Author :
    Date:
Subject: BARUA YA WAZI KWA RAIS WA ZANZIBAR

 BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA RAIS WA ZANZIBAR
DR. SALMIN AMOUR JUMA
___________________________________________________________
Mheshimiwa Rais,

Kwa wingi wa heshima, tungependa kuianza barua yetu hii kwa kujitambulisha. Sisi ni Wazanzibari ambao pia ni washiriki katika ukumbi wa Zanzinet ambao ni ukumbi wa majadiliano kwa njia ya Internet unaowashirikisha Wazanzibari wa itikadi, jinsi, na rika mbali mbali. Ni baada ya majadiliano marefu katika ukumbi huo ndio baadhi yetu tukafikia uamuzi wa kukuandikia barua hii.

Madhumuni hasa ya barua yetu hii kwako, ni kuleta mbele yako kwa heshima na taadhima, maoni yetu juu ya mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yanayotarajiwa kufanywa ili kumuwezesha Rais wa Zanzibar kushika madaraka ya urais katika vipindi zaidi ya viwili vya miaka mitano mitano.

Taarifa za mabadiliko hayo ya katiba zilisikika kwanza kutoka kwa msemaji wa Ikulu yako, na baadhi ya wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), akiwemo Waziri wa Sheria na Katiba, na pia aliekuwa Mwanasheria Mkuu. Taarifa hizo pia huonekanwa na kusikika katika vyombo mbali mbali vya habari kama radio, magazeti, na televisheni. Na hivi karibuni tu, tumepata kushuhudia habari hizo kujadiliwa na Kamati maalum ya CCM, Zanzibar.

Mpaka sasa bado hatujasikia tamko rasmi kutoka kwako la kuthibitisha au kukanusha kuwepo nia ya kufanywa mabadiliko hayo ya katiba. Kukaa kwako kimya tunakutafsiri kuwa ni kutokana na kujipa muda wa kulitafakari zaidi suala hilo. Madhumuni ya barua yetu hii ni kwa heshima na taadhima kukupa maoni yetu ili yakusaidie zaidi wakati huu unapolitafakari suala hilo.

Kuna sababu kadhaa ambazo huelezwa kuwa ndizo zilizosababisha kufikiwa mapendekezo hayo ya mabadiliko ya katiba. Tutaziorodhesha hapa chini zile ambazo tunahisi ni sababu kuu:

1. Mabadiliko haya ya katiba yana lengo la kukupa wewe, Mheshimiwa Rais, nafasi ya kuweza kuendelea na madaraka ya urais kwa kipindi kingine tena, kwa vile umeiletea Zanzibar maendeleo makubwa wakati wa uongozi wako na kuwa kwa sasa hivi Zanzibar hakuna mwengine zaidi yako miongoni mwa wana CCM anayefaa kuwa Rais na anayeweza kupambana na chama cha CUF.

2. Mabadiliko haya ya katiba yamependekezwa baada ya kuonekanwa kuwa mpango wa kuruhusu Rais kuwa madarakani kwa muda wowote ule kadri inavyowezekana, ndio mpango maridhawa zaidi katika mfumo wa vyama vingi unaotumiwa Zanzibar sasa hivi, na kuwa mfumo uliopo sasa hivi wa kuruhusu vipindi viwili tu vya urais ulifaa zaidi wakati wa mfumo wa chama kimoja ambao sasa hautumiki tena..

HALI YA MAENDELEO YA ZANZIBAR:
Kama ilivyotajwa hapo juu, inadaiwa kuwa mabadiliko haya ya katiba yamenuiwa kufanywa ili kukupa wewe Mheshimiwa Rais, nafasi ya kuweza kuendelea na madaraka ya urais kwa kipindi kingine tena. Inadaiwa kwamba katika uongozi wako uchumi wa nchi umeimarika na huduma kwa wananchi wa Zanzibar zimekuwa bora zaidi.

Mheshimiwa Rais, ingawa hatuna sababu ya kuhoji nia yako ya kuiletea maendeleo Zanzibar, turuhusu tutafautiane na madai yaliyotajwa hapo juu.

