Author :
Farouk Abdulla Amour
Date:
Thu 6 Apr 2000
Subject:
KWELI SISI NI WAISLAMU?
Nduguzangu,
Assaalaam Alaaykum,
KWELI SISI NI WAISLAMU?
VITENDO NDIO JAWABU
Kweli sisi ni Waislamu ni suala ambalo hapana shaka wengi wetu baada ya muda
na muda hutupitikia nyoyoni mwetu na kujiuliza. Kwa bahati nzuri, kwa vile
alivyotujaalia Mola wetu Mlezi tuishi basi suala hili linajijibu wenyewe.
Jawabu ni kwamba tutizame vitendo vyetu jee vinafuatana na maamrisho ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu, ikiwa vitendo vyetu vinafuatana na maamrisho ya
Mwenyezi Mungu basi hapana shaka sisi ni Waislamu, iwapo vitendo vyetu ni
kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu basi jawabu ndio vile vile – sisi sio
Waislamu. Inasikitisha na kuhuzunisha, bali ni khatari; kwa vile kuwa
vitendo vyetu havifuatani na maarisho ya Mwenyezi Mungu hata kidogo; lakini
kinyume chake ndivyo ilivyo, yaani vitendo vyetu ni kinyume kabisa na
maamrisho ya Mola wetu Mlezi.
Mwenyezi Mungu ametuambia kuwa sisi ni Umma mmoja:
“Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa
hivyo niabuduni Mimi”. (Al Anbiyaai : 92)
Hivi ndivyo alivyotufahamisha Mola wetu Mlezi, yaani sisi ni Umma mmoja na
kuwa Yeye Pekee ndio tumuabudu. Jee sisi tuko wapi katika haya. Kwanza
sisi hatuishi kama ni Umma mmoja, tunaishi hali ya kuwa ni wenye kufarikina
na kugombana na kufika kuuwana. Isitoshe, badala ya kumuabudu Yeye Mwenyezi
Mungu Pekee kama alivyotuamrisha imekuwa tunaabudu waungu kadhaa wa kadhaa,
wako wenye kuabudu cheo, wako wenye kuabudu pesa na kipato, wako wenye
kuabudu mabwana wakubwa; wote hawa tumewafanya kuwa ni waungu wetu na
kumuacha Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mola wetu Mlezi.
Katika khutuba yake ya kuuaga (ulimwengu) Mtume wetu mpenzi s.a.w.
aliwakhutubia Masahaba – lakini khasa aliukhubia ulimwengu wote kwa jumla –
kwa maneno yenye maana kama haya:
“Hakika DAMU yenu na MALI zenu na HESHIMA zenu, ni haramu juu yenu
(kudhulumiana) kama ilivyo haramu siku yenu hii, katika mwezi wenu huu na
katika mwaka wenu huu”.
Maneno haya ya Mtume wetu mpenzi - na maneno yake yote mengineo s.aw., bali
na vitendo vyake vyote - msingi wake ni Qura’an Tukufu, kama
tutakavyojaaliwa kuona huko mbele.
KUMWAGA DAMU/KUUWANA
Haya ndio maneno ya Mtume wetu s.a.w., yaani ni haramu Muislamu kumwaga damu
ya mwenziwe, ikiwa kumwaga damu ni haramu; basi kuuwana hapana shaka ni
haramu zaidi. Adhabu ya mwenye kumuuwa mwenziwe kwa makusudi ni kudumu
katika Moto wa Jahannam milele na kughadhibikiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“Mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo
atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia
adhabu kubwa.” (An-nisaai : 93)
Ikiwa mwenye kumuuwa mwenziwe kwa makusudi juu ya adhabu ya Moto ni
kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu, kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu. Sote
tunatambuwa vyema mtu kukasirikiwa na kipenzi chake, licha kukasirikiwa na
mkubwa wake, khasa mkubwa wa kazini. Jee kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu
Mtukufu – ikiwa tunamjuwa Mwenyezi Mungu. Hapana shaka iwapo yuko miongoni
mwetu anaekasirikiwa na Mwenyezi Mungu na sisi tukawa tumo tunamfanya ndio
mwenzetu basi hapana shaka natija ya kukasirikiwa huko itatufikia na sisi
vile vile, hayo ndio malipo ya kuambatana na waovu. Madhali tumeuwana basi
hapana shaka ghadhabu za Mwenyezi Mungu ndio tunazoishi nazo hadi hii leo.
