Waraka Kutoka Unguja

August 25, 2005

By

Jabir Idrissa



Headline: SMZ twataka Daftari safi kwa Uchaguzi safi

 

Wiki iliyopita nilianza kwa kusema kwa bakhti mbaya, yanayotendeka kadiri siku ya uchaguzi inavyosogea karibu, ni ushahidi wa hofu walizokuwa nazo wananchi hawa tangu awali. Na baada ya kueleza mengi ndani ya mada kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura la Zanzibar, nilihitimisha hivi:

 

Naamini Wazanzibari hawakubali uchaguzi usite wala hawakubali uende bila ya Buku (daftari). Hawakubali manyuva. Uchaguzi ufanyike tu tena akwa Daftari safi ya shuka. Itakuaje? Idumu amani na utulivu na uchaguzi huru, wa haki na wazi.

 

Kwa yaliyotokea na yanayotokea, inazidi kupandikizwa hofu ndani ya akili za Wazanzibari. Wanaendelea kujiuliza wanaweza kuvuka salama uchaguzi huu? Waamini itaendelea kuwa uchaguzi wa mazonge na shaghalabaghala? Waamini ya kuwa utawala na watawala hawajawa tayari bado kuona nchi inapata uchaguzi madhubuti, inajenga msingi mzuri wa kupatikana amani ya kweli, kupatikana haki kwa urahisi na huduma kwa ufanisi?

 

Tukubali kwamba hofu inazidi kwa sababu kila kukicha wanasikia na kushuhudia kauli za kuvunjana moyo. Kauli zinazoashiria mazonge na shaghalabaghala. Ni kwa sababu mambo yanazidi kufunuka na mitego iliyo ikitengenezwa kwa malengo, inaonekana kuvuna kilichotakiwa.

 

Tunazungumzia Daftari la wapiga kura wa Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani. Tushajua mpaka sasa kwamba ndani ya daftari kuna majina machafu yasiyotakiwa kubaki kwa sababu kubaki kwake ni kutishia umadhubuti wa uchaguzi wetu. Kwa uhakika hili sasa tunalifahamu, na kilichotarajiwa na umma, ni hatua zinazochukuliwa kusafisha uchafu huu ndani ya Daftari.

 

Kitu kimoja hakijafurahisha umma. Kitendo cha suala la usafishaji wa uchafu huu kutoelezwa bayana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Tume hii ina wajuzi, ina wataalamu waliobobebea katika Sheria, Teknolojia, Utawala, Hesabu, Uandishi wa Habari, na isitoshe, watu waliojaa hekima na busara kubwa, lakini bado taaluma hizi hazijatumika ipasavyo kuthibitisha kuwa taasisi hii imepewa watu makini. Watu wa kujenga matumaini ya Zanzibar kuondokana na uhuni na uzandiki. Uwazi na ukweli ingali tatizo kwa tume yetu. Hili ni tatizo sugu.

 

Pamoja na kupiga debe na kukumbusha mara nyingi juu ya umuhimu wa Tume kufanya shughuli zake kwa uwazi, bado kuna mtindo wa Siri Kali (SK). Kila uamuzi siri, kila hatua siri, kila taarifa siri, kila hati siri. Basi hivyo tu, Kila Kitu Siri (KKS). Utendaji wa ajabu tunaendelea kuushuhudia ndani ya tume hii. Utendaji unaoiweka tume kuwa moja ya Taasisi muhimu za kinchi zisizowapa wananchi kile walicho na wanachotaka kukipata: uchaguzi huru, wa haki na katika amani ya kweli.

 

Nimesema unapojifunua, unaondoa hofu wananchi. Unaondoa uwezekano wa kujengwa hisia za ajenda ya siri katika taasisi yao. Ndio jamani, Tume ni Taasisi ya Wazanzibari maana ndio wanaoilipia. Viongozi na wafanyakazi wa Tume wanalipwa kwa fedha ya wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwemo ya kodi. Basi inatakiwa Tume iwarudishie wananchi hawa fadhila kwa kutenda shughuli zao kwa uwazi na kwa haki. Waione tume si tu inatenda maamuzi ya haki na kwa uwazi, bali pia maamuzi yenyewe yanafanywa kwa wakati muafaka. Hayacheleweshwi.

 

Baba unapofika nyumbani ukakuta chakula hakijakamilika kuandaliwa unafoka. Kwanini? Ni kwa sababu si haba ulipoondoka bajeti imekaa vizuri, kila kitu kimetimia, sasa ziko wapi sababu za chakula kuandaliwa. Ina maana umetimiza wajibu wako, isipokuwa mwingine hakutimiza wake. Hakuwajibika. Sasa kufoka kwako ni kumzindua ya kuwa awe mtimiza wajibu wake na kwa wakati. Unalazimika kurudi tena kazini kwako bila ya kula kwa sababu hakikukamilishwa na mwenye wajibu wa kukiandaa. Kosa zito.

