Author : Farouk Abdulla Amour
    Date: Thu, 09 Mar 2000
Subject: DHULMA NI MOTO

Nduguzangu,

Assalaam Alaaykum,

HAZIDI DHAALIM ISIPOKUWA KHASARA

Hazidi dhaalim isipokuwa khasara, haya ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, 
kwa hivyo hayana shaka wala hayendi pongo; ni lazima iwe hivyo tukitaka 
tusitake. Msiba wetu mkubwa sisi ni kuwa tunajiita Waislamu, tuna sali, tuna 
funga, na tuna kwenda Maka, Hijja na Umra mara kwa mara;  kutoa Zakaa ni 
wachache miongoni mwetu wenye kutenda hivyo, japo kuwa tunao uwezo, kutoa ni 
pagumu. Khatari yetu ni kwamba tunajiita Waislamu lakini tunakubali baadhi 
ya maamrisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na tunayakanya mengineyo. Ubaya 
ulioje kitendo hichi.

……. Je!  Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake?  Basi hana 
malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya dunia, 
na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa.  Na Mwenyezi Mungu 
si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda. (Al Baqara : 85)

Ubaya zaidi ni kwamba yale maovu mno ndio tunayo yatenda.  Uchafu wa jinsi 
ndio tumebobea nao, wangapi wanazaliwa bila ya ndoa za sharia, vinywaji vya 
kulevya ndio humo tulimo zama, wangapi wamepoteza akili kwa ovu hili, na 
mengi yamfano wake.  Mengi ya haya mara nyingi huwa ni baina ya mja na 
Mwenyezi Mungu, kama vile kutumia vinywaji vya kulevya.  Kuna yale baina ya 
mja na mja mwenziwe, kama vile kumgusia na kumharibia mwenzake watu wake, 
kuuharibu Umma kwa vinywaji vya kulevya na kuwatia katika haramu kwa 
kuidumisha nchi katika haramu.  Inasikitisha kuwa serikali imekuwa ni sababu 
ya mengi ya haya maouvu yanayotendwa nchini mwetu.  Haya mahoteli na hawa 
(wanaoitwa) watalii, ambayo sio chochote isipokuwa ni vichaka vya uchafu tu, 
yote haya yanazaa haramu juu ya haramu nchini mwetu.  Wangapi wa watoto wetu 
wanaharibika kutokana na vichaka vya uchafu hivi.  Walioko katika utawala 
ndio mas-uli wa yote haya,  Kesho itawabidi waeleze mbele ya Mwenyezi Mungu, 
jamani hisabu ni nzito!

Ovu zaidi katika haya ni dhulma ya kumnyan’ganya mtu mali yake.  Dhulma hii 
ni kubwa mno, dhulma hii ni sababu ya kila balaa nchini mwetu. Na kwa nini 
isiwe hivyo na hali ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuonya juu ya ovu hilo 
kwa maneno yenye maana kama hii:

“Wala haimuongezekei dhaalim isipokuwa ni khasara”.

Vile vile kuna Hadithi ya Mtume wetu s.a.w. yenye maana ya kwamba  dua ya 
mwenye kudhulumiwa hairejei (husibu tu).

Wenye kuamini na kuyaogopa haya, yaani kuogopa kudhulumu; baada ya jitihada 
yao mwisho wa uwezo wao kujiepusha na kudhulumu, basi daima humuomba 
Mwenyezi Mungu amkinge na kudhulumiwa, lakini huomba mara nyingi zaidi 
Mwenyzi Mungu amuepushe na kudhulumu.  Hivi ni kwa vile anavyojua na kuogopa 
malipo ya kudhulumu - tangu hapa duniani na mpaka Kesho.  Dhulma ni moto, 
unateketeza kila kilichoingia ndani yake dhulma. Kijana mdogo, aliemjuwa 
Mwenyezi Mungu na akamchelea; kijana huyo amekataa kurithi kutoka kwa baba 
yake mali ya dhulma. Mtoto hakukubali kurithi mali hio; kwa sababu 
alimuogopa Mwenyezi Mungu na kufahamu natija ya kula haramu.  Pia tunasikia 
kuwa wako baadhi ya nduguzetu ambao wamewarejeshea wenye haki zao haki zao, 
baada ya kutambuwa uovu wa dhulma na uovu wa kutumia mali ya kunyan’ganya.  
Mwenyezi Mungu awazidishie imani na awajaalie na wengine nao wapate uongofu 
na imani wajivue kutokana na uovu wa mali ya dhulma na wao watende kama hao 
nduguzao – Amin.  Msiba ni kuwa mashekhe wetu wamefumba macho na wametia nta 
masikioni,  wamejifanya mabubu hawataki kuisema haki – mwenye kunyamaza 
kuisema haki ni sawa na shetani bubu.  Tusisahau jamani ya kwamba wenye 
elimu - mashekhe - wao ndio wa mwanzo kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa 
vile kukaa kimya wasiiseme haki na kuwanasihi nduguzao, khasa waongozi.  
Mashekhe ni wajibu wao kuwanasihi viongozi - kwa hikima, upole na busara.  
Viti, magari na majumba yamekuwa ni bora zaidi kwetu kuliko Akhera yetu, 
jamani kwa nini tunakubali kuuza Akhera yetu kwa hii dunia chafu na yenye 
kupita.  Subhanallah.  Dunia ina khatari mashekhe wanakubali hata kuishi 
katika majumba ya kunyan’ganya, ati tumepewa na serikali. Jawabu hii itafaa 
Kesho?  Wako wapi waliokumba, jee wamekwenda na chochote?

