Waraka Kutoka Unguja

April 28, 2005

By

Jabir Idrissa



Pateni waraka uliochapishwa katika Rai ya Apr28.

Someni mfahamu maana mengine hayapatikani katika news coverage za kawaida.

 

Jabir Idrissa+

 

Waraka kutoka unguja

Headline: Mauaji ya ovyo ndo hatima aliyoikusudia Mzee Karume?

 

Hatujachoka. Ni uhakika ya kuwa ujenzi wa nchi na ustawishaji watu wa Unguja na Pemba ungali mbali. Ni mbali kwa sababu kila jitihada za kuitupa Zanzibar nyuma inaonekana. Ingawa utawala ungependa hata kupitia safu hii ya waraka, upigiwe debe kwamba uko dhatini kuinua hali za watu, hayajaonekana matokeo ya kupigiwa mfano. Bado.

 

Kulingana na ahadi zilizowahi kutolewa wakati ule wa kampeni, hali halisi ya utekelezaji wake, namna hali za watu zilivyo, namna maisha ya watu yanavyojongomea na kuonyesha wamo katika lindi la umasikini, bado. Maendeleo fulani yanaonekana wazi, yapo, lakini hakuna kitu kizuri kwa uongozi kama kuwashinda watu nyoyo zao kupitia kuwaunganisha, kuwajengea upendo na kuachia utamaduni wao udumu. Iwe yote safi, nyanja hii ya kudumisha utamaduni wa watu wa kuishi kwa utulivu na kusaidiana, upo katika mtihani mkubwa.

 

Hivi ninavyoandaa, kuna kundi la watu waliokataliwa kuandikishwa kwa sababu ya siasa za chuki na za ubinafsi zinazopaliliwa na utawala. Kuna malalamiko ya wananchi wa kindakindaki wa Unguja na Pemba kunyimwa haki ya kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) kisiasa tu huku wakishuhudia wageni fresh kutoka kwingineko wakipitishwa mezani na kuandikwa.

 

Inashangaza kuona siasa petu zinageuzwa njia ya mkato ya wakubwa kutimiza dhamira zao za kutenga watu, za kunyanyasa watu, za kugawa watu, za kuwagonganisha kwa nasaba za watokako na kadhalika. Wakubwa wamegeuza mtaji watu wasioshabikia chama wanachokifanya wao ni mali yao. Basi huwajengea chuki na siku hizi tunaona waziwazi wakitumia vyombo vya dola kutetea madaraka yasiwatoke. Si vizuri hata kidogo.

 

Nikidhani na kwa hakika ndivyo ninavyoamini, ukimtaka mtu akufuate upande wako, apende ukipendacho wewe, basi utumie lugha nzuri ya kumpendezesha na kumtia imani ya kuwa unamhitaji kikwelikweli. Nyendo zinazoelekeza watu katika mirengo zinapaswa kuwa nyofu na siyo zilizopindapinda zikionyesha zimegubikwa na mikikimikiki inayoambatana na vitisho vinavyofanywa na mawakala wa ulinzi na usalama. Popote penye vitisho nia huwa ni kujengea watu nidhamu ya woga, na penye nidhamu hiyo, hapeshi fitina na ndani ya fitina ni jamii kuvutana siku hadi siku. Haifai.

 

Leo wakati tuna zaidi ya mwaka tangu kutokea milipuko ya mabomu nilopata kuipachika jina la milipuko ya kishetani na umma wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla, pamoja na ulimwengu mzima, ukisubiri ripoti ya waliohusika nayo, milipuko mingine imeanza. Ati bomu litegwe na wapinzani na kila siku likose shabaha. Bomu linavunja sentimita chache za ukuta usiku wa saa 2 ambao kwa muda sasa hukosi wafuasi ndani ya maskani za Chama cha Mapinduzi (CCM). Ajabu ya mwaka.