 

Basi Tume ya Uchaguzi nayo ni hivyo hivyo. Inapochelewesha uamuzi au taarifa muhimu kwa wananchi, itambue inawakosea kwa sababu imeshindwa kutimiza wajibu juu yao. Wao ndio walipaji hivyo wanataka kuiona faida ya kulipa kwao. Nilipata kusema Tume ina waandishi mahiri wa habari wanaoweza kutengeneza taarifa za kwenda kwa umma kupitia vyombo vya habari tele tulivyonavyo. Watumiwe basi ili wajisikie wamekwenda pale kufanya kazi yao waliyoisomea kuliko kuwabebesha makaratasi ya kutoa nakala bila ya mambo yenyewe kufikishwa kwa walaji. Walaji wa taarifa za shughuli za Tume hakuna isipokuwa, wananchi. Haifai kila wakati kuwakalisha njaa wakati wana uhakika ghalani chakula kinamwagika ovyo.

 

Mpaka naandika waraka uliopita, hakuna maelezo ya Tume kuhusu fununu za kusimamishwa mkataba ilioingia na kampuni ya Waymark Infotech ya Afrika Kusini. Hata sisi tunajiingiza tu bila ya kupata uthibitisho rasmi wa Tume hii. Lakini tufanyeje na tunayasikia yanasemwa nje ya milango ya taasisi hii, wakati wenyewe wapo hawataki kuyasema kwa bayana? Tutaendelea kuyasema kwa njia hiyo waionayo wao ndio sawa kuliko wao kutupatia taarifa za uhakika zitakazoua uvumi.

 

Jumapili kukafanyika halfa ya utiaji saini wa Waraka wa Maadili ya Uchaguzi Zanzibar. Alhamdulillah, wakubwa wa Tume wakawepo pale. Nililazimika kushuhudia hafla hii kwa sababu kubwa moja: nitapata fursa ya kuwaona wakubwa hawa na kuwauliza kulikoni mambo yenu yanasemwa nje bila ya kauli yenu wakati ndio tuliowapa mdomo? Na kweli, Mwenyezi Mungu kanisikia. Wakubwa wote walikuwepo na tukawauliza swali hili.

 

Cha kufurahisha nao wameamka vizuri walikuwa laini kuliko siku nyingi sijapata kuona. Mwenyekiti Masauni Yussuf Masauni na Makamu Jaji Agostino Ramadhani wakasema si haba. Nawapongeza wakubwa hawa kwa kuamua kueleza japo katika harakaharaka na katika kuchelewa ile tunayoilaumu kwa nguvu zote. Waswahili twasema kupata hakuna kudogo. Tulilalamika pale kwamba mbona hatuwasikii Tume kusema kwa wakati mambo yanapoharibika?

 

Mwenyekiti anasema wanaachia magazeti yaseme yatakavyo. Si mshasema nyie maana nyinyi ni mafundi wa kutengeneza uongo. Mnaandika mambo hata bila ya kutuona hata mnathubutu kudanganya watu kudai mmemuuliza nani na nani sijui wakati si kweli aliyetajwa alikuwa nje ya Zanzibar. Acheni nyie acheni haifai. Hatukumuachia hapo, tulimwambia Tume nanyi mseme matatizo na mafanikio yenu badala ya kukaa kimya. Mkisema mapema mnaondoa uvumi na taarifa potofu. Basi hata zinapotolewa potofu pia mnabaki kimya tu sasa watu waseme nini kama si kuyaamini. Na si muwaite wanaoandika uongo muwarekebishe.

 

Basi Tume inasema: Mkataba wa Waymark wa kuhakiki majina ya wapiga kura walioandikishwa ni kweli umetakiwa na Serikali usimamishwe kwa sababu utaratibu wa kiserikali haukufuatwa japokuwa hiyo ni Taasisi huru. Tume haitoki kuwa ni taasisi ya kiserikali ambayo inapotaka kuingia kwenye mikataba na kampuni za nje inapaswa kushauriana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yeye ndiye atakayeiwakilisha kutetea kilichofanyika. Baada ya yote, Mwenyekiti anasema wamepata barua ya uamuzi kutoka Serikalini, msainiji akiwa Mwanasheria huyu.

 

Serikali imeamua mkataba uvunjwe kwa sababu hakuna mantiki ya uhakiki wa majina kufanywa nje ya nchi na wataalamu wa nje ya nchi. Hiyo si kwa maslahi ya nchi iliyo huru na yenye heshima yake inayopaswa kuheshimiwa. Mzee Masauni na Makamu wake wakasemaje? Walijadili uamuzi wa Serikali Agosti 20 na wangetoa uamuzi stahiki jana. Uamuzi wenyewe ni wa kupiga hatua kutoka hapo si kurudi nyuma. Ndio maana yake. Hatuwezi kurudi nyuma bali kwenda mbele.