Sisi katika ukumbi huu tulikuwa na sauti kali kwa Bwana Mohd Yusuf 
(Observer) pale alipokuwa akieleza “mapinduzi matukufu”, hapana shaka sauti 
za kukataza mawazo hayo zilikuwa ni ndivyo.   Hakuna kuuwa, kunajisi, 
kunyan’ganya mali za watu, kufunga, kuadhibu na kufukuza wananchi kutoka 
katika nchi yao, haiwi vitendo hivi kuwa ni vitendo “vitukufu”; kwa hivyo 
mapinduzi hayawi ni matukufu.  Msiba ni kwamba tumeteta kwa sauti kali juu 
ya Bwana Mohd Yusuf (Observer) aliposema “mapinduzi matukufu”, lakini ndugu 
zetu – viongozi wa CUF – wamesema zaidi ya mara moja kuwa wao “wanaheshimu 
mapinduzi”.  Sio hivyo tu, bali wamefika kusema - ikiwa ni kwa kujitetea au 
kwa kujinasibisha na kujifakharisha -  kuwa na wao, yaani viongozi wa CUF 
(baadhi yao) wameuwa.  Subhaanallah!  Binadamu anajisifu kuwa ameuwa, sio 
hivyo tu;  Muislamu anajisifu kuwa amemuuwa nduguyake. Hebu fikiri vipi 
unakuwa unapotokezea kwa ajali tu ukamponda paka, hapana shaka unahisi 
vibaya bila ya kiasi, leo baada ya kuuwa bado unajisifu kuwa umeuwa.  
Muislamu anatakiwa akimuasi Mwenyezi Mungu basi ajisitiri,  kuna maasi 
kuliko kuuwa, kubwa zaidi ya kuuwa ni fitina.  Jee ndio ipo dalili ya 
kupatikana Nusra ya Mwenyezi Mungu hapo?  Jawabu ni kuwa aslani haipatikani 
Nusra ya Mwenyezi Mungu katika hali hii.  Mwenyezi Mungu ametwambia:

"Enyi mlioamini! Mkiinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, naye atakunusuruni na 
ataithibitisha miguu yenu”. (Muhmmad : 7)

Mwenyezi Mungu hahitaji Nusra ya yoyote yule wala hapana mwenye Nusra, sisi 
ndio wenye kuhitaji Nusra ya Mwenyezi Mungu, sisi ndio wahitaji, wahitaji wa 
kila kitu kutoka kwa Mola wetu Mlezi.  Kupata Nusra ya Mwenyezi Mungu ni kwa 
kufuata yale aliotuamrisha na kuepuka yale aliotukataza.  Moja katika 
aliotukataza ni kunyan’ganyana mali zetu, kitendo hichi ni haramu, na mwenye 
kukitenda anapata dhambi kubwa.  Mwenyezi Mungu amesema katika Aya ya 188 ya 
Surat Al Baqara:

“Wala msiliane mali zenu kwa baatili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate 
kula sehemu ya mali za watu kwa dhambi, na hali mnajua”.

