Waraka Kutoka Unguja

June 23, 2005

By

Jabir Idrissa





Wanaukumbi Aslaam Aleykum;

Huu ni waraka mpya baada ya kifungo cha siku 11. mtaona kama nimepunguza ukali wa kalamu.

Faida kubwa sana kwa mlio mbali na Tanzania ambako gazeti la Rai halijafika mkausoma.

Haya nufaikeni.

Jabir Idrissa+

 

Heko ni huru! Muafaka CCM/CUF ulishavunjwa tayari

 

Naam kifungo kimeondolewa. Kile kifungo kilichokuwa kimewekwa shingoni kwangu kimeondolewa. Ilikuwa kifungo kikali kile kwa sababu hakina muda kitakaokuwa kimekwisha: inaitwa indefinite ban. Kwa bahati mbaya inaonyesha kifungo chenyewe kilitokana na kazi ya watu wachache ndani ya Serikali kwa hivyo wakubwa walipoulizwa na wakubwa wenzao wakaishia kusema hawafahamu na wanahitaji kufuatilia ili kuchukua hatua muafaka. Kama ni kweli inashangaza.

 

Kifungo hakikuzingatia Sheria namba 5 ya Magazeti na Machapisho ya mwaka 1988, ingawa ni kweli ina vifungu vinavyotaka mwandishi wa habari apewe kibali na Idara ya Habari Maelezo. Sheria inataka mwandishi ambaye atakuwa hakusikia wito wa kuchukua kitambulisho, aitwe na kufahamishwa ya kuwa anapaswa kuchukua kitambulisho. Sijapuuza wito wa kuchukua kitambulisho hiki kiasi cha kutajwa mimi ni mhalifu wa sheria ya magazeti.

 

Wala Idara hii haina uthibitisho kuwa imewahi kuniita na kunieleza, kama alivyosikika mkuu wake akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Yote ya muhimu kabla ya kuadhibiwa hayakufanyika na ndiyo maana ninasisitiza kwamba kifungo kile hakikuwa na uhalali wowote kisheria.

 

Nina thubutu ya kusema haya kwa sababu ninaamini katika utawala bora. Utawala wa sheria wa kwelikweli unaohimiza ufuataji Katiba, Sheria na Taratibu zilizowekwa katika kuendesha mambo ya umma, la kama ni kuonyeshana ubabe kwamba fulani ana mamlaka, ni sawa kusema kwamba waliosuka mpango huu wamefanikiwa lakini bado njia ni chafu.

 

Nimekuwa nikieleza katika safu hii umuhimu wa kila mtu kuwajibika kuisaidia nchi kwenda mbele. Sote tuwe na hima hiyo, isipokuwa tukubaliane katika njia za kufikia huko. Tofauti ni chachu ya maendeleo popote pale. Lililo muhimu zaidi katika kufanya kazi ya kuhudumia umma, ni kwa mtu, wakiwemo maofisa wa serikali, kuhakikisha anachokifanya au anachokiamua hakitaitia nchi aibu mbele za macho ya watu. Aliyekusudia kunidhalilisha kwa kunitangaza mhalifu wa sheria, atambue nimedhalilika kidogo kuliko ilivyodhalilishwa serikali.

 

Zanzibar ni nchi ya watu na serikali ni ya watu si ya mtu au kikundi cha watu. Ofisa wake anapofanya uamuzi na ukahojiwa na umma pamoja na wawakilishi wa kibalozi kwa kuona hauna mantiki ya kisheria au hata kwa kuzingatia hali halisi ya wakati, inakuwa ni aibu. Aibu kama hii haibaki tu kwa ofisa mhusika peke yake, inageuka aibu ya nchi.

 

Nchi inaonekana ina watu wasioheshimu mipaka ya kazi yao. Wazanzibari wangependa ofisi zao zipewe watu wenye ujuzi na utulivu katika kutoa huduma. Watu wanaoangalia athari za maamuzi yao kabla ya kuyatoa. Katika uanasheria, kuna haja ya Hakimu anapotaka kutoa hukumu, kupaswa kujiuliza mara kadhaa umma utaichukuliaje hukumu atakayoitoa? Basi kila ofisa wa ofisi ya umma (ya serikali) naye anawajibika kufikiri kwanza kabla ya kuamua. Ndio hapa tunasikia kuna mahitaji ya viongozi bora siyo bora viongozi. Katika utendaji kazi, tusiwe kama pweza kuvutia maslahi upande wetu. Tafakuri jambo jema.

 

Mkono wangu uko huru kama zilivyo fikra zangu. Huru huru kabisa hakuna kifungo tena. Lazima nisifu ujasiri uliotumika kwa Idara na Serikali baada ya tukio lile. Kwa vile halikupendeza na kujenga taswira nzuri kwa nchi, wamechukua uamuzi wa busara ule niliouomba katika waraka uliopita na kukubali tu maombi yangu ya kitambulisho. Nilitimiza wajibu wangu nimepata haki yangu. Sina ubaya na Idara, Mkuu wake wala Serikali ila mambo kama haya yanatupa mafunzo mengi na kila mtu ajifunze. Zanzibar haiwezi kuishi peke ikajificha.

 

Kwa kuwa safu hii haikupata kusimama kutokana na umuhimu wake kwenu wasomaji na kwa umma kwa jumla, itazidi kuchanua kwa sababu yanayofaa kuandikiwa waraka yangalipo. Tena mengine mapya ja shuka. Sifanyi utani ninaposema kungekuwa hakuna madhambi katika jamii yetu ningeshindwa kuijaza safu. Yapo madhambi kwa sababu haijaonekana dhamira ya kuyazuia kutokea. Waraka utaendelea Mungu akipenda.