 

Mwenyekiti alisema kitu kizuri pale cha kwamba kazi ya uhakiki ni muhimu ifanyike kwa vyovyote vile kwa sababu itajenga imani kwa wananchi. Na kweli, Ofisa wa Kibalozi wa Uingereza, Andrew Massey alituambia wiki iliyopita kwamba kuhakiki daftari ni hatua ya lazima na muhimu kwa sababu inachochea wananchi kujenga imani na daftari na hiyo ni namna pekee ya kuwajenga imani kwamba wanaweza kupata uchaguzi mzuri.

 

Daftari madhubuti litatoa uchaguzi na matokeo madhubuti. Bila ya umadhubuti katika kumbukumbu za wapiga kura, hupati uchaguzi madhubuti kwanza umma kufahamishwa kuhusu daftari ni hatua ya lazima kwa sababu ni haki ya umma kulifahamu daftari lilivyo. Daftari si mali ya mtu au kikundi chao, mali ya umma, alituambia waandishi wa habari na wawakilishi wa vyama vya siasa waliokusanyika ukumbi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ofisi ya Zanzibar, pale mtaa wa Shangani. Ilikuwa katika mjadala wa masuala ya uchaguzi kwa uzoefu wa Uingereza. Tunacho cha kujifunza.

 

Leo daftari lina uchafu na ndio uliotakiwa usafishwe ili liwe madhubuti na liwe njia ya kupatikana uchaguzi madhubuti, Tume imejigonga na Serikali imeingia tele. Serikali inajaribu uhuru wa Tume ya Uchaguzi. Njia inayotumia si nzuri kwa sababu inajieleza kwamba Tume ni huru lakini papo inaiingilia inapofanya maamuzi yake. tumesikia tamko la Serikali kupitia Mheshimiwa sana, Ali Juma Shamhuna. Amewarukia wafadhili na watendaji wa Tume, kwa hakika amewadhalilisha wote kwa pamoja na mmoja mmoja anaposema kuna ajenda ya siri imetengenezwa na wafadhili kwa kushirikiana na Tume.

 

Tangu lini taasisi ya kiserikali ipange njama na wafadhili dhidi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar? Imeanzia wapi njama hii hata leo iwe ya pili? Wanaofanyiwa njama wako wapi kwamba wasijue kinachoendelea, wasifahamu nini kinafanyika ndani ya Tume ya Uchaguzi wanayoilipa? Serikali haina watu mle ndani ya Tume? Hainao kweli? Si wengi wakubali. Serikali ina watu wake mle wanajulikana. Hawajifichi hata wenyewe wapo.

 

Lakini serikali inapohoji wajibu wa Tume ijiulize pia inatekeleza wa kwake na kwa wakati unaofaa? Mara ngapi Serikali imetoa kauli kuhusu lawama kwamba haiipatii Tume fedha ilizoahidi kuipa kwa ajili ya shughuli za uchaguzi? Haijui kwamba wahasibu wa Tume hupanda na kushuka kutwa nzima mara chungu nzima kuhangaikia fedha? Haijui kwamba inatakiwa kuipa tume fedha kwa wakati ili itimize huo wajibu wake wa kutumikia umma? Kwani umma haujui kwamba Mwenyekiti amewahi kumfikia Rais kulalamikia fedha? Umma unajua hili na majibu ni yale yale: Tutajitahidi kuwapatia fedha kwa wakati. Zimepelekwa kwa wakati? Mbona ubandikaji majina ya walioandikishwa ulisimamishwa dakika za mwisho baada ya kutangazwa ungefanyika? Sababu ni moja tu: Tume haijapatiwa fedha kwa ajili ya kufanikisha hatua muhimu hiyo ya kulihakiki daftari.

 

Wazanzibari tunaambiwa leo kwamba Serikali hairuhusu uhakiki kufanywa nje ya nchi na eti Waymark waliondoka na majina 30,000 badala ya 10,000 waliyotakiwa kuyachunguza. Hawa ni wataalamu wanaoshirikiana na wataalamu wa teknolojia waliopo Tume kwa hivyo majina hayakuibwa yametolewa. Kama hawakupewa kihalali nani amehoji kati ya Serikali na Tume yenyewe? Tuambiwe badala ya kulaumiwa wataalamu.

 

Na kama Serikali ilihoji basi tuioneshee kidole tume haikusema kwamba imehojiwa mapema kabla ya kusaini nao mkataba. Serikali nayo ina wajibu kuufahamisha umma pale mambo yanapoonekana yanakwenda kombo. Njia hii Serikali kutoa taarifa baada ya mambo kuharibika, kama inavyosema, ni mbinu za kizamani za kutatua matatizo. Serikali yetu, labda tuseme yetu tukufu, inatuambia kwani nchini hakuna wataalamu wa kufanya uhakiki ule, au kwamba mbona wapiga kura milioni 16 wa daftari linalosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wamehakikiwa hapa hapa nchini, kulikoni majina yasiyozidi 500,000 yahakikiwe nje.

