Author : Faraj
    Date: Wed, 14 Jun 2000
Subject: KIONGOZI KAZALIWA

Ndugu zangu Waislam
Assalaam aleikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

KIONGOZI KAZALIWA

Ulimwengu ulikuwa katika ukingo wa shimo la kuangamia. Watu wake
walikwishaipoteza dini yao, itikadi yao, uhuru, uadilifu, ukweli, amani.
Walipoteza kila sababu inayoweza kuwaletea tumaini katika mwelekeo wa
maisha yao ya siku zijazo, katika Mustakbali wao.
Watu wa Bara ya Arabu waliibadilisha ibada ya Mungu mmoja
waliyofundishwa na Nabii Ibrahim (AS) na badala yake wakawa wanayaabudu
masanamu waliyokuwa wakiyachonga wenyewe kwa mikono yao kisha wakawa
wanayaporomokea na kuyasujudia. Walikuwa wakiwauwa watoto wao wa kike
wangali bado wadogo, eti  kwa kuogopa aibu. Vita baina ya makabila yao
havimaliziki. Kwa muda wa miaka arubaini, na kwa ajili ya farasi tu,
makabila mawili makubwa yaliyokuwa yakiishi katika mji wa Madina,  Aus
na Khazraj, yalipigana vita vikali vilivyoangamiza maelfu ya watu.
Wahabeshi nao walifuata dini iliyogeuzwa na kubadilishwa waliyoipokea
kutoka kwa Waroma, na wakati huo huo walitaka kuwalazimisha Waarabu nao
pia waifuate dini yao hiyo na waache kwenda Makka kuizuru Al Kaaba.
Waliposhindwa, wakaamuwa kupeleka majeshi yao yakiongozwa na tembo
wakubwa ili kuibomoa nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kuuondoa udhia
huo?!.
Wafursi nao walikuwa wakiabudu moto,  na watu wao walikuwa
wakidhalilishwa na makuhani wao walinzi wa moto huo waliokuwa wakieneza
jeuri katika ardhi yao,  huku majeshi yao yakijaribu kuiteka Bara ya
Arabu yote na kuitia mikononi mwao. Vita baina yao na Waroma vilikuwa
haviishi.
Waroma nao baada ya kufanikiwa kuwashinda Wafursi, wakaingiwa na tamaa
na kuanza kusonga mbele na kuziteka nchi za kiarabu. Na kila walipoteka
nchi, walizidi kupata tamaa na kutaka kuiteka ile iliyo karibu nayo. Na
hali hii ndiyo iliyokuwa katika sehemu zote za ulimwengu.
Dhulma ilienea kila mahala, ulimwengu wa samaki, mkubwa kumla mdogo.
Ulimwengu ulikuwa katika hali mbaya na ya kutisha, ulikuwa katika hali
ambayo lazima mabadiliko yatokee au watu wake waangamie. Ulimwengu
ulikuwa ukimsubiri Kiongozi ambaye lazima atokee ili mabadiliko
yapatikane.
Anasema Abbas Al Aqqad katika kitabu chake 'Abqariyat Muhammad';
Ulimwengu ulikuwa ukimsubiri Mtume, na miji ilikuwa ikimsubiri Mtume,
Madina ilikuwa ikimsubiri Mtume na Makka ilikuwa ikimsubiri Mtume.
Na huyu hapa Mtume (SAW) keshazaliwa, Mtume aliyebeba kila sifa njema,
mwenye sifa za aina ya pekee asizokuwanazo mwengine yeyote yule. Mtume
mtukufu, muaminifu, muungwana, aliyebeba kila sifa ya ubinadamu mwenye
fadhila njema, ucha Mungu, moyo mkubwa na tabia njema ya hali ya juu
kabisa isiyoweza kufananishwa na yeyote yule katika Makka, Madina,
Mashariki ya Kati, bali ulimwengu mzima.
Alikuwa mtu anayefaa, kutoka katika nyumba inayofaa, na kabila linalofaa
aliyekuja katika wakati unaofaa".
Amemaliza kusema Al Aqqad.

