Author : Prof. Haroub Othman
    Date: Tue 6 Jun 2000
Subject: UTABIRI WA KISIASA NA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2000

UTABIRI WA KISIASA NA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2000

Sijui Sheikh Yahya Hussein na 'Profesa' Kajura hutumia mbinu na nyenzo
gani wanapokuwa  wanabashiri mambo, na sikufanya utafiti wa kujua ikiwa
yote wanayoyabashiri hutokea. Lakini kwa kadri ya foleni mtu anavyoziona
kwenye nyumba zao bila ya shaka kuna watu wanaoamini kwamba kuna ukweli
katika yale wanayoyabashiri.

Katika uwanja wa siasa mtu pia huweza kubashiri mambo, sio kwa kuangalia
nyota na vipi pepo za kaskazi na kusi zinavyovuma, bali kwa kuzingatia
nguvu za kisiasa za makundi mbali mbali katika jamii, vipi watu fulani
wanashawishi mambo katika siasa, hali ya kiuchumi ya nchi na uhusiano
wa nchi hiyo na jumuiya ya kimataifa. Ni baada ya kufanya utafiti kamili
na kuzingatia yote hayo ndio mtu anaweza kubashiri nini kinaweza kutokea
katika nchi au jamii fulani. Kwa kuzingatia mambo kama hayo ndio tuliweza
kubashiri katika uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 1985 kwamba Sheikh Idrisa
Abdulwakil hatopata zaidi ya asilimia 25 za kura kule Pemba na si zaidi
ya asilimia 60 ya kura zote Zanzibar. Matokeo halisi ni kwamba marehemu
Sheikh Abdulwakil alipata asilimia 26 kule Pemba na  asilimia 62 za
kura zote. Na katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995 tuliweza
kubashiri kwamba CCM na CUF havitoweza kupitana kwa wingi mkubwa wa
kura. Na hivyo ndivyo ilivyotokea. 


Kuyapuuza Matatizo

Tatizo kubwa ambalo linalikabili tabaka la kisiasa (political class)
Tanzania ni kwamba halikai kutafakari na kufanya utafiti wa mambo
yanayotokea katika jamii wala kuyakabili na kujifunza kutokana na
makosa yake. Huyachukulia mambo juu juu tu, na kuyasogeza matatizo
mbele ikitumai labda kwamba kila matatizo hayo yakikaa ndio yenyewe
yatajipatia ufumbuzi. Matokeo yake ni kwamba kunakuwepo na shehena ya
matatizo. Tatizo moja ambalo limekuwepo kwa muda mrefu na ambalo bado
halijapatiwa ufumbuzi kamili ni lile la muundo wa Muungano. Ni kweli mfumo
wa serikali mbili ni sahihi, lakini bila ya pia kuyakabili na kuyatafutia
ufumbuzi matatizo yaliojitokeza ambayo yameainishwa kwenye ripoti ya
kamati ya Shelukindo na kwenye hotuba ya mwaka jana ya Makamu wa Rais,
Dk Omar Ali Juma, kwa mabalozi wetu waliopo nchi za nje, suala la mfumo
wa Muungano litakuwa linatusumbua na kutufarakanisha. Haitoshi tu kusema
kwamba asilimia kubwa ya wananchi wanataka mfumo wa serikali mbili. Je,
mfumo huo hautaki marekebisho ambayo yatauboresha?

