Author : Faraj
    Date: Tue, 30 May 2000
Subject: SALA NDANI YA MISIKITI YENYE MAKABURI

Ndugu zangu Waislam
Assalaam aleikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
Mmoja katika ndugu zetu ameniuliza masuali matatu ambayo itakuwa vizuri
ikiwa nitayajibu mbele yetu sote ili tufaidike na masuali hayo pamoja na
majibu yake, hasa kwa vile baadhi ya masuali yake yanaingiliana na
maudhui yanayozungumziwa humu siku mbili hizi.
Kwanza kabisa ndugu yetu huyu alitaka kujuwa nini hukmu ya kusali ndani
ya msikiti wa Mtume (SAW) uliopo Madina kwani anavyojuwa yeye ni kuwa
mna kaburi ndani yake.
Jawabu;
Kwanza kabisa ningependa kusahihisha baadhi ya kauli zilizotolewa humu
na ndugu zetu, nikianzia na hoja kuwa Hagara na baadhi ya Mitume (AS)
wamezikwa ndani ya msikiti wa Makka, na kwamba maneno hayo yameandikwa
katika vitabu vya historia.
Bila shaka yoyote mwenye hoja hii anaelewa wazi kabisa kuwa waandishi wa
historia hawajiwekei masharti ya usahihi wa hadithi wanazoziandika, na
pia hawazifanyii tahakiki hadithi hizo wala hawaufanyii tahakiki
mlolongo wa wapokezi wa hadithi hizo (narrators), kwani wao hukusanya tu
habari na kuziandika.
Ama vitabu vilivyo sahihi,vile ambavyo waandishi wake wanajiwekea
masharti ya kuandika hadithi sahihi tu baada ya kuzifanyia tahakiki
hadithi hizo kabla ya kuziandika, hapana hata kitabu kimoja katika
vitabu hivyo kilichoandika juu ya jambo hilo.
Katika kitabu cha Al Jamia al Sagheer mwandishi wake Al Manari anasema;
"Hakuna hata kaburi moja kati ya makaburi ya Mitume yaliyo na uhakika
kuwa wamezikwa hapo isipokuwa kaburi la Mtume Muhammad (SAW) peke yake.
Ama yale makaburi yanayonasibishwa na Nabii Musa na Nabii Ibrahim (AS)
ni dhanna tu, na wala hapana uhakika juu yake".
Kwa hivyo kauli hizo haziwezi kuchukuliwa kuwa ni hoja, hasa katika
mambo yanayohusu itikadi za dini.

Ama kuhusu kauli kuwa katika kisa cha As-habul Kahaf, baada ya kufa kwao
kuwa palisemwa; ‘Watawajengea msikiti’, hiyo pia si hoja, kwa sababu
katika aya hiyo hiyo imeandikwa kuwa; wenzao walisema;
"Jengeni jengo juu yao (wasipate kupita watu kuja kuwachungulia) MOLA
WAO ANAWAJUA VYEMA (Basi inatosha)"
Wakasema wale walioshinda;
"Bila shaka sisi tutajenga msikiti juu yao" (yaani katika pango)"
Atakayezichunguza kauli hizi ataona kuwa wale waliotaka wajengewe jengo,
ndio waliotoa hoja ya UchaMungu kuliko hao walioshinda, na Mwenyezi
Mungu hakueleza lolote katika hali zote mbili, na maneno haya ndiyo
yanayokubaliwa na maulamaa wengi, wa zamani na wa sasa, akiwemo Sheikh
Abdullah Saleh Farsi (Mwenyezi Mungu awarehemu).
Isitoshe, hata ikiwa tutakubali kwa ajili ya mjadala tu, basi kauli hiyo
pia haileti maana yoyote ya kututaka sisi tufuate mwenendo wao huo,
kwani Mwenyezi Mungu ametuletea Mtume wetu (SAW) na akatufundisha
mwenendo wake, na miongoni mwa aliyotufundisha ni kauli yake Subhanahu
wa Taala katika hiyo Suratul Maidah, Sura ambayo ni ya mwisho
kuteremshwa, kauli  isemayo;
“Likullin ja-alna minkum shir-atan wa minhaaja)
"Na kila (Umma) katika nyinyi (binadamu) tumeujaalia sheria yake na njia
yake".
Al Maidah - 48
Kwa hivyo wao walikuwa na sheria zao na njia zao, na sisi tuna sheria
zetu na njia zetu. Kama vile wao walivyokuwa wakiruhusiwa kumsujudia
kiumbe mwenzao (Soma Surat Yusuf) na waliharamishiwa kula baadhi ya
nyama na shahamu, wakati sisi tumeruhusiwa kula vyakula hivyo na
tumeharamishiwa kumsujudia yeyote mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Na kwa vile Sura hii ya Al Maidah inajulikana kuwa ni Sura ya mwisho
kuteremshwa, kwa ajili hiyo kila kilichoandikwa ndani yake kinahesabiwa
kuwa ni hukmu ya mwisho kabisa.