Ingawaje pana khitilafu kubwa juu ya uhakika wa siku ya kuzaliwa kwake
(SAW). Kwani wapo wanaosema kuwa amezaliwa tarehe tisa Mfunguo sita, na
wengine wanaosema kuwa amezaliwa katika mwezi wa Ramadhani, na wengine
waliosema kuwa amezaliwa siku hii ya tarehe 12 Mwezi wa Mfunguo sita, na
pana kauli nyingi nyingine juu ya uhakika wa siku aliyozaliwa Mtume
(SAW).
Juu ya hitilafu hiyo, lakini wote wanakubaliana kuwa Mtume Muhammad
(SAW) alizaliwa siku ya Jumatatu Mwaka wa tembo (Mwaka ule Abraha
Mhabeshi alipokuja na tembo wake pamoja na majeshi yake kwa nia ya
kuibomoa Al Kaaba).
Hata Jaafar al Barzanji katika maulidi yake anasema;
"Wa kh-tulifa fiy yawmiha wa fiy shahriha wafiy aamiyha alaa kathiyrin
minal aqwali l marwiyya".
Na maana yake ni;
"Wamekhitalifiana katika siku yake(aliyozaliwa) na katika mwezi wake na
katika mwaka wake katika kauli nyingi zilizopokelewa".
Lakini juu ya yote hayo Al Habiyb (SAW) alizaliwa. Alizaliwa Makka
katika nyumba za Bani Hashim na kukabidhiwa Babu yake Abdul Muttalib
aliyembeba kwa furaha na kukimbia naye mpaka penye al Kaaba huku
akimbusu na kumshukuru Mola wake na kumuombea dua nzuri nzuri mtoto huyo
mchanga na kumpa jina la Muhammad, jina ambalo halikuwa likitumika sana
baina ya waarabu wakati huo.

SIFA ZAKE
Mtume (SAW) alikuwa mfasihi wa lugha, mwingi wa bashasha, mkweli,
muaminifu, mambo yaliyowafanya watu wote wampende, maadui zake na
marafiki zake.
Ufasaha wa lugha alokuwa nao haukuwa uhodari wa kuzungumza tu, bali
unajumuisha uhodari huo wa kuzungumza, ukweli, uchaguzi wa maneno na
jinsi ya kuyatamka pamoja kuyashadidisha maneno au kuyapunguzia sauti
pale inapopaswa, uhodari wa kuzitamka kila herufi kama zinavyotakikana
pamoja na haiba aliyokuwa nayo pale anapozungumza.
Alikuwa akisema;
"Mimi natoka katika kabila la Kikureshi na nimenyonya katika kabila la
Bani Saad".
Kabila la kibeduwi, kwa sababu waarabu wengi wenye uwezo walikuwa
wakiwapeleka watoto wao kunyonyeshwa na wanawake wa makabila ya kibeduwi
ili wapate kujifunza ufasaha wa lugha ya Kiarabu pamoja na ushujaa.
Bibi Aisha (RA) alikuwa akisema;
"Mtume (SAW) hakuwa akiyatamka maneno kwa haraka kama mnavyozungumza
nyinyi hivi, bali alikuwa akitamka maneno kwa kuyachambua na
kuyabainisha, jambo linalomfanya kila anayeyasikia aweze kuyahifadhi
maneno yake kwa urahisi".
Pamoja na ufasihi wake, alikuwa pia mpole sana anapozungumza, jambo
liliomfanya kila anayeishi naye ampende kwa moyo wake wote.
Zeid bin Haritha (RA) alikuwa akimilikiwa na bibi Khadija (RA), aliyempa
Mtume (SAW) kama zawadi na Mtume (SAW) akamuachia huru, lakini alipokuja
babake aliyepoteana naye kwa muda wa miaka mingi sana na kumtaka mwanawe
Zeid amfuate, Zeid (RA) alikataa na kuamua kubaki na Mtume (SAW) badala
ya kumfuata baba yake.

USHUJAA WAKE
Siku moja Omar (RA) alitoka akiwa anautikisa upanga wake huku akielekea
nyumbani kwa Mtume (SAW) ili amuuwe.  Juu ya kuwa Omar (RA) wakati huo
alikuwa akogopwa na watu kwa ukali wake na ushujaa wake, lakini
Mtume(SAW), alimtokea akamkabili na kumkunja kunja nguo zake pamoja na
ala ya panga yake huku akimwambia;
"Hivyo utangoja ewe Omar mpaka MwenyeziMungu akuteremshie Aya zikikulani
kama alivyoteremshiwa Al Walid bin Mughiyra? - Mola wangu huyu Omar bin
Khatab, Mwenyezi Mungu ipe nguvu dini kwa kumwingiza Omar katika dini
yako"
Omar(RA) pale pale akasilimu na kutamka;
"Ash- hadu an Laa ilaaha illa Llah wa ash - hadu annaka Rasulu llah".

