Author : Dr. Y. Salim
    Date: Tue, 25 Jan 2000
Subject: KISUKARI KWA MTU WA KAWAIDA 1

Muongozo kwa wagonjwa wa kawaida wa Ugonjwa wa kisukari

Utangulizi

Mara nyingi inakuwa ni vigumu kuwa mgonjwa katika nchi zetu za kimasikini 
kutokana na sababu mbali mbali, moja wapo ya sababu hizo ikiwa ni upungufu
wa 
mtu wa kawaida wa kupata taaluma ya siha ya kimsingi kinyume na zile nchi 
zilizo endelea.

Madhumuni ya maelezo haya mafupi ni kujaribu kuwa funua macho wagonjwa wa 
kawaida kuhusu kujipatia ujuzi wa magonjwa ili hatimae waweze kufahamu
sababu 
za magonjwa tofauti, kuweza kujikinga na kufuata miko matibabu
itakikanavyo.

Kwa kuanzia nitatoa makala tatu zote zikilengwa kwa wagonjwa na wale
wafanya kazi wa siha ambao hawashughulikii ugonjwa wa kisukari kila siku
pamoja na 
kuwalengea wale ambao wanawatayarishia maakulati wagonjwa wa kisukari na
ukoo 
wa wagonjwa hao kwa jumla ambao  watafaidika na ujuzi wa chakula cha siha 
bora. Ni muhimu kujua kwa kila mtu, hasa wale jamaa mlio huko ghuba na 
makanzu yenu yanayo ficha matumbo, kwamba mkipunguza utumiaji wa mafuta, 
siagi, samli na margarini katika chakula na kwa wakati huo huo mkafanya 
riadha, mtaweza kupunguza uzito na kwa mara nyingi mtaweza kuepuka na
kupanda 
kwa kiwango cha sukari katika damu. Kwa wale wengineo katika ukoo kula 
chakula bora kutawakinga na magonjwa ya kisukari na magonjwa ya 
moyo-na-mishipa-ya-damu.
Muongozo huu wa mwanzo utashughulikia ugonjwa wa kisukari kwa jumla na
baadae 
kujaribu kuchambua aina tofauti za kisukari.

Nini ugonjwa wa kisukari ?

Tunapokula chakula, sukari kutokana na chakula inaingia kwenye damu.
Insulin huisaidia sukari kutoka kwenye damu na kuiingiza kwenye mfano
musuli, pahali ambapo sukari hutumiwa kama ni nguvu (energy). Kiwango cha
sukari katika damu 
ni 3-7 mmol/l (54-126mg/dl). 

Ikiwa sukari haiwezi kuingia katika mfano musuli, basi sukari hujirundika 
katika damu. Hapo sukari katika damu hupanda na ikiwa itapimwa mara kadhaa 
kila asubuhi kabla ya chai ya asubuhi na kuonekana kuwa iko zaidi ya 6,7 
mmol/l (121mg/dl) basi hapo mtu husemekana kuwa na kisukari.

Kuna aina tatu za kisukari

Aina ya 1: (type 1) mtu huwa hafanyi insulin. Hali hii zaidi huonekana
baina ya watoto na vijana (zamani ikijulikana kama insulin dependent
diabetes 
mellitus- IDDM).

Aina ya 2: mtu anaweza kufanya insulin, lakini huwa haitoshi, na huwa 
haifanyi kwa kasi sawa na wale watu wasio na kisukari. Sababu kuu ya hali 
hii, ni kwamba mtu huwa ana mashahamu mengi tumboni au kitambini/vitambini
na 
kwa wakati huo huo huwa hafanyi riadha ya kutosha (zamani ikijulikana kama 
non-insulin dependent diabetes mellitus-NIDDM).

Kisukari cha waja wazito (Gestational diabetes) huchomoza wakati wa mimba,
na 
ili kulinda mtoto tumboni mara nyingi inabidi mja mzito apewe insulin ili 
sukari ya damuni iwe baina 4-8mmol/l. Ikiwa mja-mzito atakuwa na sukari 
nyingi damuni akiwa na mimba, kutakuwa na uwezekano mkubwa kwamba, mtoto 
atazaliwa na athari tofauti.

