Author :Abdulrahman A. Mohamed
    Date: Wed, 24 Nov 1999
Subject: SUALA LA NANI MZANZIBAR
_____________________________________________________
     
Asslam alaykum,

Ubaguzi ama wa rangi, dini, kabila au hata jinsia (Gender) ni tatizo kubwa katika sehemu nyingi ulimwenguni. Tatizo hili huanza taratibu kwa kupandikiza mbegu fulani katika jamii na baadae huota mizizi isiyon'goleka.

Kubagua kundi moja kutokana na kundi jengine ndani ya jamii moja ni dhambi isiyovumilika hata kidogo kwa vile inapoachwa kuendelea madhara yake ni makubwa mno mfano mzuri ni mauaji ya Burundi na Rwanda mwaka 1994

Kuzungumzia nani Mzanzibari si jambo baya ikiwa lengo lake ni kuweka historia juu ya jamii unavyobadilika kulingana na wakati lakini inapofika mahali ikawa kwamba lengo ni kueleza kwamba kundi fulani ndio lina haki kwa vile ndio asilia na fulani halina kwa vile sio asili hapo itakuwa mzungumzaji halengi kuelimisha bali kujenga chuki baina yetu. Mzanzibari ni Mzanzibari iwe asili ni Ngazija, Tumbatu, India, Somali, Oman au Tanganyika.

Tunalazimika kuondokana na mawazo kwamba kundi moja ni bora zaidi au lina haki zaidi ya kundi jengine kwa namna yoyote ile ndipo tutaweza kuondokana na ubaguzi wa rangi, kabila, dini au jinsia (Gender)

Tusighadhibike sana anapotokea mbaguzi na kuandika mawazo yake, kwani naye ana haki sawa na wengine katika kutoa mawazo (Freedom of Expression) ila tunawajibika kumjibu tena kwa kutumia diplomasia ya hali ya juu, kwani ikiwa anaeleta ubaguzi ni mwenye akili timamu basi huenda ataelemika kwa njia hiyo.

Tunapoghadhibika na kuanza kumshambulia mwandishi badala ya kujibu maandishi hapo ndipo nidhamu ya kielimu (Academic discipline) inapotea na hivyo kupoteza dhana nzima ya kuelimishana.

Uislamu ndio njia bora ya kuondokana na haya kwa vile umepiga vita wazi wazi mambo yote yanayopelekea kwenye ubaguzi. M/Mungu mwenyewe anatueleza sababu ya msingi ya kuwatofautisha wanadamu kimaumbile na ni yupi ni mbora mbele yake katika Qur-an kama ifuatavyo :-

"Enyi watu! Hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanamme (mmoja, Adam) na mwanamke (mmoja, Hawa). Na tukakufanyeni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika anaeheshimiwa sana miongoni mwenu mbele ya M/Mungu ni yule amchae M/Mungu zaidi . Kwa hakika M/Mungu ni mjuzi na mwenye habari" (49.13)

Kwa hiyo kupoteza muda kujadili ni nani Mzanzibari hasa au asilia au mwenye haki fulani kuliko mwingine ni jambo ambalo kimsingi halina faida yoyote kwa Wananeti na Wazanzibari wote kwa ujumla.

Ewe Mola wetu tupe uwezo wa kuchambua kiyakinifu. Amin.

 

Maintained by rai@ee.bilkent.edu.tr