Waraka Kutoka Unguja

August 18, 2005

By

Jabir Idrissa





Wapendwa Wanaukumbia wenzangu;

Kawaida inaendelea. Ufuatao ni Waraka mpya uliotoka wiki iliyokwisha baada ya kuchapishwa ktk gazeti la RAI la Agosti 18. Ni faida kubwa kwa wale walio mbali na yanakopatikana magazeti ya Habari Corporation. Wengine nanyi nia nafasi ya kuusoma kwa makini na kwa karibu.

Jabir Idrissa+

 

Headline: Uchafu wa Daftari usafishwe haraka tupate Uchaguzi Huru

Waraka kutoka unguja

Kama kuna suala linalovunja moyo wananchi wa Unguja na Pemba, visiwa viwili vikuu vinavyoiunda Zanzibar, ni tabia za kiutendaji za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zanzibar Electoral Commission, ZEC). Na kwa bakhti mbaya, yanayotendeka kadiri siku ya uchaguzi inavyosogea karibu, ni ushahidi wa hofu walizokuwa nazo wananchi hawa tangu awali.

 

Sehemu kubwa ya wananchi walikuwa na wasiwasi kama tume hii inayoitwa huru, itatimiza matumaini yao na upatikane uchaguzi huru na wa haki na utakaofanyika katika amani na utulivu. Yule asiyewafahamu vizuri Wazanzibari, anaweza kudhani kwamba hofu yao hiyo inatokana na upumbavu tu wa kupenda kutabiri.

 

Sivyo. Kama kuna watu wasiofaa kuitwa wapumbavu ni wa Zanzibar. Hawana sifa hata moja za kupewa jina hilo. Hawa ni watu makini kiasi usichoweza kukadiria wewe unayejenga imani ya kuwabez. Hawa si tu watu makini tu peke yake, ni watu wenye hekma na busara kubwa, watu wastaarabu na wavumilivu wa kweli.

 

Sifa yao kubwa ni kutosahau, na hususan kile kilicho kibaya. Wanasamehe wakosaji wao lakini katu hawasahau makosa dhidi yao, iwe ametendewa mmoja wao kama mtu binafsi, familia yake au kwa ujumla wao kama watu wa jamii moja wanaotofautiana kwa asili yao. Kwa hakika, yale mambo yanayowaunganisha watu hawa wa asli tofauti, ndiyo hasa wasiyopenda yaharibiwe. Kuyaharibu haya ni matukio yanayochefua hisia na imani zao.

 

Kwa hivyo, Wazanzibari si wasahaulifu wa maudhi, au uhuni, kedi na kejeli za aina yoyote walizopata kutendewa na watawala tangu ilipoanza historia yao kama taifa. Kila palipotokea jitihada za kuwatenganisha walikataa. Ndio maana mpaka leo watu hawa wamebaki wamoja licha ya kuendelea kwa jitihada za kuwatenganisha.

 

Ni kwa sababu ya fikra dhaifu tu za baadhi ya viongozi wao tangu huko nyuma, wanaonekana karne hii kama ni watu waliogawika mno. Ni siasa mbovu na zisizo mwelekeo zilizobomoa misingi ya umoja wao. Hili ndo tatizo lao Wazanzibari: hawajapata uongozi madhubuti kwa miaka mingi ya historia ya nchi yao Zanzibar, licha ya maamuzi na dhamiri zao kutaka iwe hivyo.

 

Sote tunakubaliana, kama nchi, Zanzibar imepitia vipindi tofauti vya utawala na mfumo wa siasa za ushindani si mgeni kwayo. Ulikuwepo miaka ya 1960 kabla ya Januari 12, 1964 yalipofanywa mapinduzi ya kuungoa utawala wa Kisultani. Serikali iliyoundwa baada ya hapo, ilikataa mfumo huu lakini ilikataa hatua nyingi za kupanua demokrasia ya watu. Ilikuja enzi ya giza nene. Kukitokea kila kituko. Ah, yamepita haya, kuyarudia ni kichefuchefu kingine na msingi wa mada hii ni kuzika vichefuchefu vya namna ile.

