Waraka Kutoka Unguja

August 11, 2005

By

Jabir Idrissa





Wanakumbi wenzangu, huu ni waraka mpya uliotoka Rai toleo la Agosti 11. Kwa wale walio mbali na gazeti hili, nufaikeni nanyi.

Ahsanteni.

jabir+

Headline:Mwalimu Nyerere, bado Rais atoke CCM tu?

Moja ya masuala muhimu ya kinchi aliyoyazungumzia Rais Benjamin Mkapa katika hotuba yake ya kufunga Bunge Julai 29, ni tatizo la rushwa. Alieleza mengi ya kuonyesha hatua thabiti alizozichochea katika serikali yake katika kupambana na tatizo hilo.

 

Maelezo yake yalitanguliwa na maneno mazito: mojawapo ya mambo niliyosema nitayavalia njuga nilipoingia madarakani ni vita dhidi ya rushwa. Yapo mengine mengi, lakini wapo wanaotaka uongozi wangu utathminiwe kwa kigezo kimoja tu cha rushwa, wakidhani sikutimiza ahadi yangu. Si kweli. Rushwa bado ipo, kama ilivyo katika nchi zote duniani kwa viwango tofauti, lakini katika miaka 10 iliyopita tumefanya kazi kubwa sana kupambana nayo.

 

Kutoka hapo, Rais anataja hatua yake ya kuunda tume ya kuchunguza mianya ya rushwa iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ambayo matokeo yake, anasema, ni kufanyika mabadiliko katika sera, miundo ya taasisi na sheria ili kuziba mianya ya rushwa. Amezitaja sheria sita zilizotungwa katika azma hiyo zikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi Nam. 5 na Sheria ya Ununuzi wa Vifaa vya Serikali Nam.3 zote za 2001.

 

Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) mara 600 kutoka sh milioni 15 za mwaka 1996/97 mpaka sh bilioni 9 mwaka 2004/05. Idadi ya watumishi pia imeongezwa wakiwapo 700 kutoka 185. Taasisi ina waendesha mashitaka na wapelelezi na imefungua ofisi zake katika Mikoa yote na Wilaya 93 Tanzania Bara kusogeza huduma karibu na wananchi.

 

Kwa hiyo tumeongeza bajeti, tumepanua mtandao na tumeongeza uwezo wa utendaji, yaani upelelezi, kuendesha mashitaka, kuhamasisha jamii na kutoa ushauri kwa Serikali. Juhudi hizo za Serikali zimewezesha kuchukuliwa hatua mbalimbali kwa waliojihusisha na vitendo vya rushwa.

 

Ameendelea akisema watumishi 456 wa umma walionywa au kukaripiwa kwa barua, 362 walisimamishwa kazi, 403 walifukuzwa au kustaafishwa kazi kwa manufaa ya umma na 138 walifikishwa vyombo vya dola. Kuanzia mwaka 1995 mpaka 2004, tuhuma 11,434 ziliripotiwa TAKURU, kati yake, 9,891 zilichunguzwa. Tuhuma 975 zilipelekwa mamlaka husika ili zichukue hatua, kesi 367 za rushwa zilifunguliwa mahakamani na 174 zimeamuliwa. Kwa kuwa mapambano ya rushwa si ya Serikali pekee, TAKURU imeanzisha na kukuza ushirikiano na zaidi ya taasisi 16 zisizo za kiserikali.

 

Hizi ni takwimu muhimu. Si tu katika kuona namna serikali inavyoshughulikia tatizo la rushwa, bali pia kuwafahamisha wananchi namna shughuli za serikali zinavyokwenda. Ni wajibu wake Serikali kuwa wazi kwa wananchi inaowaongoza kwa sababu kama ina nia nzuri, haina cha kuficha na Serikali iliyo wazi kwa wananchi wake, inajiaminisha kwao. Huwa nikisema humu kwamba kujieleza, tena mapema, huondoa shaka.

 

Rais Mkapa amezungumzia suala hili la uwajibikaji kwa serikali kabla ya kugusia suala la rushwa katika hotuba yake. Serikali inayojiamini, na inayowajibika kwa wananchi, inakuwa wazi kwao. Haina sababu ya kujificha. Kiongozi aliyejiridhisha kuwa jambo fulani ni la manufaa kwa wananchi wake hana sababu ya kuogopa kuwa mkweli, na kueleza kwa nguvu za hoja, kwa nini sera, mikakati na mambo fulani ni ya lazima.

