Waraka Kutoka Unguja
April 1, 2005.
By
Jabir Idrissa
Wanaukumbi, someni makala
hii ya Waraka kutoka Unguja iliyochapishwa katika gazeti la Rai la
Machi 31. Zaidi ni kwa faida ya walio nje ya nchi na wengine walio
mbali na yanakofika magazeti nchini TZ. Mwanaukumbi
mwenzenu, Jabir Idrissa+ Headline
yake: Twasubiri Utawala Bora kweli, Tume yetu uamuzi ni
wao
Kupitia ukurasa huu huu, nimewaletea visa na
vituko vya kupwa na kujaa vinavyohusiana na yanayotokea wakati wa
uandikishaji watu kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK).
Mengine yametokea bila ya kusahau maafa ya kupotea roho za watu, raia
wenzetu wawili, chanzo kikuu cha hayo kikiwa ni utawala wa
mabavu.
Roho ya Juma Omar Juma, mwanafunzi wa
shule ya msingi ya Ng’ombeni Mbuyuni, mjini Mkoani ilikatika ghafla
kwa sababu ya matumizi yasiyo lazima ya nguvu za dola kwa ajili tu ya
kulinda maslahi ya utawala. Alipigwa risasi na askari wa Kikosi cha
KMKM aliyekwenda na wenzake kituo cha uandikishaji wapiga kura kwa
nia ya kuzuia upinzani wa wenyeji wa eneo la Mkoani waliosimama
kidete kuzuia wageni kuandikwa hapo.
Roho ya
pili ni ya Kamanda wa Valantia Pemba, Mohamed Suleiman aliyeuawa kwa
kuchomwa kisu kifuani usiuku wakati akitoka nyumbani kwake kwenda
Msikiti wa Chachani mjini Chake Chake kushiriki sala ya Isha. Wengi
wanakihusisha kifo chake na masuala ya uandikishaji kwa vile kikosi
anachokiongoza, KVZ, ni moja ya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, vinavyotumiwa kuvuruga daftari. Uvurugaji ninaousema hapa
ni ule unaotekelezwa kwa mtindo wa kuhamisha huku na kule askari wa
vikosi hivyo kwa madhumuni ya uchaguzi tu.
Kwa
bahati mbaya (sana) kwa sababu ya kutojali haki za raia na
kutozingatia misingi ya utawala wa sheria kwa vitendo, muuaji wa Juma
hajabanwa pamoja na kujulikana. Hapo hapo, watu saba walikamatwa
wakihusishwa na kifo cha Kamanda Mohamed, akiwemo muathirika wa
matumizi ya dawa za kulevya, mwenyeji wa mjini Unguja. Walikamatwa
kivarange tu na labda miujiza itawatia hatiani. Wangali wakisota
gerezani Wete tangu walipokamatwa Disemba 5.
Tunazungumzia
utawala wa sheria wa vitendo si nadharia. Serikali inayofuata utawala
wa sheria inajionyesha si kwa kelele na viongozi kujinasibu kwenye
viriri. Utawala wa sheria au utawala bora ni kutenda haki kwa kila
raia hata pale serikali ikibidi kuumia. Askari waliomuua aliyekuwa
Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini, Kanali Imran Kombe na ushahidi
ulipothibiti wakatiwa hatiani na serikali kutakiwa kulipa mamilioni
ya fidia, ndio malipo ya haki ya kutoheshimu sheria. Na Serikali
haina isipokuwa kulipa tu wakati ukifika. Hii ndio utawala wa
sheria.
Yetu ina mwaka wa ngapi inashindwa
kumsaidia Mzee Abdalla Shariff wa Shakani haki aliyopewa na Mahakama?
Kuondolewa kwa wavamizi wa ardhi anayoimiliki kisheria kunahitaji
kupeleka vifaru vya jeshi si wanaoitwa FFU ambao huenda na kunusa
wavunja sheria; watoto na wanawake wenye bakora, na kupindisha gari
wakirudi kituoni kamanda wao akisema “du mnaona moto ule na silaha
walizokamata.” Aibu tupu kwa Polisi wanotumwa kila baya.
