Author : Farouk Abdulla Amour
    Date: Thu, 29 Jun 2000
Subject: UHURU NA UMOJA/UMOJA NA UHURU


Sheikh Machano,

Assalaam Alaaykum,


UHURU NA UMOJA/UMOJA NA UHURU
Kwanza ni wajibu wangu kukushukuru kwa kunizinduwa, kuzinduwana ni wajibu 
wetu.  Ni ndivyo kabisa ya kwamba wazee wetu wakati wa kuwania Uhuru kutoka 
kwa Muingereza ilikua kauli yao ni “UHURU NA UMOJA”.  Ama maelezo yangu kwa 
mie kusema “UMOJA NA UHURU” badala ya “UHURU NA UMOJA” ni kufuatana na 
msingi ule ule wa lengo kuu la tangu kuasisiwa Umoja wa Zanzibari – Zanzibar 
Nationalist Party – (ZNP), au kama inavyojuulikana na wengi wetu – Hizbu, 
lengo lilojengeka katika nguzo mbili   muhimu nazo ni:

1. UHURU
2. UMOJA

Umoja wa Wazanzibari (Hizbu) umejengeka katika nguzo mbili hizi kwa imani 
yake kuwa matengenezo yote ya nchi yamefunganika na mawili haya, yaani bila 
ya Uhuru na Umoja hapana maendeleo yoyote yale.  Uhuru ni lazimiko la maisha 
kwa kutengeneza nchi, vile vile Umoja ni lazimiko la maisha katika 
kutengeneza nchi.  Mawili haya ni ya lazima kupatikana kwa matengenezo ya 
nchi, moja pekee haliwezi kusaidia katika matengenezo ya nchi.  Ni vidole 
viwili, kimoja hakivunji chawa.

UHURU MWANZO
Kama tunavyofahamu kuwa:  “politics is the art of possibility”.  Kutokana na 
hali hii ni busara kurekibisha tanga kufuatana na upepo, lakini sio 
kubadilisha safari na makusudio kwa kufuata upepo au kukimbia mawimbi.  
Unabadilisha mbinu kulingana na hali lakini hubadilishi makusudio kwa 
kisingizio cha hali.

Wakati wa kuwania Uhuru kutoka kwa mtawala wa Kiingereza ilitangulizwa Uhuru 
kwa imani ya kwamba Uhuru ndio ufunguo na nyenzo ya kuleta Umoja wa 
Wananchi.  Mkoloni alikuwa mbioni kuwagawa wananchi, kwa hivyo kuweza 
kujenga Umoja wa Wananchi ilikuwa ni muhimu na dharura kuung’oa utawala wa 
kikoloni. Utawala wa Kiingereza ulikuwa ni afadhali kuliko mtawala wa leo. 
Utawala wa Kiingereza ulikuwa una demokrasia, kulikuwa na magazeti nchini, 
aliruhurusu vyama vya siasa;  pia aliruhusu harakati za kuwania Uhuru ili 
kumtoa yeye mkoloni. Kutokana na hali hii ilidhihiri la mwanzo na la haraka 
ni kudai Uhuru na kumng’oa mtawala ili tuweze kujenga na kudumisha Umoja wa 
Wananchi. Kutekeleza hili ndio sauti zikawa UHURU NA UMOJA, imetangulizwa 
UHURU kwa umuhimu wake wakati ule.

UMOJA MWANZO
Baada ya kuvamiwa nchi yetu na kutiwa chini ya utawala wa mwalimu kwa 
kisingizio cha muungano ilidhihiri ya kwmba la mwanzo ni UMOJA.  Mtawala wa 
leo – mwalimu (unyerere) ni muovu zaidi kuliko mtawala wa jana – Muingereza. 
  Mtawala wa leo ni dikteta wa hali ya juu kabisa.  Mara tu baada ya 
kuivamia nchi yetu na kuitia chini ya utawala wake alivifunga vyama vyote 
vya siasa na jumuia zote zile nchi, ameyafunga magazeti na njia zote za 
utangazaji zikawa chini ya hukumu yake yeye mtawala.  Mtawala wa leo baada 
ya kuwauwa wananchi kadhaa wa kadhaa wakiwemo viongozi wa ASP aliamua 
kuifunga hata hii ASP, chama ambacho kimemsaidia kufikia katika utawala wake 
huu muovu. Baada ya kutenda hivi mtawala wa leo alizidishi mbinu zake za 
kuwagawa wananchi mafungu mafungu na kuwa mbioni kuwafarikisha kwa kila 
mbinu.  Kutokana na hali hii ilidhihiri kuwa la mwanzo na la haraka ni UMOJA 
WA WANANCHI, kwa hivyo basi, ndio tunaposema “UMOJA NA UHURU”, tunatanguliza 
UMOJA , kwa umuhimu wake hii leo.  Haya ni kwa imani yetu sote ya kwamba 
bila ya Umoja wa Wananci hatutoweza maisha kumng’oa huyu mtawala  dikteta. 
Nyenzo pekee ya kumng’oa mtawala dikteta ni  Umoja wa Wananchi.  Hakuna 
nguvu yoyote ile itakayoweza kumng’oa mtawala dikteta isipokuwa Umoja wa 
Wananchi.  Bila ya Umoja wa Wananchi tutaendelea kufarikishwa baina yetu na 
tutaendelea kutawaliwa kwa hivyo la mwanzo la dharura ni Umoja wa Wananchi.