 

Wajibu huo (wa Serikali kuwasiliana na wananchi), katika nchi ya kidemokrasia, unatokana na haki ya wananchi kufahamishwa, na haki yao ya kusikilizwa, kwa mambo yanayowagusa au kuwahusu. Wajibu huo wa Serikali kuwa wazi kwa wananchi wake ni jambo la lazima kwa Serikali ya Kidemokrasia, si jambo la hiari. Faida mojawapo ya kuwa na Serikali iliyo wazi kwa wananchi ni kuimarisha dhana ya uwajibikaji na nidhamu katika kazi za Serikali. Tumeanza lakini bado safari ni ndefu. Wengine Serikalini bado wanadhani kila kitu cha Serikali ni Siri Kali; hata madhambi yao yawe siri. Hayo ni makosa makubwa, lakini itatuchukua muda kubadili fikra na mitazamo ya kila kiongozi. Lakini lazima twende mbele, kamwe tusirudi nyuma.

 

Serikali ya Tanzania lazima iwe ya wananchi, inayotokana na ridhaa ya wananchi, inayowajibika kwa wananchi, na isiyoogopa kuwa wazi kwao. Kwa upana zaidi, tukijumuisha na wanasiasa, lazima sasa tujenge uwezo si wa kuwa wazi zaidi tu, bali pia wa kuelekeza siasa zetu kwenye mambo ya msingi na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi.

 

Ajenda mbili hizi ni nzito. Rais Mkapa ametusalimia Watanzania kwazo akitukumbusha wajibu wetu, mtu awe ndani au nje ya serikali. Uamuzi wake kushirikisha taasisi zisizo za kiserikali katika mapambano ya rushwa, maana yake ni kutambua umuhimu wa sekta nyingine zaidi ya Serikali katika kutekeleza majukumu ya kuongoza.

 

Kazungumzia Rushwa na Utawala Bora. Hii ya pili, kama ilivyo ya kwanza, nimekuwa zikiijadili mara kwa mara katika safu hii. Ni jambo la kufurahisha kiongozi wa juu kama Rais kujadili masuala haya kwa sababu hali inazidi kuwa mbaya upande wa Zanzibar. Kila kitu ni siri na kinafichwa. Hata shughuli za Serikali, nazo Siri Kali(SK). Hata mradi wa Vitambulisho vya Wakaazi nayo eti siri. Kumbe hata siri nayo hutoka wakati ukifika. Mradi uko kweupeni na wakuu wanajitahidi kutumia fedha nyingi leo kuufahamisha kwa wananchi. Bado kazi ipo.

Ndiyo haya husema Utawala Bora si maneno matamu, ni vitendo na kuonyesha ujasiri katika kutenda huko. Nakusalimia Dk. Mohamed Gharib Bilal Mwenyezi Mungu akujaze kheri. Suala la nyumbani libaki kuwa la nyumbani, lakini la Serikali, hapana; lazima wananchi wafahamishwe. Wakishafahamishwa, na iwe mapema si magharibi imeingia, watafahamu na haziji shaka tena kwa sababu ukieleza kitu mapema unaziba mizaha na fununu. Usiposema unaitengeneza na unachochea wananchi kuwa wakaidi. Waamini vipi wakati hawakufahamishwa mpaka gazeti limeandika (si lazima iwe kwa vitambulisho). Inasikitisha una serikali ambayo gazeti linaaminika kulikoyo.

 

Rais Mkapa anasema serikali ya kidemokrasia haiwezi kuogopa kuwa wazi. Kwa hivyo anatuambia ya kwetu Zanzibar si ya kidemokrasia. Uthibitisho mwingi. Si yenyewe tu, hata taasisi zake zikiwemo zinazoambiwa zi huru kama Tume ya Uchaguzi (ZEC) inafanya mambo sirini. Orodha za majina ya wapiga kura pia siri. Kwenye vituo, majina wanasiasa wanasema yamo mikobani. Jamani haya majina si ni ya watu, yakifichwa wasiyaone ndio nini?

 

Maana yake Serikali inaogopa majina yakiwa wazi yataonekana. Lakini ni lazima yaonekane kwa sababu ni majina ya watu hai, labda kama wamekufa. Na aliyefariki dunia hatakiwi kuwemo kwenye daftari la kudumu, sasa hofu iko wapi? Kama majina yanafichwa na mtu asipoliona lake atafutiwe mkobani, ina maana kuna siri. Ipi hiyo?

