Author :
Hassan O. Ali
Date:
Tue, 21 Mar 2000
Subject:
NEWSBOT: 'Robot' la habari!
Assalaam alaykum,
Kwenye barua aliyonitumia sheikh Ali Alawi hivi karibuni
aliniulizia kuhusu "Newsbot". Pia natumai mmeshaona mara mbili
zimeletwa kwenye ukumbi habari za Zanzibar kutoka kwenye anuani
yenye jina "Zanzinet Newsbot". Sasa labda baadhi ya wajumbe
wanajiuliza, "Newsbot" hasa ni nini?
Ni kawaida ya wataalamu wa Internet kulikata jina "Robot" na kuliita kwa
ufupi "bot". Kwa hivyo "Newsbot" ni ufupisho wa "News Robot". Kikawaida,
"Robot" ni mashine inayofanya mambo yenyewe baada ya kuwekewa programu
fulani ya kuiendesha. Katika muktadha wa Internet, "Robot" ni programu
inayotumwa kufanya kazi mbali mbali (mara nyingi mbaya na ngumu) kwenye
mtandao wa Internet. Ma-robot maarufu ni yale yanayotumiwa na Search
Engines mbali mbali (Yahoo, Alta Vista, Lycos, Google, n.k.) kutembelea
websites mbali mbali na kukusanya taarifa zilizo kwenye websites hizo
na kuzitunza kwa namna nzuri ya kuweza kufikiwa tena kwa urahisi.
"Zanzinet Newsbot" ni "robot" nililolitengeneza kusaka habari za
Zanzibar zinazochapishwa kwenye sehemu mbali mbali za Internet. Kwa
sasa nimelielekeza "robot" hilo kila siku majira ya saa nane za usiku
za Tanzania, liingie kwenye website ya IPP Media na "kusoma" magazeti ya
Guardian na Nipashe. Likiona habari yoyote iliyotaja Zanzibar, au Unguja,
au Pemba, nimeliamuru "robot" hilo lizipeleke habari hizo kwenye anuani
ya Zanzinet.
Hiyo ni kwa kuanzia tu. Baadaye kidogo, inshaallah nitaliamuru
"robot" hilo liende kusaka habari za Zanzibar kwenye vyanzo vingine
mbali mbali. Ni matumaini yangu kuwa "robot" hilo litarahisisha
kazi inayofanywa kwa umahiri mkubwa na wajumbe mbali mbali akina
Sheikh Mohammed Salim, Sheikh Harib (Captain H.), Sheikh Nasser Mohammed
(Superchuwa), Sheikh Mbarouk (Peku), Sheikh Mbarouk (wa New York),
Sheikh Ali Nassor (Ali 2000), na wengine wengi ambao kwa kweli tumekuwa
tukifaidi sana matunda ya jitihada zao. Kwa kweli jitihada zao bado
zinahitajika kwani "robot" ni "robot" - linaweza kukorofisha kwa
njia kadhaa.
Nitashukuru sana kupokea ushauri wowote kuhusiana na "robot" hilo.
Wassalaam.
Hassan,
Ottawa.