Leo
tuna raia wangapi vituoni waliokamatwa siku kadhaa nyuma bila ya
kusomewa mashitaka mahakamani. Saa 48 za kisheria zimefutwa? Inakuaje
Polisi inavunja nyumba ya raia asiye na silaha usiku wa manane na
kumfungulia kesi ya uzembe na ukorofi kwa kumkuta na panga au kisu au
shoka au mtaimbo? Mzanzibari bila kisu, panga, mtaimbo, shoka, mkuki,
jembe na nyundo? Na waliogawa mapanga mchana kweupe huku mawaziri wa
SMZ wakichekelea; wanaouza zana hizi za kazi mpaka chini ya miguu ya
wapita njia mjini; na ile dhana ya kuwa Zanzibar ni nchi ya wakulima
na wakwezi? Itakuwa imekufa kwa sababu awaje mkulima au mkwezi bila
ya kisu au panga? Awaje mkulima wa maweni bila mndu, mtaimbo na
mkuki?
Utawala bora huku magazeti yanayoikosoa
serikali yanafungwa na waandishi wake kujengewa chuki? Bali
yanayochonganisha watu yanaishi baada ya kupewa leseni haraka haraka.
Leo Zanzibar si sheria, mtu azitegemee kumlinda na au kupata haki
bali mapenzi ya mtu. Si elimu na maarifa inayompatia kijana kazi,
bali ukereketwa. Mpemba leo si mali kitu ila karafuu zake? Leo
tunafundisha vijana uharamia halafu twasema tuna utawala bora na
kwamba utawala bora hauji miaka minne. Waja hata kwa miwili, dhamira
tu!
Hatujaufikia wala hatuufikii kwa hata miaka
100 kwa mtindo huu uliojaa utani wa nguvu. Tutaendelea nao utawala wa
mabavu na ushetani iwapo wenye hatamu za uongozi wa Serikali hawataki
kuwa mfano katika ufuataji sheria bali kulalamikia wapinzani tu hata
pasipo sababu ya kweli.
Changamoto iliyobaki kwa
Rais Amani Abeid Karume kuthibitisha kama anaongoza serikali
inayoheshimu sheria ni kuchukua hatua ya kumvua sare askari wa KMKM
aliyemuua Juma, afunguliwe mashitaka kwa kuwa upo uhakika ndiye
aliyehusika na yule ofisa aliyeamuru Juma atwangwe risasi naye
awajibishwe kwa kukiuka sheria hata za uaskari. Si zipo sheria za
wakati na mtu gani wa kufaa hupigwa risasi ya kumuua? Kama hilo ni
gumu kama la mtu kujua lini atakufa, basi na wale watu saba wanaosota
gerezani waachiwe.
Kama yote hayafanyiki, iko
siku muuaji wa Juma na wengine wasiokuwa na hatia, watalipa damu na
roho za Muumba, na wale watu saba watajadai haki yao wasipothibitika
kuhusika kumuua Kamanda Mohamed.
Hawataki bado
watawala kukubali hali halisi; kuamini ya juzi si ya jana na hata ya
jana si ya leo tena mwiko kwao. Ni kazi yetu kuzidi kuwapigia
baragumu ya kuwa kwa tulipo leo, haiwezekani kurudi nyuma tukaishi
kama walivyoishi babu na bibi au baba na mama zetu miaka ya khamsini
na sitini. Watambue na lazima wafike mahali wajue hasa kama ya leo ni
ya leo hayawezi kulingana na ya juzi na jana. Leo tunazungumzia
ubinafsishaji, tuna utawala bora, tuna utandawazi.
Hata
kipindi hiki tu cha kitimtim cha Chama tawala kutafuta wagombea
urais, tunapata misamiati mipya tusiyopata kuisikia kipindi kama hiki
mwaka 1995 wala 2000. Tuna uendelezaji wa mafanikio ya Serikali ya
CCM kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Ni sauti ya mabadiliko ya
kumridhisha binadamu Mtanzania kwa mahitaji muhimu ya kimaisha. Ndio
kupea kwa binadamu. Binadamu wa yale mafuvu yanayogunduliwa leo, si
tuliyepo leo, ni tofauti kwa mengi.
