Author : Ali Khamis Ali
    Date: Tue, 11 Jul 2000
Subject: Re: Elimu ya Ajira!!!!

From: Ali Khamis Ali
Subject: Re: Elimu ya Ajira!!!!


Wananet
A'Alaykum and Good morning

Nafikiria kauli ya Waziri wa Elimu, Mh. Mapuri,  kwenye vyombo vya habari,  
inahitaji kuangaliwa japo kidogo  na Wazanzibari. Kwa mtazamo wa ghafla ni 
kuwa anawavunja moyo sana Wazanzibari katika kujiendeleza elimu za juu.  
Ikiwa Wazanzibari watafuata kuwa hakuna ajira kwa hivyo watu wasisome elimu 
za juu matokeo yake yatakuwa ni kubakia nyuma kwa vijana wa Kizanzibari 
katika karne hii na zijazo.  Kuwa na watu wengi wasio na viwango vya Elimu 
ya juu ni kuwatayarisha vijana kutoweza ushindani wa ulimwengu katika 
masuala mengi sana. Ulimwengu wa leo unahitaji uoni mpana sana katika 
masuala mengi.  Wakati mwengine unaweza hata kuhisi kuwa mtu anahitaji 
achanganye nyanja tofatu (multidiscipline)  ndiyo anaweza kuyaona vizuri 
baadhi ya mambo au maamuzi ya kitaifa na kimataifa.  Kuwa na jamii ya watu 
wenye kiwango cha chini cha elimu nikuwandaa watu hao kuwa watumishi au 
watumwa tu wa wengine. Na hivi mimi nahisi kama Wazanzibari wanaandaliwa 
kuwa hivyo. Angalia vijana wazuri wa kifilipino, kiindonesia wanavyokuwa 
watumishi tu wanyumbani katika nchi nyingi kama Singapore, Malaysia na nchi 
za Mashariki ya kati.   Angalieni vile vile masaibu yanayowakumba vijana hao 
kwa waajiri wao. Hawawathamini hata kidogo na wengi wao hudhalilishwa sana.  
Naogopea sana kuwa mfumo wa Elimu wa CCM kwa vijana wa Zanzibar una ajenda 
nisiyoifahamu.  Pengine nikuwageuza vijana wetu kuwa watumisha wa nyumbani 
wa Watanganyika baada ya miaka kadhaaa ikiwa mfumo wa huu wa Elimu 
utaendelea.

Jengine ninaloweza kusema ni kuwa hii inatia muhuri tu kufeli kwa SMZ chini 
ya CCM katika kuiendeleza Zanzibar na Wazanzibari. Mfumo wa elimu unaoweza 
kutoa ajira ni ule ambao unakwenda sambamba na maendeleo ya jamii hiyo.  
Hapa nakusudia mfumo wa elimu katika mtizamo wa maendeleo huangalia jamii 
hii inataka kufikia nini katika kipindi fulani. Hapo mfumo wa elimu huwa ni 
njia ya kuifikisha jamii kule inakotaka. Hapo ndipo inaweza kutoa ajira na 
kila siku kuongezeka kwa sababu jamii kila siku itakuwa na mwelekeo wa 
kufikia kiwango chengine cha juu zaidi cha maendeleo.  Kwa hivyo mfumo duni 
wa maendeleo huwa na mfumo duni wa elimu kwa sababu mfumo huo wa elimu huwa 
unaendelea kufikia malengo duni. Kwa hali hivo mfumo huo hauwezi kutoa ajira 
za kuendelea kwa jamii hiyo.

Wakati nikisema ajira si lazima iwe Serikalini tu, na naamini sana kuwa 
Serikali haiwezi kutoa ajira kwa kila mtu na ni lazima Serikali wenyewe 
ikubali hivyo.  Pamoja na Serikali kukubali kuwa haiwezi kutoa ajira kwa 
kila mtu lakini jukumu la kupanga mipango ya maendeleo bado linakuwa jukumu 
lake. Ni lazima ijenge mazingira mazuri sana kuwa mipango mingi ya maendeleo 
inaweza kufikiwa katika sekta binafsi na kutoa ajira nyingi kwa wasomi wa 
jamii hiyo.  Kwa hivyo ni lazima Serikali ijenge mazingira mazuri  sana 
katika kuzipa jumiya binafsi nafasi za kuendeleza mambo mbali na maendeo. 
Bahati mbaya kwanza hiyo mipango ya maendeleo haionekani na jumuiya binafsi 
zinazojaribu kuleta maendeleo zinabanwa sana kama vile Serikali iko tayari 
kufanya kila kitu kwa wananchi wake.