 

Ukiitizama Zanzibar ya muongo wa 1990 na tulionao wa 2000, utagundua ya kuwa imekuwa ikiongozwa na watu wa namna yake kwa vigezo vya ubabe, ubinafsi na unafiki juu ya vingi. Uongozi usioruhusu uhuru wa kweli wa watu wake kuamua yanayowahusu, licha ya kujua kwamba haki yao hii ya kufanya uamuzi wa mwelekeo wao imetandikwa katika matamko ya kimataifa na hata katika Katiba ya nchi yao.

 

Hivi karibuni, nilikutana na mgeni mwenye asili ya Ulaya. Aliniuliza: Hivi unafikiri (mimi) nyinyi (Wazanzibari) hamna watu ndani ya visiwa vyenu hivi wanaoweza kuwaongoza vizuri. Nilipotaka kumjibu haraka alishangaa na kunizuia. Akaendelea: sipendi unijibu haraka. Alitaka nitafakari swali lake kwa sekunde chache ndipo nimjibu na jibu liwe na ufafanuzi mpana. Nilikataa rai yake ya kutumia sekunde kwa sababu hapakuwa na sababu hiyo. Lakini pili, nilikuwa tayari kutoa jibu lenye ufafanuzi. Kwanini?

 

Naam. Tangu nianze safu hii Agosti mwaka jana, nimekuwa nikihangaika kutengeneza hoja zenye mwelekeo wa kuiingiza nchi yetu katika utawala unaojumuisha watu wenye hekima na busara. Watu wanaoogopa aliyewaumba, watu wanaotembea na maneno yao, watu wanaojali utu, watu wenye uchungu na uzalendo wa kweli na nchi yao. Nimekuwa nikipiga kampeni nzito (si ya kisiasa ivyo, ya kifikra) ilengayo katika kuipatia Zanzibar hatima njema).

 

Wanaodhani napiga siasa humu wanacheza. Si mwanasiasa mie isipokuwa kijana mbichi niliyejifunza nikatambua na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, amenipa thubutu ya kusaidia wananchi wenzangu watambue utu wao, utamaduni wao, utaifa wao. Watambue dhamira za kuumbwa kwao japo si katika mtizamo wa kidini hasa. Watambue ukweli kwamba kinachowaunganisha ni uzanzibari wao, utanzania wao na historia yao kama nchi.

 

Katika kuwatandikia misingi ya kufahamu elimu hii ya utambuzi wa asili yao, utu wao na utamaduni wao na kile rafiki yangu mmoja hupenda kunieleza tukikutana; taarikh (tarehe), ndio huwa ninadadisi hili na lile, kati na kati, nikizindua viongozi wenye dhamana ya kuongoza wenzao mwenendo mwema wa kuufuata. Nazungumzia watu kuheshimiana, kupendana, kutakiana mema badala ya mabaya, kustahmiliana na kusaidiana.

 

Naingia katika kuchochea watu wenye misimamo ya kijinga ya kujijali wao tu ndio wazalendo wa kweli wa Zanzibar, wabadilike kifikra kwa sababu nchi hii ilikuwepo hata kabla ya wao, lakini pia historia yake

haiwezi kutumika kuendeleza chuki na hasama miongoni mwa Wazanzibari. Tunao wale waitwao wahafidhina wa kutupwa wanaotaka watu waamini kwamba wao tu wana haki zote.

 

Hawa ni watu wa hatari kwa sababu misimamo kama yao ndiyo iliyozibomoa Rwanda na Burundi. Ndizo zinazoitafuna Zimbabwe kwa kuamini kila mpinzani ni wakala wa Waingereza. Uhuni mtupu mwanasiasa kusimama jukwaani akiita jamii moja ndani ya nchi iichukie nyingine. Eti jamii hiyo ndiyo yenye hatimiliki na Zanzibar. Mimi wa jamii moja lakini mbona sioni ulazima wa kujitambulisha kwayo kwa sababu sijathibitisha kuwa ni fakhari kuwa hivyo?

