozungumzia
umuhimu wa harakati za kidemokrasia yeye husema kwamba hizo haziwezi
kukidhi haja ya kisiasa katika jamii yetu ya Kizanzibari.
Na hitimisho lake huwa badala ya kupigania demokrasia (secularism) basi
ingefaa kupigania uislamu.

Shabaha yangu kwa leo ni kujaribu kujibu suala moja: Jee kweli kuna kuna
mgongano (incompatibility) baina ya mfumo wa kiutawala wa kidemokrasia
na mfumo wa kiutawala wa kiislamu?

Kwanza ingefaa kujuwa hoja ya kutokuwepo kwa uwiano baina ya demokrasia
na uislamu inatoka wapi? Kimsingi hii hoja inatoka kwenye vyanzo viwili
tofauti. Chanzo cha kwanza ni wasiokuwa waislamu. Wasomi wengi wa
Kimagharibi wasiokuwa waislamu wameandika maelfu ya vitabu kuonyesha
uislamu na demokrasi haviwiani kabisa.

Sababu kubwa inayotolewa ni kwamba katika demokrasia raia ndio wenye
mamlaka ya mwisho (popular sovereignty) na hivyo maamuzi kimsingi lazima
yaendane na dhana hiyo. Sambamba na hoja hiyo, uhuru wa mtu binafsi
(individual liberty) inadaiwa kwamba ni moja katika misingi mama ya
demokrasia na kwamba msingi huo hautekelezeki katika mfumo wa kiislamu
kwa vile huangaliwa zaidi uhuru wa jamii (commnunal liberty) ambayo
hudhoofisha uhuru wa mtu binafsi kujiamulia atakacho yakiwepo mambo
yasiyopendeza kwa jamii kama vile abortion, kuoana watu wa jinsia moja
nk.

Hoja hujengwa kwamba nchi zenye utamaduni wa Kiislamu ndio za mwisho
katika harakati za mwelekeo wa kidemokrasia duniani. Nadhani haihitaji
kueleza shabaha hasa ya wasomi hao katika kujenga hoja hizo.

Chanzo cha pili kinachoshikilia hoja ya kutokuwepo uwiano wa demokrasia
na uislamu ni wale waislamu wanaoitwa wenye ‘msimamo mkali’ (radical
Islamic movement). Sheikh Sayyid Qutb, mwanafalsafa wa Muslim
Brotherhood, Misri ambaye aliuliwa na serikali mwaka 1966 ni miongoni
mwa wanaoshikilia hoja hiyo. Sheikh Sayyid Qutb msimamo wake ulikuwa
kwamba kumuachia binadamu kufanyia maamuzi binadamu mwengine siyo haki.
Mungu pekee ndiyo ana uwezo wa kuwachagulia binadamu.

Tukiachana na msimamo huo ambao hadi hivi sasa unaonekana kuwa na
wafuasi wachache, kuna misimamo mingine mitatu ya kadiri (moderate)
ambayo ina wafuasi wengi zaidi katika wakati huu. Misimamo hii mitatu
yote inajaribu kuchanganya shari’a na mamlaka ya watu (popular
sovereignty) katika viwango tofauti tofauti.

Msimamo wa kwanza unapendekeza kuwepo na mfumo wa kiutawala wa kiislamu
unaongozwa na kusimamiwa na Shura (baraza la mashauriano na maamuzi).
Katika mfumo huu Shura hufanya maamuzi kwa maslahi ya watu kwa kufuata
maadili ya kiislamu bila kulazimika kufuata maoni ya watu. Kwa maneno
mengine, viongozi na sheria wanakuwa na mamlaka inayotokana na Muumba
(divine authority).

Msimamo mwengine wa kadiri ni ule uliojengwa na Ulamaa’ Abul A’la Maudud
ambao unajulikana kama ‘theo-democracy’. Maudud alikuwa anapingana sana
na demokrasia ya Kimagharibi lakini akapendekeza mfumo ambao unaingiza
msingi wa  mamlaka ya watu (popular sovereignty) pamoja na msingi wa
dini. Lakini inapotokea ukinzano baina ya uamuzi wa watu na sheria’ basi
sheria’ ndiyo hutawala.

Msimamo wa tatu ni ule unashikiliwa na akina Rashid al-Ghannoushi wa
Tunisia. Huu unakaribiana sana na demokrasia ya Kimagharibi. Katika
msimamo huu inadaiwa kwamba dhima ya dola iko zaidi kwa raia wake kuliko
kwa Mungu. Sharia’a inatakiwa tu kutowa misingi inayoelekeza maamuzi.
Wanaofanya maamuzi wana uhuru wa kuwakilisha matakwa ya waliowachaguwa
ilimradi tu matakwa hayo yasipingane na misingi ya kijumla ya sheria ya
kiislamu.

Ni wazi kwamba misimamo yote mitatu iliyotajwa hapo juu inaweza
kuonekanwa na baadhi ya waislamu kwamba inaachana na misingi ya mfumo wa
utawala wa uislamu asilia (orthodox Islamic doctrine) kama iliyovyokuwa
ikifuatwa na Mtume (SWA) na masahaba zake, lakini kwa vile mazingira
yamebadilika sana kuna kuna haja kutafakari na kuchambua vipi misingi ya
dini inaweza kutafsiriwa kulingana na mazingira tuliyo nayo hivi sasa
yenye mabadiliko makubwa kielimu, kisayansi, teknolojia, kiuchumi,
kidiplomasia na mahusiano na nchi za nje zikiwemo zisizokuwa za waislamu
nk.

Mwisho ningemuomba Dr Amour akatufafanulia yeye msimamo wake ukoje
katika masuala hayo. Jee anakubaliana na upi katika hiyo minne
iliyotajwa hapo juu, au kama kuna mwengine anaupendelea zaidi basi pia
atusaidie kutuelimisha.




Wassalaam,

Mohammed,