Waraka Kutoka Unguja

September 15, 2005

By

Jabir Idrissa



Headline: Kampeni ya kubomoa umma itaikifisha z'bar wapi?

 

Kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 30 mwaka huu zimeanza. Wiki ya pili inakatika tangu Septemba 5 kampeni ilipoanza baada ya  Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kupitisha majina ya wagombea.

 

Kama ilivyotarajiwa, tayari kampeni zimekumbwa na uhalifu. Yale yale yaliyokuwa yakitokea wakati wa uandikishaji wa wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu, ya watu kuvamiwa na kujeruhiwa kwa mapanga na marungu, yameanza kutokea.

 

Yanatokea hayo, huku mitaani wengine wakipanga kuhujumu raia kwa sababu ya picha za wagombea, kila chama kikidai uhalali wa kubandika za wagombea wake na vingine kujiona ni vyenyewe tu vyenye haki ya picha za wagombea wake kudumu.

 

Zote hizo ni fitna za uchaguzi ulio huru, wa haki na unaotakiwa kufanyika kwa amani na salama. Nchi yetu sote tusisahau, itatusuta.

 

Kama vile haitoshi, kwenye majukwaa ya kampeni, kumeanza visa pia. Wanasiasa wanatumia fursa hiyo adhimu ya kusikilizwa na watu, kulipua mabomu bila ya sababu za msingi. Wapo wapotoshaji wa mambo, wadanganyaji watu na watoa kauli za kutisha watu.

 

Cha kushangaza ni kwamba hayo yanafanyika wakati vyama vinavyoshiriki uchaguzi, vimetia saini makubaliano yanayoitwa maadili au misingi mahsusi kwa lengo la kuhakikisha hatua iliyobaki ya kuelekea upigaji kura ikianzia na kampeni inafanyika kwa utulivu na heshima na hatimaye Zanzibar inapata viongozi watakaokuwa na thubutu ya kujitapa kuwa wametokana na uchaguzi madhubuti.

 

Zanzibar ipate chama madhubuti kitakachounda Serikali imara na itakayokuwa Serikali ya watu, kwa ajili ya watu na kwa manufaa au maslahi ya watu. Serikali itakayoongoza watu si kutawala watu, itakayojali haki za kila raia na kila sehemu ya jamii kwa usawa na bila ya kutumia ubaguzi wa aina yoyote ile. Nchi inahitaji Serikali madhubuti itakayoheshimu haki za binadamu na itakayokuwa mfano wa utawala bora na utawala wa sheria. Kila mtu atumikie sheria siyo mwingine au kundi fulani liwe juu yake.

 

Hali inaonyesha nchi inapita katika kipindi kigumu kweli. Kipindi kigumu kwa sababu wakati huu tunapaswa kufikiria maendeleo yetu mtu mmoja mmoja na ya nchi kwa jumla. Hata hivyo, baadhi yetu tungali na mawazo ya umimi na mtizamo wa kuwa watu fulani tu ndio halali wa kuongoza nchi na wengine, wao ni watizamaji tu.

 

Tunaposema vyama vimekubaliana kuendesha kampeni za kistaarabu na zinazojali msingi wa utaifa wa nchi yetu, vipo vyama vinavyoamini kwamba tungali katika zama za kutiliana fitna kwa kutajana majina mabaya majukwaani. Mwanasiasa anatumia sehemu kubwa ya muda jukwaani kwa kutoa maelezo yanayolenga mtu katika namna ya kumchonganisha na umma. Dalili ya kukosa hoja?

 

Muflis kwa sababu anafahamu fika anachotakiwa kukizungumzia ni sera za chama chake na vile zitakavyotumika kubadilisha hali ya maisha ya Wazanzibari na nchi yao (kwa maana ya ustawi zaidi) katika nyanja za kiuchumi na huduma za kijamii. Hilo ni kwa chama kinachoomba ridhaa ya kuongoza kwa mara ya kwanza.