Inaaminiwa na wengi kuwa haya masaibu yanayoendelea kutufika Zanzibar ni 
malipo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa hii dhulma iliofanywa na inayoendelea 
kufanywa mpaka hii leo na bila ya kuwasana walaa kukatazana.  Sote 
tunafahamu ya kwamba wamelaaniwa Banu-Israil kwa vile walikuwa hawakatazani 
maovu waliokuwa wakiyatenda.  Ikiwa wao waliokuwa hawakatazani wamelaaniwa, 
jee sisi ambao juu ya kuwa hatukatazani bali zaidi tunafundishana kutenda 
maovu. Viongozi wetu wanatupeleka katika maovu, wanatufanya tuishi katika 
haramu, tangu katika chakula, malazi, mavazi; bali hata tunaposalia ni juu 
ya ardhi ya haramu.  Ardhi ya kunyan’ganya haifai hata kusali juu yake.  
Uovu ni wetu, uovu ni wetu kwa vile sisi hatuwaambii viongozi wetu kuwa ni 
wajibu wao watuepushe na dhulma, watuepushe na haramu.  Mwenyezi Mungu 
Mtukufu ametuamrisha tujiokoe nafsi zetu na za watu wetu kutokana na Moto.  
Kujiokoa huku ni kwa kukatazana kutenda maovu na kuwasana kutenda mema.  
Mwenyezi Mungu ametwambia:

" Enyi mlioamini!  Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu, na Moto ambao kuni zake 
ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu hawamuasi Mwenyezi 
Mungu kwa amri zake; na wanatenda wanayo amrishwa (yote)”  (At’Tahriim : 6).

Ni wajibu wetu tuwanasihi viongozi wetu kwa busara, upole na maarifa ya 
kwamba ni wajibu wao kuziokoa nafsi zao na zetu  kutokana na adhabu ya 
Mwenyezi Mungu.  Kuziokoa ni kwa kutuepusha na dhulma, kutuepusha na 
machafu, tangu ya jinsi, madawa ya kulevya na mengineyo.  Ni wajibu wao 
watupangie mipango ya kutuvua kutokana na haramu, kutuvua kutokana na 
dhulma.  Sio watwambie kuwa watahalalisha haramu.  Vipi utampa mtu fidia ya 
mali yake alionyan’ganywa miaka 36 iliopita, ameharamishiwa na manufaa ya 
mali hio, ametiwa katika umasikini kwa kunyan’ganywa ile sababu ya riziki 
yake na ya watu wake.  Kwa kunyan’ganywa mali yake amepata khasara ya kipato 
na zaidi amepata maudhi ya kinafsi. Wengi kwa natija ya kitendo hichi 
iliwalazimu waihame nchi yao bila ya kujuwa wapi wanakwenda. Jee haya yote 
yatatolewa fidia, sio hivyo tu, jee wamekubali wao kuchukuwa hio fidia?  Au 
ndio wakitaka wasitake utawala ndio ushasema. Na hio fidia inatoka katika 
mfuko wa nani, mfuko wa mwananchi, jee hao wananchi wamekubali haki yao 
wapewe wengine ili wathibitishiwe haramu.  Hio ndio haramu juu ya haramu. 
Haki haitendwi hivyo.  Waliopewa mali hayo sio kuwa wamenufaika kwa hicho 
walichopewa, wameingizwa katika khasara ya duniani na ya Akhera.  Wamekula 
haramu wao, wamelisha haramu watu wao na watu wa nchi nzima;  haramu ikaenea 
kwetu sote, hata yule anaekwenda kwa kutembea tu huingia katika haramu hii.  
Haya yametokea, ndio yeshatokea;  waliofanya haya wamefanya ama kwa kutojuwa 
uharamu wake, au kwa kutekeleza maamrisho ya mabwana wasiotutakia kheri.  
Lakini jee ndio inatujuzia kuwa tuendelee kulishana haramu na hali ya kuwa 
sote sasa tunatambua vyema malipo ya kitendo kiovu hichi?   Hapana shaka 
sio, ni wajibu tutokane na haramu.  Ikiwa nduguzetu upande wa serikali, CCM 
kwa sababu yoyote ile wanashindwa kujivua na uovu huu;  ni wajibu wa 
nduguzetu wa upande wa pili - CUF kuwasaidia nduguzetu CCM kujivua wao na 
kuivua nchi yetu kutokana na balaa hili la dhulma na haramu.   Msiba ni 
kwamba wao, yaani CUF ndio wanashadidia - khasa unapokaribia uchaguzi - kuwa 
wakishika serikali basi hawatarejesha mali yaliyonyan’ganywa lakini watawapa 
fidia wale walionyan’ganywa.  Hebu na watufahamishe hukumu hii inatoka wapi, 
  katika Sharia ya Dini yetu tukufu, au katika dini gani?  Hakuna dini 
yoyote ile au wema wowote ule ulimwenguni unaojuzisha kunyan’ganya mali ya 
watu.  Sisi Waislamu badala ya kuwa waongozi wema imekuwa ndio wa mbele 
katika kuweka mifano miovu. Ubaya ulioje juu yetu. Ikiwa tutabakia katika 
hali hii basi tusitarajie maisha kuwa tutatengenekewa, tutaendelea hivi hivi 
kuishi katika  dhila  na kila maafa na balaa. Sote tunatambua vyema uovu wa 
kudhulumu haki ya mtu, ikiwa ni ardhi, nyumba au chochote kile.  Ardhi ya 
kunyan’ganya haifai kusali juu yake, haifai kupanda juu yake, haifai hata 
maji ya kisima kilicho chimbwa katika ardhi ya kunyan’ganya haifai kunywa 
maji yake.  Haifai kuishi katika nyumba ya kunyan’ganya, wala katika ardhi 
ya kunyan’ganya. Ikiwa haya, yaani kunyan’ganywa mali za watu yametokea 
miaka 36 nyuma katika hali mbali mbali, ni busara kutafuta njia na mipango 
ya kuiondoa dhulma hii.  Kufanya hivyo sio tu itapatikana radhi ya Mwenyezi 
Mungu kwa vile kupatikana radhi ya binadamu waliodhulumiwa haki zao, lakini 
pia itakuwa ni kuwatendea vyema zaidi wale ndugu zetu waliopewa kutumia hayo 
mali yalionyan’ganywa.  Mipango ya kulitengeneza suala hili ipo,  na itakuwa 
ni kwa faida yetu sote, itakuwa ni kwa faida ya yule alienyan’ganywa mali 
yake, kwa faida ya yule aliepewa hayo mali na pia itakuwa ni kwa faida ya 
serikali na nchi nzima.