Dunia ya leo ni kama kijiji. Jambo litokeapo sehemu moja ya dunia
linajulikana na kufuatiliwa na sehemu nyengine ya dunia. Masuala ya haki
za binadamu, utawala bora, vita dhidi ya rushwa, kupingwa kwa unyanyasaji
na kuondoshwa kwa ubaguzi wa aina yeyote ni vitu ambavyo haviwezi kuwekewa
mipaka, wala mtu hawezi kujitetea kwa kusema kwamba litokealo katika
nchi yangu ni langu na lisiingiliwe na mwengine. Jumuiya ya kimataifa
imeshakubali kwamba binadamu ana haki fulani za msingi, na hata katiba na
sheria za nchi haziwezi kumnyima binadamu haki hizo. Na mwananchi hata
wa kijiji cha Tumbatu , Mbamba Bay na Biharamulo  anayajua haya. Kuna
nchi duniani ambazo zimejiwekea misingi fulani kwamba ndio itayoongoza
mahusiano yake na nchi nyengine; inapoona kwamba misingi hiyo haifuatwi
na inadharauliwa na nchi ilizo na uhusiano nazo, tusifikiri kwamba nchi
hizo zitanyamaza kimya. Na nchi hizo zinapokataa kutupa misaada, hata
katika dawa za chanjo kwa watoto, tusishangae na kulalamika!     

Ni kweli kwamba siasa ya ujamaa haikutuleta shibe wala kutufikishia
maji safi kwenye kila nyumba, lakini ilileta matumaini kwa mamilioni ya
Watanzania.  Kwa kubadilisha mfumo wa kiuchumi na kuleta mfumo wa 'uchumi
huria', tunahakikishaje kwamba maisha ya mwananchi wa kawaida yanakuwa
bora zaidi. Katika hili tusitegemee takwimu za ukusanyaji kodi na pato
la serikali zinasemaje, bali vijana wangapi wapo mashuleni na wanapata
elimu ya aina gani, zahanati ngapi zipo vijini na zinatowa huduma ya
aina ipi, asilimia ngapi ya wananchi wanapata maji safi, na maisha ya
mwananchi wa kawaida yanaendelea kuwa bora au yanazidi kudidimia. 


Uongozi ni Dhamana

Viongozi wa aina ya Mwalimu Nyerere huja kwa nadra, na waondokapo hupita
muda kabla hawajachomoza wengine wa aina yao. Katika karne iliyomalizika
hivi karibuni viongozi wa aina hiyo wanaweza kuhesabiwa kwa viganja
viwili tu vya mkono. Mfano ni Mahatma Ghandhi wa India na Mao Tse-tung
wa China. Watanzania kwa hivyo wasiwe na ndoto kwamba katika miaka ya
hivi karibuni tutampata kiongozi mwengine wa aina ya Mwalimu Nyerere. Cha
kuomba tu ni kwamba hao viongozi tutaowapata wawe angalau wanataka kumuiga
Mwalimu Nyerere kwa uadilifu, unyeyekevu, uzalendo, utu, kutotumia vibaya
madaraka, kujali watu, kutopenda fakhari na kuchukia rushwa.

Kwa bahati mbaya hatuna taratibu zinazojulikana na zilizo wazi na
sifa zinazotambulika za kupata viongozi wa aina yeyote ile na wa ngazi
yoyote. Sio katika vilabu vya michezo wala kwenye vyama vya siasa. Sura
inayojitokeza ni kwamba uongozi umekuwa ni njia tu ya ubabaishaji na
kujinufaisha tofauti na ilivyokuwa wakati wa kupigania uhuru. Inafikiriwa
tu kwamba viongozi watajitokeza na sio kwamba wataandaliwa, na kila
mmoja atatumia bahati yake na mbinu zake kujipatia uongozi. Na hata
baada ya kuchaguliwa hatuna vipimo tulivyojiwekea vya kujua ikiwa huyo
aliechaguliwa anatekeleza wajibu wake au anapoteza muda tu na kujinufaisha
binafsi. Ingefaa sasa tukafikiria upya juu ya suala zima la uongozi,
na kutilia mkazo kikweli kweli ule usemi kwamba 'uongozi ni dhamana'.

Pa kuanzia ni chaguzi zijazo za Rais wa Jamhuri, wabunge wa Muungano, Rais
wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani wa Zanzibar na
Tanzania Bara ambazo zitafanyika mwezi wa Oktoba mwaka huu. Pirikapirika
za shughuli hizo zimeshaanza kupamba moto. 