 

Yale yale ya kwamba lisiloweza kutokea popote duniani, huweza kujiri kwa petu Zanzibar. Milipuko inayokwepa watu kwa maksudi imeanza upya. Inajulikana wazi nani anaisuka na kuifanikisha isipokuwa kwa sababu Dola inataka inayoyataka kushuhudia, hakuna wa kuidhibiti. Hakuna maana dola ndivyo itakavyo, itokee milipuko halafu wakamatwe wasioshabikia CCM. Balaa, balaa na fadhaa tupu.

 

Kwanini inakuwa nongwa watu kupenda upinzani? Sioni tatizo kwa sababu napenda demokrasia na katika demokrasia ya kweli (si ya majukwaani na ofisini tunapokaribisha mabalozi) lazima chama tawala kipate chama makini cha kukipinga. Kisipopingwa kitakuwa kinalala tu huku kikishindwa kutekeleza ahadi na majukumu yake ya kuongoza watu. Watu wanataka kuongozwa siyo kutawaliwa. Si tulifukuza Usultani ili tusitawaliwe? Mbona kuna nyendo za kutawaliwa raia.

 

Raia anapokuwa hana raha na maisha kwa sababu ya hofu ya kuchukuliwa na polisi na hawa vijana wa kisasa wa Janjaweed (askari wa vikosi vya SMZ wasio mafunzo ya kweli) au raia anapojisukuma kurudi nyumbani ikiingia tu magharibi kwa sababu ya kuhofia kukutana nao vijana hawa kwenye maeneo yao ya maskani, si dalili ya ushuwari bali hofu kuu iliyotanda akilini mwake. Raia wanashambuliwa kama watoto wadogo na wanaporipoti vituoni mwa Polisi wanageuziwa vibao; wanabambikizwa mashitaka. Si ishara njema bali uasi wa Dola kwa wananchi wake. Na lini wananchi walioasiwa na vyombo vya kuwalinda watatoa ushirikiano?

 

Inakuaje kila uchao ni watu wa mrengo wa upinzani tu ndio wachafu wa kufuata sheria. Hii tabia ya kuwa kila siku kutokee matukio ya fujo kwenye nyumba zao hata kuchomwa moto na kuteketezewa mali zao huku wakishuhudia wahujumu wao wakichekelea kwenye maskani ndio nini? Ndio kutesa kwa zamu huku kulikopata kusemwa na waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi? Nilipata kuuliza katika safu hii; raia watatesa lini wao na hawana bunduki? Sikupata jibu ila nafahamu fika bunduki haishindi umma, watatesa nao.

 

Kunatokea matukio yanaacha maswali mengi kuliko nguvu ya kuyajibu. Kwanza nakumbukia kauli ya Serikali kuhusu mauaji ya Juma Omar Juma ya kule Ngombeni Mbuyuni, Mkoani Pemba. Kujigongagonga kutupu kusiko na njia wala dalili za utawala kujifunza kwamba yanayofanyika si halali na hayawezi kujenga jamii nyofu. Juma inaelezwa kafa katika mazingira ya kutatanisha maana alikuwa aingie shule mchana si asubuhi alipokutwa na risasi ya moto; inaelezwa kuwa baada ya kufa alichukuliwa harakaharaka na watu wa chama cha siasa na jeneza alimobebwa likazongwa vitambaa vya bendera ya chama.

 

Hivi nani asiyejua kati ya viongozi wa juu wa nchi ya kuwa Juma alisokomezewa mbalini kwenye mtaro wa maji machafu? Kwanini alitupiwa huko kama si kwamba asionekane abadani kwa sababu angebururwa na maji ya mvua yaliyokuwa yakivuka kama treni iliyo mwendoni. Kwa hivyo utawala ulitarajia Juma angebaki hapo kwenye mtaro kwa maisha yake yote ya akhera? Kuchukuliwa na wenye imani ili kumsitiri ilikuwa kosa? Ninaamini ingetaka, Serikali ilikuwa na uwezo wa kulinda mpaka awe amechunguzwa mwili wake nini sababu ya kufa kwake. Haikutaka, haikutaraji kwa sababu ingeumbuka!

