Author : Maalim Khamis
    Date: Tue, 29 Feb 2000
Subject: SALMINI BADO ANA KETE

Wapendwa wananeti,

      kwanza sina budi kuungana na umma wa wazanzibari wenzetu popote pale 
walipo katika kuuunga mkono uamuzi muhimu kabisa kupata kutolewa na 
halmashauri kuu ya CCM( kwa serikali zake tawala) kwa ajili ya manufaa na  
maslahi ya wazanzibari. Busara kubwa iliyofanywa na Halamashauri hiyo baada 
ya kuona kuwa hakuna njia yoyoye itakayomwezesha Salmini asimame kwa mara ya 
tatu, zaidi ya ile ya ubabe na ghasia, ambayo ingeiletea Zanzibar maafa 
makubwa. Hongera halmashauri kuu ya CCM kwa kuukubali ukweli huo kwa mara ya 
kwanza katika historia ya Zanzibar.

    Lakini kwa wakati huo huo, ninaunga mkono maoni ya Dk. Yussuf Salim 
kuhusu hatma ya Salmin Amour. Itakuwa si busara kumdharau rais Salmin Amour 
kwa wakati huu. Na vile vile itakuwa pia si busara kushadidia ripoti za  
vyombo vya habari vya Tanzania bara dhidi ya Salmin. Kwani maslahi ya vyombo 
vya habari hivi na washirika wao wa uongozi wa serikali ya Muungano sio 
maslahi ambayo sisi wazanzibari tunayatarajia, yaani kupigania heshima ya 
visiwa vyetu .

    Yaliyotokea katika Halmashauri kuu ya CCM yanapaswa yawe funzo na onyo 
kwa sisi wazanzibari, ya kuwa Dola, Nchi na Taifa huru ambalo sisi 
tunalililia kila siku bado lina kazi ya kulitetea. Ukweli kwamba hatma ya 
nchi bado inaamuliwa Dodoma, na ukweli kuwa rais wetu (hata iweje!) 
anavyodhalilishwa pamoja na kuwa yeye anawakilisha maslahi ya wazanzibari 
milioni moja, nchi mshirika sawa katika muungano, sio jambo la kushangilia 
hata kidogo. Tujaribu kutofautisha safu za dhamana za kisiasa na watu wenye 
dhamana hizo. Ni kweli kuwa Salmin Amour mwenyewe ndiye mhusika mkuu katika 
mambo yote haya. Lakini ni wajibu wetu kulinda na kuheshimu na kutetea sare 
zinazowakilisha utaifa wetu na utambulizi wetu.

    Ninapendekeza tutoe mwito kwa wananeti na kumpelekea Rais Salmin Amour 
ujumbe utakaomfanya afahamu kuwa sisi wazanzibari kila siku tumekuwa 
tukimsihi atetetee maslahi ya wazanzibari wote kwa jumla na kutetea haki na 
utaifa wa Zanzibar, na kuwa ikiwa sasa yeye amekwishafahamu, basi sisi 
hatutamtupa kamwe katika kutetea maslahi ya utaifa wa Zanzibar katika 
kurekebisha muundo wa Mungano wake ulio sasa na Tanzania Bara. Rais Salmin 
bado anayo kete ya kucheza, sasa ni wakati bora kabisa wake yeye kujaribu 
kuunganisha maslahi ya wazanzibari wote, bila ya kujali chama, au itikadi.

   Ninatoa mwito kwa wenzetu wa CUF kumkaribia Salmin Amour kwa maslahi mya 
wazanzibari wote. Inshallah, pengine matokeo ya mkutano wa Dodoma umekuwa 
ndiyo njia ya kuleta mafahamiano baina ya wazanzibari wote. Tafadhalini 
tusitupe nafasi hii. Inaweza ikafungua kurasa mpya ya maslahi ya wazanzibari 
katika muungano.

  Ikiwa Salmin Amour kweli anapigania maslahi ya wazanzibari wote, basi 
atuonyeshe wazanzibari. Mwache aweke kando sakata za kisiasa baina yake na 
CUF na amwalike Seif Sherriff Hamad katika mazungumzo ambayo, pindipo 
yakitokea, basi huenda ikailetea zanzibar afueni mpya ya siasa.

  Ninaomba tena kwa wazanzibari wenzangu. yaliyotokea Dodoma hayamgusi 
Salmin Amour tu! Bali yanatugusa sote wazanzibari katika kutetea uhuru na 
heshima ya visiwa vyetu.

  Mungu Ibariki Zanzibar.