 

Kwa sababu siamini atokaye Unguja ndiyo mbora, nawaona watokao Pemba ndugu zangu kama wa damu vile. Nachukia jitihada zozote za kunitenganisha nao. Pemba kujitenga na Unguja haiwezekani kwa sababu historia imewajenga na anayenuia kuifuta, huyo ndiye adui wetu. Walipokuwa na hata leo wakisimama wanasiasa na kuchochea utenganishi wa jamii hizi mbili, ninawaita wehu wakubwa kwa sababu kilichojengwa na aliyetuumba hakibomoki kwa kauli ya mwanasiasa huyu. Lakini imani yangu hii, ina maana tu kama hakuna jitihada za kutaka kulazimisha kujitenga huko.

 

Halafu anapotokea mwingine akajaribu kutenganisha Wazanzibari kwa sababu ya vyama vya siasa, huyu ni mwehu mwingine maana vimeanzishwa kama hatua ya kujenga hoja za kisiasa katika jitihada za kutuongoza vizuri. Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipokubali maoni ya wachache kutaka mfumo wa vyama vingi, kilisema maoni ya wachache nayo yana haki ya kuheshimiwa. Si kwa sababu ya wengi ni mabaya, bali ya wachache hayakwepeki ili kwenda na dunia.

 

Leo napata matatizo kuamini CCM, au niseme baadhi ya viongozi wachache wa chama hiki, kama ilikusudia kwa dhati yake kuleta mageuzi ya kidemokrasia nchini. Niamini vipi wakati nashuhudia (sina maana ninaona kwa macho kila kitu) matukio yasiyoijengea Zanzibar hatima? Matukio ya kuudhi watu, matukio ya kukejeli utu wa Wazanzibari, matukio ya kuangamiza umoja wao, historia na utamaduni wao. Haiwezekani na ndio maana lazima akina sisi tuendelee kuwatia darasani wahafidhina.

 

Ni ukweli kwamba ni kazi ngumu kuzungumza nao kwa sababu wamejipa nguvu hata kuliko za Firauni. Wamesahau alishindwa na jeuri yake, na kutoweka kupitia kifo kibaya. Lakini nakiri hawa ni Firauni wa uhakika kutokana na matendo yao. Kuna uhuni unafanyika na sura yake inakuja kuonyesha kuwa kama hawakushiriki kwa mikono yao, basi kwa fikra zao. Wanayasababisha matukio machafu.

 

Yule mgeni ndipo nilipomwambia kwamba mbona kuna madazeni ya watu wenye hekima na busara wanaoweza kuiongoza Zanzibar? Wapo na wengine wamo ndani ya CCM. Tatizo lao wamegubikwa na mtindio wa akili kwa kuwa kila wakiamka wanakutana, wanapanga na kutekeleza nao. Wachache hao wenye thubutu ya kuchanganyika, wanayaona matokeo yake. Hawapati taabu ya kununua vitu madukani au kusaidiwa wanapokuwa na shida za kifamilia au za kikazi. Wanaonyeshwa utu kwa sababu nao wanaujali. Wanaamini ni mazingira tu yaliyosababisha huko waliko lakini kila kitu kinawezekana. Hata CCM inasema kila kitu kinazungumzika. Tatizo ni kweli yanazungumzika? Yakizungumzwa na muafaka kuwekwa, yanatekelezwa kwa udhati wa moyo? Hili ndo tatizo letu.

 

Tunao watu wanaoweza kuongoza vizuri nchi na ikapata baraka. Katika upinzani kuna watu makini ukichanganya na waliomo ndani ya CCM wenye moyo na uzalendo wa kweli, nchi inaendesheka. Nilipata kusema wanaoona hawawezi waachie ili wananchi watengeneze mustakbali wao. Waachie kwa sababu Wazanzibari wamechoka kuendeshwa puta ja punda asiyekuwa na haki ya kusema nimechoka. Wao wanaweza kusema na wanasema ila, uhafidhina unawanyonga.

 

Turudi ZEC kwa sababu imekumbwa na wahafidhina hawa wasioitakia nchi mustakbali. Mawazo ya kuwa hii nchi ni kwa ajili yao tu yanazidi kutinga fikrani mwao. Hawajatulia kwelikweli kwa sababu wangali wakiamini kwa kuiingilia Tume ya Uchaguzi, yao yatakuwa. Hizi ni dalili za muflis. Mfalme ana pembe lakini wao hawana maana zimefujika na hazipigi tena. Zikipiga zinapiga ukuta, zikitumiwa zinagonga mwamba. Nguvu ya umma inasimama.