 

Kwa chama kinachotawala, chenye kuongoza watu tayari na kinachoshindana ili kibaki kwenye madaraka hayo, kinapaswa kueleza kimepiga hatua gani kutimiza mambo hayo kwa mujibu wa vile kilivyoahidi wananchi katika Ilani yake ya uchaguzi uliopita, wapi kilikosea na wapi kinakusudia kupaimarisha ili kuonyesha uwajibikaji kwao. Chama hiki ndicho kinakuwa na changamoto zaidi kwa sababu kuna vipimo vingi kwake kukionyesha kama ni kina dhamira ya kweli ya kujenga nchi na wananchi wake.

 

Kipo madarakani, na kwa sababu tunazungumzia Chama cha Mapinduzi (CCM), kule kuwa kwake kwenye utawala wa nchi kwa miaka 41 ni nafasi nzuri ya kujilabu lakini kwa hoja zinazoendana na uhalisia wa mambo. Kila kitu kinaonekana. Kama Serikali ya CCM imekifanya hakuna haja ya malumbano, kinaonekana. Nimepata kusema kama maendeleo yanaonekana hakuna sababu ya kupigiwa debe kwa sababu kila mtu anayaona.

 

Kama ni barabara imejengwa, kila mtu anaiona, kama tangi la maji linaonekana, kama ni skuli na vifaa vya kisasa kulingana na wakati tulionao wa sayansi na teknolojia, vilevile. Kama ni kituo cha afya au hospitali na uhakika wa dawa na umadhubuti wa madaktari na wafanyakazi wengine ni sawa, kama uwanja wa ndege na vifaa vyake, au uwanja wa michezo, vyote vinaonekana si vipo?

 

Katika kueleza mafanikio ya Serikali inayoomba ridhaa ya wananchi, ilitarajiwa hicho kuwa ni kitu rahisi kisichohitaji kuitisha mkutano na kuchukua watu kutoka kisiwa kimoja na kuwapeleka kisiwa kingine. Kule uendako kuna watu na kama wamesaidiwa katika jitihada za kuondokana na umasikini wa kipato, umasikini wa miundombinu, watamsikia muombaji kura. Hakuhitajiki mzo wa bunduki kuhutubia watu hawa.

 

Basi ingetarajiwa kampeni za uchaguzi zingeanza vizuri kwa sababu tunapaswa kuamini kuwa kila chama kina nia thabiti ya kutaka uongozi wa nchi kwa maslahi ya umma si maslahi ya taifa. Chama kinataka ridhaa ili kiwatendee watu yale wanayoyataraji siyo yale yanayotarajiwa na chama chenyewe.

 

Ilani ya uchaguzi ya chama inatakiwa kutizama mahitaji ya jamii kulingana na mazingira wanayoishi. Umma wa Wazanzibari hauhitaji sera za njozi bali thabiti zitakazowezesha watu kutoka katika balaa la umasikini, ujinga na maradhi. Watu wanahitaji sera makini za kuwapatia makaazi bora, maji safi na salama, kupata uwezo wa kununua wanachokitaka.

 

Lakini unaweza kuwa na sera nzuri zikashindwa kutekelezeka kwa sababu tunakosa umadhubuti katika viongozi. Wakiwa legelege watatoa Serikali legelege na hatimaye, mipango legelege na huduma legelege. Ilani inatakiwa kutandika misingi ya kuijenga upya nchi iliyovurugika kutokana na mifarakano isiyokwisha. Panataka tafakuri Zanzibar ipo wapi; kwenye umoja madhubuti au mgawanyiko wa aibu? Ilani itizame hapa na kuendeleza umoja uliopo, si hivyo ijenge msingi wa kuunganisha watu waliofarakana. Ilani ya uchaguzi ni muongozo wa chama kuipeleka nchi kwenye neema si kuzidi kuitia katika shida.

 

Haya ndiyo mambo muhimu ya kuzingatiwa na vyama vya siasa vinavyojitayarisha kuchukua hatamu ya kuongoza nchi. Safari hii tunavyo sita vyama namna hii. Hivi ni vyama vilivyosimamisha wagombea urais wa Zanzibar.