Nduguzangu Wazanzibari, jukumu ni juu ya shingo zetu (wachaguzi);  viongozi 
ilivyo khasa ni kufuata waongozwa kwa mashauri mema, iwapo waongozwa wakiona 
uharibifu na wakakaa kimya basi jukumu ni lao wao waongozwa zaidi kuliko hao 
viongozi. Viongozi ndio wanaeleza kinagaubaga kuwa wakishika utawala mali 
yalionyan’ganywa hawatarejesha, yaani nchi itaendelea kuishi katika haramu.  
Iwapo wananchi wanaridhia haya na wakakubali kuwafikisha mabwana hao katika 
huo utawala, basi viongozi hawatakuwa na dhima wala kosa (kwao wao 
waongozwa) kwa sababu wameridhia wenyewe kuendelezwa kuishi katika haramu, 
kwa sababu wao mabwana wameeleza dhamiri wazi nao kabla ya kuingia katika 
uchaguzi na wachaguzi wakakubali kuwachaguwa ili wafike katika serikali na 
watekeleze haya walioahidi kuyatenda, yaani kudumisha na kuthibitisha 
haramu.

Iwapo tunayo nia basi mipango ipo madhubuti ya kulishughulikia suala hili 
bila ya kuleta mashaka kwa wale waliopewa hayo mali, vile vile Inshallah 
italeta ridhaa za walionyan’ganywa mali zao.  Inshallah rai kukhusu mipango 
hii tutaileta humu kwa kuizingatia na kutoa mawazo yetu.  Muhimu ni kwamba 
dhulma ni lazima iondolewe kwa manufaa ya wale waliopewa na kwa wale 
walionyan’ganywa mali zao na kwa manufaa ya nchi nzima kwa jumla.  Dhulma 
haileti isipokuwa ni khasara tu.

Kwa kumaliza, jengine, ni wajibu wetu tuwatake viongozi wetu kuwa watuletee 
mfumo wa “Serikali ya Umma”,  “National Government”  tuepukane na huu mfumo 
muovu wa “Serikali/Upinzani”. Tunafuraha kusikia kua nduguzetu CUF wamelipa 
umuhimu suala hili - Inshallah na nduguzetu CCM na wao watatambuwa umuhimu 
wa suala hili na kuliunga mkono na kutekelezeka na kuthibitishwa katika 
Katiba ya nchi - Amin.  Hili neno upinzani ndio sumu ya masikilizano, 
kushirikiana na kushauriana;  kukosekana haya ndio msingi wa mvutano na 
bughdha na natija yake ni kukosekana maendeleo ya aina yoyote ile na kubakia 
nchi inasononeka katika umasikini na kubakia nyuma. Tusisahau dhamana yetu 
kwa Mwenyezi Mungu na kwa vizazi vyetu, tunahisabu ambayo itatubidi tueleze. 
  Dhamana ni mzigo mzito

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azidi kutusaidia tuweze kujisaidia na 
atutoe katika haramu na kila la shari na atuongoze katika kila la kheri na 
baraka – Amin.

Wa Billah Tawfiq

Farouk