Kisukari kinazidi Zanzibar

Ingawa sina takwimu za karibuni kuhusu kisukari huko Zanzibar lakini, ni
siri 
ya wazi, kwamba idadi ya watu wenye kisukari ya Aina ya 2 wameongezeka
mara 
dufu. Hali hii inatokana na upungufu wa wataalamu wa kutosha wa magonjwa 
haya, upungu au bei za juu za madawa haya, mabadiliko ya malaji, umasikini
na 
upungufu wa mipango maaluum kwa upande wa serikali. Sio masikini tu 
waliokumbwa na ugonjwa huu bali hata wale wanaoishi Mazizini, Mbweni,
Mombasa 
na kwengineko kunakoishi wanaojiweza nao wamekumbwa. Kwa kawaida kila pale 
penye mzazi mmoja mwenye kisukari watoto  2 kati ya 5 wana hatari ya
kupata 
kisukari.

Watoto khususan wana hatari ya kurithi upungufu wa kasi ya kazi ya insulin.
Hata ikiwa wazazi wamepata kisukari baada ya kuwazaa watoto  wao, wazee 
tayari wanakuwa wameshawarithisha watoto wao hatari ya upungufu wa kasi
hiyo.

Ingawaje, kisukari bila ya shaka kinaweza kukingika, yaani mtu asipate 
ugonjwa, ikiwa mtu atajikondesha kwa kula chakula bora na kufanya riadha.

Ikiwa mmoja kati ya wazazi ana kisukari, inatakiwa wale watoto wakubwa 
wapimwe sukari katika damu asubuhi kabla hawakula kila baada ya miaka
miwili.

Sukari na shahamu katika damu zinaambatana

Ikiwa sukari katika damu itakuwa iko juu kwa muda mrefu, shahamu katika
damu nayo itapanda.

Kisukari kwa hivyo ni ugonjwa wa kisukari na wa kishahamu

Kiwiliwili kina athirika ama ikiwa sukari itakuwa imepanda au shahamu
itakuwa 
imepanda katika damu. Haya mambo mawili yanaleta matatizo kama yale ya 
magonjwa ya moyo (heart attack), kiharusi (stroke) kupungua kasi ya macho 
(hatimae upofu), magonjwa ya mafigo, upungufu wa usambazaji wa damu na 
kupungua kuhisi miguuni (wengine hadi ya kuungua bila ya kuhisi) hali
inaweza 
kusababisha kukatwa vidole, sehemu ya nyayo na  miguu (Seyyid Abdulla Bin 
Khalifa). Zaidi ya hayo kasi za udume za mwanamume hupungua.

Chakula bora chenye shahamu kidogo, riadha na hatimae dawa vinaweza
kupunguza 
idadi ya sukari na shahamu katika damu ikawa ya kawaida. Hali hii
inamfanya 
mtu ajihisi vizuri kiakili  na kuweza kuishi maisha mazuri na ya kawaida.

Upimaji wa sukari damuni

Kwa wale wenye uwezo ni jambo la maana kununua mashine ya kupimia sukari 
damuni au vituo vya siha viwe na mashine angalau mbili ili moja itaweza
kui 
chunga nyengine ikiwa ina fanya makosa ya kupima hasa pale vifaa vikiwa 
vimekwisha muda au kuathirika kwa sababu hii au ile. Angalia ! upimaji wa 
damu ni muhimu sana.

Pima damu yako mara moja kwa wiki kabla hujanywa chai ya asubuhi na saa
moja na nusu baada ya kunywa hiyo chai.

