Author : Farouk Abdulla Amour
    Date: Sat, 08 Jan 2000
Subject: KUMFURAHISHA MUISLAMU MWENZIO NI SADAKA

Nduguzangu,
Assalaam Alaaykum ,

Kwa sote Iddi Mubarak.

Hivi kiasia ya saa mbili unusu asubuhi ndio tulisali Salaa ya Iddi hapa Muscat - Al Hail. Kwa hikika japo kuwa nalikwenda msikitini na furaha hivyo hivyo, lakini hata hio pia ilizidi kupungua kwa kuingiliwa na majonzi.

Katika khutba ya Iddi imam ilihimiza ya kwamba baada ya Salaa tuchungue mitaani mwetu kama kuna yatima, kizuka au dhaifu yoyote yule alipekee, aliekosa mahitajio ya Iddi ili tuwasaidie. Alihimiza tuhakikishe kuwa tunawasaidia watu wetu, wazee, ndugu, marafiki wa wazee na kadhalika. Aliendelea kwa kusema, haiwi furaha kwetu iwapo atakuwepo miongoni mwetu hata mmoja ambae hata pata neema hii ya Iddi. Aliendelea kwa kusema kuwa leo ni siku ya kuzidi kusameheana, kuondoa ghadhabu na chuki baina yetu. Alihimiza juu ya faida na fadhila ya kusamehe.

Kwa hakika kila akiendelea katika khutba yake mie nilikuwa sipo kabisa, nalikuwa mbali. Akili na fikara zangu zote zalikuwa juu ya wale ambao wanaouwezo wa kutenda haya, lakini hawatendi. Wanauwezo wa kusamehe, lakini hawasamehe, wanauwezo wa kunyosha mikono yao na wengi wakanufaika, lakini hawafanyi hivyo. Badala yake wengineo ikawa kinyume chake ndivyo wanavyotenda, badala ya kurehemu, wao hudhulumu na kuadhibu. Mwenyezi Mungu atunusuru, binadamu anapewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kutenda mema ikawa anakataa na badala yake ikawa maovu ndio mengi anayoyatenda.

Leo sisi tunakula sikukuu, mie niko nyumbani kwangu Alhamdulillah nimezungukwa na watu wangu, tunakila neema, siha, furaha, chakula na pia tunan'gara kwa mavazi. Lakini ni mie mie ambae kwa uwezo wangu - madaraka - ndio nimesababisha ndugu yangu kuwa mbali na watu wake katika siku hii, ni mie nimesababisha watoto wake wakose mapenzi ya baba hata katika siku hii; ni mie mie ndio nimesababisha bwana akose kumuona mke hata hii leo. Ni mie mie ndio nimesababisha bibi amkose bwana hata hii leo. Inafaa nijiulize nini nitamjibu Mwenyezi Mungu, ambae kufika mbele yake ni kusita pumzi tu. Jee sitizami wangapi kabla yangu waliokuwa na uwezo wakafanya vile walivyopenda, leo wako wapi. Yuko wapi Firauni, yuko wapi Haamana, yuko wapi Qaarun; hao ni wazamani wa hizi siku zetu, yuko wapi Shah wa Iran, yuko wapi Helesalasi (sp?) wa Ethopia? Yuko wapi? Yuko wapi? na wangapi. Jamani hii dunia ni njia tu, tunakokwenda kuzito!

Mzee wetu alinambia kuwa yeye akiomba Mwenyezi Mungu amnusuru na dhulma basi huomba mara mbili anusurike na kudhulumiwa na mara tatu huomba Mwenyezi Mungu amnusuru na kudhulumu, yaani anaogopa zaidi kudhulumu kuliko kudhulumiwa. Mwenyezi Mungu ameahidi kumnusuru mwenye kudhulumiwa japo baada ya muda. Hebu natuzingatie na tuchunguwe vipi wamemalizikia wote wale waliokuwa majabbari waliokuwa wakifunga na kufungua, kuuwa na kutesa. Hebu natuchungue walimalizikia vipi kabla ya hata kufika mbele ya Mwenyezi Mungu na kukuta hisabu yao. Tunasikia wengine walifika kula kinyezi chao, wengine walidhalilika wakawa mamwehu na kupita wakiomba, wengine tunasikia walizikwa na kaburi halikubali kusita maji. Hebu tuwatazame waliokuwa tukiwastahi kuwa ni wazee wetu wema, wameuaga vipi ulimwengu; tumtizame Sayyid Omar bin Sumeit, Sheikh Suleiman Al Alawy, Sheikh Haji Muhamadi, Sheikh Ameir Tajoo. Kutokana na haya tutazidi kutambuwa kuwa hisabu ya Mwenyezi Mungu huanza tangu hapa ulimwenguni.

Jengine la kukumbushana ni juu ya kuhifadhi amana. Miongoni mwa amana na dhamana za walioko katika madaraka ni kuhifadhi na kutumia ifaavyo mali ya Umma. Katika mali ya Umma muna mali za mayatima, mali za Mwenyezi Mungu - Wakfu, muna mali za wasiofahamu. Hizi zote ni dhamana katika mabega ya waliomo katika madaraka. Israfu na ubadhirifu ni haramu na ni miongoni mwa vitendo vya shetani:

"Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashetani (wanamfuata Shetani). Na Shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake." (Al-Israa : 27)

Hayeshi.
Kwa kumaliza, tumuombe Mwenyezi Mungu Mtukufu atusaidie tuweze kujisaidia -
Amin.

Wa Billah Tawfiq
Farouk