Waraka Kutoka Unguja

September 1, 2005

By

Jabir Idrissa



Headline: Muradi uhakiki wa Daftari unafanywa, Tume kaeni kimya!

warakaSpt01

Khabari ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) inazidi kuwa muhimu. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) bado haijataka kusema huku ikijua fika ya kuwa inatakiwa iseme ili wananchi wanaoilipa wajue nini kinaendelea kuhusu suala hili.

 

Umma unachokifahamu mpaka sasa ni kwamba Serikali imetamka kuvunjwa mkataba wa uhakiki wa majina yaliomo katika Daftari la Wapiga Kura kufanywa nje ya nchi na wataalamu wa kampuni ya  Waymark Infotech ya Afrika Kusini. Isitoshe, Serikali kupitia Waziri wake wa nchi katika Ofisi ya Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna, imesema kuanzia sasa itagharamia shughuli zote za uchaguzi.

 

Inasema imeamua kuchukua hatua hii baada ya kubaini kuwepo ajenda ya siri kwa wafadhili wanaosaidia shughuli za uchaguzi mkuu. Wafadhili hawa, Canadaa, Denmark, Jumuiya ya Ulaya (EU), Finland, Sweden, Norway, Uholanzi na Uingereza, wanaambiwa na Serikali yetu tukufu kwamba wanakula njama na vyama vya upinzani kuingilia uchaguzi huru, wa haki na unaotakiwa kufanyika katika hali ya amani na utulivu.

 

Wakati bado Tume haijataka kutoa kauli yake na kuzidisha hofu waliyonayo Wazanzibari, kuna matukio ya kutia moyo yanatokea nchini petu Zanzibar.

 

Siku chache baada ya Serikali kutoa kauli yake kuhusu uhakiki wa Daftari la Wapiga kura, nchi wafadhili nao walisemaa. Haikutosha tu kusema, waliamua kufunga safari kuja Zanzibar na kuonana na viongozi wakuu wa Serikali. Wakitaka kupata ufasaha wa kauli hiyo na mantiki yake nini hasa.

 

Basi walikuwa Balozi Mdogo wa Uingereza, Mike Kroll pamoja na Balozi mwenzake kutoka Norway. Walikutana na Waziri Shamhuna na Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) ikarusha taarifa kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesisitiza msimamo wake wa kuachiwa kugharimia uchaguzi yenyewe.

 

STZ imekariri mazungumzo ya Waziri na mabalozi hao ikisema kwamba nia ya uamuzi wa Serikali ni kutaka kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 30 unafanyika kwa uhuru, kwa haki, na katika mazingira ya amani na utulivu. Hakuna kingine.

 

Lakini wapashaji wa khabari wanasema kulikuwa na mengi yaliyosemwa na pande zote mbili. Tunaambiwa kwamba Mabalozi hawa walimtaka Waziri atoe uthabiti wa msimamo wa Serikali kuhusu suala la wafadhili kusaidia shughuli za uchaguzi. Kwamba ni hakika kabisa Serikali haihitaji msaada wa wafadhili? Hii maana yake ni wafadhili kutaka Serikali itoe msimamo wake kwa maandishi kwa kuwa wafadhili hawakuamua tu kusaidia Zanzibar kufanikisha uchaguzi wake.

 

Wafadhili walifanya mazungumzo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, walizungumza na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa undani (sana) kuhusu utekelezaji wa Muafaka uliofikiwa na kusainiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), vyama vyenye udhibiti mkubwa zaidi wa siasa kwa Zanzibar. Kwa hivyo baada ya mazungumzo na wafadhili na serikali hizi mbili, palifanywa makubaliano ya wafadhili kusaidia utekelezaji wa Muafaka.

 

Makubaliano haya hayakufanywa kwa maneno matupu, palikuwa na mkataba wa kuthibitisha kwamba pande hizi husika, Serikali na Wafadhili, wamekubaliana kushirikiana katika hatua ya kufanikisha uchaguzi wa Zanzibar. Uchaguzi si siku ya kupiga kura tu, la hasha. Uchaguzi ni hatua kubwa inayoanza mbali. Unapozungumzia hatua (kwingineko wanaita mchakato) katika uchaguzi, hata ukataji wa majimbo ya uchaguzi ni shughuli ya uchaguzi.

 

Uandikishaji wapiga kura ni sehemu ya hatua ya uchaguzi. Wanasiasa kuchukua na kurudisha fomu za kuomba uteuzi wa Tume ya Uchaguzi zikiwa tayari zimejazwa na kuambatanishwa wadhamini kwa idadi inayotakiwa kutegemea na nafasi mtu anayoiomba, ni sehemu ya hatua za uchaguzi, wanasiasa kuteuliwa kugombea ni sehemu ya hatua za uchaguzi.

 

Hatua ya vyama na wagombea wao kufanya kampeni ya kuomba kura kwa wananchi, upigaji kura, uhesabuji wa kura, utangazaji wa matokeo ya kura kwa maana ya matokeo ya uchaguzi wenyewe, ni hatua zinazokamilisha mtiririko mrefu wa shughuli nzima ya uchaguzi.