 

Lakini bado inaumbuka hata sasa kutokana na kauli zake zinazogongana. Si wakati ule ilipata kuelezwa kuwa alifariki kwenye msongamano wa watu waliokuwa wakipambana kuandikishwa? Na kwani kuna mabadiliko ya serikali? Si ni ileile iliyopata kutuambia raia kwamba mtu wa Shumba mjini alipatwa na risasi ilipotoka juu baada ya askari yule mjuzi kuilenga angani? Tungali tunakumbuka na ya leo ni muendelezo tu wa mbinu chafu zinazotendwa hadharani.

 

Juma kauawa kwa risasi ya askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) waliopelekwa kituoni kuwapa wenzao ulinzi ili waandikishwe kwa lazima. Kwanini uchunguzi usingeanzia hapo pa kuletwa sababu ya KMKM kuwepo pale? Si sheria askari kuwepo vituoni baki tu wale askari polisi wawili watatu wa kuweka ulinzi tena wakiwa wameficha silaha. Raia wa kikwetu ni watulivu hawasukumwi ja punda; kwa bakora. Ni maridhia kwelikweli Wazanzibari ila unapowanyenyekea.

 

Muuaji wa Juma atakufa tu naye na tunajua anaangamia taratibu kwa sababu roho ya binadamu imeumbwa na muumbaji kaapa hatamsamehe anayeiondoa bila ya haki. Eti Serikali inauliza nani kamuua Juma? Anayemjua atuambie tutamlinda? Yetu serikali imemlinda nani siku zote? Twasema muuaji wake tunaye khabari angalipo hai anadunda, afichwe popote, aliyemuumba hata naye, ajua aliko na kila akifanyacho. Mauaji kama hayo hukumu yake anaitimiza yeye Subhana. Wala hafundishwi.

 

Leo kuna mauaji mengine ya kihuni yametokea: Chande Rashid Saleh, aliyekuwa wakala wa CCM katika kituo cha uandikishaji cha Kinuni. Kakutwa mfu akiwa amezikwa nusu yake, huku nusu ikiwa juu. Mazingira ya tukio yanaacha maswali mengi kuliko majibu yake. Hebu tuelezwe sababu ya Chande kuondolewa kituoni. Ni dhahiri itakuwa akikataa kupinga kila mtu hata anayemfahamu ni mkaazi halali wa eneo lake. Lakini uadilifu wake huo pengine ndio chanzo cha yaliyomfika. Alitafuta rehema za muumba kuliko za siasa, akaachia haki isimame. Mhh kosa kubwa kwa sababu bila ya rafu, bao la kisigino.

 

Ufuatiliaji umebaini kuna vitisho vimecheza ndani ya familia ya marehemu. Wamelazimishwa kuamini wasiyoyaamini na kuyasema yanayowatia uchungu kwa kuona sivyo ukweli ulivyo. Serikali iliyo makini kutenda haki haipati shida katika matukio kama hayo kama inavyojitia leo. Unakamata wakala wa upinzani wakati waliohusika wanajulikana. Ni nini kama si kudanganya watu. Lakini watadanganywa wote mpaka lini kwa wakati mmoja?

 

Kama kuna matukio ya hujuma dhidi ya raia yanatokea huku Dola ikishuhudia bila ya kuyasimamisha, umma uamini vipi kwamba uko katika utawala wa mabavu ambao kwa kawaida huwa hautaki haki isimame, sheria ifuatwe kama msumeno. Kinachoendelea ni hali ya Serikali kujikosesha uhalali katika kutawala. Raia ni muhimu alindwe ili atumikie nchi yake kwa upendo. Asipolindwa na akiamini hasa ya kuwa halindwi kwa sababu ya utashi wa kisiasa, afanyeje?