Tukirudia katika maudhui yetu ya Kaburi la Mtume (SAW), nilikwishanukuu
hapo mwanzo kauli mbali mbali za maulamaa zinazotofautisha hali baina ya
kaburi la Mtume (SAW) na yale makaburi wanayozikwa watu ndani ya
misikiti au kujengewa juu yake misikiti.
Ndugu zangu Waislam, hadithi sahihi ziko nyingi sana na zinaeleza kwa
uwazi kabisa kuhusu maudhui yetu haya;

Kutoka kwa bibi Aisha (RA) kuwa Ummu Habiba na Ummu Salama (RA)
walimhadithia juu ya kanisa waliloliona walipokuwa katika nchi ya
uhabeshi, ndani yake mna picha nyingi, na bibi Aisha (RA) akamhadithia
Mtume (SAW), na Mtume (SAW) akamwambia;
"Watu wale anapokuwa nao mtu mwema baina yao, basi anapokufa mtu huyo
wanajenga juu ya kaburi lake msikiti (mahala pa ibada), kisha wanachora
juu yake picha hizo, hao ni watu wabaya kabisa kwa Mwenyezi Mungu".
Bukhari na Muslim

Hadithi nyingine;
Mtume (SAW) amesema;
"Ghadhabu ya Mwenyezi Mungu imekuwa kali sana juu ya watu wanaoyageuza
makaburi ya Mitume yao na watu wema wao kuwa misikiti".
Bukhari na Muslim

Na akasema;
"Mola wangu usilijaalie kaburi langu likawa sanamu linaloabudiwa".
Muslim
Na akasema;
"Msisali kuyaelekea makaburi wala msikae juu yake.”
Muslim

Na akasema
"Mwenyezi Mungu amewalani Mayahudi na Manasara wamegeuza makaburi ya
Mitume yao kuwa misikiti".
Imepokelewa na Maimamu wa Sunnah wote

Imesimuliwa na Abdul Razak katika Musanaf yake kuwa;
"KAULI YA MWISHO KABISA ALIYOITAMKA MTUME (SAW) kabla ya kuirudisha roho
yake iliyotahirika kwa Mola wake aliyeiumba, alisema;
"Mwenyezi Mungu awaangamize Mayahudi na Manasara, wameyageuza makaburi
ya Mitume yao kuwa mahali pa ibada, pasibaki na dini mbili katika bara
ya Arabuni".
Hadithi hii pia imo katika Muwata-a ya Imam Malik

Hadithi katika maudhui haya ziko nyingi sana, na tukiendelea kuzitaja
tunaweza kujaza kurasa nyingi, isipokuwa ningependa kuongezea jambo
moja, nalo ni kuwa, Imam Annawawiy amezielezea hadithi hizi katika
kitabu cha Adhkar katika mlango wa kutujulisha juu ya watu wanaostahiki
kulaaniwa, akawataja hawa wanaotenda mambo haya kuwa ni miongoni mwa
watu hao wanaostahiki kulaaniwa.
Kwa hivyo ni bora mtu ayakimbie mambo kama haya yenye kutatanisha
(kubabaisha) na kufuata yale tu yaliyo dahiri na wazi, yale
yanayomkaribisha kiumbe na radhi za Mola wake mbali kabisa na matendo
yanayoweza kumuingiza katika hatari ya kupata laana za Mola wake.

Kutokana na hadithi zote hizi, maulamaa wetu wakatuambia kuwa ni haramu
kusali ndani ya misikiti iliyo na makaburi ndani yake, yote haya kwa
ajili ya kuogopa laana za Mwenyezi Mungu zisije zikatusibu kama
zilivyowasibu Mayahudi na Manasra kwa ajili ya kuyageuza makaburi ya
Mitume yao kuwa ni mahali pa ibada.
Maulamaa wanasema kuwa waliotangulia walikuwa wakiyajengea makaburi hayo
kwa nia njema ya kutaka kuwaigiza watu wema hao katika juhudi zao za
kufanya ibada, lakini baada ya kupita miaka mingi wakaja vizazi
wasiotambua kusudi la kujengewa huko, shetani akaanza kuwatia wasiwasi
wake na kuwaambia kuwa wazee wao na babu zao walikuwa wakiwaabudu watu
wema hao, kisha na wao wakawaabudu.. Na hii ndiyo sababu  Mtume (SA)
akatukataza kufanya hivyo ili kuufunga mlango wa fitina tokea mwanzo
wake.