Tofauti na uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 1995, uchaguzi wa mwaka
huu itabidi wananchi wajishirikishe kikamilifu katika hatuwa zake
zote. Jukumu la kuwaelimisha wananchi katika elimu ya uraia na ya upigaji
kura isiwachiwe tu serikali, Tume ya uchaguzi ya Muungano na ya Zanzibar
au vyombo vyengine vya dola, bali vyama vya siasa, jumuiya za wananchi,
mashirika yasio ya kiserikali na vikundi mbali mbali lazima vichangie
kwa uwezo wao wote katika kuhakikisha jambo hili linafanikiwa. Na isiwe
tu kwamba wanalengwa watu wa mijini bali mkazo mkubwa utiliwe katika
kuwafikia wananchi vijijini na kwenye vitongoji. Lakini la umuhimu ni
kwamba serikali zote mbili itabidi ziandae mazingira mazuri ya kufanyika
chaguzi hizo.


Chaguzi za Zanzibar

Zanzibar ina historia ndefu ya uchaguzi kuliko Tanzania Bara. Uchaguzi wa
mwanzo kufanyika visiwani ulikua mwaka 1957 wakati Bara ilifanya uchaguzi
wake wa mwanzo mwaka 1959. Ushindani wa kisiasa visiwani umekuwa mkubwa;
na mbali ya uchaguzi wa mwaka 1957 ambapo ASP ilipata viti vitano
dhidi ya kimoja ilichopata Indian Muslim Association, katika chaguzi
za Januari na Juni mwaka 1961 na Julai mwaka 1963,  imekuwa kwamba
chama kinachoshinda huwa hakishindi kwa kura nyingi mno au viti vingi
sana. Wakati sikubaliani na wazo kwamba vyama vya sasa, yaani CCM na CUF,
ni vioo vya vyama vilivyopita, lakini matokeo ya uchaguzi uliopita wa
mwaka 1995 hayakutafautiana na yale ya  chaguzi za huko nyuma.

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu huko visiwani yatategemea mambo
yafuatayo. Kwanza, nani watakuwa wagombea wa kiti cha Urais. Wakati
inaelekea kwamba CUF watamueka tena Maalim Seif Shariff Hamad, mgombea wa
upande wa CCM atajulikana tu baada ya kikao cha mwezi huu cha Halmashauri
Kuu ya CCM. Lakini tayari inadhihirika kwamba kuna mgawanyiko ndani ya
uongozi wa CCM Zanzibar. Kushikilia huko nyuma kwamba Dk Salmin Amour
agombee tena kwa mara ya tatu kumeinyima CCM kumuandaa kiongozi ambae
angeonekana na wananchi kwamba ndie mrithi wake. Halafu wale wale ambao
mpaka hivi karibuni walikuwa wakisema kwamba 'hakuna mwengine isipokua
Dk Salmin Amour' kuonekana sasa kwamba kumbe walikuwa wakikinyemelea kiti
cha Rais, sio sifa nzuri ya kwenda kugombea kiti cha Urais. Lakini yeyote
atakaeteuliwa na CCM kugombea kiti cha Urais Zanzibar, chama hicho itabidi
kifanye kazi ya ziada kumtangaza vizuri mgombea wake mpaka akubalike na
kuweza kuchaguliwa. 

Ifahamike kwamba CUF Zanzibar inaingia katika uchaguzi wa mwaka huu
ikiwa imejizatiti na kuwa iko macho wazi. Vitimbi vinavyofanywa na
SMZ dhidi ya chama hicho badala ya kukidhoofisha, kwa hakika, tofauti
na inavyokusudiwa, inakipa nguvu, na kuonekana kwamba kinaogopwa,
kinanyanyaswa na kwa hivyo kuvutia hisia za kukionea huruma. Ulimwengu
wa kimataifa unaviona vitimbi hivyo dhidi ya CUF kuwa ni dalili za SMZ
kutokuwa na uvumilivu wa kisiasa, kuendesha mambo kimabavu na kuwa tayari
kwa lolote almuradi tu CCM inabaki madarakani. 