Sisi sio tumeuwana tu, bali wako walionajisiwa kisha ndio wakauliwa na
kutoswa baharini, wako walio chimbishwa makaburi (mashimo) yao kisha
wakauliwa kwa kupigwa marisasi mbele ya wenziwao mmoja baada ya mmoja; kisha
kusukumizwa humo mashimoni, miongoni mwao wamo waliofukiwa na bado
wanatweta. Wako waliofungwa na gari na kubururwa mameli na mameli huku
wakijipiga na minazi kisha – haijulikani hivi vijapande vya mwili na mifupa
vilivyobakia kama vilifukiwa au vilitumbukizwa baharini. Na mengi na mengi
ya kashfa na idhlali tumefanyiana. Ujabari ulioje huu, au dhulma ilioje hii
– hisabu Kesho. Haya yamepita na yeshapita, kuyataja madhumuni yake sio
kunyoosheana vidole tu, makusudio na ambalo ndio lenye faida ni
kukumbushana, kuzingatia, kujuta, kutubia na kujiepusha tusiyatende maovu
haya tena.
Msiba ni kwamba badala ya kutubia na kuwaomba samahani waliokosewa haki zao,
imekuwa sisi tunatenda kinyume chake. Tunajisifu kuwa tumeuwa. Tunanadi
kuwa haturejeshi haki ilionyang’anywa. Maana yake ni kwamba tuliotenda sio
maovu, bali ni ndivyo. Haya yamenadiwa juu ya majukwaa, na binadamu –
wananchi – wakayashangilia na kuyapigia makofi; kutilia nguvu kuwa vitendo
vile viovu na huku kunadi viongozi ni ndivyo bila ya ila wala aibu. Jee
sisi ni Waislamu? Kabla ya kuendelea mbele, inafaa kwanza tujiulize yote
yale tuliofanyiana, kuuwana na mengi mengineo, nini khasa ilikuwa makusudio
yake, yaani kwa nini tukafanyiana yote yale? Hapana shaka kila kitu kina
sababu na makusudio yake. Ikiwa ni kuchukuwa serikali na mali za watu basi
serikali siku ya tatu tu ili kuwa yote iko chini ya mikono ya mabwana na
mali ndio hivyo hivyo. Sasa kule kuuwana kulioko endelea kwa miezi na miaka
ili kuwa ni kwa sababu gani? Katika mauwaji haya waliuliwa kila aina ya
watu, tangu Mahizbu, Wa- Afro-Shirazi, na wengineo ambao siasa ilikuwa mbali
na wao – muhimu wote waliokuwa ni Waislamu wema ndio makusudio katika
mauwaji hayo.
KUNYANG’ANYANA MALI ZETU
Kitendo hichi ni haramu, na mwenye kukitenda anapata dhambi kubwa. Mwenyezi
Mungu amesema katika Aya ya 188 ya Surat Al Baqara:
“Wala msiliane mali zenu kwa baatili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate
kula sehemu ya mali za watu kwa dhambi, na hali mnajua.”
KISA CHA AMR NA UMAR r.a.
Misri ilipoingia katika Dola ya Kiislamu Liwali wake, Amr bin Al A'as
alijenga msikiti ambao upo mpaka hii leo. Walipo zidi Waislamu wingi alitaka
kuupanua msikiti, lakini ilikuwepo nyumba ya mwanamke wa Kikristo ambayo
ililazimika ivunjwe kwa ajili ya kuupanua ule msikiti. Liwali alikuwa
tayari kununua nyumba ile ili ivunjwe na utanuliwe msikiti. Mwanamke
kakataa. Liwali aliivunja nyumba akautanua msikiti.
