Waraka Kutoka Unguja

May 5, 2005


By


Jabir Idrissa


Kwa wale walio mbali na magazeti ya Tanzania, pateni uhondo wa waraka uliochapishwa katika gazeti la Rai la Mei 5.

Headline: Yakhe Zanzibar hatuachi mazonge siye?

Wengi wetu binadamu tumejengwa katika kuamini ya kuwa mmoja wetu anapoanzisha jitihada za kuelekeza njia sahihi kwa kukosoa juu ya maovu yanayotendwa, anatumaini wale wanaokosea wamsikie na waache maovu hayo. Tunaamini hivyo kwa kuwa tunaamini pia kuwa siku zote mwisho wa maovu ni chuki na kulipizana visasi.

Pale inapotokea wanaotenda au kuchochea maovu wakawa hawasikii na ikawa hawasikii kwa makusudi tu siyo kwa sababu hawasikii kilio cha hayo maovu wanayoyasaidia, basi mkosoaji anavunjika moyo. Anaacha kukosoa. Kwa hivyo kama ni muandishi wa habari kama mimi niache kalamu; ninyamaze kimya. Inakuwa nifunge mdomo wangu.

Kwa karne ya leo, kama ilivyokuwa za huko nyuma walipoishi waliotutangulia, hili haliwezekani. "Mhh hiyo ni ngumu," wanasema wenyewe. Na kweli, kwangu ni ngumu kufunga mdomo kwa sababu kufanya hivyo si ishara ya kukomaa kiakili bali kudidimia. Jamii inafikia enzi, lazima kujitolea kwa sababu hata nasi tungependa kuishi bila ya kuhofia maisha yetu. Ikiwa hali inaonyesha ni ya kutiwa hofu kila siku, ni vigumu kusalimu amri. Basi waraka mtaendelea nao mpaka pale aliyetuumba, Allah (SW) atakaposema basi!


Kwanini tuendelee? Jibu ni rahisi: bado tunaowaelekeza njia hawajaamua kutulia, wangali wakiamini ni wao tu na si wengine. Wanaamini bado zama hii ni yao tu ya kutesa, na wala haitakuja ya wao kuwa nje ya utawala. Wao hawafanani asilani na akina Adolph Hitler, Haile Sellasie, Shah na Mboutu Sese Seko. Wao ni wao tu hawana mfano. Basi wataendelea kutesa tu na wala Mwenyezi Mungu hawapitii wao. Wamejiumba hawa si waumbwa. Tunaomuamini na kupata ushahidi kuwa yupo karibu nasi kwa kila tutendalo, tuseme tu ukweli utadhihiri wakati ukifika.

Ni kwa sababu tu maovu yanaendelea kusawiri katika Zanzibar yetu tuipendayo, na kwa vile walio madarakani hawajaamua kutia akili kubadilika wakayasimamisha, ndio inabidi tuendelee kueleza haya. Si mmeona nilitumia nafasi kubwa wiki iliyopita kuelezea suala hili lakini wakati mkiendelea kusoma, ndo kwanza yakaibuka mengine, si mapya. Tukisema zamani "chungu ndo kwanza kiko jikoni."

Kupita kwenye baraza za watu walio katika utekelezaji wa uhuru wao, wa haki zao, wa utamaduni wao, na kupigwa bila ya kuchagua. Rungu, tako la bunduki, waya, teke na matusi ya nguoni pamoja na kauli za kashfa za kisiasa bado inaonekana ndio silaha ya kukifanya Chama Dola kiungwe mkono uchaguzi ujao. Ni kweli naamini sasa binadamu anapoporomoka kiakili hajifichi; hufanya mambo hadharani maana hana soni tena. Hana wa kumuogopa angeogopa.

Kwa hivyo wanaamini lazima watumie Polisi. Wapite mitaani na kwenye baraza za watu waendeshe vipigo na vitisho halafu si watatengeneza tu taarifa za kuzitoa kwenye vyombo vya habari wanavyovimiliki? Ni kitu kidogo tu kupiga na kudhalilisha raia kwa sababu haiwi chochote maana hakuna wa kuogopwa. Mambo safi na amani na utulivu vinaendelea kawaida. Hivi ndivyo inavyotakiwa maana tupo katika nchi ya kusadikika; Zanzibar, panapotokea yasivyoweza kutokea kwingineko duniani. Hapa si ndio kwenye jumba la ajabu; Beit el Ajaib? Basi na mambo yake yawe ya ajabu ajabu. Haya.