Kusema kweli katika mitazamo ya kisiasa na sera za kiuchumi, huwezi kuona
tofauti za kimsingi baina ya CCM Zanzibar na CUF Zanzibar. Tofauti ni
kwamba CUF inasema hadharani yale ambayo CCM Zanzibar inayasemea kwenye
faragha: mtafiti yeyote wa mambo ya siasa Zanzibar anajuwa kwamba uongozi
wa CCM Zanzibar na ule wa SMZ unapendelea mfumo wa serikali tatu. Mtu
yeyote mwenye kufuatilia mambo ya kisiasa na kijamii Zanzibar anafahamu
kwamba hakuna njia ambayo CUF, pindipo ikishika madaraka, itaweza ama
kurejesha usultani au kurejesha mali zilizotaifishwa. Kufanya hivyo ni
kuleta mtafaruku na kusababisha ghasia na vurugu. 

Tofauti na nchi nyengine ambapo huwepo na kiasi kikubwa cha wapiga
kura na huja kuamuwa dakika za mwisho juu ya nani wa kumpigia kura au
chama kipi kukitakia kitwae madaraka, kwa Zanzibar wapiga kura huwa
wameamuwa zamani sana. Labda ambao inawezekana kuwa bado hawajaamuwa ni
wale ambao mwaka huu ndio wanafikia umri wa kupiga kura. Kwa hivyo hata
ikiwa majimbo ya uchaguzi yatagawanywa upya, yatabadilishwa, kupunguzwa
au kuunganishwa, isitumainiwe kuwa jumla ya kura ambazo kila kimoja
kati ya vyama vikuu viwili itapata zitatafautiana sana. Inawezekana,
kwa mgawanyiko wa majimbo, chama kimoja kikashinda katika uchaguzi wa
Baraza la Wawakilishi na ule wa madiwani, na tusishangae ikiwa chama
cha pili kikashinda katika uchaguzi wa Urais. Mfano wa haya ni kura ya
maoni (refrendum) iliyofanyika hivi karibuni kule Zimbabwe: ukiangalia
kura zilivyopigwa kwenye majimbo ya uchaguzi, basi ingekuwa ule ni
uchaguzi wa kawaida ZANU-PF ingeshinda wingi wa viti; lakini kwa vile
kura zote zilichangywa ndio maana wale waliopinga mabadiliko ya katiba
walishinda. Kwa hivyo tusistaajabu ikiwa chama kimoja kikashinda wingi
wa viti na kwa hivyo kudhibiti Baraza la Wawakilishi; na chama kengine
kikapata wingi wa kura na kwa hivyo kupata kiti cha Urais. 

Nalipokuwa London hivi karibuni kwenye studio za idhaa ya Kiswahili ya
BBC, mtangazaji mmoja aliniuliza: nani mgombea wangu katika kiti cha
Urais Zanzibar? Nalimjibu, sina. Na kwa maskhara, nikamwambia: mgombea
wangu bado hajazaliwa! Lakini kusema kweli, mimi nimesikitishwa kwamba Dk
Omar Ali Juma hakuchukuwa fomu za kugombea kupitia CCM. Bila ya kuonekana
kwamba nnaleta ujimbo, lakini uchaguzi wa Zanzibar ambapo Dk Omar Ali
Juma anagombea dhidi ya Maalim Seif Shariff Hamad ungepunguza kwa kiasi
kikubwa uhasama na joto la kisiasa visiwani. Nalipowauliza wataalamu
wa vyombo vya dola kwa nini Dk Omar hakuchukuwa fomu, majibu naliyopewa
ni kwamba, kwanza wananchi wa Pemba wanamuona yeye kama ndie aliechochea
siasa za uhasama wakati akiwa Waziri Kiongozi; pili, kwamba wengi ndani ya
Halmashauri Maalumu ya CCM ya mambo ya Zanzibar hawamuungi mkono; tatu,
hakubaliki kwa Rais Dk Salmin Amour; na nne, kwamba utafiti uliofanywa
na idara ya usalama wa taifa unaonyesha hawezi kushinda.