Kwa vile mfumo wa jamii hauko katika misingi ya kuiendeleza jamii ifikie 
kiwango fulani cha maendeleo basi mfumo huo utakuwa hauwezi kutoa ajira kwa 
vijana wake wanaomaliza na pengine hao walioajiriwa wataachishwa kazi kwa 
sababu hakuna uzalishaji unaofikiwa. Na hii ndivyo ilivyo jamii ya Zanzibar. 
Hakuna kinachotarajiwa kufikiwa katika suala la maendeleo kwa hivyo mfumo wa 
elimu utadumaa na si hasha wengine wakaona hakuna faida yoyote ile kupoteza 
wakati mwingi shule wakati elimu wenyewe haitumika kwa lolote katika jamii 
niliyo.

Hata hiyo Elimu inayoitwa ya kujiajiri wenyewe basi haitaweza kutoa ajira 
ikiwa hakuna mipango madhubuti ya maendeleo kwa Wazanzibari. Wazanzibari ni 
lazima waone vipi mfumo huo unaweza kuondoa tatizo kwa vijana wao.  Tatizo 
kubwa si uwanja wa Elimu tu bali mfumo mzima wa maendeleo Zanzibar. 
Ukiangalia tunao wahandisi wangapi wanaotukimbia kila siku wakati wengi wa 
wahandisi hao wanaweza kujiajiri na kuajiri wengine kama kuna mazingira 
mazuri ya maendeleo. Tunao madaktari wangapi wanaohitajika katika hospitali 
zetu na kufunguwa hospitali zao lakini wameondoka. Tunao mafundi wangapi 
ambao wanaweza kujiajiri lakini wameihama Zanzibar. Tunao wafanyabiashara 
wangapi walio na wanaoendelea kuihama Zanzibar kwa kutokuwa na mazingira 
mazuri ya biashara.  Nionavyo hata kama itakuwepo Elimu ya vijana kujiajiri 
wenyewe ikiwa hakuna mipango ya maendeleo itakayoungana na mfumo huo wa 
Elimu mambo yatabakia hivyo hivyo au mbaya zaidi.


La kusikitisha wakati wenzetu wanapanga kuwa kila raia wao aweze kufikia 
angalau elimu ya chuo kikikuu baada ya miak fulani sisi ndiyo mambo ni kama 
anavyoyaeleza Mh. Mapuri.

Nakumbuka pamoja janga la uchumi lililoikumba Malaysia miaka mitatu 
iliyopita nikimsikia Waziri wa Mkuu akiwahimiza Wamalisia kuwa waliotolewa 
kazini basi na wajiunge na masomo ya juu zaidi kwa sababu watawahitaji 
baadaye. Serikali ilikuwa na tamaa kubwa sana kuwa janga hilo si la maisha 
na wamo katika kulitatua. Na kweli hivi sasa mambo yameshakuwa mazuri  na 
wanawahitaji watu wao kwa wingi sana. Sasa kauli kama ya Mheshimiwa ianweza 
kutoa maana kuwa kama vile viongozi wa SMZ imekata tamaa.

Tafadhalini kama mmeshindwa katika kuiendeleza Zanzibar, na ndivyo ilivyo,  
msione haya wala vibaya kusema mmeshindwa na kutoa nafasi kwa wengine ambao 
wanahisi wana uwezo wa kuiendeleza Zanzibar. Binadamu ni yule anaekubaliana 
na ukweli na siye anayen'gan'gania matendo yake tu japokuwa anakiri kuwa 
ameshindwa.


Kila la kheri,
Ali