Yule mwanamke akafunga safari ya ngamia (siku hizo hakuna ndege wala
motokari ya kupanda) tangu Misri mpaka Madina kwa Khalifa Omar bin Khattab
r.a. kwa ajili ya kutetea nyumba yake aliyo pokonywa na serikali kwa nguvu.
Sayyidna Omar r.a. alimpelekea Liwali Amr "Jibu Sharia" yaani "Summons" aje
mahkamani Madina kuwa kashtakiwa na yule mwanamke Mkristo ambaye ni raia
katika Dola ya Kiislamu. Liwali kujitetea alisema:
"Sikumnyan'ganya huyu bibi haki yake. Fedha zake zipo. Na nimechukua nyumba
yake kwa maslaha ya umma kuupanua msikiti, kwani wenye kusali wamekuwa
wengi."
Sayyidna Omar akamkhiarisha mwanamke achukue fedha au ajengewe nyumba yake
pahala pengine. Mwanamke akakataa kata kata. Alisema:
"Naitaka nyumba yangu vile vile ilivyo kuwa, pahala pale pale ilipo kuwa."
Sayyidna Omar akatoa amri yake kumwambia Liwali: "Vunja sehemu ya msikiti
pale ulipo ongeza, na mjengee huyu mwanamke nyumba yake vile vile kama
ilivyo kuwa."
Hiyo ndiyo hukumu ya haki sawa - haki sawa kwa wote . Haki sawa kwa tajiri,
haki sawa kwa masikini, haki sawa kwa mkubwa, haki sawa kwa mdogo, haki sawa
kwa mwongozi, haki sawa kwa mwongozwa. Haya ndio mafunzo ya Dini ya binadamu
ambayo ndio njia ya maisha yetu hapa na kuendea Kesho.
Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo
hukumu baina ya watu muhukukmu kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri
sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona. (An-nisaai
: 58)
KUVUNJIANA HESHIMA NA KUDHALILISHANA
Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukataza kuvunjiana heshima na kudhalilishana:
“Enyi mlioamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake
wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala
msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia
jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu.”
Haya ndio mafunzo ya Dini yetu, jee sisi tuko wapi na mafunzo haya; sisi
tuko kinyume cha haya. Wako waliowapiga wazee wao bakora mbele za watu,
ikiwa hawakufanya wao kwa mikono yao, basi wameridhia wazee wao watendewe
uovu huo. Vipi hawakuridhia na wao walishirikiana na waovu hao katika yote
yao tangu wakati huo na baada yake. Tunasaha utukufu wa mzee na maamrisho
ya Mwenyezi Mungu juu ya wazee wawili. Wako miongoni mwetu walio dhalilishwa
kwa kukaharishwa kwa mdomo wa bunduki kuachishwa ahli zao ili waolewe na
mabwana wenye nguvu, (sijui ndoa gani hizi). Wako walio fanyiwa uchafu
ahli zao mbele ya macho yao na huku wameekewa mdomo wa bunduki vifuani mwao
wasifurukute. Wako walioekwa mbele ya Umma katika mikutano ya hadhara na
kukejiliwa na kuadhiriwa kisha kusukumizwa jela na mwisho wao ni kuuliwa.
Wako walioosheshwa vyoo, vyoo vilivyo tapika uchafu wa binadamu kuenea nje
kufikia mpaka magotini. Wako waliotukaniwa ahli zao mbele ya wakuu wenzao,
kumalizikia kwako ni kuuliwa. Wako waliokogeshwa makobe, basi kwa idhilali;
kobe tokea lini akataka kukogeshwa. Wako na wako, na wako; hatumalizi.
Hayo ni ya jana, jee ya leo. Maovu kama haya bado yanaendelea, viongozi juu
ya majukwaa kwa sauti kali wamefika kuvunjiana heshima (kama neno heshima
lingaliko bado). Yametendeka haya kwa kutia arusi juu ya majukwaa,
yametendeka haya kwa kutajiana juu ya majukwaa majumbani na watu wa
nyumbani. Hawa ndio viongozi wetu. Lakini waongozwa wako hali gani? Ndio
wao waongozwa wenye kuyashangila haya na kupiga makofi na vigelegele.