Tukilinganisha hali za maisha ya Wazanzibari hivi sasa na ilivyokuwa miaka kumi iliyopita, tunaiona kuwa hali hivi sasa ni mbaya kupita kiasi, kama tutakavyoonyesha hapa chini kwa mifano halisi:

i) Kumekuwepo na ucheleweshwaji mkubwa wa mishahara ya wafanyakazi ambayo tangu hapo ni midogo mno na haitoshelezi mahitaji ya lazima ya wafanyakazi hao.

ii) Huduma za maji na umeme zimekuwa mbaya mno.

iii) Huduma za matibabu zinahuzunisha; tunashuhudia Wazanzibari walio masikini wanavyohangaika sana kutafuta huduma hizo, kwa vile hawana uwezo wa kugharimia matibabu yao ikiwemo kujinunulia dawa wanazoandikiwa na madaktari.

iv) Hali ya skuli zetu inahuzunisha kwa kukosekana hamu ya kufanyakazi (morale) miongoni mwa walimu na pia ukosefu mkubwa wa vitendea kazi.

Hivi sasa kwa hakika uchumi wa Zanzibar una hali mbaya sana licha ya kauli za kupotosha zinazotolewa na viongozi wa SMZ kwamba uchumi umekua. Kwa mfano, hadi kufikia mwezi Julai 1998, SMZ ilikuwa inadaiwa kiasi cha TSh. 141.3 bilioni. Hii ina maana kwamba kila Mzanzibari hata aliyezaliwa leo ana deni la TSh. 176,625 sawa na dola za Kimarekani 281 kwa wakati huo, wakati ambapo pato la wastani la Mzanzibari halifikii hata dola 150. Hivi sasa deni hilo litakuwa limeongezeka zaidi.

Kutokana na hali ya migogoro ya kisiasa iliyoikumba Zanzibar tangu baada ya uchaguzi wa Oktoba 1995, takriban miradi yote ya maendeleo imesita kwa kipindi kirefu hivi sasa kwa vile SMZ yenyewe haina uwezo wa kuigharamia na wafadhili wengi wamesitisha misaada.

Katika mwaka wa fedha 1994/95, SMZ ilichangia katika shughuli za maendeleo fedha kiasi cha TSh. bilioni moja, na katika mwaka wa fedha 1997/98 ilitowa kiasi cha TSh. 1.6 bilioni. Ukiangalia kiwango hicho utaona ni kidogo sana na cha kusikitisha mno. Ili kujua udogo wa kiwango hicho ingefaa kulinganisha na gharama za sherehe za Mapinduzi za mwaka huu na milenia mpya, ambazo zinakisiwa kufikia TSh. bilioni moja. Hiyo inadhihirisha wazi namna SMZ chini ya uongozi wako isivyotoa kipaumbele kwa mambo ya msingi ya maendeleo ya Zanzibar.

Mbali na kudorora kwa miradi ya maendeleo, serikali hivi sasa inashindwa hata kugharamia matumizi ya kawaida katika mawizara. Wizara nyingi hupata chini ya asilimia 60 ya makadirio ya bajeti zao. Hivi sasa ofisi nyingi za Serikali hazina hata huduma za simu; madeni yamewazidi na serikali haina uwezo wa kulipa. Kadhalika wafanyakazi wengi huripoti tu kazini na kupiga soga bila ya kufanya chochote cha maana siku nzima kutokana na kutokuwepo vitendea kazi vinavyohitajika.

Mheshimiwa Rais, kutokana na mambo tuliyotataja hapo juu, tunafikia kushangaa ni mwananchi gani wa Zanzibar asiyeona madai ya kuimarika kwa uchumi na huduma muhimu kwa wananchi katika kipindi cha miaka 10 ya urais wako, ni ya kubuni tu?

MAPENDEKEZO YA WAZANZIBARI:

Inadaiwa pia kwamba Wazanzibari wenyewe wamependekeza mabadiliko hayo ya katiba. Alipoulizwa Msemaji wako hivi karibuni na waandishi wa habari kutoa idadi ya wananchi wa Zanzibar ambao wamependekeza mabadiliko yatayokuwezesha kuwa mgombea kwa mara ya tatu, alisema kwamba katika mikutano kadhaa ya CCM wananchi walipendekeza hivyo. Hata katika mkutano wa kamati maalum pia, takwimu za wana CCM wanaodai mapendekezo hayo hazikuweza kutolewa.

