Waraka Kutoka Unguja

March 17, 2005

By

Jabir Idrissa




Wanaukumbi wenzangu, ifuatayo ni makala ya kila wiki katika gazeti la Rai. kwa kufahamu baadhi yenu hampati nafasi ya kulisoma gazeti hili, nawatilia hii makala mpate kufaidika na yanayotokea kwetu Zanzibar. Ahsanteni.

Jabir idrissa+

Kichwa cha habari: Hivi tuendelee kutiana misukosuko ya maisha hadi lini Z'bar?





Niliahidi wiki iliyopita kutumia safu hii leo kuibana Polisi kama taasisi ya kulinda usalama wa raia na mali zao ikiwemo jukumu kuu la kusimamia utekelezwaji wa sheria za nchi. Ahadi yangu ilitokana na imani ya kuwa taasisi hii imekuwa haitekelezi majukumu yake ipasavyo wakati mwingi.


Imani hii haikuja leo wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, nimekuwa nayo zamani ndio maana huko nyuma taasisi yenyewe iliona makala zangu kupitia gazeti la Mtanzania, na kabla ya kuingia hapo.


Kipimo changu cha utendaji kazi wa taasisi ya Polisi wala hakitumii vigezo vigeni. Ni kutizama tu namna inavyoyachukulia na kuyashughulikia matukio mbalimbali. Kumepata kutokea mauaji ya raia wasio na hatia, wengine ndani ya mamlaka ya taasisi hii lakini hakutolewi maelezo ya kuridhisha, basi huwa nalaumu na kushauri utendaji wa kweli.


Lakini pia nimepata kupima utendaji wa Polisi kwa kutizama inavyoshughulikia matukio yenye mitizamo ya kisiasa, na hususan yanapokuwa yametokea upande huu wa Zanzibar. si jambo geni kwangu kuitia taasisi hii katika mtihani wa kuibana iwajike kikwelikweli kwa kufuata sheria za utendaji wake na za nchi. Iwajibike katika usawa si kwa kubagua matukio.


Nimepata kutamka wazi mara kadhaa kwamba Polisi huwa inajibadili na kuwa sasa taasisi ya kutumikia wanasiasa wa chama tawala badala ya kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu unaohimiza usawa kwa vyama vyote vya siasa. Polisi inajitambulisha kuwa ni taasisi ya kutumika kutekeleza matakwa ya utawala badala ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria. Na hii kutumika kukidhi matakwa ya kisiasa ya chama tawala, CCM, haipatikani mpaka kwanza 'waumizwe' wananchi, viumizwe vyama vya upinzani, waumizwe viongozi wa upinzani.


Niliposema waraka uliopita ya kuwa taasisi hii imedekeza kwa muda mrefu vitendo vya fujo mitaani vinavyofanywa na wakereketwa wa CCM kiasi cha kujiona wako juu ya sheria, nilikuwa nalenga hali inayotokea Zanzibar kipindi hiki. Walimzoesha mbwa kuingia mwilini na sasa anawafuata hadi wanapoingia msikitini.



Fujo tupu mitaani, vurugu haziishi kwenye maeneo wanayokaa zaidi wafuasi wa upinzani. Imeanza kuwa fasheni kwa wiki ya pili kutokea vurugu eneo la Amani penye Ofisi Kuu za CCM Mkoa wa Mjini Magharibi. Kwanini patokee vurugu hapa kama Polisi wanapalinda. Jumapili walikuwemo ndani ya jengo na silaha zao, zitatokeaje vurugu wakiwemo ndani kama si kuishiwa maarifa katika utendaji kazi?


Wala hali hii haiji kwa bahati mbaya. Si bahati mbaya asilani. Kwanini magari mawili ya Polisi yalikaa mbele ya geti kuu la uwanja wa Amaan kabla ya mkutano wa Chama cha Wananchi kumalizika? Wanamlinda nani pale, raia wanaopita au pale ndio wanalinda Ofisi ya CCM, iliyo mita 100 hivi kutoka hapo? Lakini kwanini pale uwanjani wawepo halafu na ndani ya jengo la CCM wawemo tele na silaha nyingi?


Na kwanini suala la vurugu za kisiasa ndani ya Mkoa sasa ziwe ni tukio la kushughulikiwa kihabari na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Makao Makuu ya Polisi Ziwani? Kwanini isiwe Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), George Kizuguto tunayejua ndiye mwenye dhamana ya ulinzi wa raia mkoani? Vurugu hizi ni kubwa kuliko za kusambaratisha biashara za raia wema pale Jua Kali usiku wa manane? Mbona operesheni ile ndiyo ilitia hasara kubwa raia wa nchi hii walioajiri baada ya serikali yao kushindwa kuwajengea uwezo kielimu wakakabili mazingira ya utandawazi?