Mapendekezo ya viwangovya sukari damuni:

-4-7 mmol/l (72-126 mg/dl) kabla ya chai/chakula cha asubuhi
-si zaidi ya 10 mmol/l (180 mg/dl) saa moja na nusu baaba chakula cha
asubuhi

Kama sukari yako damuni iko juu zaidi, ni muhimu kwamba, unaji shajiisha 
zaidi kupunguza kiwango cha sukari damuni. Wasiliana na tabibu wako,
ukihisi hufanukiwi

Riadha

Riadha inaleta siha njema ya akili na kiwiliwili. Fanya ile riadha
uipendayo mwenyewe. Wakati una kisukari, ni lazima ufanye riadha ambayo
inaambatana na mwendo wa miguu wa mchapuo  muwafaka kwa kiasi cha saa
moja. 

Faida ya riadha
-unakusaidia kupunguza uzito
-insulin yako itafanya kazi bora
-viwango vya sukari na shahamu katika damu vitaanguka
-moyo utapata nguvu - kwa hivyo kuweza kujikinga na heart attack
-presha itashuka

Matibabu ya dawa

Kama riadha na chakula bora havisaidii itabidi kutumike dawa za aina ya 
vidonge au insulin.

Shahamu nyingi kwenye damu inatibika kwa vidonge, riadha na chakula bora. 
Tabibu wako ataamua aina gani ya matibabu utahitajia.

Ni muhimu kwamba unatumia dawa zako kila siku ili dawa ziweze kufanya kazi 
yake barabara. Insulin haina gelatine na kuna patikana vidonge bila ya 
gelatin.

Inaendelea

Chakula cha kila siku

Inafaa tukumbuke tena kwamba ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa wa shahamu
vile 
vile.

Mtu anaweza kuendelea kula chakula chake cha kawaida ili mradi anakumbuka 
kwamba ni suala muhimu sana kupunguza utumiaji wa mafuta, siagi, samli na 
margarin.

Mtindo wa kumimina mafuta moja kwa moja katika sufuria au kikaangio si
mtindo 
wa busara hata kidogo. Ni jambo la maana na busara kutumia kijiko cha
kulia 
katika kupima kiasi gani cha mafuta mtu anatia katika mapishi: hakikisha 
kwamba unatia kijiko kimoja cha kulia kwa kila mtu mmoja katika ukoo.

Chakula cha kuchemsha ni cha siha zaidi kuliko cha mikaango kwa sababu ya 
upungufu wa mafuta.

Afadhali kula chapati/mkate wa kusukuma wa ngano nzima upikwao mkavu bila
ya mafuta kushinda ule unaokaangwa kwa mafuta.

Epuka pilau na wali wa nazi na afadhali ule wali wa maji.

Hakikisha kwamba unaitoa, kuikeketa na kutupa shahamu yote ya nyama kabla 
hujaitia chunguni.

Idadi ya milo ya kila siku

Si busara kula rundi la maakulati bora kupendelea kula milo midogo midogo
ya mara kwa mara. Njia hii inasaidia kupunguza uzito wa mtu vile vile na 
kuifanya insulin  kufanya kazi kwa kasi au bora zaidi.

Tahadhari na kukwepa chai au mlo wa asubuhi kwa vile unahitaji kuanza siku 
ukiwa na chochote tumboni. Baada ya mlo wa asubuhi unaweza kuendelea kula 
mara mbili zaidi kwa kutwa ikiwa umezoea kula hivyo. Lakini hakikisha
kwamba unakula kiwango kidogo kidogo, tofauti na ulivyozoea. Kula ndimba
kubwa kubwa 
asoruka paka hazina tija kwa siha yako.

Inawezekana kuwa huna njaa baina ya nyakati za kula, lakini inafaa
utambuwe 
kwamba ni vyema ukila vitu vidogo vidogo vikavu kama ya ngano nzima na ule 
pamoja na tunda moja. Ulaji huu wa udoho udoho utakufanya usiwe na njaa
kali wakati wa milo mikuu na kwa hivyo utakula kidogo zaidi.