 

Inafaa ielezwe wazi kwamba kuna mradi unatendeka ndani ya Jeshi la  Polisi: kunabuniwa hujuma isiyodhuru mamlaka ya nchi, kwa makusudi tu ya kukamata watu wa mrengo wa kushoto, halafu unakuta ndugu zao wahangaike kuwatoa na hawatoki ila kwa Kitu Kidogo (KK). Ni mpango maalum wa kuwatumia raia kushibisha matumbo yao: ni dhulma ya nguvu hiyo. Malipo ya dhulma mnayajua au mwayasikia tu kwa sababu mko mbali na aliyewaumba? Tabaan muache dhulma wakubwa ili hata hija zenu ziingizwe kwenye amali zenu.

 

Hivi wakubwa hawaoni kwamba mafuriko yalokumba ndugu zetu ni mtihani kwao wajifungue waone wapo walipo na wapi wanatakiwa kwenda. Si huambiwa tuna watabiri wa Hali ya Hewa, walikuwa wapi wasitupe indhari ya kuwa kuna mvua nyingi zitanyesha na kusababisha gharika? Haiwezekani kujua kila kitu, mengi yanahitaji kubakishiwa mwenyewe muumba. Mvua imekuja ya kutosha na imeleta madhara hatujaona tu nguvu zake Allah? Tufumbuke macho kwa kutangulia kuacha maovu.

 

Mafuriko yanapita hata mule mulimotengenezwa kwa mamilioni ya fedha. Mitaro mikubwa mikubwa imepitisha maji yasiyo kiasi chake na makalavati kuvunjwavunjwa. Uko wapi mtaro wa Kwahani Uwanja wa Farasi ulojengwa kwa fedha nyingi? Uko wapi na ule wa Jangombe uliojengwa kwa mbwembwe? Uko wapi mtaro wa Kariakoo wa kupeleka maji kwao yasidhuru jamii? Hakuna kishindacho muumba. Mafunzo haya tupate.

 

Nifunge basi kwa kutanabahisha ya kuwa umma na jamii ya Unguja na Pemba iko katika hatari ya kudidimia zaidi na zaidi kwa mtindo unaoendelea. Vitendo vya kuangamizana kwa sababu ya siasa lazima vipigwe kumbo. Tungependa kuona watu wanasabihiana kikawaida badala ya ile staili ya kumjibu mtu kwa mgongoni. Serikali ina wajibu wa kutandika misingi ya maelewano ya kweli si ya juujuu.

 

Utawala unapaswa kuheshimu haki za watu. Kwa hakika haupaswi kuingilia walioteuliwa kutenda haki ili wasiitende. Yaliyotendwa na masheha ni aibu katika nchi kama Zanzibar inayojulikana kwingi kwa huruma, ukarimu na ustaarabu miongoni mwa watu wake. Haya kama viongozi hawa walikuwa nusu mitume katika siku 21 si zimekwisha. Watabaki kwenye vituo vya kuandikisha wampinge nani? Warudi basi kwa jamii waliyoitia katika misukosuko isiyo lazima. Kila anayeingia kituoni Sheha hamfahamu au anasema sikutambui utatambua wangapi ngurumbili wewe?

 

Masikini nao kutokana na kutotambua kwao haki, wakakubali kutumiwa kama ngazi ya wakubwa kupandia kwenda watakako; nchi ya kusadikika Zanzibar. Walisema mapema nchi haitolewi kwa karatasi, itolewe kwanini basi na malendo ya mapinduzi yametupwa? Tulio nao ndio Muungano aliouasisi Mzee Abeid Amani Karume? Si kweli. Mzee mwenziwe, Ali Sultan bin Issa alitukumbusha juzi pale Bwawani ya kuwa mzee akiipenda Zanzibar, akivutana chini kwa chini na Mwalimu Julius Nyerere ili kuijengea hatima. Tuliyonayo ndio hatima aliyoikusudia hii ya kuhujumiana sisi kwa sisi? Heko miaka 41 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na udumu!!!

Ends.