HIZBU INGALIPO
Ni ndivyo iwapo nitajiuliza mbona kila mara ninataja Hizbu (ZNP), kwani hii 
sio imepigwa marufuku na haipo tena?  Nikijijibu suala hili nitasema kuwa 
laa, Hizbu ipo wala hapigiki marufuku wala haifutiki.  Hivi ni kwa sababu 
Hizbu sio mtu wala watu, wala chama;  Hizbu ni fikra, fikra za kizalendo.  
Hizbu ni mimi, hizbu ni wewe na yeye na yule, sote sisi ndio Hizbu.  
Kutokana na hali hii ndio ilivyo ya kuwa Hizbu haitokufa milele, na kama 
wanavyosema wazee ya kwamba hata akibakia Muhizbu mmoja tu basi Inshallah 
Zanzibar  itatengenea – Amin.

TUWACHE MFARAKANO
Wazanzibari leo kilio chetu ni kimoja tu nacho ni UMOJA WA WAZANZIBARI, 
kutokana na hili ndipo tunapowataka nduguzetu walioko katika uwongozi waache 
kuleta sababu za mfarakano na tujenge Umoja baina yetu kwa maslaha ya nchi 
yetu na vizazi vyetu.  Adui mkubwa wa Zanzibar leo sio matawala mambo leo, 
adui mkubwa wa Zanzibar ni yeyote yule mwenye kushirikiana na matawala 
kuleta na kukuza mfarakano baina ya Wazanzibari.  Yeyote yule mwenye 
kusaidia kuleta mfarakano basi huyo ndio muovu mkuu wa Zanzibar na ni wajibu 
wa Wazanzibari kumuepuka na kuwa mbali nae  kwani huyo ni muovu menye 
kupanda uovu.  Ni wajibu wa Wazanzibari hivi sasa tukikabiliwa na uchaguzi 
wa kuchaguwa Wawakilishi na Raisi,  ni wajibu tuhakikishe kuwa mabwana 
tutakao  wachaguwa ni hakika wataleta Umoja wa Wazanzibari, kama tunashaka 
juu ya hili basi bwana huyo hatufai, tusibahatishe; lakini ni lazima  
tuhakikishe kuwa bwana tunaemchaguwa ataleta Umoja wa Wazanzibari.  Katika 
kuchaguwa hakuna kubahatisha kuna hakika, kwa sababu kura ndio nyenzo pekee 
ya kutufikisha kwenye matarajio yet, kwa hivyo  ni wajibu tuwe na hakika 
kuwa kura zetu tunawapa mabwana wenye uwezo wa kutufikisha kwenye mahitajio 
yetu.  Mahitajio ya Mzanzibari leo ni moja nalo ni Umoja wa Wananchi.  
Tafadhali tuwe na hakika – majuto mjukuu.

Vile vile tunapopima kuchaguwa tuhakikishe kuwa tunaemchaguwa anamjuwa 
Mwenyezi Mungu Mtuukufu, anaujua mlango wa msikiti.  Kumjuwa Mwenyezi Mungu 
ndio kipimio kikubwa cha mwenye kufaa kubebeshwa dhamana ya uwongozi.  Bila 
ya kumjua na kumcha Mwenyezi Mungu basi kitu gani kitamzuia bwana baada ya 
kupewe uwezo kutenda vile anavyopenda, hakipo hata kimoja.  Kizuizi pekee ni 
imani, sio nguvu zozote zile,  bila ya imani hakuna kutekeleza majukumu ya 
uwongozi.  Kutokana na hali hii ndio maana mabwana waovu wanapotwambia kuwa 
tusichanganye siasa  na dini,  yaani dini ndio imani, na bila ya imani ni 
kuwa bila ya  kizuizi cha kukulinda kutenda khiana na kuvunja amana na 
ahadi. Kwa hivyo wanavyotaka wao ni kuwa hatuna imani ili tusitekeleza 
amana.  Tukimchaguwa bwana asiemjua Mwenyezi Mungu na kumpa amana basi sisi 
ndio wakosa na hesabu ni juu ya shingo zetu.  Sisi tuna dhamana na amana ya 
vizazi vyetu, kwa hio ni lazima tutekeleza amana hii kwa kumuwakilisha bwana 
muaminifu kutekeleza  kwa niaba yetu wajibu wa dhamana tulizochukua sote 
sisi.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtuukfu atujaalie uwezo wakuchaguwa waongozi wema 
ambao wataweza kutekeleza amana kwa niaba yetu – Amin.

Wa Billah Tawfiq

Farouk