 

Sasa itakuaje wananchi wasiamini kwamba kuna mchezo mchafu umeandaliwa katika kuyatoa majina ya wapiga kura? Ndio huo usirikali anaousema Rais Mkapa. Halafu ni wa nini? Wananchi wana dhana tu si uhakika. Kwa hivyo, Tume, ili kujiridhisha mko wazi na hamsimamii mchezo mchafu, yatoeni hadharani majina ya wapiga kura badala ya mtu kutumia saa mbili za kuhangaikia jina lake. Muda huu ni adhimu watu wautumie kuhangaikia chakula.

 

Inatia moyo Rais Mkapa aliingia vizuri akitoa ahadi na leo anatupa maneno yanayomuweka katika nafasi ya kuondoka vizuri. Ila anaondoka na mtihani mgumu kwa tulivyozoea; uchaguzi mkuu wa Zanzibar. Huu ni mtihani kwake Rais na kwa sababu amekwishaambiwa namna vya kuushinda, ili aishi vizuri maisha ya ustaafu, namuachia mwenyewe na mambo yake. wanasiasa wa upinzani wanamwambia: Tembea juu ya maneno yako Rais Mkapa.

 

Amenikuna kuzungumzia rushwa leo. Ameikuta imestawi alipoingia na anaondoka ikiwepo, lakini ikiwa imezidi kustawi licha ya juhudi nyingi alizochukua kama inavyoonyesha katika hotuba yake. Kazi bado ni ngumu kwa sababu wakati anazungumzia rushwa ndani ya serikali na taasisi zake, hali halisi inaonyesha mbaya katika chama chake, CCM.

 

Tatizo la rushwa alilitumia kama bilhamu ya kuomba kura akijua kweli ni tatizo. Leo anaondoka rushwa imeingia ndani kabisa ya chama cha siasa dhamana wa dola. Tusemeje? Hiki ni chama cha rais na chama ambacho Mwalimu Julius Nyerere alisema ndicho kitoe tu rais si kingine, lakini kinanuka rushwa ndani ya viongozi wake wakiwemo hawa wanaohangaika kutafuta ubunge na uwakilishi.

 

Chama hiki kilitumia mwanya wa tatizo la rushwa kutengeneza Ilani ya Uchaguzi mwaka 1995 na kutamka kuwa serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi, itakuwa haina huruma wala aibu na wala rushwa: watoaji na wapokeaji.

 

Kwa kuwa rushwa ilikuwa na ingali tatizo kubwa nchini petu, wapiga kura wengi, kama si wote, waliamini serikali, yeye rais akiwa kinara, itasimama na maneno yake kwa kuonyesha kwa vitendo, si kwa maneno tu peke yake, ujasiri wa kupambana na wanaoipalilia. Haikuwa tabu wapiga kura kuamini tatizo la rushwa litatoweka kutokana na ahadi zilizotolewa na mgombea na chama chake. Ndipo mgombea huyo alipochaguliwa kwa asilimia 61.

 

Mengi ya mfano huo yalitendeka kabla ya kutolewa ripoti ya uchunguzi wa ukubwa, chanzo na mbinu za kutokomeza rushwa. Ni rais mwenyewe aliyeunda tume ya uchunguzi wa suala hili, lakini ripoti yake ikapata mtihani mkubwa: ilionekana kama ingefaa isiwepo maana sasa mapambano ya dhati dhidi ya wala rushwa, hususan watu wakubwa kiserikali, ilionekana ni kazi ngumu kuliko. Rais ameanza kuzoeleka si mpya tena kama ilivyokuwa pale mwanzo.

 

Wakati ule Rais alipata kusema ofisa akituhumiwa tu kuhusika na uovu wa rushwa, hata kama kutakosekana ushahidi wa kumfungulia mashitaka mahakamani, serikali yake itamchukulia hatua za kumuondoa kazini kwa kuwa itakuwa amekwishaharibu sifa ya serikali inayostawishwa. Serikali ya uwazi na ukweli. (Alikanusha haya, sijui kama bado anakanusha).

 

Kidogo kidogo kasi hiyo ikaanza kufifia na tukaanza kushuhudia kauli za kutofautiana na dhamira halisi ya mapambano ya kutokomeza rushwa nchini.