 

Kwa hivyo, yapo makubaliano ya maandishi yaliyowekwa na Wafadhili na Serikali zetu. Makubaliano hayo yanaleta maelewano ya wafadhili kuingiza fedha kupitia Tume ya Rais ya Pamoja ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Muafaka (Joint Presidential Commission on Muafaka, JPC). Fedha zote zinazohusu msaada wa nchi wafadhili kwenye masuala ya uchaguzi zimekubaliwa kuingizwa kwenye mfuko wa JPC.

 

Ndani ya mfuko huo, ndiko Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inapata fedha zile ambazo Wafadhili wameahidi kutoa kama mchango wao katika kufanikisha uchaguzi mkuu Zanzibar. Palipotokea matatizo ya ubadhirifu wa fedha za Wafadhili katika JPC, pamoja na mambo mengine, iliamuliwa na Wafadhili na  Serikali, kwamba fedha za uchaguzi ziingizwe moja kwa moja katika akaunti ya ZEC.

 

Tume ya Uchaguzi inapolalamika haina fedha, tutambue kwamba si zile zilizoahidiwa na Wafadhili. Zi hizo jamani, ni fedha ilizoahidi Serikali yetu tukufu kutoa kwa ajili ya kuchangia gharama za uchaguzi. Serikali ina mchango ilokubali kuutoa usiopungua sh bilioni 1.6. Taarifa zinaonyesha kwamba mpaka Serikali inatoa tamko la kuwa tayari kugharimia yenyewe uchaguzi wote, ilikuwa imeipatia Tume ya Uchaguzi sh milioni 110 tu. Kiasi hicho hakijafikia nusu ya mchango wake kwenye ufanikishaji hatua za uchaguzi. Shilingi milioni 110 katika sh bilioni 1.6 maana yake ni asilimia 11 tu ya mchango wote inaotakiwa kuutoa.

 

Kitu kimoja sina ubishi nacho: kwamba Serikali yetu tukufu inazo fedha za kutoa lakini haijaona kama ni muhimu kuzitoa. Kwanini nasema na ninaamini inazo? Ndio inazo kwa sababu inafanya matumizi mengi mbalimbali yasiyo muhimu kwa mbwembwe nyingi. Kuna mambo mengi yanafanywa kwa gharama kubwa lakini hayana ulazima wowote kulinganisha na hali halisi. Lakini ndiyo Serikali yetu tusemeje kama inatueleza bila hofu kwamba fedha nyingi zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo kwa hivyo wafanyakazi wavumilie mishahara inapochelewa? Fedha ya mshahara kuhamishiwa kugharimia mradi wa maendeleo? Tunaambiwa familia za wafanyakazi si muhimu mbele ya azma ya Serikali kuleta maendeleo ya barabara na maji? Mtajaza nyinyi.

 

Serikali haijatoa kauli kwa maandishi ya kutowahitaji Wafadhili kusaidia uchaguzi. Kama si kweli tutaelezwa kama tulivyoelezwa kupitia tamko kama tulilolishuhudia ndani ya STZ wiki iliyopita. Ni kwa sababu hiyo bado Wafadhili wanafuatilia ufanikishaji hatua za uchaguzi mkuu Zanzibar. Hawajatoka maana hawajaambiwa watoke. Waliingia kwa ruhusa ya maandishi watatoka kwa ruhusa ya maandishi. Kauli ya Serikali ni maoni tu.

 

Nilisema na kauli ingalipo kwamba Wafadhili wawepo wasiwepo, Serikali ipige kifua kugharimia isipige, Daftari la Wapiga Kura lazima lisafishwe kama kweli tunataka, umma, na Serikali ya CCM inataka, uchaguzi uwe madhubuti, kwa maana ya huru, wa haki na wa amani na utulivu. Kuwa na daftari madhubuti ni njia ya kuwa na matokeo madhubuti ya uchaguzi. Uchaguzi madhubuti hutanguliwa na Daftari madhubuti la wapiga kura. Lazima umadhubuti upatikane kwanza kwenye Daftari ndipo uje uchaguzi madhubuti na matokeo madhubuti. Hakuna namna nyingine, kama alivyosema Andrew Massey wa Ubalozi wa Uingereza nchini. Ni haki kwa umma kupatiwa Daftari safi, lakini ni wajibu wa Serikali kufanikisha hilo. Kwa sababu haki inakwenda na wajibu kwanza, basi wajibu unatakiwa utimizwe ili haki ipatikane.

 

Okay! Tume ya Uchaguzi haitaki kusema lakini inasema. Niwaambie ukweli inasema Tume kwa njia zake. Zipo taarifa za kutosha ya kuwa kazi ya uhakiki haijasimama kusema la haki. Inaendelea. Wataalamu wa Waymark wapo wanaendelea kufanya kazi hii wakishirikiana na wataalamu wa ZEC. Ndio wanaifanya kwa sababu ni kazi muhimu kufanywa kwa maslahi ya kweli ya umma. Uzoefu wa demokrasia za Kiafrika unaonyesha kuna maslahi ya umma na maslahi ya taifa. Ya umma ni yale yanayohusu watu, lakini ya taifa ni yale yanayohusu watawala. Ndivyo nionavyo.

