Author :
Hashil Seif Hashil
Date:
22 May 2000
Subject:
NDEGE AMERUKA MOYONI NAMKUMBUKA
Ndugu zangu Wazanzibari, 22.05.2000
Nimeona nikuleteeni shairi la kutuliza mawazo kidogo:
NDEGE AMERUKA MOYONI NAMKUMBUKA
Ndege waajabu, miujiza amepewa
Mbawa za dhahabu, umbo alotunukiwa
Kula kwake tabu, hakuna asomjua
Ndege ameruka, moyoni namkumbuka.
Usingizi tabu, mwenzenu ninaunguwa
Nakwenda nikihisabu, nimwehu nimeshakuwa
Nachekwa kwenye vilabu, kuwa nimepungukiwa
Ndege ameruka, moyoni namkumbuka.
Mawazo ghadhabu, upweke waniraruwa
Nyimbo za hijabu, nakumbuka zaniuwa
Jina la ndege kitabu, namuita ametuwa
Ndege ameruka, moyoni namkumbuka.
Mahonda hadi Bububu, waganga kuniaguwa
Nimekonda kama mbu, jendaeka nimekuwa
Hakuna nisojaribu, kujua alikotuwa
Ndege ameruka, moyoni namkumbuka.
Nikiumwa hunitibu, pasi na dawa kupewa
Maneno yake ya Bubu, akinena nimepowa
Mkimkwaa sahibu, milioni nitatowa.
MWISHO
wakatabahu
Hashil S. Hashil