 

Nilipata kueleza katika makala za uchambuzi miaka ya nyuma, kwamba kijana wa Manyoni, mkoani Singida, alinifichulia siri ya watendaji wa TAKURU. Walimtia kati akakosana na Mahakama, Polisi na Taasisi yenyewe ya Manyoni. Alifunguliwa kesi bandia ya wizi wa vitu vya gari ya Padri. Polisi hawakuwa na ushahidi lakini wakala njama na Padri kumhilikisha. Hakimu, Polisi mpelelezi na wakuu wao wakamuandama. Chuki alizojengewa nao zilimsukuma atoke Singida ende Dodoma kutafuta wa kumlalamikia.

 

Akanikuta nikiwa ofisi za Business Times Ltd (BTL) Dodoma wakati ule. Akaeleza ya kupwa na ya kujaa. Nikatumia ujuzi kuyatoa na nilimpigia Msaidizi Mwandishi wa Habari wa Rais kumhimiza afuatilie. Kama alifuatilia au laa, anajua kwa sababu hakunieleza kitu. Ninaamini yule kijana aliendelea kusakamwa kwani hata TAKURU Dodoma haikumsaidia na Mkurugenzi wa Operesheni Makao Makuu hakuwajibika ipasavyo. Maofisa aliowatuma Dodoma na Manyoni nao hawakuwajibika, walimfuata Padri na Hakimu kutaka Kitu Kidogo (KK). Kama walipewa sijui, lakini chuki hazikwisha dhidi ya kijana huyu.

 

Ni kweli mvuto wa mikakati ya kupambana na rushwa imepungua na leo kiasi kinachodaiwa cha rushwa na wakubwa ni kikubwa mno lakini wadogo ndio hubanwa haraka. Tunajua kumbana mkubwa kwataka meno, lakini kwanini vyombo visishughulike tukaona? Tunaona watendaji wa vyombo hivi wanavyojigongagonga linapotokea suala la kufuatiliwa.

 

Hata leo nasoma habari za Stephen Kazi, aliyemaliza ubunge wa jimbo la Mwanza Mjini akiilaumu TAKURU kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya rushwa vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya waomba kuteuliwa na CCM kugombea uchaguzi ujao.

 

Mdudu rushwa anasemwa kutumika (sana) katika utaratibu wa CCM kupata wagombea wake. Utaratibu wa wagombea kupatikana kwa njia ya kupigiwa kura za maoni na wanachama wa majimboni, umeonyesha kwa mara nyingine mwanya ulioshindikana kuzibwa na inatia hofu kama kweli CCM imekomaa kisiasa. Kukomaa kisiasa ni kujenga utaratibu unaochochea uwazi badala ya kuchochea rushwa kutawala.

 

Zanzibar haikuachwa nyuma katika uovu huu. Taarifa za wajumbe wa kupiga kura za maoni kugaiwa simu za mkononi na fedha za kuanzia pamoja na chakula cha kuacha nyumbani, ni nyingi. Muombaji mmoja alifungua duka (au alitenga idadi fulani ya simu dukani kwa mtu) na kugawa simu kwa waliopitia kwake. Ukipata tu memo aliyoisaini, umeibua simu ya fedha. Na huyu kashinda kura na pengine ataingia Bungeni. Mwingine aligawa simu siku nyingi kabla ya kura. Mkinihitaji tu nipigieni kwa sababu nyumbani si kuzuri kwenu kunifuata, naambiwa muombaji mwingine wa ubunge amesema.

 

Waziri mmoja aliyeshinda kura aliahidi kitita kikubwa mtu aliyetaka kuchukua fomu kupingana naye. Mwambieni nitampa milioni 4.5 na gari ndogo asichukue fomu, naambiwa ametuma mpambe wake atoe ujumbe huu. Kashinda kura na ataingia Baraza la Wawakilishi pengine. Ni wengi hawa nafasi imekwisha.

 

Kwa nukta hii, ni jambo la wazi tukisema sehemu kubwa ya washindi wa kura za maoni ndani ya chama tawala, wamehonga na ndio watakuwa wawakilishi wa wananchi katika Bunge na Baraza la Wawakilishi. Sasa Mwalimu Nyerere akija leo, atasemaje? Bado Rais atoke CCM?.

Ends.