Mheshimiwa Rais, tumeshuhudia na kusikia kauli za watu wanaokuzunguka kuelezea kuja kwa mabadiliko hayo ya katiba hata kabla hao wanaoitwa wananchi wanaokutaka hawajajua nini kinakuja. Utekelezwaji wa mabadiliko hayo ya katiba ulijadiliwa na kamati ya sheria na katiba ya Baraza la Wawakilishi mwaka 1998, wakati Wawakilishi wa chama cha CUF walipokuwa kwenye mgomo.

Wewe binafsi, ulishuhudia wakati wa mikutano ya hadhara ya CCM iliyofanyika baada ya kutoka hadharani tetesi za kuwepo kwa mabadiliko hayo, suala la kugombea kwako kwa mara ya tatu likitajwa na kutakiwa watu wanyooshe mikono kuliunga mkono.

Kitendo cha wanachama wa CCM kupendekeza hadharani kuwa ugombee tena nafasi ya urais wa Zanzibar, chenyewe kilikuwa cha ukiukwaji wa katiba kwa sababu suala la kugombea tena halipo katika katiba ambayo wewe uliapa kuilinda na kuitetea. Hukuwahi kusikika hata siku moja kuwaasa wanachama hao kuwa mapendekezo hayo ni kinyume cha katiba na hivyo yatahitaji hatua maalum za kisheria.

Mheshimiwa Rais, la muhimu pia ni kuzingatia kwamba Wazanzibari sio wale tu wanachama na wafuasi wa CCM - walioko kwenye vyama vya upinzani na hata wasiokuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa pia nao ni Wazanzibari. Ukweli wa mambo ni kwamba, hata ndani ya chama tawala kuna wengi wasioafiki mpango huo wa mabadiliko ya katiba kama ilivyodhihirika hivi karibuni, ingawaje kutokana na mfumo uliopo wa kisiasa wanakuwa na kigugumizi cha kusema wazi wazi. Kubadilishwa kwa katiba hiyo kwa hivyo kufanywe kwa ridhaa ya Wazanzibari wote na sio CCM tu peke yao. Hii ni kwa kupitia baraza la Wawakilishi au kwa kura ya maoni , na sio kwa njia nyengine zisizokuwa za haki.

Kwa hivyo, dai kwamba ni Wazanzibari 'wenyewe' wanaopendekeza mabadiliko hayo ya katiba, halina ithibati yoyote, Mheshimiwa Rais. Kwa namna jambo hili linavyoshughulikiwa na serikali yako, tunafikia kuamini kwamba ni Wazanzibari wachache tu ndani ya CCM ambao wamependekeza mabadiliko haya na siyo kwa ajili ya maslahi ya nchi ila kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

MZANZIBARI ANAYEFAA KUWA RAIS:

Inadaiwa kwamba wewe ndiye kiongozi pekee kutoka CCM Zanzibar mwenye uwezo wa kuiongoza Zanzibar hivi sasa.
Tusingependa kuisemea CCM katika hili, lakini tunahisi kusema maneno haya ni kuwadhalilisha sana viongozi hodari ambao wamo katika CCM Zanzibar. Kwa mara ya mwanzo katika historia ya CCM Zanzibar, uongozi wa CCM Zanzibar umekuwa na viongozi wengi wenye elimu za juu mno. Hivi sasa katika safu ya viongozi wa CCM Zanzibar, kuna viongozi wenye shahada za juu za fani mbali mbali na uzoefu mkubwa katika uongozi kwenye nyadhifa kubwa kubwa. Tunaamini kwamba dai hili linawapaka matope na kuwadhalilisha.

Mheshimiwa Rais, tunavyofahamu ni kuwa, moja kati ya kazi za Rais ni kuwaandaa watu wake kiuongozi ili mara tu muda wake utakapomalizika wawe wako tayari kumpokea kushika uongozi huo. Jee, dai hili la kuwa hakuna mwana CCM mwengine anayefaa kuwa Rais wa Zanzibar, huoni kuwa linatia kasoro uongozi wako? Ikiwa katika miaka kumi ya uongozi wako hukuweza kuwatayarisha wanachama wa chama chako kuwa warithi wako, basi huko si kushindwa kiuongozi? Au ndio imependekezwa uendelee na urais ili upate nafasi ya kusahihisha kile ulichoshindwa kukifanya katika kipindi halali cha uongozi wako?

Mheshimiwa Rais, ni imani yetu kwamba hoja hii haina ukweli na haina nguvu. Tunaaamini kwamba viongozi madhubuti sana wamo kwenye CCM Zanzibar. Ni wajibu wa CCM Zanzibar chini ya uongozi wako, kuwatangaza kwa wanachama wao ili wawajue.