Zanzibar imeona mengi, Wazanzibari wamefanyiana mengi. Mwenyezi Mungu
atunusuru na adhabu Zake na atujaalie moyo wa toba, tutubie na tuombe Rehema
Zake na atutakabalie – Amin, Amin.
MWENYE KUONJA ASALI HAONJI MARA MOJA
Huu ni msemo maarufu wa wazee wetu, na Waarabu nao husema: “man shabba ‘alaa
shay-in shaaba ‘alaaih”, maana yake ni kama hivi: “mwenye kukulia na kitu
basi hukonga nacho”, yaani huendelea kukitenda katika umri wake. Ni
maumbile ya nafsi ya binadamu kupenda kutenda maovu iwapo haikatazwi na
kuzuiliwa. Ilivyokuwa viongozi wanafika kunadi maovu na kujisifu kwa maouvu
hayo juu ya majukwaa, na wananchi wakapiga makofi kuyawafiki na kutilia
nguvu maneno hayo; hapana shaka huku ni kuthibitisha kuwa tuendelee kutenda
haya na sisi tunayaridhia na tuko pamoja na nyinyi, na tutatenda tena
mukituamrisha tu. Umma uovu ulioje huu!! Inavyotarajika na ni ndivyo kabisa,
ni kwamba viongozi walaani vile vitendo viovu vyote, na kutaka samahani kwa
wale waliiotendewa maovu haya na kutengeneza lile linaloweza kutengenezeka;
sio kujisifu na kutafakhari na maovu. Ilivyokuwa viongozi hawakutenda hivyo
wala hawakukaa kimya, bali wanajisifu, ilikuwa ni wajibu wa wananchi
kuwazindua waongozi wao na kuvikanya vitendo vyao hivyo na kuwataka
wavikanye mbele ya Umma, kama walivyovitangaza mbele ya Umma. Yote haya
hayakutendwa, badala yake viliitikiwa vitendo viovu hivyo kwa makofi na
vigelegele. Kwa hivyo basi, ilivyokuwa viongozi (wakiwa katika hali ya
upotofu) weshapewa na wafuasi wao (wakiwa katika hali ya upotofu) heko -
“green-light” - kwa maovu ya kuuwa na kunyang’anya na mengi mengineo, basi
ni ndivyo kabisa kuwa na wao viongozi kwa upande wao kupanga na kutilia
nguvu kutendeka tena maovu hayo. Katika misingi hii ndipo waliposikilikana
viongozi hao hao kunadi “jicho kwa jicho na jino kwa jino”, na wengine kati
ya viongozi hao hao kunadi kugawa na kuweka tayari mapanga. “Mwenye kuonja
asali haonji mara moja” na “Kipofu haachi mkongojowe”. Wazanzibari, mti
na jicho. Jamani huu sio mchezo mwema.
KUUWANA HAKUTENGENEZI
Ikiwa mauwaji ya 1964 na ya baada yake, yamethibitisha na kuzidi
kuthibitisha kila siku kuwa hayawezi kubadilisha imani ya binadamu; basi
haitayumkinika mauwaji yoyote yale kubadilisha imani za binadamu.
Ilivyokhasa ni kuthibitisha kwa wale binadabu wema - bali na hata kwa waouvu
watakaokubali kuzingatia na kuuona ukweli - kuwa mauwaji hayaleti ila ni
khasara kwa pande zote, bali zaidi ni kwa wale walinaotenda kuliko
wanaotendewa hayo maovu.
Maovu ya 1964 na kuendelea mpaka hii leo yamebakisha Umma wa Zanzibar katika
mafungu mawili makubwa vile vile kama yalivyokuwa kabla ya hio 1964.