Lililo bora
ni kutafuta yatakayotusogeza mbele na kuwa sambamba na mataifa yenye
dhamira za dhati kuendeleza watu wao, yenye kujenga misingi ya kweli
ya uongozi yenye maslahi na nchi na watu wake, uendeshaji
unaozingatia umuhimu wa raia kwanza ndipo mgeni, uendeshaji unaojali
haki na usawa wa watu bila ya ubaguzi kwa rangi, kabila au dini. Tu
katika zama inayohitaji uendeshaji wa nchi unaoshirikisha kila raia
hata aliye nje ya serikali na nje ya nchi muradi ni raia
mwenzetu.
Tunasema tena kwamba dunia ingali
kubwa kama zamani lakini leo kumeongezeka kitu kwayo; dunia i kama
kijiji kutokana na maingiliano ya watu na mataifa yaliyowezeshwa na
kasi ya ajabu ya ukuaji wa sayansi na teknolojia. Leo watu wanasafiri
juu angani kuchunguza kuna nini. Wanashinda na kula mwezini kama vile
mungu hayuko tena kumbe sivyo. Ni ujanja wa kisomi wa watu kutaka
kuweka rekodi za mafanikio ya kitaaluma badala ya kushinda kwa babu
kutafuta madaraka na vyeo. Kwenda kwa mganga leo kutafuta cheo?
Lakini tutafika lazima tupate mabadiliko ya kujenga nchi zetu.
Na
katika yote hayo, ukweli na uwazi ni msingi. Hata katika siasa, kama
fani, lazima washiriki wawe wakweli; na kuwa mkweli kunaanza kwa mtu
na nafsi yake kabla ya kutoka nje. Siasa za kileo si za kale katika
vigezo vingi na lazima nasi tuingie na tuogelee hasa kwa sababu
hatuwezi kuishi kwa kujitenga.
Sote tunakumbuka
uandikishaji ulianza Novemba 29 katika Mkoa wa Kusini Pemba na kwamba
keshokutwa Mkoa wa Mjini Magharibi unaanza. Mkoa huu, kama ilivyokuwa
jiji la Baghdad wakati wa vita vya kusaka silaha za maangamizi nchini
Irak, ndio mama wa vita vyote. Takwimu zinabainisha kwamba una
asilimia inayozidi 42 ya kura zote za Zanzibar. Kwa hivyo kila chama
kinautegemea kwa mavuno.
Bado kauli ya
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mjini, Borafia Mtumwa Silima ya kuzuia
wenye wa Pemba kuandikisha kura wilayani kwake haijafutwa, na tunaona
mikakati ya kutekeleza amri yake inavyofanywa. Tuna Operesheni
Dondola ya Polisi. Makumi ya wenzetu wako na Polisi hivi
tunavyozungumza wakisubiri huruma ya dola kurudi makwao na
kuhangaikia riziki. Wanasubiri huruma ya dola maana wengi wao
wamekutwa na visu au mapanga yakiwemo yaliyoota kutu kwa kutotumika
kwa miaka, wamekutwa na jembe au nyundo, wamekutwa na mtaimbo au
mkuki na shoka.
Wamekutwa na zana hizi za
mkulima na mkwezi. Kosa la jinai leo Zanzibar kukuta mtu ana kisu
nyumbani kwake. Uhuni mkubwa kiasi cha masheha sasa kulindwa usiku
kucha. Wanalindwa kwa sababu wamesababisha chuki dhidi ya raia badala
ya kuwasaidia kuendesha maisha yao na kuipunguzia serikali mzigo wa
kuondoa umasikini.
Tu katika nchi ambayo japo
mfumo wa vyama vingi ni ruhusa ya kikatiba, kutokuwa mfuasi wa CCM ni
kosa la jinai, unakamatwa, unatiwa katika mtihani, anachukuliwa mkeo
kama mtekwa nyara mpaka mume upige ripoti kituoni. Siku moja tu mume
kuondoka nyumbani shida je wiki anayotiwa korokoroni, nani analisha
watoto zake? Serikali inapunguzia raia zake umasikini? Mashudu!!!