UWEZO WA KUIDHIBITI CUF:

Mheshimiwa Rais, inadaiwa kwamba wewe ndiye pekee unayeweza kupambana na CUF na kuidhibiti ipasavyo ili isiweze kuwa washindi katika kura inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Tunaamini kwa dhati kabisa, na kutokana na ushahidi madhubuti, kwamba kinachowafanya watu kukipigia kura chama fulani zaidi ni sera za chama hicho na sio mgombea. Kwa hivyo, tunaamini kwamba CCM kama chama kikongwe chao Zanzibar, kinachohitaji ni kuwa na sera nzuri tu za kuwavutia Wazanzibari na hizo ndio zitakazokifanya kishinde.

MPANGO UNAOFAA KWA MFUMO WA VYAMA VINGI:

Mheshimiwa Rais, hoja nyengine inayotolewa katika kuunga mkono mapendekezo ya katiba yanayotarajiwa kufanywa ni kuwa mpango wa kuruhusu Rais kuwa madarakani kwa muda wowote ule kadri inavyowezekana, ndio maridhawa zaidi katika mfumo wa vyama vingi, kwa vile Rais asiyependwa hatabakishwa madarakani na wanachi kwa muda mrefu. Inadaiwa kuwa, mpango wa kuruhusu vipindi viwili tu vya urais vilifaa wakati wa mfumo wa chama kimoja.

Hoja hiyo ina matatizo kadhaa. Kwanza inaonyesha kuwa katika mfumo wa chama kimoja, rais, kama hakuzuiwa na katiba, anaweza kulazimisha kukaa madarakani kwa muda mrefu sana. Kwa maneno mengine, hoja hiyo inaashiria kuwa katika mfumo wa chama kimoja, matakwa ya wananchi wanayoyaonyesha kwenye kura wanazozipiga, hayatoshi kumuondoa madarakani Rais huyo kama hapendwi. Yaani kuwa matokeo ya kura yanaweza yasiheshimiwe kwenye mfumo wa chama kimoja.
Inabidi kuzingatia kuwa, iwapo Rais ataruhusiwa kikatiba kuendelea na madaraka kwa muda wowote ule, hofu ya Rais aliye madarakani kufanya mizungu kuendelea kubaki kwenye madaraka milele bado ipo hata wakati huu wa mfumo wa vyama vingi. Mgogoro mzima uliofuatia kura ya Oktoba 1995 ni kutokana na tuhuma hizo. Na kwa kweli si tuhuma tu bali inafahamika kuwa matokeo ya kura ya 1995 Zanzibar hayakuwa bila ya doa. Tuna hofu kubwa kuwa, Rais aliye na uwezo wa kikatiba kukaa madarakani milele, hakuna kinachomzuia katika hali iliyopo kufanya mizungu na kuendelea kubaki madarakani kwa njia za ujanja. Tuna hofu kubwa kuwa, iwapo itatokezea hivyo, Zanzibar itaingia tena kwenye mgogoro mwengine wa kisiasa pengine ulio mkubwa zaidi ya ule uliotokezea baada ya uchaguzi wa Oktoba 1995. Ikitokezea hivyo, usalama na hali za Wazanzibari zitazidi kudorora na kuhatarika.

HITIMISHO:

Sababu zote tulizozichambua hapo juu, zimetupelekea sisi kuamini kwamba huu mpango wa kubadilisha katiba ni wa kubuniwa kwa manufaa ya watu wachache tu.

Mheshimiwa Rais, siku zote umekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza demokrasia na kupanuka kwa fikra za wananchi. Kuamini kuwa hakuna mwana CCM ataeweza kushika nafasi yako ni kuviza demokrasia na ni hatari kwa nchi changa kama yetu. Fikra za kuwa kiongozi mmoja tu ndie anaetufaa zitatuweka pabaya pindipo kiongozi huyo akiondoka ghafla bila ya utaratibu mzuri wa kurithishana madaraka.

Mheshimiwa Rais, katiba ya nchi ni muongozo na dira katika shughuli za kila siku za nchi hiyo. Kwa hivyo, ni vyema kuiweka katiba yetu katika mazingira ya kuheshimiwa na kutochezewa kwa manufaa ya wachache.