 

Jitihada zao za kutiribua Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) zimefika mwisho na ndivyo uchafu walioutengeneza wakiwa ufichoni unaanikwa hadharani leo. Ujanja si kuwahi bali kupata wanasema. Lakini wahafidhina hawajawahi wala hawajapata kitu. Inashangaza vijana wabichi wanadhamini kupiga raia wema virungu na nondo kwa sababu anautaka ubunge. Asahau kwa sababu nguvu ya umma inasimama.

 

Uhuni mtupu. Tunajua jawabu ya mbili na mbili ni nne, lakini kwa wahafidhina hawa, aibu hawana kwa kuleta jawabu ya 20 tukijumlisha kumi katika tano. Basi kiwewe kimewazidia kwa kujumlisha hesabu zisizojumlishika. Wanacheza na takwimu kama vile ni mali yao. Wapi? Takwimu mali ya magwiji wanaojua namna ya kuleta majibu mazuri kwa hesabu nzuri. Na majibu mabaya huja kwa hesabu mbaya. Acha waambiwe ni machuruchuru hawa, hawapati maana nguvu ya umma inasimama.

 

Inakuaje ripoti ya uandikishwaji watu kwenye daftari itoke elfu 499 na kidogo baada ya uandikishaji kukamilika Aprili 29, lakini majina yaliyobandikwa (mengine hayakubandikwa bali wahafidhina walituma mawakala wao wayatie vibindoni kama mali yao), yazidi elfu 500 (500,000). Haya natuambiwe hayo mengine yametokea wapi? Hawa ndio wale tulio tukiambiwa kuna vitabu vya pembeni, nje ya kituo.

 

Mtakumbuka ngangari wa Ghana, jimboni kwa Waziri Muhammed Seif Khatibu walibaini kada mmoja wa CCM alilaghai waandikishaji wasaidizi na kufanikiwa kuondoka na vitabu vya Tume? Mnakumbuka kulivyokuwa na kituo cha Pangatupu? Mnaweza kurudisha memori zenu Mahonda palipotumwa basi la Polisi? Hata Jangombe Maandalizi walifungua kituo na meja mzima akageuka msimamizi wake. Labda kama Tume ilifanikiwa kuharibu uandikishaji huo, ujanja wa bure.

Rudini mjini mkumbuke ya Tumekuja na Forodhani, mwende Kusini takwimu zilikopandiana baada ya uchafu wa wahafidhina. Tume ilipoambiwa wakakasirika, lakini ndo ukweli watu wamezidi leo katika daftari na nguvu ya umma inasimama.

 

Leo tunaambiwa Mpapa, jimbo la Uzini kuna watu wamezidi, Kizimkazi na Mtende watu wamezidi na Mji Mkongwe nako wamezidi karibu 3,000. Wamezidi vipi? Ofisa mmoja kati ya waliosimamia uandikishaji anatamba eti ni kutafuta kisingizio. Kwa maoni yake, ni kasoro za kibinadamu kumuacha huyu na yule. Anataka watu waamini anavyoamini yeye, kwamba alikuwa makini katika kazi yake. Alikuwa muadilifu katika kazi yake, aliheshimu sheria na taratibu alizopatiwa na Tume. Yeye alikuwa shujaa katika kupalilia hatima njema ya nchi. Asahau, uchafu uliopitishwa kwa kujua au kutokujua kwake, umekuja hadharani. Kisingizio hakipo kuna kauli thabiti na nguvu ya umma inasimama.

 

Vyama vya upinzani vikilalamika kila wakati uandikishaji ulipokuwa ukiendelea kwamba kuna michezo ya rafu inafanywa vituoni na nje yake lakini hawakusikilizwa na wakaishia viongozi wake kubezwa kuambiwa wanatunga mambo kwa manufaa yao. Wameitwa wachochezi kama ninavyokumbuka baadhi ya barua za majibu kutoka Tume. Haya nani watungaji kati ya viongozi wa vyama hivi na Tume? Nguvu ya umama inasimama.