Kusambaratisha biashara za raia masikini wale ambao hadi leo hawajapatiwa eneo la kufanyia biashara kama vile si raia kitu, ni hasara. Kuvunja maghala ya bidhaa za wafanyabiashara kando ya Soko Kuu la Mwanakwerekwe na kuzitia kwenye magari ya wazi baada ya kuwapiga walinzi, ni hasara nyingine hii.


Hasara iliyowapata wafanyabiashara kwa sababu bidhaa zao ziliibwa na walioendesha operesheni safisha mji na kupelekwa kusikojulikana kwa magari yenye walinzi wa kipolisi na wa vikosi labda vya Valantia au Mgambo, yakianzia kituo cha Polisi Mwanakwerekwe na kuelekea Kwa Mchina, ni kubwa si mchezo. Na bado ilifanikiwa kutokana na mipango iliyoandaliwa na ofisi ya RPC Kizuguto, chini ya mwamvuli wa Baraza la Manispaa la Mji wa Zanzibar. Mbona kazi nzito ile ilifanikiwa isiwe hii ya kujenga mazingira ya kuvuruga akili za watu mitaani mjini Unguja?


Au RPC Kigutuo amekwenda likizo na hakuna ofisa wa kushika nafasi yake kihabari mpaka waandishi tuitwe kwa DCI saa 8 mchana kuelezwa tukio la kihuni lililotokea zaidi ya saa 12 zilizopita. Unaitwa saa nane mchana ili iwe nini? Sisi waandishi bwana tunafanya kazi kwa muda. Au ni makusudi ili tusipate kuwabana wakubwa wa Polisi kutaka ufafanuzi?


Na leo Polisi iite waandishi pale vurugu zinapokuwa na mwelekeo wa kuwa zilipangwa na wenyewe zitokee: zimeandaliwa mapema ili kukidhi matakwa ya wakubwa. Na bado unaambiwa eti hakuna mtu aliyeumia wakati watu kadhaa wamepigwa na kuumia. Hiki ni kitanzi kwa Polisi kama taasisi, na haiwezekani muendelee kukaa nacho. Kitoeni shingoni mfanye kazi zenu kwa ufanisi, msemwe vizuri na wengi si watu nusunusu.


Vurugu zitokeazo kwenye mitaa kwa wiki ya pili sasa ni mpango madhubuti usiokuwa wa bahati mbaya, kwa namna nionavyo. Mpango maridadi uliobuniwa kuzusha hofu miongoni mwa raia hasa wanaodhaniwa hawaipendi CCM. Raia ambao haki zao zinategemea huruma ya mtu si sheria na kanuni. Raia ambao hawana la ukweli wala nini, kwao ni kuonekana waongo tu na watungaji sababu ili ionekane eti wanaonewa.


Wataalamu wa masuala ya kijamii wanaziita vurugu kama hizi state-organized chaos. Watumishi wa umma wanatumwa kubuni na kutekeleza mipango ya kuhujumu baadhi ya raia wema (kwa sababu zao wao, wanawaona adui raia hawa) ili tu kundi fulani au watu aina fulani wapate kutiwa katika msukosuko na vyombo vya dola. Utawaona watumishi hawa baadhi wanakuwa mbele au nyuma wakisimamia utekelezaji wa mipango hii ya hujuma dhidi ya raia wema.


Ikitekelezwa mipango namna hii, wahusika katika utawala wanatumwa kutoa matamko ya kulaani vurugu au matukio ya uharibifu wa mali, nyingine huwa za umma, na utasikia waziwazi wakitaja kwamba chama fulani cha upinzani au wapinzani ndio waliohusika.


Kufahamu zaidi hoja hii, niwakumbushe ya milipuko ya mabomu; nikiita mabomu ya kishetani ambayo mpaka leo ripoti ya uchunguzi wake umma na ulimwengu unaisubiri. Inajulikana matokeo ya uchunguzi ule lakini itolewe wapi wakati hakuna mtuhumiwa aliye nje ya mfumo wa dola? Ndio maana tunaendelea kuisubiri mwezi wa 12 kamili leo.


Natuendelee tu kuisubiri maana labda akina Afande R.M waliopewa kazi ya kuchunguza ikiwemo kutumia mbwa wanusaji, hawajamaliza kazi ya kuiandaa. Haitatokea siku kwa utawala huu tulonao ikatolewa hadharani ripoti ile. Naweza kutia dau la shilingi mia moja, haitoki labda yatokee mabadiliko na wake watu wenye utashi wa kuona demokrasia na utawala wa sheria vinafanya kazi kwa kuonekana si nadharia.