 

CCM, chama tawala, kimemsimamisha Amani Abeid Karume; Chama cha Wananchi (CUF) kinaye Seif Shariff Hamad; Democratic Party (DP) yupo Abdalla Ali Abdalla; Jahazi Asilia wao ni Haji Mussa Kitole; National Reconstruction Alliance (NRA) wanaye Simai Abdulrahman Abdalla na Sauti ya Umma (SAU) wamempa dhamana Mariam Ahmed Omar, mwanamke pekee.

 

Nilieleza awali kwamba kampeni ya fitna, uzandiki na vitisho imeanza. Kama vile hatujajifunza kitu muda wote tangu tuanze hatua ya uchaguzi. Tunaendelea kushuhudia vitisho si tu kwa wanasiasa wanaogombania, bali kwa raia wasio na hatia. Tunashuhudia umma wa Wazanzibari ukilazimishwa kuishi katika hofu kuu.

 

Wanasiasa wanapotaka kukisema kitu lakini wanajua kuna ukuta unawazuia, hutafuta njia ya kusema wakianzia na maneno ya kuonyesha hawana nia mbaya ya kuruka ukuta ule. Nami sikusudii kufanya kampeni ya kumtakia yeyote kati ya hao wagombea sita au vyama vyao kushika dola. Umma unajua unachohitaji. Langu ni masikitiko ya namna mambo yanavyokwenda.

 

Tunacho chama dola tunachotaraji kiwe mbele katika kuheshimu yale maadili na misingi ya uchaguzi huru, wa haki na katika mazingira ya amani na salama. Mbona hali haiendi hivyo? Mbona kuna wingu na hivyo giza nene la kufika huko tutakako? Tupo kwelini au tunadanganya? Hatudanganyi tunajidanganya tukidhani hatuonekani. Tuko wazi kila kitu kinaonekana.

 

Picha tu za wagombea inakuwa nongwa kuzivumilia? Watu wazima wanapanga namna ya kuharibu picha za wagombea. Kama vile hawana kazi ya kufanya, wanajadili namna ya kubomoa picha za wenzao. Wanajadili namna ya kuziharibu halafu kutafuta wachawi. Mtu mzima anamwambia aliyekutwa anatoa picha za wagombea bila ruhusa akabadili maneno. Eti aseme alitishiwa kuuawa kwa kisu. Kwani zikiwepo picha za wagombea wote sehemu, ndio wa kushinda atashindwa? Mgombea hashindi kwa uzuri wake, bali anavyoutizama umma kama binadamu?

 

Watu wazima wanapanga namna ya kuvuruga mkutano wa mpinzani wake. Mkutano wa kampeni kwa ajili ya kuomba kura unapangiwa njama uvurugike, bado mwanasiasa anajitokeza na kutamba jukwaani yu katika chama kinacholea demokrasia. Demokrasia gani ya kuharibu mkutano wa kampeni. Demokrasia inahimiza uvumilivu kutokana na kukubali hali halisi ya mambo. Kuvuruga mkutano kwa kutumia watoto wanaochipukia, ndio uvumilivu?

 

Bado hatujajifunza kitu miaka 13 ndani ya mfumo wa vyama vingi. Uvumilivu ni neno muhimu la kutiwa akilini mwa kila mtu, awe kiongozi wa chama au mwanachama, awe raia tu asiye chama cha kukipenda. Uvumilivu unapoondoka akilini, kinachofuata ni hamasa na hatimaye uhuni.

 

Inakuaje mtu na akili yake amfundishe mwingine kuchukua jiwe, kubeba nondo au rungu lilovishwa misumari na kuagiza uharamia dhidi ya raia. Upunguani wa hali ya juu katika nchi yenye historia kubwa ya ustaarabu na upendo miongoni mwa watu wake. Ndani ya jamii ya watu wanaoishi tangu zama wakipendana na kuelewana licha ya kutofautiana kidini na kiasili, wachochewe kuvurugana.