Taasisi hii kwa hapa kwetu muflis. Imekwisha kwa vigezo vyote. Dondola imejihidhirisha si ya kulinda raia bali Dola chini ya CCM, yalopangwa kutokea wakati wa uandikishaji yametimia, nini kimebaki? Hakuna lakini bado, malengo hayajafikiwa kwa sababu bado uchaguzi, tulipo ni kwenye maandalizi tu. Hizi ni rasharasha bwana, mvua bado. Raia wema inabidi tuendelee kustahmili maana safari ni ndefu mpaka siku ya kusema na kisanduku. Lakini kwa sababu sisi hatukujiumba tumeumbwa, tutavuka salama usalimini ili tuje tuseme. Amin.

Hapo kati nimesema yaliyopangwa wakati wa uandikishaji yametimia. Ni kweli, si Wapemba, CUF na wa vyama vingine hawakuandikishwa. Basi ni kweli yale walo wakiyasema akina Borafia Mtumwa Silima, na yale aloyasema Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, Vuai Ali Vuai alipokuwa Pemba baada tu ya kuanza uandikishaji Mkoa wa Kusini na mambo kuanza kuwa magumu (kumbukeni MNM). Alilalamikia alodai yanayofanywa na Tume ikishirikiana na CUF mpaka akasema: "uandikishaji ndo tumeanza tu wajue watakuja Unguja." Tumeona wala si uongo. Mamia kwa mamia wamerudi wao tu kutoka vituoni, hawana shahada wala fomu za 2D, wao peke yao; wavyokwenda ndo wavyorudi. Patupu.

Haya kama ndo hivyo nini sasa? Ndo Chama dume kimeshinda? Kama kimeshinda uchaguzi wa nini tena? Si kitangaziwe tu kimeshinda uchaguzi wa 2005, na wagombea wake wote wa kiti cha Ikulu na majimbo 50 ya Unguja na Pemba. Kumbe? Ikiwa chama kimoja tu katika uendeshaji Serikali si basi, ndo kukosa kula? Si tutakuwa tumerudi kwenye mfumo wa chama kimoja kwa mlango wa nyuma. Bado ipo kazi kubwa ya kutendwa hata CCM itangazwe bingwa. Mechi imeanza tu magoli bado na hakujawa cha kutambia.

Angalau tulipo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imekiri vituo vya uandikishaji vilitekwa na masheha. Lakini hawajamaliza kusema ukweli, vilitekwa hata na makarani wake wa uandikishaji; walikubali kunyongwa shingo namna ile kwa sababu hawakuwa makarani kweli, walikuwa mawakala wengine wa CCM. Wangapi mliwaondoa vituoni kwa kutotimiza uadilifu mloutaka iwe ndio ngao ya utendaji wao? Nilipata kusema "semeni mkiwatoa" hamkusema tukiamini hakuna muandikishaji aliyeondolewa zaidi ya yule mmoja kituo cha Kwamtipura ambako hata Sheha mlimuondoa lakini akarudishwa na Mkuu wa Mkoa kwa jeuri ya nguvu. "Atokee atakayekuambia uondoke niletee jina." Afanyeje na kituo kile ni chini yake mwakilishi wa rais si Tume?

Haya na yule ofisa wa jimbo la Mikunguni aliyekamatwa na nailoni za kubandikia vitambulisho mlitutangazia kuwa ameshikwa? Hamkufanya hivyo wakati mna watu wawili wa idara ya uhusiano. Ninawafahamu walivyo wachapa kazi hodari hawa lakini naweza kuamini hawakupewa mamlaka ya kutangaza hata tukio hili ambalo limepelekwa mahakamani tayari. Ndo nini. Ndio utendaji gani kuajiri maofisa wa habari halafu habari hazitoki. Ni aibu kuwafanya hawa wapeleka makabrasha tu kwenye vikao vya wakubwa. Acheni kugeuza waandishi wazuri ni matarishi, wapeni nguvu na uhuru wafanye kilichowaingiza kazini ZEC. Nanyi waandishi tumikieni fani yenu si utarishi, mtajaulizwa.