Anasema Ali bin Abi Talib (RA);
"Vita vinapopamba moto, tulikuwa tukijificha nyuma ya mgongo wa Mtume
(SAW)".

REHMA KWA WALIMWENGU

NANI ATAKAYEKUOKOA?
Siku moja Mtume (SAW) alipokuwa amelala chini ya mti, akamtokea mbedui
aliyemtolea upanga na kumuelekezea nao huku akimwambia;
"Nani atakayekuokowa leo?"
Mtume (SAW) akamjibu kwa sauti kali iliyoingiza khofu ndani ya moyo wa
bedui huyo;
"ALLAAH".
Yule mbedui akastuka na kuutupa upanga wake chini, na Mtume (SAW)
akauokota na kumuelekezea nao yeye upanga wake huo, huku akimuuliza
suali lile lile;
"Nani atakayekuokoa wewe sasa?"
Yule mtu akajibu;
"Hapana wa kuniokoa".
Mtume (SAW) akamrudishia upanga wake na kumwambia;
"Nenda kwa wenzako ukawahadithie".

NYAMA ILIYOTIWA SUMU
Bibi mmoja wa Kiyahudi alimualika Mtume (SAW) chakula na kuijaza sumu
nyama ya mbavu, na hii ni kwa sababu alikuwa akijuwa kuwa Mtume (SAW)
alikuwa akiipenda sana sehemu hiyo ya nyama.
Alipokata kipande cha nyama na kukitia ndani ya kinywa chake kitukufu,
Mwenyezi Mungu akaijaalia nyama hiyo itamke na kusema;
"Usinile, kwa sababu mimi nimetiwa sumu".
Mtume (SAW) akainuka na kumwendea bibi huyo wa Kiyahudi na kumuuliza;
"Kitu gani kilichokufanya unitilie sumu?"
Bibi akasema;
"Nilitaka kuhakikisha, kama wewe ni muongo basi ungeila nyama ile na
kufa, na kama ni mkweli, basi Mola wako angekujulisha".
Bila shaka maneno hayo ni uongo mtupu, na Mtume (SAW) aliyajuwa hayo na
angeweza kuamrisha anavyotaka juu ya bibi yule, lakini hakufanya hivyo.

KIONGOZI WA WANAFIKI
Abdillahi bin Ubay bin Salul alikuwa mnafiki anayejulikana na kila mtu
kwa unafiki wake, na Mwenyezi Mungu alikwishateremsha aya nyingi
zikimkashifu mnafiki huyo.
Miongoni mwa unafiki wake ni ile kauli yake iliyotajwa katika Qurani
kuwa alisema;
"Wanasema; "Tukirudi Madina, Mwenye utukufu atamfukuza mnyonge" (yaani
hilo kubwa lao la unafiki linaloitwa Abdalla bin Ubay litamtoa Mtume)".
Al Munaafiqun - 8
Akimaanisha kuwa yeye Abdillahi mnafiki eti ndiye mtukufu, na kwamba
atamfukuza Mtume (SAW) ambaye eti ni mnyonge. Na hii ni kwa sababu yeye
ni mtu wa Madina na Mtume (SAW) ni mgeni pale Madina.
Si hivyo tu, bali alifika hadi kusema;
"Sammin kalbak yaakulak"
(Ukimnenepesha mbwa wako, mwisho atakuja kukula mwenyewe)
Akimaanisha kuwa watu wa Makka waliopokewa pale Madina na kukaribishwa
vizuri, sasa baada ya kupata nguvu wanataka kuwala (au kuwatawala) watu
wa Madina.
Si hivyo tu, bali alithubutu kumsingizia  uongo Bibi Aisha (RA)  mke wa
Mtume (SAW), mama wa Waislam. Na Mwenyezi Mungu akateremsha kutoka
mbinguni aya 20 katika Suratul Nur ili kumtakasa bibi huyo (RA) na
kuukanusha uongo huo.
Na mwisho wa aya hizo Mwenyezi Mungu akasema;
"Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirudi kabisa (msirejee tena) kufanya kama
haya, ikiwa nyinyi ni Waumini! (Waislamu) kweli.”
ANNUR–17
Juu ya yote hayo, siku aliyokufa Abdillahi bin Ubay, Mtume (SAW)
alisimama mbele ya jeneza lake ili amsalie, na Omar (RA) hakuweza
kustahamili, akasimama mbele ya safu na kujaribu kumsemesha Mtume (SAW)
ili asimsalie khabithi huyo.
Omar (RA) ambaye ni Kipenzi cha Arrahmani
Anayeogopwa na mashetani
Ambaye maneno yake yanakubaliana na Qurani
Akasimama mbele ya safu na kumwambia Mtume (SAW);
‘Unamsalia adui wa Mwenyezi Mungu?"
Akawa anamkumbusha kila ubaya alomtendea, huku Mtume(SAW) akitabasam, na
kumwambia;
‘Nipishe ewe Omar, mimi nimehiyarishwa na nikachaguwa, Mwenyezi Mungu
amenambia;
‘Ewe Mtume! Waombee msamaha (hao wanafiki) au usiwaombee; (yote sawa
sawa) Hata ukiwaombea msamaha mara sabini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe’
At Tawba –80
Na kama nikijuwa kuwa nikiongeza zaidi ya mara sabini atasamehewa, basi
ningeongeza".
Kisha akamsalia na akalifuata jeneza lake na akasimama kaburini pake.
Baadaye Mwenyezi Mungu akateremsha aya katika Suratul Tawba zikisema;
"Wala usimsalie kamwe mmoja wao yoyote yule akifa, wala usisimame
kaburini kwake (kumuombea dua). Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na
Mtume Wake, na wakafa na hali wenye kuvunja amri za Mwenyezi Mungu".
At Tawba - 84

