Waraka Kutoka Unguja
April 21, 2005
By
Jabir Idrissa
Nilisahau kuwatilia waraka wa wiki ilopita. upitieni huu leo ili
kesho, niwatilie waraka wa wiki hii inokwisha ambao tayari
umechapishwa katika Rai. Naamini itawasaidia mlio mbali na magazeti
ya Tanzania kujua yanayotokea kwetu Z'bar. Karibuni.
Jabir
Idrissa+
Headline: Hadithi ya Kinuni, ya Maalim ushahidi
wa aibu Z'bar
Waraka kutoka unguja
"Heko,"
wanasema wacheza bao pale mshindani anapogusa mtaji au kutakasha
vizuri. Katika uandikishaji unaoendelea Mkoa wa Mjini Magharibi
kumekuwa na heko nyingi lakini hizi si za kucheza au kutakasha
vizuri, ni za matatizo yaliyozidi kipimo na kuonyesha wenye mamlaka
wasivyotaka mabadiliko.
Wanaona muda wa mabadiliko
haujafika hivyo wangali na haki ya kucheza shere na kuonyesha vitimbi
na manyanyaso kwa raia wema kila waipatapo nafasi. Si lazima wafanye
kwa mikono yao na huwa hawafanyi wao, bali hutumia mawakala wao. Basi
mtandao wa wenye mamlaka unapita kila mahali. Umejaa tele ndani ya
mfumo wa utendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Itakuwa
unajiuliza kwamba hivi chama tawala kinaweza kuwa ndicho
kinachoshajiisha shere na vitimbi wakati huu? Mbona chao ni chama
kilichosaini Muafaka na Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 2001 na
kukubaliana kuendesha siasa bila fujo bali taratibu na misingi ya
siasa za kidemokrasia ndiyo ya kuzingatia? Kwamba yale maafa
yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa 1995 na 2000 yatoshe kuwa ni
fundisho la ubaya wa siasa za chuki na fujo na huwa si jawabu ya
migogoro ya kisiasa.
Vyama vimekubaliana ndio, lakini
kukubaliana ni jambo moja na kuheshimu na kutekeleza makubaliano
yenyewe ni jambo jingine. Hali inavyokwenda ni ushahidi wa kuwa wenye
mamlaka hawajakubali kidhati Muafaka japo ndio wa mbele kulaumu
wapinzani wao. Katika makubaliano yanayohusisha chama chenye dhamana
ya Dola (nchi), ndicho kinachokuwa na wajibu mkubwa zaidi kwa sababu
kinashika taasisi za kidola zilizo muhimu katika ufanikishaji masuala
mbalimbali ya kinchi: ndicho chama chenye mamlaka ya uongozi wa nchi.
Unapoona viongozi wake wanaratibu mipango ya kupeleka
wapiga kura bandia (bandia kwa maana ya kutokuwa na haki ya
kuandikishwa humo wanapopelekwa) vituoni ili waandikishwe kuja kupiga
kura, magari yao na hata ya Serikali yakitumika, unapata picha gani?
Hivi hawa ndo wamekubali kidhati Muafaka, wanauheshimu kuwa ni njia
ya kuondokana na migogoro, na wanausimamia ili kuhakikisha
unatekelezwa kwa vitendo si maneno matupu? Hali inaonyesha dhahiri
hawajakubali na hawauheshimu Muafaka kama tutakavyoendelea kuona
mbele.
Wenye mamlaka kwa hakika hawajatulia kwa sababu
hawataki nchi iende mbele katika namna ambayo kila mwananchi, bila ya
kumbagua yeyote kwa namna yoyote ile, anaguswa na mafanikio yake,
bali ile tu kwamba wao tu ndio waguswe na mafanikio hayo ndiyo
dhamira yao wanayotaka iendelee hivyo. Maana yake wao, wanajiona,
wana haki zaidi ya wengine na ni sahihi basi hao wengine kuwaamulia
kila kitu. Hakuna haki, uhuru wala nini kwa wengine bali wao tu peke
yao. Zanzibar ni yao tu wao na wawatakao. Haiwezekani.
Haiwezekani
kwa sababu nchi ni ya wote waliomo ndani yake hata wageni. Wana haki
zao kwa mujibu wa sheria na Katiba. Serikali na vyombo vyake
wanapaswa kuzisimamia zipatikane, nao walindwe na mali zao. Na hii
ndio kazi na jukumu kuu la Jeshi la Polisi. Ndiyo maana tunasema hata
ile Operesheni Dondola ya IGP Omari Mahita, ilitakiwa itekelezwe
katika misingi ya kuheshimu jukumu hilo, si kupalilia fujo kwa
kusindikiza vijana wa kiharamia na kuachia wapige watu vituoni na
majumbani mwao. Na bado wanaokamatwa kwa matukio hayo ni wanaoonekana
si wapenzi na makada wa CCM tu. Wafuasi wa CCM safi sana!