Inawaongezea. Wengine zamu zetu hazijafika tutakamatwa tu na
kufunguliwa kesi za kuteka nyara wanawake kama ilivyokuwa mwaka 2000.
Mwandishi ameteka nyara mwanamke? Salam zako Ally A. Saleh wa
BBC.
Siondoki kabla ya kuigusa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC) chini ya uongozi adhimu wa Mwenyekiti Masauni Yussuf
Masauni. Khadithi ya takwimu za tume kwa wanaoandikishwa kuingia
katika DKWK la Zanzibar. Vituko na hila ambazo wenyewe wanasema
kulalamikia ni kukurupuka maana bado kazi ya kuzifanyia kazi
haijesha. Tume haijasema nini kinasubiriwa hadi leo kubandika orodha
za majina ya walioandikishwa hata yale ya Mkoa wa Kusini Pemba, miezi
mitano tangu uandikishaji umalizike.
Na kama
hata za miezi mitano hazijabandikwa, hizi zilizomaliza mwezi uliopita
na zinazoanza keshokutwa zitaja bandikwa lini? Tuelezwe labda
inasubiriwa mpaka mwisho wa uandikishaji ndio takwimu za nchi nzima
zibandikwe kwa pamoja, pingamizi zitolewe kwa pamoja nchi nzima, na
mahakama zishughulishwe kwa pamoja nchi nzima. Kwa hapa ndipo
tutapata takwimu sahihi za kuzitegemea kuingizwa kwenye buku. Mhh ni
ngumu!!
Watu wanalalamikia takwimu kwa sababu
haziendi na hali halisi. Hazifungamani wala hazitengamani. Ni maji ya
ziwa na bahari, ya tofauti ingawa yote ni maji; ya bahari yatakuwa na
chumvi hata iweje kwa sababu ndio asili yake. Wataalamu wa takwimu
wanasema penye watu 100 wa kutosha kuwa watu wazima wa umri unaozidi
miaka 18, kwa kulingana na hesabu ya ukuaji wa idadi ya watu, basi
watu angalau 50 ndio wapite umri huo. Inapokuwa watu 60 na ushei
haieleweki.
Mfumo wa takwimu ndivyo ulivyo.
Zisipoendana hazifichi zitajionyesha, zitajidhihirisha hasa pale
tunapoambiwa makisio ya Tume yametokana na takwimu za Sensa ya Watu
ya 2002. Hebu tuangalie hapa. Katika kituo cha Skuli ya Cheju,
makisio ya watu kuandikishwa ni 971, wameandikishwa 1,163 (asilimia
119); wametoka wapi watu 192 na Cheju si kijiji cha wavuvi kwamba
ilipopita Sensa walikuwa dago. Kiuto cha Dungabweni makisio ni watu
1,520 walioandikishwa ni 2,106 (asilimia 139); wametoka wapi watu 586
napo si kijiji cha wavuvi; Skuli ya Jendele makisio ni watu 907
walioandikishwa ni 1,386 (asilimia 153); wametoka wapi 479 na Jendele
si kijiji cha wavuvi kama ilivyo Marumbi walikozidi watu 315 kutoka
makisio ya 561 (asilimia 156), bali wakulima wa mpunga ambao itakuwa
walinakiliwa Sensa ilipopita maana waliamka kwao.
Lakini
hata kwenye vijiji vya wavuvi kama Pongwe, Michamvi, Uroa,
Ukongoroni, Bwejuu, Paje, Jambiani na kwingineko, baadhi yake takwimu
zimepungua isivyo kawaida na kwingine zimezidi pia huku katika baadhi
ya sehemu hizo kukiwa na malalamiko mengi ya watu kukataliwa
kuandikishwa kwa amri za masheha. Mfano halisi ni Michamvi: makisio
ni kuandikishwa watu 750 lakini wameandikishwa 602 (asilimia 80),
watu 148 wako dago hawakuandikisha? Kijiji cha Pongwe makisio ni watu
318 walioandikishwa ni 912 (asilimia 287); watu 594 walikuwa dago
wakati wa Sensa?