 

Serikali inaposema haijaona umuhimu wa uhakiki kufanywa nje ya nchi inatizama maslahi ya taifa si ya umma. Kuhakiki majina ya wapiga kura hakuhitaji wataalamu kuondoka Zanzibar na Buku lenye majina 500,000 na zaidi, ni kitu cha kufungua kompyuta na kuelekeza mshale panapotakiwa, na mtu unakuta majina yote, moja baada ya jingine. Unalitazama utakavyo na unaliona kama lina kasoro au vipi. Kwa hivyo hata aliyeko Marekani na Uchina, akitaka analitazama Daftari letu huko aliko badala ya kulazimika kufika Maisara ya kufungua mitambo ya Tume. Wanasema majina yapo kwenye vidole tu kutokana na teknolojia iliyokua.

 

Maslahi ya umma ni yanayotaka majina yatizamwe tu iwe isiwe ili machafu yatoke kwenye Daftari. Hapa ndipo tutapata Mtu Mmoja Kura Moja. Afrika Kusini walihangaika kwa miaka mingi kupata kitu hiki kiitwacho One Man One Vote. Zanzibar hatuna chaguo leo kama tuko kwelini kupata uchaguzi huru, wa haki na katika mazingira ya amani na utulivu. Mtaalamu anapolitizama jina langu anakuta maajabu ndani. Ati linakuja na jina jingine kwenye picha inayoonyesha uso wangu? Uso wa mtu mmoja unakuja na majina mawili na hata matatu tofauti tofauti. Nini hii kama si maajabu. Uthibitisho wa kuwepo watu walioandikwa zaidi ya mara moja. Ndiyo yale ya kubainika majina zaidi ya yale yaliyoandikwa vituoni wakati wa uandikishaji. Tukaambiwa ah hiyo ni jambo dogo unapozungumzia takwimu. Jambo dogo Tume kutoa isabu ya watu 499,000 baada ya uandikishaji kukamilika na ikatoke isabu iliyozidi orodha za majina zilipobandikwa kwa uangalizi. Mimi si bingwa wa hisabu, lakini mabingwa hawakubali. Siwezi kubisha.

 

Ukisafisha maajabu haya ya uso mmoja kukutwa na majina tofauti yasiyoendana na alama za dole gumba, unatengeneza Daftari. Haitoshi, kumbe unaondoa siri za watu kuzidisha idadi ya kura. Zimbabwe walipofanya uchaguzi miezi michache iliyopita na chama cha ZANU PF cha Mzee mpigania uhuru maarufu barani Afrika, Robert Mugabe, kuibuka na viti vingi vya Bunge, kulikuwa na malalamiko ya kura hesabiwa kuzidi kura pigwa. Waliopiga kura ni watu 30 lakini kilichohesabiwa ni kura 50, hizi 20 zilitoka wapi? Labda Zanzibar, twenye uhusiano mzuri unaostawishwa kwa ziara, tunataka kufuata nyayo zao. Uchaguzi huru na wa haki una kazi Afrika.

 

Yote kwa yote. Uhakiki unafanywa na wala msishangae kuwa unafanywa kwa sababu hata gazeti lao linalouza (sana) kulingana rekodi za mawakala(?), limeandika likiisema Tume imeipuuza Serikali kwa kuendelea na kazi ya uhakiki ambao kwayo gazeti na wamiliki wake mabwana wa waandishi wa habari wenzetu maskini, ni kizungumkuti. Kama ni kizungumkuti sawa, lakini si ni kwa maslahi ya umma? Au ni bora maslahi ya Taifa?

 

Uhakiki uendelee kufanywa maana ni muhimu. Ufanywe kwa umakini huku tukisubiri na wale walioshinda rufaa zao mahakamani, na wale wengine waliokwamishwa tu kwa sababu za kiufundi zisizowahusu, watangaziwe na Tume njooni sasa muandikwe ili nao waingie katika Daftari kwa ajili ya kuja kupiga kura ambayo ni haki yao ya kikatiba. Wanachotakiwa kufanyiwa si upendeleo ni haki yao kama tunakubali Katiba ndio msingi wa uendeshaji mambo yetu. La kama tuna mengine na tunaweka kando Katiba, basi hakuna atalalamika ila Nguvu ya Umma itaja simama. Mahangaiko kwa nchi zilizokuwa hazijataka demokrasia ya kweli, ni jambo la kawaida. Haki haipatikani mpaka ipiganiwe. Ndani ya sahani hii haki raia, haiwezekani.

 

Tume msiseme kama hamtaki kusema. Tunawakubalia mbaki hivyo hivyo kimya muradi kazi ya uhakiki inafanywa. Hilo la kufanywa uhakiki ndio muhimu zaidi kuliko hili la kwamba kila kinachofanyika umma ujulishwe. Tusipojulishwa leo tutajulishwa hata kesho mkitaka. Ndio uzuri wa tunavyopeana dhamana, anayepewa ndiye muamuzi: akitaka itakua asipotaka haiwi. Sivyo mbele ya muumba, atakavyo yeye huwa wala hakuna kizuizi.

Ends.