Tunaamini kuna marekebisho mengi yanahitajika kufanywa kwenye katiba yetu, lakini kama Wazanzibari tunaoipenda nchi yetu, tungependa kuona kwamba mabadiliko hayo ni yale yenye kuitakia kheri Zanzibar na jamii yake yote na sio mtu au kundi dogo tu la Wazanzibari.

Kama wazalendo wa nchi yetu, tutakuwa pamoja na yeyote yule, au chama chochote kile ambacho kitapendekeza au kufanya mabadiliko ya katiba kwa manufaa ya Wazanzibari wote. Kwa mfano, mapendekezo yatayoirejeshea Zanzibar nguvu za dola na hadhi yake; mapendekezo yatayopanua demokrasia Zanzibar; na mengine yote ambayo yatakita katika kuwaunganisha Wazanzibari kuwa kitu kimoja - hayo tutayaunga mkono kwa nguvu zote, Mheshimiwa Rais.

Mheshimwa Rais, sisi kama Wazanzibari tunaoipenda nchi yetu, tungependa kuona Wazanzibari wanaishi katika hali ya usalama bila ya mivutano baina yao. Hatuna wasi wasi wowote kuwa, wewe, kama Rais wa wananchi wa Zanzibar una hisia nzito zaidi ya zetu juu ya hili. Kwa hivyo, tunakuomba uchukuwe kila juhudi na uwezo wako wa kiutawala katika kuepusha hili suala la mabadiliko ya katiba yatayomuwezesha Rais kuongoza zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Kauli yako ya kutoridhia mapendekezo haya ingetosha Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Rais, suala hili la marekebisho ya katiba limekuwa likizungumzwa sana na baadhi ya wakuu wa CCM kutoka Tanzania Bara, kama vile Jaji Warioba, Wabunge kadhaa wa CCM, Wanasheria mbali mbali, Wasomi kadhaa wa mambo ya sheria na Jumuiya mbali mbali zinazohusika na mambo ya siasa. Pia tumemsikia Dr. Omar Ali Juma akilipinga suala hili. Na hivi karibuni wajumbe kadhaa wa mkutano wa kamati maalum ya CCM uliofanyika Zanzibar, inasemekana wamelipinga vikali suala hili. Hii ni kuonyesha kwamba jambo hili lina kasoro nyingi na linaweza kuleta madhara kwa CCM, kwa Wanzanzibari, na Watanzania kwa ujumla .

Katika barua hii Mheshimiwa Rais, tungependa kunyanyua sauti zetu kwa unyenyekevu kwako juu ya mapendekezo haya na tunasema:

SISI WAZANZIBARI TULIOILETA BARUA HII KWAKO, HATUKUBALIANI KABISA NA MAREKEBISHO YA KATIBA YATAKAYOMUWEZESHA RAIS WA ZANZIBAR KUCHUKUA MADARAKA YA URAIS KWA ZAIDI YA VIPINDI VIWILI VYA MIAKA MITANO MITANO, NA TUNAKUOMBA UTUMIE NGUVU ZAKO ZA KIUTAWALA KUYASITISHA MAREKEBISHO HAYO.

Mheshimiwa Rais, tungependa kukukumbusha kuwa, kila raia ana wajibu katika nchi yake, lakini kiongozi wa nchi anabeba dhima kubwa katika taifa. Ustawi wa nchi na utengamano wa kijamii hautegemei tu utiifu wa raia, kiongozi mkuu wa nchi anawajibika siyo tu katika shughuli za kila siku za kiutendaji, lakini vile vile ni muhimu kutoa mwelekeo unaofaa katika kuendeleza nchi. Hasara iliyoje itakayoikabili Zanzibar kama Rais wake ataamua kuzibia masikio ushauri wa wengi walio weledi na wenye busara. Kwa hivyo tunakuomba tena Mheshimiwa Rais kutumia uwezo wako kusitisha mabadiliko haya ya katiba na tunamuomba Mungu akupe nguvu za kufanya uamuzi huo. Amin.

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR NA WAZANZIBARI!

Ahsante sana.

Wazanzibari Wanaoipenda nchi yao.
________________________________________________________________________
Nakala kwa :

Rais wa Jamhuri ya Tanzania,
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Mwanasheria Mkuu, Zanzibar,
Mabalozi wa nchi za nje Tanzania,
Vyama vya Siasa Tanzania,
Mashirika ya haki za binaadamu,
Vyombo vya Habari