Matunda

Matunda ni chakula bora, lakini mengi yao yana sukari nyingi, kwa hivyo ni 
vizuri kula si zaidi ya mawili-matatu kwa siku ukihakikisha kupunguza
ulaji 
wa zabibu, embe, ndizi mbivu, matunda makavu kama tende, zabibu kavu,
zeituni 
kwa vile matunda haya yana sukari nyingi.

Maziwa na mitindi

Maziwa yana sukari-ya-maziwa (lactose) , kwa hivyo mtu anahitajiwa asinywe 
zaidi ya nusu liter kwa siku, hii ina maana maziwa ya aina mbali mbali
kama 
mtindi na yoghurt bila ya matunda.

Vidonge vya utamu haviathiri kiwango cha sukari katika damu kwa hivyo mtu 
anaweza kutumia vidonge hivi kwa kutayarishiya maakulati badala ya kutumia 
sukari ya kawaida. Vidonge hivi viko vya aina tafauti kwa mfano saccharin 
(sakkarin), cyclamate, acesulframe, aspartame (Nutra-sweet) n.k.
Cyclamate na acelsulframe zinaweza kuchemshiwa bila ya kuharibu ladha.
Nutra-sweet inapoteza ladha yake tamu ikiwa itachemshwa au kubekiwa kwa
zaidi 
ya dakika chache. Sakkarin inageuka kuwa chungu ikiwa itachemshwa zaidi ya 
digrii 70 kwa muda mrefu.

Epuka na vitu vilvyo tiwa ladha ya utamu kwa matumizi ya sorbitol na au 
fructose kwa vile vina ongeza sukari katika damu.

Inafaa mtu anywe vinyaji vilivyo punguzwa utamu au kutiwa utamu wa vidonge 
yaani vinyaji bila ya sukari. Hakikisha kusoma kama sharubati fulani ina 
sukari au haina sukari.

Epuka na vyakula vya utamu-utamu kama vile haluwa, jelebi, laddu-laddu, 
peremende-pipi, asali, matunda ya kuchemsha, jamu, makeki-keki, kashata
n.k. na ujizoweshe kula vyakula visivyo vitamu tamu.

Mboga-mboga ni vyakula bora na haziongezi sukari katika damu :
mabilingani, 
mabamia, vitunguu, squshi, kebeji, kerot, tungule/nyanya, tango,
koliflower, fiwi, kisambu, mchicha n.k.

Njegere, kunde, mbaazi, maharage, njugu mawe, muhogo, ndizi mbichi,
majimbi, viazi vikuu ni vyakula vyenye mizizi mizizi ambavyo vinateremsha
sukari 
katika damu. Tahadhari na ndizu mbivu, za mkono wa tembo, boga na viazi 
vitamu.

Ukila chizi hakikisha kwamba haijajaa shahamu yaani iwe  ya kiasi cha 18% 
ambayo itakuwa na shahamu ya kiasi cha gramu 18 kwa kila gramu 100 za
chizi. Kwenye pakiti unaweza kusoma kiasi cha asili mia cha shahamu kwenye
chizi.

Samaki ni wenye manufaa makuu kisiha na aina zote zinaruhusiwa
Usile mayai zaidi ya 2-3 kwa wiki.

Wasia wa Chakula bora    
Punguza utumiaji wa mafuta, siagi, samli na margarini
Kula udoho udoho na viwango vidogo vidogo
Kula mboga mboga kwa wingi, ama za kuchemsha au mbichi
Kula vyakula vya mizizi mizizi
Kula vyakula vyenye ngano nzima na chapati za ngano nzima
Pale inapomkinika soma kwenye paketi/chupa  kuhusu kuwemo au kutokuwemo 
sukari ndani 

Maakulati/machopo chopo

Ikiwa mtu atafuata mapendekezo ya hapo juu, anaweza mara 1-2 kwa mwezi
kula 
maakulati kama vile kwenye shughuli,  maaliko, sherehe yenye vyakula
vyenye 
mafuta/siagi na sukari kwa wingi.