Au siku ile walipoingia na kuuteka mji wa Makka baada ya kuwashinda
Makafiri, Mtume (SAW) aliwakusanya mateka wote.
Mateka hao ni wale watu wa Makka waliowatesa na kuwaadhibu Waislam hapo
mwanzo kabla ya Hijra, wakawauwa na kuwanyang'anya mali zao, na baada ya
kuhama wakawa wanawafuata huko huko Madina walikohamia na kuwapiga vita,
mara wakishirikiana na Mayahudi na mara nyingine na makabila mbali mbali
ya kibedui.
Juu ya yote hayo, Mtume (SAW) aliwakusanya wote hao mahali pamoja kisha
akawauliza;
"Nini mnadhani nitakutendeeni?"
Wakasema;
"Kheri (bila shaka utatutendea) ewe ndugu mwema na mwana wa ndugu
mwema".
Mtume (SAW) akawaambia;
"Nendeni makwenu, nyote mko huru".
Huyu ndiye Mtume wa Rehma aliyekuwa akifanya yote hayo kwa sababu
alikuwa kama alivyosema Mola wake;
"Wamaa arsalnaaka illa rahmatan lil - aalamin".
((Nasi hatukukutuma ila uwe REHEMA kwa walimwengu (wote))".
Al Anbiyaa - 107

Ameeleza Imam Bukhari na Imam Ahmed na wengi wengine kuwa Bibi Aisha
(RA) amesema;
"Hakupata Mtume (SAW) hata siku moja kunyanyua mkono wake na kumpiga
mtumishi, wala kumpiga mwanamke wala kumpiga yeyote yule au chochote
kile isipokuwa katika vita vya Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na
anapotakiwa achaguwe moja katika mambo mawili, basi siku zote huchaguwa
lililo jepesi, ikiwa si la dhambi. Na alikuwa akiikimbia dhambi mbali
kabisa. Na wala hakupata kujilipia kisasi kwa ajili ya nafisi yake ila
linapokuwa jambo la kupindukia mipaka katika kumuasi Mwenyezi Mungu, na
hapo hulipa kisasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu".

Kiongozi mwenye sifa zilizokamilika keshazaliwa. Amezaliwa wakati
ulimwengu ulikuwa ukimsubiri kwa hamu kubwa sana, kwa sababu ulikuwa
ukimuhitajia sana. Kiongozi aliyemiliki kila dalili zinazomfanya mtu
aweze kulibeba jukumu hilo. Kwa nini basi watu wasimfuate? Ikiwa alama
zote za Utume zimejikusanya katika dhati ya mtu mmoja huyu, katika
wakati ambao watu walikuwa wakimsubiri mtu aliyebeba sifa za aina hiyo,
kwa nini basi wamuache huyo na kumfuata mwengine?

