Author : Harith Ghassany
    Date: Fri 7 Jul 2000
Subject: MABADILIKO YA KWELI

Wapenzi Wana Zanzinet

Assalam Alaykum,

Sidhani kama yupo mkereketwa hata mmoja wa CCM/SMZ ambaye anaweza kukataa 
kuwa SMZ/CCM imeshindwa kuyapatia ufumbuzi wa kudumu masuala yafuatayo 
yanayolikabili taifa:

1. Kuondosha rushwa nchini na ubadhirifu uliokithiri.
2. Kuzoroteka kwa:

a. Huduma za afya.
b. Elimu.
c. Kilimo.
d. Umeme na maji.
e. Mahakama na uadilifu.

Pamoja na yote hayo, wakereketwa wa SMZ/CCM wanaamini ya kuwa ASP/CCM ndicho 
chama pekee kilichowaletea Wazanzibari Mabadiliko ya Kweli ambayo ni 
kuuondoa utawala wa kifalme wa kiomani Zanzibar.

Sina hakika kama wanachokichukia wakereketwa wa SMZ/CCM ni utawala wa 
kidhalimu au mfumo wa kiutawala wa kifalme. Hawafahamu kama utawala wa 
kijamhuri unaweza ukawa wa kidhalim zaidi hata kuliko wa kifalme na kuna 
aina za tawala za kifalme ambazo ni za kidhalim zaidi kuliko tawala za 
kijamhuri.

Jambo muhimu ambalo wakereketwa wa SMZ/CCM na CUF inafaa walizingatie ni 
kuwa mapinduzi au mabadiliko ya kisiasa peke yake hayana nguvu ya 
kukabiliana na matatizo sugu ya kiuchumi na kijamii.

Baada ya mauaji na utesaji wanamapinduzi wenyewe hujikuta wamekata tamaa na 
kutambua kuwa walichokuwa wakikipigania hakijenda mbele hata hatua moja; na 
si hivyo tu, wameyarudisha nyuma mapinduzi yenyewe! Sababu ni mbili.

Misingi ya umaskini na unyanyasaji ipo pale pale na inangojea mabadiliko 
mapya kuirudisha katika hali ile ile ya kwanza ya kabla ya kufanyika 
mapinduzi na pengine hata hali ya kabla ya mapinduzi inakuwa ni vigumu 
kuifikia.

Sababu ya pili ni madhila na mateso ambayo yanavunja yote yalio ya 
kiungwana, yanajenga chuki ndani ya nyonyo za wananchi na kusababisha 
wabadilishe msimamo wao kutoka kuyaunga mkono mapinduzi na kumuunga mkono 
yoyote atakayewaahidi atawaletea mabadiliko ya kweli, ikiwa kweli au hata 
ikiwa ni porojo tu la kujipatia madaraka.

Kwa sababu tafauti chama cha CUF kimeshindwa kuja na ushahidi au rekodi 
yoyote kwa wapiga kura katika uchaguzi ujao wa Oktoba kwa njia ya kuonyesha 
kimeweza kuleta mabadiliko ya kweli katika kuyapatia ufumbuzi hata kama ni 
mdogo katika midani za:

1. Kuondosha rushwa nchini na ubadhirifu uliokithiri.

2. Kuzoroteka kwa:

a. Huduma za afya.
b. Elimu.
c. Kilimo.
d. Umeme na maji.
e. Mahakama na uadilifu.

Tumeona Hizbu Allah ya Lebanon. Hawana serikali mikononi mwao lakini wana 
kila aina ya huduma za jamii kuanzia mahospitali, maskuli, na mengi 
mengineyo. Vyama va upinzani Egypt vilifanya kazi kubwa sana kuwasaidia watu 
waliokhasirika wakati Masri ilipopigwa na mtetemeko wa ardhi hata ikawa aibu 
kubwa juu ya serikali.

Bila ya kuyapuuza mateso na madhila ya SMZ/CCM dhidi ya CUF, zipo sababu 
nyengine ambazo zimekifanya chama cha CUF kisijishughulishe na kueneza 
huduma za jamii Pemba au Unguja kabla ya kuingia Ikulu?

Pamoja na yote hayo wafuasi wa SMZ/CCM wanaamini ya kuwa CCM ndicho chama 
pekee kilichowaletea Wazanzibari Mabadiliko ya Kweli. Wafuasi wa CUF pia 
wanaamini ya kuwa chama cha CUF ndicho chama pekee kitakachowaletea 
Wazanzibari Mabadiliko ya Kweli.

Haya ni masala ya imani kuwa CCM imeshafeli na ushahidi upo; CUF 
haijajaribiwa kwa hivyo inafaa ipewe fursa halafu ihukumiwe.

Let us wait and see.

Wenu,

Harith Ghassany