Chama
kinachojiheshimu hakiwezi kuachia viongozi wake hata iwe wa ngazi
gani waratibu mipango ya kuvuruga masuala muhimu ya kutekeleza
demokrasia kama hili la uandikishaji. Viongozi wa CCM si wanyama bali
binadamu kama tulivyo wengine. Wanafahamika na maana wanaishi mitaani
kama wanavyoishi wengine, wana jirani wana ndugu wana jamaa zao.
Unapowakuta wanaratibu mipango ya hujuma kwa raia walio vituoni
lazima ushangae. Lakini kwa muda mrefu, wananchi hawawashangai tena
kwa sababu imekuwa tabia.
Katibu wa moja ya wilaya za
Mkoa wa Mjini Magharibi, aliongoza wenzake na kufika kituo cha
kujiandikisha wapiga kura cha Kinuni, Jimbo la Mwera, nyuma yao liko
kundi kubwa la vijana. Wakawatenga kando wasiingie eneo la kituo ila
wachache mno. Wakafanya mawasiliano, na ghafla hali ya kituo
ikabadilia. Viongozi wa upinzani waliokuwa waangalizi hapo
wakamkabili msimamizi wa kituo. Alisikiliza hofu yao na kupiga stepu
mbili tatu hadi walipo akina Katibu na kuwaambia waondoke kituoni na
makundi yao.
Katibu akamaka "tuondoke".
Haiwezekani, sisi ndo twenye nchi hii si wengine." Na kweli,
haikuchukua muda makundi yakaitwa naye yaingie ndani ya kituo. Vijana
waliobeba mapanga, nondo na marungu wakiwa wanatoka nje ya jimbo
hilo, wakajipenyeza kwenye foleni kama vile wanataka kuandikishwa.
Masikini. Ikatoka amri wapige watu katika foleni na wakapiga huku
Polisi wenye bunduki wakiangalia.
Watu kumi wakaumizwa
kwa silaha zile za kikulima na wangali hospitalini wakiwa na majeraha
vichwani na kila mahali. Mmoja ameshonwa nyuzi 40 kichwani. Maharamia
wakaondoshwa kituoni kwa kutumia magari ya viongozi. Siku ile
nilisema ya Kianga ya kutia moto nyumba za raia kwa sababu za
kisiasa. Nyumba ya kwanza ilitiwa moto chini ya amri ya Mbunge,
mtunga sheria kiongozi wa watu.
Mnaona? Wahalifu
wanalindwa na kuengwaengwa huku raia wema wakidhalilishwa na kutiwa
ulemavu na hizi ndio siasa za wenye mamlaka Zanzibar. wanakaa
majukwaani wakisifia wanasimamia sheria ifuate mkondo huku
wakilihifadhi na kulisha wahalifu wakubwa. Huu si Muafaka bali uhuni
ni siasa za kijambazi alizoziita aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Ali
Omar Juma akizungumzia upinzani. Angekuepo angeona si upinzani leo
bali chama alicho akikipenda. Mwenyezi Mungu amrehemu aliko.
Tuna
wenzetu wenye mamlaka hawa, ni watu wazima na wenye akili timamu ila
yote haya wayasimamiayo kutekelezwa, ni dalili za wazi ya kuwa Mambo
Ni Magumu (MNM) na kutulia haiwezekani. Lazima kupangwe shere ndiyo
watapata utulivu wa muda maana utulivu kamilifu kwao inaonyesha
umefika mwisho. Dalili hizi ni za kuanguka mbuyu mshindo huwa mkubwa.
Ndivyo walivyoanguka akina Hitler, Cheusescu na wababe wengineo.
Tunataka mbuyu uanguke kwa salama kwa sababu hauna pa kushika tena.
Nimekuwa na jambo na Polisi kwa sababu hawatendi haki.
Hawazuii uhuni dhidi ya raia isipokuwa kuahidi kufanya uchunguzi tu
kila siku. "Tunafanya uchunguzi" ndio mbiu yao huku raia
wakiteseka kama vile wako ukimbizini. Aibu kubwa maana imethibitika
Dondola si ya kulinda sheria bali wahalifu. Ukiuliza wakuu si tuseme
tu kuwa Polisi imeelemewa na ulinzi wanasema "ah hiyo si kweli
hatujafikia huko bado tunafanya kazi yetu." Mpaka lini?
Safari hii Dola ikapata aibu ya mwaka. Hesabu zikaangukia
pabaya. Kwa sababu wenye mamlaka wanaona kila jambo ni rahisi
kulitenda, walipanga mpango wao na kutumia mawakala wao. "Mzuieni
mzee asiandikwe na sababu ni moja tu 'hana sifa ya ukaazi.'"
Maalim Seif Shariff Hamad anasema leo kwamba alijua mpango huo mapema
na wakisubiri siku tu utimizwe. Kwa miaka 17 anaishi Mtoni Kidatu
lakini Afisa Uandikishaji kituoni, Suleiman Ame Vuai, anaidhinisha
Katibu Mkuu huyu wa CUF asiandikishwe maana hana sifa ya ukaazi.
Kwake yeye, sifa ya ukaazi ni mtu kutoondoa mguu kwenye nyumba yake
kwa miezi 36, miaka mitatu. Anajisifu amepita kidato cha nne mwaka
1980.