Anasema Abbas Al Aqqad;
"Muhammad (SAW) ameumbwa kwa ajili ya kuwa Mtume, ama ikiwa si hivyo,
basi  kwa ajili gani amekuja akiwa amebeba sifa zote zile. Mtu mwenye
sifa kama hizi mnadhani amekuja kwa ajili ya kazi gani nyingine
isipokuwa hii?

JINSI YA KUSHEREHEKEA
Njia tunayoitumia katika kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume (SAW) siku hizi
haiendi sambamba na lengo alokuja nalo Al Habiyb (SAW).
Lengo alokuja nalo Mtume (SAW) ni kubwa sana na tukufu sana kuliko
kuisubiri siku ya Maulidi, tukakaa na kuisoma na kupiga vitari.
Waislam wanapaswa kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume wao katika maisha yao
yote, katika kujifunza Sira yake, Fiqhi yake, Khuluqa zake na kila
tulilojulishwa katika maisha yake na kuyafuata.
Kumpenda Mtume (SAW) ni kumfanya awe mfano wako mwema wa hali ya juu
katika maisha yako, kumpenda kuliko hata wazee wako na nafsi yako.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Bila shaka mnao mfano mwema (ruwaza njema) kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu
kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho na kumtaja
Mwenyezi Mungu sana".
Al Ahzab - 21
Na akasema;
"Sema; "Kama baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa
zenu na amali mlizochuma na biashara mnazoogopa kuharibikiwa na majumba
mnayoyapenda (ikiwa vitu hivi) ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi
Mungu na Mtume wake na kupigania dini yake basi ngojeni mpaka Mwenyezi
Mungu alete amri yake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu maasi".
At Tawba - 24

Katika kumpenda Mtume (SAW) pia ni kuwapenda Watu wa nyumba yake, wake
zake na wanawe pamoja na jamaa zake, na kuwapenda Masahaba zake wakarimu
(RA), kwani msingi wa utiifu na mapenzi unasema;
"Habiybu habiybiy habiybiy wa Aduwa habiybiy aduwwiy"
Na maana yake ni;
((Kipenzi cha mpenzi wangu naye pia kipenzi changu, na aduwi wa kipenzi
changu naye pia ni aduwi yangu)).
Kwa hivyo ndugu zangu Waislam, tuwafunze watoto wetu kumpenda Mtume
(SAW) na kuwapenda Ahli Bayti yake pamoja na Sahaba zake wakarimu (RA)
pamoja na kufuata njia zao walizopita.
Wallahu waliyyu Ttawfiyq
Wassalaam aleikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

MAKALA HAYA CHINI NILIKWISHATANGULIA KUYARUSHA SIKU ZA NYUMA

MUHAMMAD (SAW)

Sheikh Safiu Rahman AlMubarak Furi kutoka India aliandika kitabu
kiitwacho,  Al Rahiyq Al Makhtum (Kinywaji kizuri kilichofungwa na
kizibo), ambacho ni juu ya Sira (historia) ya Mtume (SAW). Kitabu hicho
kilishinda katika mashindano ya kuandika juu ya Sira ya Mtume (SAW).
Katika kukamilisha kitabu chake , mwisho kabisa, mwanachuoni huyu
aliandika juu ya baadhi ya Sifa na Tabia za Kipenzi chetu Al Habiyb
Muhammad (SAW) .
Mimi nitanukuu baadhi tu ya sifa zilizoandikwa ili tuzisome na kufaidika
nazo.
Anasema Mwanachuoni huyo ;
"Mtume (SAW) alikuwa akijulikana kwa ukamilifu wa umbile lake na
ukamilifu wa Tabia Zake na kwa ajili hiyo nyoyo zililia kwa utukufu wake
na zikamuandama kila aendapo. Masahaba wake walimpenda sana kutokana na
tabia zake njema, hata walikuwa tayari vichwa vyao vikatwe kwa ajili
yake.
Yote haya ni kutokana na Tabia zake njema zilizokamilika, ambazo
hajapata kupewa kiumbe chochote kingine,  pamoja na upole wake juu yao .