Zile siku 21 zimekwisha na masheha mmerudi mitaani. Mzungumze na nani wakati wakaazi wenu mkiwaambia vituoni hamuwatambui? Je bado mnalindwa na kuchukuliwa na kurudishwa kwa gari majumbani? Tuliwaeleza mkadhani tunawafitinisha na wakubwa zenu. Sivyo, tulikuwa tukiwaaidhi mtambue mamlaka yenu na mipaka yenu. Mchunge uadilifu dhidi ya kutumikia watawala, au hamkujua uadilifu ni jambo la kheri. Mkaacha kukubalia mnaowajua mkaingiza msiowajua wakaandikishwa kiulaini.

Mtu mmoja aliniambia alipokwenda kituoni Jang'ombe akapingwa asiandikishwe kwa sababu eti alitukana Sheha mtaani. "Niliumia kuona naondoshwa kwa mtutu huku akipitishwa mtu aliyetoka Mtima hata hajui alikuwa jimbo gani?" alijisemea. Hadithi kama hizi ni nyingi mno. Wapi umesikia mtu anamkataa mtu aliyemfia baba yake mzazi mapajani kwake? Ulisikia wapi itafika siku baba anamkatalia mwanawe, mkewe, mkwewe na jirani yake kwa sababu tu anaona si mwenzetu katika CCM? Na ikathibitika kuwa masheha wote ni CCM. Ndio ukweli, Masheha mliukwepa uadilifu kwa sababu ya mshahara kiduchu na zile elfu arubaini mlizolia kiapo mtatekeleza matakwa ya Serikali hata kama kufanya hivyo ni uhuni. Nawaachia wenyewe. Wanasema mtajiju, maana kusudi haiambiwi pole.

Uhuni wa masheha na undembendembe wa Tume kwa hakika umesababisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar liingie waliomo na wasiokuwemo. Nilipata kusema uchaguzi huru na wa haki utapatikanaje kwa daftari la waliomo na wasiokuwemo. Bado nauliza itakuaje, tutafanyaje katika hali kama hii. Sawa Tume mkisema mtachunguza madai ya watu kutoandikwa na kutopewa fomu za kulalamika, lakini matokeo ya uchunguzi yatatolewa hadharani au ndo yamekwisha? Na kuwa yamekwisha haiwezekani kwa sababu mmeapa uadilifu mbele na mtafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi. Tunataka Tume mjirudi mtimize matumaini ya umma si hivyo mkubali kubeba lawama.

Ni vitendo vinavyomjenga au kumbomoa mtu au taasisi, si maneno matamu kwenye majibu ya barua. Hapana, hakukuwa na maneno matamu katika barua zilizotumwa vyama vya upinzani. Nyingi nilizoziona kutokana na kazi yangu, zilikuwa na lugha ya kukirihisha; mbaya ajabu kama vile kila mtu katika Tume aliamua kuacha ustaarabu wa uungwana tuliouzoea. Lugha chafu tupu isiyoleta matumaini kwamba tumekusudia kweli kujenga jamii yetu.

Matokeo yake watu kwa maelfu wameingia kwa hila ndani ya daftari. Sasa ndo daftari gani hili mlotakiwa kulisimamia huku wenyewe mkikiri mamilioni ya fedha zikiwemo za wahisani yametumika kuligharimia? Siamini kama Wahisani walitoa fedha zao ili kutuletea daftari bomu Zanzibar na wabaki radhi kwa yaliyolisibu. Siamini na yahitaji mtafakari kwa makini na kuondoa uozo huo ili walio wa kweli wabaki na wasio watoke.

Leo vituoni mwa uandikishaji Daftari la Muungano ni aibu tupu. Kutwa nzima makarani wanasinzia ovyo maana hawana kazi ya kufanya. Wamuandike nani? Hawapo eti maana watu waliopaswa kuingia humo wameingizwa kwa hila za Dola katika Daftari la Zanzibar. kilichobaki ni kupoteza muda wa watu na fedha za umma. Na hayo ndiyo matokeo ya mipango mibovu ya waliopewa mamlaka. Ni matokeo ya uvimbishaji vichwa wakubwa usio na kifani. Ni aibu jamani aibu. Hatuachi yakhe Zanzibar mazonge?
Ends.