Akili ya darasani si akili ya kichwa. Aliambiwa
hakujiambia na ni yeye anayekamatwa uchawi. Kijana huyu atafanywa
kafara kwa sababu ya akili zake kutotulia kwa kila aambiwacho.
Wasemaji wa Tume ya Uchaguzi wanakiri alitumia ukereketwa wa kisiasa
kumnyima haki Maalim kwa sababu sheria haikusema mtu asiondoke
kutafuta riziki nje ya eneo analoishi. Mmojawao anasema "na
ingekuwa hivyo basi wengi wangekosa sifa hiyo."
Wala
hii si fitna kwa sababu kama sheria ndivyo itakavyo, basi hata Rais
Amani Abeid Karume alikwenda Ulaya; Sweden, Finland na Norway mwezi
uliopita baada ya kufanya safari Uchina na Uarabuni hapo kabla. Mbona
hakuulizwa kuhusu safari yake hiyo kama imemkosesha sifa ya ukaazi.
Kilichotokea alipofika kituo cha Kiembesamaki kujiandikisha, makarani
walitetemeka hata mpiga picha akashindwa kufanya kazi yake. Waziri
Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha naye alisafiri kwenda nje aliulizwa
kuhusu hilo?
Kwa mara ya kwanza nakubaliana na kauli ya
wakuu wa Tume kwamba ukereketwa wa kisiasa ulitumika. Ni ukereketwa
kweli kwa sababu msimamizi yule wa kituo aliamua kumsainisha Maalim
isivyotakiwa katika fomu ya 2D. Muombaji kuandikishwa husaini upande
mmoja tu bali yeye alitaka na upande wa pili usainiwe. Matokeo yake,
ile sehemu aliyopaswa kueleza yeye na kutia saini, alimjazisha
Maalim. Masikini Suleiman Vuai Ame.
Kwa kuwa kada mmoja
maarufu mjini kaniambia kuwa Maalim atalazimika kufika Mahakama Kuu,
nakubali kuwa ule ni mpango ulioandaliwa mapema na wenye mamlaka ili
kumkomoa na kumdhalilisha kama alivyosema mwenyewe tangu pale
kituoni. "Nakwambia hapati mpaka atafika Mahakama Kuu sisi
hatutaki mchezo bwana hiki ni chama kinachojiamini. Nawe subiri
utaona kama itaishia wilaya," ananieleza kada huyu mwenye makeke
mengi kama vile chama ni mali yake.
Hawakujua kwamba
kumnyima haki Maalim itakuwa pigo kwao kwa sababu dunia itathibitisha
uhuni unaofanyiwa raia halali wa Zanzibar wanaokataliwa kuandikishwa
na hawapewi fomu ya 2D ya kudai haki yao. Leo kila pembe ya nchi na
kila pembe ya dunia kituko kile kinajulikana maana kimetangazwa na
vyombo vya habari vya nchini na vya kimataifa. Tukio lile limeamsha
ari mpya kwa raia kudai haki zao na lazima Tume isimame kidete
kuhakikisha watu wanapata haki zao za kuandikishwa. Nimekuwa nikisema
kwamba Tume ina meno na makali ila hayajaamuliwa kutumika.
Wenyewe
wanaweza kusema wanayatumia vilivyo. Kuyatumia kunahitajika kuonekana
hadharani. Kama tume imefukuza karani uandikishaji, msimamizi wa
kituo, imewakurupusha masheha vitimbi, iyaseme haya hadharani ili
wananchi wajue ni kweli inachukua hatua kukomesha uzembe na ukorofi
katika kazi muhimu. Wanaoweka pembeni sheria na kujiamulia kwa utashi
wao ndio wazembe na wakorofi si mtu anayepita karibu na uzio wa
Vikokotoni kuelekea kituo cha kujiandikisha.
Mwalimu wa
watoto wetu, Tahir Hussein Abdalla (30) analalamika ameshikishwa
adabu na Polisi kwa kugusa uzio wa Stendi ya daladala. Anachukuliwa
mzobemzobe na askari wasio mafunzo, na Polisi anayewasimamia
anaamrisha apigwe. Nimekuwa nikiwaasa Polisi kudhibiti ukorofi na
uhalifu wa kweli. Sasa kama wachukuaji wa hatua dhidi ya ukorofi na
uvunjaji haki za watu, wamshughulikie askari aliyeamrisha mwalimu
huyu kudhalilishwa katika tukio la Aprili 14 kituo cha Vikokotoni,
ambalo limeripotiwa kwa kumbukumbu MAD/RB/1520/05 Kituo cha Polisi
Mwembemadema.
Hili liwe fundisho kwa sababu kuna matukio
mengi ya Polisi kushiriki kudhalilisha raia bila ya sababu. Hata
baadhi ya makamanda wamo wanapita na ukereketwa wao wanapiga raia.
Hivi inakuaje RPC mzima anapiga raia usiku huku akipayuka
"Mnazungumza siasa hapa enh basi huyo Seif wenu hashindi
chochote hatumpi." Nasisitiza mna kazi kubwa ya kurudisha imani
kwa raia ili washirikiane nanyi kuzuia uhalifu.
Ends.