Al Bar- raa (RA) alisema;
'Mtume (SAW) alikuwa na uso mzuri na tabia nzuri kupita watu wote.'
Na alipoulizwa,  'Uso wake ulikuwa kama Upanga?'
Akajibu ;  Bali ulikuwa kama Mwezi
Bukhari

Bibi Al Rabia bint Muawadh (RA) alisema ;
'Unapomuona Mtume (SAW), kama umeliona Jua linapochomoza'.
Amma Jabir bin Samra (RA) amesema ;
'Nilimuona usiku wa mbaa mwezi , nikawa ninautizama mwezi kisha
ninamtizama Mtume (SAW), na alikuwa amevaa kitambaa chekundu,  alikuwa
mzuri kuliko mwezi'.
Attirmidhy

Amma Abu Huraira (RA) amesema ;
'Sikuona kitu kizuri kuliko Mtume (SAW), kama kwamba jua linatembea juu
ya uso wake, na sijapata kuona mtu anaekwenda kwa haraka kuliko Mtume
(SAW), kama




kwamba ardhi inajikunja chini yake, sisi tunajitahidi kukazana nyuma
yake lakini tunachoka, amma yeye anakwenda bila taabu yoyote.'
Attirmidhy

Na Kaab (RA) alisema ;
'Mtume (SAW) akifurahi , uso wake unang'aa mfano wa mwezi.'
Bukhari

Amma Umar (RA), anasema ;
'Anapoghadhibika uso wake unakuwa mwekundu kama kwamba chembe ya
komamanga imepasuliwa usoni pake'.
Attirmidhi

Ibni Abbas (RA) anasema ;
'Alikuwa ana mwanya, na alikuwa anaposema kama kwamba nuru inatoka penye
mwanya wake'.
AlDaarimiy

Jabir (RA) amesema ;
'Akipita njia, basi mtu yeyote atakayepita njia hiyo baada yake, atajua
kwamba Mtume (SAW) alipita hapo kutokana na harufu yake nzuri.'
AlDaarimiy

Baina ya mabega yake alikuwa na alama ya mhuri wa Utume, mfano wa yai la
njiwa. Na katika riwaya nyingine, ukubwa wake kama dengu.
Muslim

TABIA NJEMA
Ulimi wake ulikuwa wa fasaha na alikusanya kila aina ya misemo,
akizungumza misemo yote ya lugha za kiarabu.
Alikuwa Mpole na akisamehe hata kama anaweza kulipa kisasi, na alikuwa
na subira nyingi,  sifa alizopewa na Mola wake .
Kila mpole kwa kawaida huteleza baadhi ya wakati anapoudhiwa sana,
lakini Mtume (SAW) juu ya kuudhiwa, kudharauliwa na kufanyiwa kila aina
ya vitimbi na majahil, hakupata hata siku moja kughadhibika kwa ajili ya
nafsi yake.
Bibi Aisha (RA) anasema ;
"Anapotakiwa achaguwe moja katika mambo mawili, basi siku zote huchaguwa
lililo jepesi, ikiwa si la dhambi. Na alikuwa akiikimbia dhambi mbali
kabisa. Hakupata kulipa kisasi kwa ajili ya nafsi yake, isipokuwa hulipa
kisasi inapoondolewa heshima ya dini, kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Alikuwa hakasiriki upesi na mwepesi wa kuridhika na kusamehe.
Alikuwa mkarimu na alikuwa akitoa (sadaka), mfano wa mtu asiyeogopa
kufilisika.
Anasema Ibni Abbas (RA) ;
Alikuwa mkarimu sana na alikuwa mkarimu zaidi katika Mwezi wa Ramadhan
anapokutana na Jibril(AS), na Jibril hukutana naye kila usiku wa
Ramadhan, anamfundisha na kumsikiliza Qurani, na Mtume alikuwa akipenda
kuzidisha katika kufanya kheri siku hizo .