Mengineyo
Matatizo
Baadhi ya nyakati mtu anaweza kufikwa na maafa kama misiba, matatizo ya 
kifamilia n.k. Na kwa hivyo mtu hupendelea kujiliwaza kwa kula zaidi au 
kupoteza hamu ya kula kabisa. Hali hizi zina athiri ugonjwa wa kisukari na 
kwa hivyo mtu inambidi aendelee na kula kama ilivyopendekezwa ingawa mara 
nyengine inaweza kuwa ni vigumu.

Magonjwa mengine

Hutokea kwamba mtu anapata magonjwa mengine juu ya ugonjwa wake wa
kisukari, anatakiwa aendelee na matibabu yake ya kisukari kama kawaida. Na
anategemewa apime sukari katika damu mara kwa mara zaidi kuliko kawaida
kwa vile magonjwa 
mengine yanaweza kuifanya sukari ikapanda zaidi ingawa matibabu
yanaendelea 
kwa kawaida. Kwa hivyo kumbuka kuwasiliana na tabibu wako pindi sukari 
ikipanda.

Safarini

Jambo la mwanzo kumubuka kuchukuwa dawa yako na kipima sukari chako.

Ramadhani

Ikiwa unapata insulin na kisukari chako kina matatizo kurekibishika ni
bora 
uepuke na kufunga

Ingawaje ikiwa unahisi uko timamu na umedhibiti utibabu wa kisukari chako 
unaweza kuendelea na kufunga. Ikiwa unakula vidonge, ingefaa kuvila baada
ya futari na kwenye daku. Inayumkinika kwamba dozi ya dawa zako
ikabadilika kwa hivyo wasiliana na tabibu wako.

Macho

Nenda kwa mganga wa macho mwaka mara moja, ambae atachunguza hali ya ndani
ya 
maicho yako kwa kutumia kama kijidarubini. Ikiwa kwa muda mrefu sukari
yako 
imekuwa juu katika damu, inawezekana ukatoka damu kutoka mishipa ya damu 
ndani ya jicho na kutawanyika ndani ya jicho. Ikiwa hali hii haijatibiwa 
mapema inaweza kusababisha upofu !!!!

Viganja vya miguu (feet)

Mara kwa mara wagojwa wa kisukari watapata vidonda katika viganja/nyayo za 
miguu kati ya wale wenye kisukari. Kuna hatari kwamba vidonda havitapona 
ikiwa vitapuuzwa, kwa hivyo chukua hadhari kubwa na vidonda hivyo.

Unapopata kidonda nyayoni/miguuuni kiangalie kidonda hicho kwa makini na
kama 
hakiponi kama kidonda cha kawaida kwa muda wa siku chache wasiliana na
tabibu 
wako haraka.

Unapo tawadha chunguza kama kuna alama ya wekundu-wekundu miguuni/nyayoni, 
alama ambazo hatimae huweza zikawa vidonda, hususana kama viatu vina bana.

Sigara

Wavutaji sigara wameonekana kuwa na hatari ya kupata heart attack mara
tatu 
zaidi ya wale wasio vuta sigara. Kwa hivyo kama unavuta, wacha kuvuta na
kama 
huvuti usianze kuvuta.

Udume/Uume

Kati ya wanaume 6-8 katika wanaume 10 wenye kisukari cha aina ya 2 hupata 
matatizo ya kupungua kasi ya uume ikiwa sukari damuni imekuwa iko juu kwa 
muda mrefu. Usione haya, wasiliana na tabibu wako ambae atakushauri kuhusu 
uwezekano tafauti wa matibabu.

Kumbuka kwamba una wajibu mkubwa na ugonjwa wako wa kisukari na wewe
mwenyewe 
ndiye mwenye dhamana ya mwanzo kabisa na matabibu bila ya shaka matabibu
wako 
wata kuwa tayari kukusaidia.

Ni matumaini kwamba mapendekezo haya yatakusaidia kudhibiti viwango vya 
sukari na shahamu katika damu yako - kama vile vilivyodhibitiwa kabla ya 
ugonjwa wako.

 
Mwisho wa sehemu ya kwanza

Wasalaam
Yussuf