 

Tuendelee kuambiwa basi hao wahakiki wa majina ya NEC ni wepi? Jamani ni hawahawa Waymark na kwa utaalamu unaodaiwa haupo Tume? Kwa kuwa mpaka sasa sijasikia kauli thabiti ya Tume kuruhusu majina yachukuliwe nje ya nchi kwa uhakiki, nakubaliana na Serikali hakukuwa na haja hiyo. Na kwa sababu NEC walifanya uhakiki ndani ya nchi, kadhalika hoja ya serikali ni nzito. Lakini bado, nini maana ya kukosoa kasoro hii dakika hii wakati majina hayakuchukuliwa jana?

 

Inafurahisha Serikali yenyewe imekiri hakuna muda wa kutosha wa uhakiki wa daftari. Bado serikali haijatoa jibu la kuondolewa majina machafu kwenye daftari kwa sababu njia ya Mahakama ishakamilika na bado serikali haikutoa kauli ya kuwathibitishia wananchi wale kuwa wataandikishwa kabla ya siku ya uchaguzi. Isitoshe, wangapi waliopewa haki ya kuruhusiwa kuandikwa? Hivi tuseme Serikali haijui kwamba kuna watu kwa maelfu walizuiwa kujiandikisha kutokana na vituo kuhodhiwa na mawakala wao? Serikali inataka kujivua lawama za uhuni uliotokea wakati wa uandikishaji? Imechelewa kwa sababu kila kitu kilijidhihirisha vituoni.

 

Kwa mfano, kitendo cha kuwazuia masheha kufika mkutano wa Tume, Mkuu wa Mkoa kumrudisha Sheha aliyekuwa ameondolewa kituoni na Tume kwa sababu ya kutokuwa muadilifu, kuvamiwa watu wa Kinuni na Jangombe, kujeruhiwa kwa mapanga Mzee Juma Muhunzi, kuchomwa moto viwanda vya mbao Kidimni, Nyerere na Kinazini. Yote haya yalitokea na serikali haikutoa kauli yake. Hakuna aliyekamatwa. Tukubali uhuni mwingine ni kazi ya dola.

 

Nani anafadhili kambi za vijana wanaojitambulisha kuwa ni wakereketwa wa CCM, chama dola? Kama si Serikali ni lini imekubali kwamba kambi hizi zinazalisha uharamia ukiwemo huu wa kupiga watu waliostarehe bukheri wa afia kwenye baraza zao? Tunaposhuhudia matukio ya kihuni mitaani mwetu usiku na mchana huku serikali ikikaa kimya tusemeje? Ndio utawala bora huu na utawala wa sheria? Hii si ni Operesheni Dondola kuwarudia raia wema wakati tuliambiwa ni ya kuwalinda? Lazima tufike mahali kila mtu aseme ukweli. Kama sisemi ukweli basi ni jukumu la Serikali kueleza ukweli kwa wakati.

 

Shughuli zote za uchaguzi kugharimiwa na Serikali. Ni jambo zuri lakini hili nalo linazua maswali mengi kuliko nguvu za kuyajibu. Leo Serikali yetu tukufu inazo fedha za kutosha kugharimia uchaguzi, leo? Kumbe kama tunavyoamini wengi, inazo fedha ila inazitoa inapojisikia. Siku wakubwa wanapoamka vizuri wanaifikiria Tume siku wanayolala bwi na kuamka nao nongwa. Zinapotakiwa fedha na Tume hazipatikani ila inapotaka Serikali inatoa, huu ni ujanja na kibri na Serikali adilifu haipaswi kuonyesha kibri katika suala la kutimiza wajibu wake. Ifanye tu bila ya kujidai.

 

Kauli ya Serikali kuhusu Daftari ni kichekesho cha mwaka. Kauli yake kuhusu kugharimia uchaguzi ni kituko pia. Lakini upande mwingine naipongeza Serikali kwa kuona inayo njia ya kutokea. Ipo kumbe njia ya kuzidisha mazonge kwa sababu kwayo, nina hakika Daftari litabaki chafu na maana yake uchaguzi utakuwa mchafu. Serikali imetoa ahadi ya kulisimamisha Daftari kuhakikiwa na inatuambia kuwa acha tu tuende kwenye uchaguzi bila ya Daftari madhubuti. Wataalamu weshasema Daftari Madhubuti Uchaguzi Madhubuti vinginevyo mazonge matupu. Tunasubiri ukweli utadhihiri na Nguvu ya Umma inasimama.

Ends.