Mauwaji na kutesa nguvu hakukuweza (wala hakutaweza) kubadilisha imani za
watu. Ingalikuwa wema umetendeka na kuuondowa uovu basi nyoyo
zingalibadilika na kuelekea kwenye Umma wa kheri na kupunguza kubakia katika
kundi la shari na uovu. Na kwa nini isiwe hivyo na hivyo ndivyo alivyo
tuhakikishia Mola wetu Mlezi:
“Mambo mazuri na mabaya hayawi sawa. Ondosha (ubaya unaofanyiwa kwa
mema); tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui atakuwa kama
ni jamaa (yako) mwenye kukufia uchungu. Lakini (jambo hili) hawatapewa ila
wale wanaosubiri, wala hawatapewa ila wenye hadhi kubwa (kwa Mwenyezi
Mungu)”. (Fusilat : 34-35)
Pia Mola wetu Mlezi ametufunza faida ya kutendeana wema na kusameheana pale
alipomfunza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa maneno haya:
“Basi kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu umekuwa laini kwao
(Ewe Muhammad). Na kama ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka
wangalikukimbia. Basi wasamehe wewe na uwaombee msamaha (kwa Mwenyezi
Mungu) na ushauriane nao katika mambo. Na ufangapo nia mtegemee Mwenyezi
Mungu (tu ufanye hili uliloazimia). Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda
wamtegemeyao”. (Al ‘Imraan : 159).
Jee kweli sisi ni Waislamu? Suala hili kila tukiendelea mbele tunalijibu
kwa vitendo vyetu sisi wenyewe.
VITA VYA PANZI NEEMA YA KUNGURU
Natunowe mapanga, na upande wa pili (labda na wao) wanapiga mdeki bunduki
zao (aundae hadumbi). Jee ni nani huyu anaekusudiwa kwa silaha zote hizi,
nguruwe au chui wameingia mitaani. Makusudio ni Mzanzibari, Mzanzibari
amuuwe Mzanzibari. Hili sio ajabu kwetu sisi, ni mazoea yetu; tumefanya
hayo 1961 na tumefanya zaidi ya hayo 1964; kwa hivyo kufanya tena 2000 sio
ajabu ni ada yetu kufanya hivi baada ya kila muda. Kuuwana kwetu ni mchezo
mwema na ni furaha na sifa kutenda hivyo. Bado tunajiita Waislamu.
Lakini basi, mti na jicho. Kunguru yeye hahitaji kutia girisi mizinga yake,
kazi chafu tutatenda sisi wenyewe kwa mikono yetu wenyewe, yeye bwana
mkubwa atangojea tumalizane wenyewe kwa wenyewe hapo tena yeye ateremke na
adondowe kwa raha na furaha. Baada ya kutenda hivyo, na kuwa wenye hawapo
tena; hapo tena ndio bwana mkubwa atatia muhuri wake kwua “Zanzibar haipo
tena”. Azma ya kuviburura visiwa hivi kati ya Bahari Hindi itatimia.
Badala ya mkuu wa mkoa atawekwa “Major” kuwa ndio mkuu wa Zanzibar mpaka
pale hali ya khatari itakapo ondolewa. Kuondolewa hio hali ya khatari
inategemea bwana kunguru atakapo penda kutenda hivyo. Jee nduguzetu mulioko
katika uwongozi hili ndilo munalolitaka liwe, jawabu ni ndio; hili ndilo
munalotutakia liwe. Jawabu ni kutokana na vitendo vyenu. Suala ni kwa nini
au nini maslaha yenu katika kututakia balaa hili, balaa la kutaka tumalizane
na kuimaliza Dola yetu kabisa kabisa? Tafadhali tuelezeni. Ikiwa sio hivyo
basi tunalokuombeni ni kwamba muitambue hii khatari iliotukabili na mukae
pamoja mushauriane na mushirikiane tuiokoe nchi yetu na balaa hii. Sisi
wananchi tuko bega kwa bega na nyie waongozi wetu katika matengenezo, lakini
iwapo mutang’ang’ania maslaha yenu (yako wapi maslaha hayo ikiwa nyie ndio
zaidi munao dhalilishwa) na kutupeleka katika kuangamia basi itatubidi
tuseme: “Inatosha, inatosha, hatuwezi kubakia na nyinyi.” Itatubidi
tufikiri njia za kutuokoa.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azidi kutuongoza katika kila la kheri sisi
na waongozi wetu na kila la shari – Amin, Amin.
Wa Billah Tawfiq
Farouk