Amesema Jabir (RA) ;
'Hajapata kuombwa kitu akasema La. (hapana).'
Ushujaa wake ulikuwa wa hali ya juu kabisa, alikuwa akipanga na
kushiriki katika vita , alikuwa Imara, hatetereki katika mapambano .
Anasema Sayiduna Ali (RA) ;
"Vita vikipamba moto na mambo yakituzidi, tulikuwa tukijificha nyuma
yake (SAW), na yeye daima alikuwa yuko msitari wa mbele akipambana na
adui."
'Siku moja tulisikia sauti kali sana katika mji wa Madina', alisema Anas
(RA), ‘watu waliposhtuka na kwenda kuelekea palipotokea sauti hiyo,
wakamkuta Mtume (SAW) akiwa juu ya farasi, panga mkononi anarudi kutokea
penye sauti hiyo, akawaambia;
'Msiogope msiogope'.
Bukhari na Muslim

Alikuwa mwingi wa haya (SAW), na anapochukizwa na jambo hujulikana usoni
pake, na alikuwa hamshangalii mtu usoni, alikuwa akipenda kutizama chini
zaidi na kidogo mbinguni, na mtu anapotenda makosa hamtaji kwa jina lake
bali alikuwa akisema;
'Kwa nini baadhi ya watu wanafanya hivi au vile'
Alikuwa Msema kweli na Mwaminifu, hata maadui zake wanatambua hayo na
hivi ndivyo alivyokuwa akijulikana hata kabla ya Uislam.
Imepokelewa kutoka kwa Attirmidhy kuwa Sayiduna Ali (RA) alisema;
"Aba Jahal siku moja alimwambia Mtume (SAW);
'Sisi hatukukadhibishi wewe (tunajua kwamba husemi uwongo), lakini
tunakadhibisha hayo uliyokuja nayo.'
Ndipo Mwenyezi Mungu alipoteremsha kauli Yake;
"Basi wao hawakukadhibishi wewe, lakini madhalimu hao wanakanusha hoja
za Mwenyezi Mungu."
Al An-am  33
Abu Sufyan alipoulizwa na Herakul mfalme wa Warumi iwapo Muhammad huyu
(SAW), alikuwa akisema uwongo kabla ya kutamka anayotamka, alijibu;
'La hakuwa mwongo katu'.

Alikuwa hana kiburi abadan, na alikuwa hakubali kusimamiwa kama
wanavyosimamiwa wafalme, na alikuwa akiwatembelea maskini na akikaa na
mafakiri na alikuwa akikaa pamoja na Sahaba wake kama mmoja wao na
alikuwa akisaidia kazi za nyumbani na akipenda kujihudumia mwenyewe.
Siku moja alipokuwa katika safari zake, aliamrisha achinjwe mbuzi , mtu
mmoja akasema, 'Mimi juu yangu kumchinja', mwingine akasema , ' Mimi
nitamchuna ngozi', mwingine akasema, ' Juu yangu kumpika', Mtume (SAW)
akasema;
‘Juu yangu kukusanya kuni'.
Masahaba wakasema, 'Sisi tunakutosheleza ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu',
Mtume (SAW) akasema;
‘Ninajua kwamba mnanitosheleza, lakini sitaki niwe bora baina yenu , kwa
sababu Mwenyezi Mungu anachukizwa na mja wake anapofanywa kuwa ni bora
kuliko wenzake'.
Akainuka na kuanza kukusanya kuni.

Hind bin Abi Hala (RA) anasema ;
'Uso wa Mtume (SAW) daima ulikuwa na huzuni na daima alikuwa akifikiri,
hastarehe na hasema isipokuwa panapo haja, mkimya sana,  alikuwa
akiitukuza neema (chakula) hata ikiwa kidogo, hakitii ila chakula, wala
hakisifii na alikuwa anapoashiria haashirii kwa kidole, basi huashiria
kwa mkono wake wote.
Ulimi wake hautamki isipokuwa yanayomhusu, na alikuwa akiwapatanisha
Masahaba wake(RA) na hakuwa akiwafarikisha , akimheshimu mkuu wa kila
kabila na kuwatahadharisha juu ya kugombana.
Alikuwa hakai wala hasimami bila ya kumdhukuru Mwenyezi Mungu na hakuwa
akijihusishia (akijitengea) mahali maalum pa kukaa, bali hukaa popote,
na alikuwa akiamrisha hivyo , na akimpa kila anayekaa naye haki yake ya
kusema asihisi kwamba labda hathaminiwi.
Alikuwa mfano wa baba kwao, na majlis yake ilikuwa mahala pa kuoneana
huruma upole subira na amana, sauti hainyanyuliwi, akiheshimiwa mkubwa
na kuhurumiwa mdogo na mwenye shida.'
Ndiyo maana Mwenyezi Mungu katika kumsifia akasema ;
'Na bila shaka una tabia njema kabisa"
Nuun- 4