Kwa yeyote ataeshinda katika uchaguzi wa kiti cha Urais Zanzibar na kwa
hivyo kupewa dhamana ya kuongoza visiwa hivyo mnamo miaka mitano ijayo,
ningemuomba akayazingatia yafuatayo: Jamii ya Zanzibar imegawanyika vibaya
mno. Bila ya kutaka kunyosheana vidole nani kasababisha hali hii, suala la
kwanza na muhimu ni kuleta umoja wa kitaifa na kumfanya kila Mzanzibari
kuhisi kwamba ni kwao na ana jukumu na wajibu kwa Zanzibar. Na hapa
sikusudii kwamba Mzanzibari ni yule tu mwenye asili ya Tumbatu, Makunduchi
au Kengeja. Hii itahitaji kampeni maalumu na ya makusudi ya kuielimisha
jamii ya Kizanzibari juu ya haja ya kuondosha uhasama na chuki, kufuta
hisia za kiujimbo na kikabila, kusahau yaliyopita na kushikamana katika
kutafuta mustakabali mzuri wa visiwa hivyo na Tanzania kwa ujumla. Pili,
utawala ataouunda Rais mpya uwe unajumuisha jamii nzima, kila kikundi
kihisi kwamba kimeshirikishwa na kuona kwamba kina hisa (stakeholder)
katika utawala wa nchi. Tatu, ateuwe kamati ambayo haitokuwa ya ushabiki
au ya upande mmoja ambayo baada ya kuzungumza na makundi mbali mbali
na wananchi kwa jumla, itaandaa rasimu ya katiba mpya na sheria mpya ya
uchaguzi, na pia kuangalia mfumo wa mahakama. Ikiwa kazi hii itafanyika
mapema, haitoonekana kwamba madhumuni yake ni kukipendelea chama hiki au
kile katika uchaguzi wa mwaka 2005. Nne, misingi imara ya demokrasia na
vyombo vya utawala bora vitiliwe mkazo na kuimarishwa.  Tano, apendekeze
kuangaliwa upya sera za kiuchumi na kijamii. Sita, awatumia kikamilifu
waatalamu waliopo Zanzibar bila ya kujali itikadi zao za kisiasa. Saba,
awavutie wataalamu, wafanyabiashara, wasomi na wenye rasilimali wa
Kizanzibari ambao wapo nje ya visiwa hivyo wasaidie katika maendeleo ya
nchi. Nna hakika ikiwa mikakati hii na mengine mizuri kama hii itafuatwa,
sura ya Zanzibar katika miaka mitano ijayo itabadilika sana. Vyenginevyo,
ikiwa atayetuongoza katika miaka mitano hii ifuatayo atazidi kupalilia
siasa za uhasama na chuki, kuendekeza malumbano yasio na msingi na
kuwabagua Wazanzibari kwa misingi ya kabila au jimbo atokalo mtu, basi
tusintegemee chochote isipokuwa kuzidi kurejea nyuma kimaendeleo, na
yale ya Rwanda, Kosovo na Sierra Leone hayatokuwa tena kwetu ni hadithi
za kusimuliwa.  