 

Nguvu ya umma inasimama kutaka kujua ukweli wa uchafu ndani ya Daftari la Wapiga Kura. Umma wa Wazanzibari unataka uelezwe, kwanza, wale waliorudishiwa haki zao na Mahakama baada ya kunyimwa kihuni, wanaandikishwa lini na vipi? Na je wale waliokosa lakini bado ni haki yao kwa sababu Mahakama iliwageuka kutokana na matatizo ya kiufundi yasiyowahusu, na ambao ndivyo Rais Amani Abeid Karume alivyosema wapewe haki zao wote baada ya kukiri kasoro za kiutawala, wataingiaje kwenye Daftari?

 

Mambo haya ni rahisi isipokuwa uhuni tu wa baadhi ya watu kujiona wao ni bora kuliko wenzao. Yote haya yaliulizwa lakini wapi, majibu ya Tume yakawa tunachunguza, tunafuatilia, tunapitia, tunatafakari, tunashughulikia, tuna. Hivyo tu huku mambo yanaharibika na leo yapo hadharani. Pengine walidhani hawataadhirika. Kwao ni sawa na pundamilia kujificha kwenye minjugu, akisahau yu mrefu mno asoweza kujificha hapo. Shingoye i nje, kefu mgongo wake. Mambo hadharani leo na kila mtu anaona. Hawajali kuvunja moyo wahisani wanaotia fedha za walipa kodi makwao. Huu ni ukosefu wa fadhila na kutojali jasho la watu.

 

Haya tunasubiri Tume itafanya nini wakati tukipata taarifa kwamba imeridhia matakwa ya utawala kutakiwa iondoe mkataba ilioingia na kampuni ya wataalam ya Waymark ya Afrika Kusini wa kuchambua majina ya walioandikishwa ili kutambua yale machafu. Sitaki kuamini Tume hii yenye wanasheria wajuzi kama Jaji wa Mahakama ya Rufaa na mtu mwenye hekima na busara kubwa kama Mwenyekiti Masauni Yussuf Masauni ilikosa kuwajibika hata kuamua kuusaini.

 

Naweza kuamini ninapoambiwa ya kuwa kila kitu kiliangaliwa kwa undani, na kila kifungu cha mkataba kilijadiliwa kabla. Sina sababu ya kuamini makamishna wa Tume na watendaji wao walikosa uadilifu kama inavyodaiwa kuwa wameuza uhuru wa nchi yetu kwa kutia mkataba na kampuni ya nje. Na tangu lini tukawa wazalendo wa kutoa zabuni kwa wazalendo? Mbona nyingine hazitolewi hivyo? Iwe hii tu kwanini?

 

Tumelijua tatizo lao wahafidhina: kisu cha kule kinakata kisawasawa si butu. Asiyestahili hawezi kuingia iwe usiku iwe mchana. Kompyuta na kwa mfumo wao, haikubali jina langu liingie katika Daftari mara mbili eti kwa sababu ni mpiga domo gazetini. Eti hiyo iwe ndiyo zawadi yangu. Likiingia mara ya pili jina, mtiaji ataulizwa, unataka kufuta la awali (liliopo). Kwa hivyo ni kusuka au kunyoa. Unakubali yaishe, si hivyo mpaka usiku usitoke kuingia mchana: kiyama.

 

Kwa panga hilo, itakuwa yale yale ya siku zote tangu 1995, Mambo Ni Magumu (MNM). Haya, mkataba umesimama kutokana na hujuma za wahafidhina lakini tatizo lipo bado; uchafu wa Daftari walioupalilia kwa nguvu ya Kidumu Chama cha Mapinduzi utasafishwa vipi? Naamini Wazanzibari hawakubali uchaguzi usite wala hawakubali uende bila ya Buku. Hawakubali manyuva. Uchaguzi ufanyike tu tena kwa Daftari safi ja shuka. Itakuaje? Idumu amani na utulivu na uchaguzi huru, wa haki na wazi.

Ends.