Tuchukuwe mfano wa kaburi la Mtume wetu (SAW). Mtume (SAW) alipokuwa
yuhai alitufundisha kuwa isifungwe safari ndefu kwa ajili ya ibada
isipokuwa iwe safari ya kwenda katika misikiti mitatu. Akasema;
“Isifungwe safari ndefu (kwa ajili ya ibada) isipokuwa kwenda katika
misikiti mitatu; AlMasjidul Haraam(Makka), na Msikiti wangu huu(Madina),
na Msikiti wa Ilyaa(Baytul Maqdis).”
Bukhari – Muslim – Attirmidhy na wengineo
Na Akasema;
“Sala katika msikiti wangu ni bora kuliko sala elfu katika misikiti
mingine, na Sala katika Msikiti wa Makka (Masjidul Haraam) ni bora mara
elfu mia kuliko misikiti mingine.”
Imam Ahmed bin Hanbal
Baada ya kufa kwake (SAW) na kaburi lake kuingia ndani ya msikiti kwa
sababu tulokwishazitaja, baadhi ya watu wakawa hawasemi tena kuwa
wanakwenda kuuzuru msikiti wa Mtume (SAW) wanapokwenda Madina, bali
husema kuwa wanakwenda lizuru kaburi la Mtume (SAW), hata wakabadilisha
zile hadithi zinazosema :
"Baina ya nyumba yangu na membari yangu bustani katika bustani za
Peponi", na wakawa wanasema;
"Baina ya kaburi langu na membari yangu bustani katika bustani za
Peponi"


Ama kuhusu kaburi la Mtume kuwepo ndani ya msikiti, hali yake
inakhitililafiana kabisa na maudhui haya, kwa sababu kwanza msikiti huo
haukujengwa juu ya kaburi hilo, wala Mtume (SAW) hakuzikwa ndani ya
msikiti, isipokuwa katika upanuzi wa msikiti wakati wa utawala wa Bani
Umayya, kwa vile Mtume (SAW) alizikwa ndani ya nyumba yake iliyokuwa
imegandana na msikiti, ikabidi kaburi hilo liwe ndani yake, na maulamaa
wakafanya jitihada na kuweza kuuzungushia ukuta na kuutenga mbali na
watu wanaosali pamoja na kuweka ulinzi mkali sana ili mtu asije akafanya
yale yasiyotakikana..
Haya ndiyo waliyoweza kufanya, pamoja na kujenga viti vya saruji upande
wa kaburi unaoelekea kibla mahali ambapo watu wangesimama kwa ajili ya
kusali, na kwa ajili hiyo haiwezekani mtu kusimama na kusali hapo, na
wanaweza kukaa tu na kumsalia Mtume (SAW) pamoja na kumuombea dua.
Kwa ajili hii hukmu yake inakhitilafiana na hukmu za wale waliozikwa
ndani ya msikiti au waliojengewa msikiti juu ya kaburi lao kwa sababu ya
kuwaadhimisha.

Amma suali la pili la ndugu yetu huyu aliuliza hivi;;
"Na naomba unipe hukmu ya mwanamke anayesali akavisitiri viungo vyake
vote hata vile alivyotakiwa avidhihirishe kama viganja vya mikono, ikawa

anasali viganja vimefichika chini ya shaungi au nguo aliyojitanda".
Jawabu;
Haina neno, isipokuwa la muhimu ni kuwacha wazi sehemu ya uso na pua
yake kwa ajili ya kusujudu

Ama suali lake la mwisho ni hili;
"Naomba pia unipe maelezo ya mtu anayetia udhu hali ya kuwa yuko uchi
jee
udhu wake unasihi?"
Jawabu;
"Naam unasihi, na mtu anaweza kutia udhu wake baada ya kuoga hata kabla
ya kuvaa nguo zake isipokuwa ajiepushe na kugusa utupu wake kwa sehemu
ya ndani ya viganja vya mikono yake na kwa matumbo ya vidole vyake"

Wallahu Taala aalam
Wassalaam aleikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
Ndugu yenu
Muhammad Faraj Salem