Chaguzi za Muungano 

Kwa yeyote mwenye kuangalia mwenendo wa kisiasa nchini katika miaka mitatu
iliyopita angeweza kuona kwamba vyama vya upinzani (isipokua CUF Zanzibar)
havingeweza kutoa ushindani mzito kama ule uliotowa katika uchaguzi wa
mwaka 1995. Juu ya hivyo, CCM haikuwa na hakika. Baadhi ya mabadiliko
ya katiba yaliofanyika mwaka jana (kama yakutaka mgombea wa kiti cha
Urais kutangazwa mshindi kwa kupata tu wingi wa kura na sio zaidi ya
asilimia hamsini) yalikua na lengo la kuiwezesha CCM kupata ushindi wa
rahisi. Uchaguzi uliopita mgombea wa CCM alipata asilimia 60 ya kura
wakati wagombea wa vyama vya upinzani kwa jumla walipata asilimia 40 ya
kura. Lakini tusisahau kwamba katika uchaguzi ule Mwalimu Nyerere alikuwa
ni 'mgombea'; na alifika sehemu zote za nchi, isipokuwa Zanzibar tu,
kumnadi mgombea wake. Tutake tusitake, kuna wananchi walimpigia kura Rais
Benjamin Mkapa kwa kuona tu kwamba anadhaminiwa na Mwalimu Nyerere.   

Kitu ambacho kinaweza kuleta sura ya ushindani mzuri ikiwa vyama vya
upinzani vitakubaliana kuweka mgombea mmoja wa kiti cha Urais wa Jamhuri
na hata kuweka mgombea mmoja katika kila jimbo la uchaguzi. Vyenginevyo
ni kuihakikishia CCM ushindi tena mkubwa kuliko ule wa mwaka 1995. 


Demokrasia Ndani ya Vyama

Namna ambavyo vyama vya siasa vinaendesha mambo yao na demokrasia iliyomo
ndani ya vyama hivyo ndivyo ambavyo vitaendesha nchi. Kwa chama ambacho
kiongozi wake anakiona kuwa ni mali yake basi apewapo uongozi wa kitaifa
ataiona nchi kuwa ni shamba lake binafsi na sisi sote ni vibaruwa
wake. Tusisahau pia kwamba madaraka hulevya; na hata kiongozi mzuri
wakati hayupo kwenye madaraka hufaa kuchungwa anapokuwa kwenye madaraka. 

Sijui vyama vya upinzani vitatumia utaratibu gani katika kuwateua
wagombea wake wa viti vya Rais wa Muungano na wa Zanzibar, vile vya
Baraza la Wawakilishi na Wabunge, na vile vya madiwani. Lakini dosari
imekwisha kujitokeza kwenye chama tawala cha CCM. Kwa yeyote mwenye
kufuatilia mambo ya kisiasa ilikuwa dhahiri kwamba CCM isingekuwa na
mgombea mwengine wa kiti cha Urais wa Jamhuri isipokuwa Mheshimiwa
Benjamin Mkapa. 'Vipigo' alivyopata Mheshimiwa John Malecela mwaka
1995 kutoka kwa Mwalimu Nyerere sidhani kwamba angefikiria kupendekeza
tena jina lake. Mheshimiwa Pius Msekwa, labda kwa kufuata lile tamko la
'Mwongozo wa TANU' kwamba 'kiongozi ni mtu alietosheka', inaonyesha kuwa
ametosheka na nafasi ya Spika na kufuatana na katiba ya Jamhuri, yeye
anakuwa ni watatu kwenye uongozi wa taifa na anakaimu nafasi ya Rais ikiwa
Rais na Makamu wa Rais wote hawapo nchini. Mheshimiwa Edward Lowassa na
Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kwa kujuwa bado ni vijana, inawezekana kwamba
labda wanasubiri mwaka 2005. Kwa kuzingatia haya haikuwa ni busara kwa
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana
wa CCM na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kutia vishindo na kutisha
kwamba hakuna mwengine ataechukuwa fomu ya kugombea kupitia CCM isipokuwa
Rais Mkapa tu wakati Rais Mkapa mwenyewe alikaribisha wana CCM wenziwe
wanaotaka kugombea wajitokeze. Hata hatuwa za jumuiya za CCM kumchangia
fedha za udhamini Rais Mkapa haikuwa sahihi. Ingetokea wanachama wengine
wakataka kugombea, jumuiya hizo nazo zingewachangia? Uamuzi wa kugombea
hufanywa na mtu mwenyewe binafsi; ni baada ya kudhibitishwa na vikao
vinavyohusika vya chama ndipo mgombea anakuwa ni mgombea wa chama. 