Sisi Waislam tunaamini kazi ya Mwenyezi Mungu haina makosa, akitaka inakua hakuna wa kuzuia asipotaka haiwi hakuna wa kushinikiza, ndio maana hata tunapoomba dua ya kutaka mema, huwa tunategemea ukubalifu wake. Hapa si kama Zuia Uhuru ya miaka ya kabla ya 1963. mtu azuie uhuru lakini si atakayo Mola.


Wengine mnaweza mkawa mnajiuliza "huyu kawa kichaa leo" kwa kuamua kuropokaropoka tu humu, au amechukua hulka za kasuku kutoa maneno aliyolishiwa. Asilani abadani sijapata kulishiwa na siko tayari kwa sababu kichwa changu bado "kinaona mbali" hakihitaji kutengenezewa mada. Wala sijafikia hali ya kuchanganyikiwa na kuhitaji kwenda Kidongochekundu (mfano wa Mirembe kwa walioko Tanzania Bara). Niko fiti.


Kama hamuamini kuna hujuma hupangwa kwa makusudi kwa nia ya kutia baadhi ya raia katika msukosuko, nikupeni ya mwandishi wa vitabu wa Kimarekani, Charles Evers, mwenye asili ya Mississipi. Katika kitabu chake alichokiita Have no Fearkilichochapishwa mwaka 1997 na John Wiley & Sons Incl.; anasema katika ukurasa wa 5-6: niache alivyosema kwa Kiingereza nitatafsiri.


But when the police and the politicians wink at these killings and cover them up - that's worse than violence. That's state-sponsored terrorism. And that was Mississipi in my childhood. Cops killed Negroes all the time and called it justifiable homicide.

(Lakini pale polisi na wanasiasa wanapochekelea mauaji haya na kutoyashughulikia - hiyo ni hatari zaidi kuliko ghasia. Hiyo ni ugaidi uliopangwa na dola. Na hiyo ndiyo Mississipi ya utotoni kwangu. Polisi walikuwa wakiua Waniga (Wamarekani weusi) siku zote na wakihalalisha (mauaji hayo).


Bado hatujashuhudia mauaji tangu yale ya mwanafunzi Juma Omar Juma yaliyotekelezwa na mlinzi wa kidola Disemba 3, mwaka jana Mkoani Pemba, lakini naona hatuko mbali na huko. Kama utawala utaendelea kukubaliwa mambo yake na taasisi ya Polisi tunayoitegemea kwa ulinzi wetu na mali zetu, mauaji haitakuwa jambo lisilowezekana. Tunapoelekea kwenye uandikishaji mkoani Mjini Magharibi penye zaidi ya asilimia 40 ya wapiga kura, makubwa tunayasubiri kutokea.


Ufanyeje utawala wakati Mambo Ni Magumu (MNM)? hata ingekuwa mimi kama sijataka kubadilika na kuwa wa kukubali hali halisi ya mambo, nikiwa niendelee tu kubaki mhafidhina wa kutupwa, lazima nitumie mbinu zote ili kulinda utawala wangu kwa sababu nisipofanya hivyo, jamaa watanikwapua kwenye utawala. Wakishanikwapua pale nitakula wapi wakati pale ndio pekee pananipatia riziki yangu na wanangu na lile kundi dogo la mawakala zangu? Ndio maana nitashikilia kusema nitashinda kwa kishindo kingine na sababu ni moja tu "chama hiki kina watu wanaokiunga mkono."


Itabaki kuonekana kwamba Zanzibar pangali mahali pasipo shwari, bali kila wakati raia zake watiwe katika mtihani wa kuhofia maisha yao kama vile kuishi si haki yao ya msingi. Mohamed Ali Maalim leo anahangaika kujiuliza hivi atamaliza lini kufuatwa na Polisi kila panapotokea hali ya wasiwasi mjini wakati hana kosa. Hajapata kuthibitishwa ni mkosaji wa jinai hata mara moja, licha ya kukamatwa mara kwa mara, lakini bado anafanywa chambo.


Na hafuatwi mchana kweupe, usiku wa manane maana ndipo atapojua kwamba kuna dola inayohitaji kuheshimiwa na kutetemekewa kila wakati. Jamani dola ipi hii inayotia hofu raia kila wakati kama si namna ya utawala utumiao sheria za mwituni? Ndio huendelea kusema lazima ifike wakati tubadilike sote, kila mmoja na kwa ujumla wetu, ili tujenge Zanzibar ya kukaliwa kwa utulivu na watoto zetu. Si hivyo, haya natuendelee kutiana kwenye mitihani ya kimaisha.

Ends.