 

Watu waliumizwa vya kutosha 2001, wameumizwa vya kutosha ndani ya utekelezaji wa Muafaka uliozaliwa kutokana na maumizaji yale. Watu wameumizwa wakati uandikishaji ukiendelea vituoni, watu waliuawa kinyama kwa mtutu na visu. Mali za watu zilihujumiwa wengine hawajasimama tena kibiashara, wazee kwa vijana walitiwa kwenye mitihani kimaisha na wahuni. Haijatosha tu? Aibu na ajabu.

 

Zanzibar lazima turudi kwenye mstari. Kila mtu arudi. Ajiweke nafasi ya kuwa miongoni mwa wale walioongoka si katika wale aliowaghadhibikia Mola. Tumeumbwa kupendana na kusaidiana si kuhujumiana. Kama tuhujumiane tofauti yetu na wanyama mwitu iko wapi? Tunakubali madaraka ni matamu, lakini gharama ya kuyahakikisha ndio iwe kuhujumiana? Kwa kumtusi mwenzio, kwa kumchonganisha, kumharibia jina mwenzio, kwa kusema ya nyumbani kwake, kwa kutumia historia kummaliza? Ni upotoshaji usio na sababu wala tija.

 

Ningekuwa mimi ningezungumza mazuri matupu niliyoyafanya bila ya kusahau kueleza kasoro kwa sababu zinajulikana kuwa zilinisaidia kukwamisha azma ya kuiletea jamii neema. Kasoro ni kupotea njia ambako ni kujua njia, maana zimenifunza namna ya kubadilika na leo nina ari mpya na nguvu mpya lakini ndani ya fikra mpya na kwa hakika za kileo si za kale za mwaka 47. Leo nitende mambo kwa ustadi zaidi kwenda na teknolojia.

 

Hii ndiyo kuungama, nasi tunapaswa kuungama kwa kutoukiuka ukweli japo unauma. Ni sawa tu kama ulipanda kokwa ya papai, wewe uliye madarakani, na wewe uliye nje unahitaji kuingia ndani, usitaraji kuvuna mbaazi. Zipo hadithi za kokwa ya chungwa kuzaa danzi lakini hiyo ni miujiza si uhalisia. Ni katika Mola kuonyesha yeye ndiye yeye.

 

Tatizo langu siku zote limekuwa ni kuona tuna Serikali iliyosahau majukumu yake kwa umma. Sigusii uchumi wala huduma za jamii, nabaki hapa kwenye usalama wa raia. Ni udhaifu mkubwa wa kiuongozi, unapokuwa na Serikali isiyojali amani ya raia zake. Kujali kuwe kwa vitendo si maneno tu ya amani na utulivu huku raia wengine wanajiona bora kuliko wenzao. Wanachukua rungu na mapanga kupiga wenzao, wanachoma nyumba za raia wenzao, wanahujumu mali za wenzao, na haiwi chochote. Sasa huu si utawala bora wala wa sheria. Huo ni ushahidi wa utawala mbovu. Raia ndiye mchangiaji mapato ya serikali ili iwe kujiendesha, ukimhujumu ndiyo unajenga maisha yake au unambomoa? Ukimbomoa ndio unazalisha mapato?

 

Wagombea tuzungumzie siasa, tuzungumzie sera, tujikite katika masuala ya kujenga nchi na jamii. Tuache fitna majukwaani, tuache uongo na uzandiki, tuache matusi na kejeli, tuache uchonganishi, tuache kumalizana kwa chuki. Tuitumie vizuri historia, tujenge kutokana nayo. Tujenge hoja na tuitie nguvu hoja ili ikubalike. Tusilipue mabomu hayatusaidii.

 

Yote haya yamehimizwa kwenye maadili au misingi mahsusi ya kuleta uchaguzi mzuri ambayo vyama vimesaini. Tuyaheshimu basi kwa maslahi ya umma. Tutimize wajibu wetu kwa umma tunaotaraji kuuongoza kwa kuuletea neema.

Ends.