Mustakabali wa Tanzania 

Kwa jinsi siasa za nchi zinavyokwenda, CCM inaonyesha itashinda kiti
cha Urais wa Jamhuri. Huku sikuvikatisha tamaa vyama vya upinzani, bali
kama usemi unavyosema, mtu huvuna anachopanda. Wakati bado upo wasaa wa
vyama vya upinzani kuweka mgombea mmoja na kwa hivyo kutowa ushindani
mkubwa, vyenginevyo kwao safari ya Ikulu itaishia Chalinze. Kitu ambacho
wangetilia mkazo ni kupata viti vingi bungeni. Na hii inategemea pia
vipi vyama hivyo vitashirikiana.  

Kwa yeyote atakaeshinda kiti cha Urais wa Jamhuri, kuna mambo
matatu ningeomba akayafikiria. Kwanza, ni amani, utulivu na umoja
wa kitaifa. Hakuwezi kuwepo amani baina ya alieshiba na mwenye njaa;
hakutokuwa na utulivu baina ya watoto wa wachache wanaopata elimu nzuri
na wale wa wengi wanaoambulia patupu; hakutokuwa na mshikamano baina ya
wale wanaolindwa na polisi na kupata usingizi mzuri na wale wanaolala
madarini kwa kuwaogopa polisi. Vile vile ikiwa hakuna utulivu Zanzibar
tusifikirie kwamba kutakuwa na utulivu Tanzania. Pili, sera zetu za
kiuchumi na kijamii ingefaa zikangaliwa upya. 'Uchumi huria' haina maana
kujenga taifa la ombaomba na tegemezi. Katika taifa kama letu haina maana
kusema kwamba serikali inajitowa kwenye hili na lile na wajibu wake ni
ulinzi na usalama tu. Hakuna nchi iliyoendelea bila ya dola kusimamia
kikamilifu mwenendo wa uchumi, kuendeleza sera za kijamii na kulinda
maadili na utamaduni wake. Tatu, isiwe ni nyimbo tu kuwa hii ni 'karne
ya sayansi na teknolojia'. Mkazo mkubwa utiliwe katika kukuza elimu
kwenye viwango vyote; rasilmali nyingi ziwekwe kwenye sekta ya elimu;
na kila kijiji, mtaa na wilaya zihamasishwe kutilia mkazo elimu.  


Uongozi wa Baadae

Hapo juu nalielezea juu ya haja ya kuandaa viongozi na sio kubahatisha
tu. Nchi za wenzetu viongozi wake huandaliwa wakati bado wapo shuleni,
wakiwa kwenye vyuo vikuu na kupewa uzoefu aina mbali mbali kabla hawajawa
viongozi wa kitaifa. Hivi karibuni kulifanyika utafiti kule Uingereza
ambao umeonyesha kwamba vipaji vya kuongoza vinaweza kuonekana wakati
mtu yupo shule ya msingi na kilichopo ni kuvikuza tu vipaji hivyo. 

Kuna haja kwa sasa kuona uongozi wa aina mpya, mawazo mapya  na sura mpya
katika nyanja zote za taifa. Na hii ifanyike bila ya vurugu. Uzuri wa
uongozi ni kuandaa watu ambao watakuja kukurithi na taratibu za kufuatwa
katika kubadilishana uongozi. 

2 Juni 2000

Profesa Haroub Othman
Monrovia, Liberia