Hebu tuchukue namna nyingine:
Kituo cha Skuli ya Machui; makisio ni watu 696, walioandikishwa ni
1,060 (152); watu 364 wametoka wapi na hiki ni kijiji cha wakulima?
Skuli ya Ubago makisio ni watu 441, walioandikishwa ni 1,402
(asilimia 318); ziada ya watu 961 imetoka wapi? Skuli ya Kiboje
makisio ni watu 693 walioandikishwa ni 923 (asilimia 133); hawa 230
wa ziada wametoka wapi? Skuli ya Uzini makisio ni watu 561
walioandikishwa ni 914 (asilimia 163), hawa wametoka wapi? Umbuji
makisio ni watu 766 walioandikishwa ni 952 (asilimia 124), wametoka
wapi 186? Pagali makisio ni watu 363 walioandikishwa ni 890 (asilimia
245), watu 530 wametoka wapi? Bambi makisio ni watu 1,336
walioandikishwa ni 2,125 (asilimia 159); ziada ya watu 789 imetoka
wapi?
Vyote hivyo ni vijiji vya wakulima
wanaoamkia nyumbani kwenda shambani hivyo Sensa iliwakuta. Sasa uwapi
uhalali wa ziada ya watu iliyofikia hata zaidi ya nusu ya makisio? Na
hizi tunabaini ni sehemu ambako watu wengi walipandikizwa wakiwemo
vijana wa makambi ya CCM na watu wasiokuwa na sifa wakiwemo watoto
waliokuwa wakipelekwa vituoni kwa magari. Hayo ni maeneo yenye ufuasi
mkubwa wa CCM hivyo kuingiza wageni ni rahisi. Panya ajitawala pasipo
paka!
Vipo vijiji idadi haikufikiwa kwa sababu
wengi wa wenyeji walikataliwa kwa kuaminika ni wafuasi wa upinzani.
Mfano Michamvi walikoandikisha asilimia 80 tu. Zipo taarifa kwamba
Katibu wa Jimbo wa CUF alipigwa na vyombo vya dola kiasi cha kuumizwa
vibaya kwa sababu ya kusimama kidete kulinda haki. Chwaka
waliandikisha asilimia 90, Mwera Pongwe asilimia 83, Mwera
waliandikisha asilimia 81, Pete waliandikisha asilimia 82 na hususan
Bwejuu waliandikisha watu 1,738 kutoka makisio ya watu 2,392
(asilimia 73). Bwejuu, Wilaya ya Kusini, kama ilivyo Ndijani, Wilaya
ya Kati walikoandikisha asilimia 88, ni watu kama Naila Majid Jidawi
tu wenye ubavu ndio walifanikiwa kuandikisha.
Tutizame
kidogo kituo cha Kitogani: makisio ni kuandikisha watu 543,
wameandikisha 1,073 (asilimia 198). Hapa kuna kambi ya Kikosi cha
Zimamoto, pitio kuu la wasiohusika kama zilivyo kambi nyingine za
vikosi vya ulinzi.
Hii ndio picha inayopatikana
kutokana na takwimu zilizotolewa na Tume baada ya uandikishaji wapiga
kura Mkoa wa Kusini Unguja. Zinapingwa inakuwa nongwa, wapingaji
wanaambiwa hawana cha maana bali kuleta vichekesho tu. “Unaonekana
hukuwa na la kulieleza katika barua yako, badala yake umekuwa
ukifanya vichekesho tu” ni majibu katika barua ya Mwenyekiti
Masauni akimjibu Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad, mgombea
pekee wa chama hicho kwa nafasi ya urais Zanzibar. anaambiwa
amekurupuka angesubiri uchunguzi kwanza. Malalamiko yanatolewa majibu
yanachefua (si hapo tu ndio mtindo wa Tume barua zake nyingi za
majibu kwa viongozi wa upinzani zina lugha mbaya ajabu kama si wadau
wa uchaguzi) je yasipotolewa kutakuwa na uchunguzi wa kweli? Wamesema
takwimu za Tume zinaisuta. Tunaiona changamoto kubwa inayo taasisi
hii kujisafisha.
Ends.