 

Tunazidi kwenda katika tarehe za uchaguzi. Nikasikia kumetokea vurugu Bagamoyo. Kabla ya wakuu wa Polisi kutaja wahusika, nikasikia kauli za wanasiasa. Chama cha Mapinduzi (CCM) kikalaumu Chama cha Wananchi (CUF), wapinzani wao wakuu kwa namna inavyoonekana sasa hata Tanzania Bara. Mtangazaji mkuu wa sera na maamuzi ya CCM akatoa sauti CUF ndio waliofanya vurugu. Kauli ya mwisho ikawa lazima waombe radhi chama, wamuombe radhi mgombea si hivyo Chama kitafikiria upya uhusiano wake na CUF juu ya Muafaka.

 

CUF hawakuomba radhi na viongozi wake wakasema wazi vurugu zilizochochewa na wafuasi wa CCM waliokuwa na nia ya kusambaratisha mkutano wa CUF. Inaonyesha Bagamoyo kungali na ushindani mzito wa udhibiti wa siasa katika mji unaofanana kimazingira na Zanzibar. Mwenendo wa demokrasia nchini petu, unaonyesha udhibiti wa siasa unaruhusika kwa CCM tu si vyama vingine. Hiki ndio chama dola, kinacholea demokrasia inayoendelea kuitwa changa haijapea. Basi kinavyotaka ndio iwe.

 

Twaha amekuwa akionekana mwiba kwa siasa za CCM Bagamoyo. Wapo wanauliza hivi Twaha kapata lini uchechemeaji mguu. Eti wanasema zote ni siasa tu. Amekuwa akichukuliwa kama ni kiongozi madhubuti wa chama cha upinzani kwa hivyo dawa yake ni kumsukumiza. Na kweli wiki ya pili hii sasa amekuwa ndani na yanaibuka maswali yuko katika gereza gani Bagamoyo?

 

Ametiwa kitanzini baada ya wanasiasa wa CCM kusema vurugu zimefanywa na CUF. Bagamoyo na Zanzibar si mbali lakini tunapozungumzia Muafaka wa kisiasa uliosainiwa na vyama vya CCM na CUF, kila mtu anajiuliza vurugu za kihuni zilizoandaliwa Bagamoyo zitakuwa na uhusiano gani na Muafaka uliohusu matatizo ya kisiasa yanayoihusu Zanzibar? Na mpaka sasa wapo wanaojiuliza sababu ya Muafaka kuhusishwa na vurugu za Bagamoyo. Lakini majibu yapo.

 

Wakati CCM wanatishia kuuhalifu Muafaka waliousaini kwa mbwembwe na ahadi nyingi mwaka 2001, CUF wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kwamba utekelezaji wa masuala muhimu yaliyobainishwa kwenye hati ya Muafaka umepuuzwa na Serikali za CCM, hususan hii ya Mapinduzi Daima (SMZ). Viongozi wa CUF wamekuwa wakilaumu ya kuwa mambo yanayotokea Zanzibar yanatia hofu kwamba muafaka umewekwa kando na CCM na kuamua kutumia mbinu za medani kuendesha siasa.

 

Hapatafutwi mchawi lakini mshikwa na ngozi ndiye mwizi wa ngombe. Tunapoambiwa gari za chama zinakutwa kwenye matukio ya kihuni usiku na mchana huku yakiwa yamebeba vijana wanaofanana na wale wa Sudan, tusemeje? Tatizo ni kwamba hata machafu yaliyopangwa kufanyika yawe yamefanywa kwa ustadi namna gani, dalili za uchaguzi hazitoki zote. Dalili za kuwepo mkono wa chama tawala katika matukio mengi wakati wa uandikishaji wapiga kura Zanzibar hazikufutika hadi leo.

 

Wafuasi wa upinzani wakifanya uhuni haichukui siku kukamatwa na huchukua zaidi ya saa 48 ndio hufikishwa mahakamani. Wengi wao huachiwa vituoni mwa Polisi kwa hongo inayoshibishwa wakuu wa jeshi hili. Wanaotiwa katika mitihani ya kushikwa kila wakati kunapotokea uhuni uliopangwa ni watu tunaoishi nao mitaani kwa hivyo hawafichi yanayowasibu wanapokuwa vituoni na njia wanayolazimishwa kuingia ili kuachiwa.

 

Kama vikosi vya vijana waliopangwa kando ya barabara wakati wa mapokezi ya wagombea wa viti vya enzi katika uchaguzi ujao walikutwa na fulana nyekundu, si rahisi kuwatenganisha na wale waliokutwa na fulana kama hizo kwenye matawi ya chama na kukutwa na madumu na chupa za petroli wakichoma viwanda vya mbao. Walinzi hawakuficha chochote waliposhikwa Polisi lakini nani kafunguliwa mashitaka ya uharibifu wa kiwanda cha Sana Express cha Kinazini (Saateni), nani kashikwa kuhusu kiwanda cha Magogoni (Msumbiji) na nani kashikwa kuhusu kiwanda cha Kidimni (Koani)?

 

Nani kashikwa kuhusu uhalifu dhidi ya nyumbani kwa mwakilishi wa Chambani uliosababisha madhara makubwa kwa Mzee Juma Muhunzi? Nani kashikwa kuhusu ukatili na uharamia wa nguvu wa kuvamia raia wasio na hatia katika foleni ya kusubiri kuandikishwa kuwa wapiga kura Kituo cha Kinuni, Tumekuja, na uharamia mwingine wa kuteketeza kwa moto nyumba za raia wa Kianga Kijijini? Eti usiku kucha doria ya Polisi wakiondoka tu alfajiri, nyumba zinachomwa moto. Uhuni mkubwa.

 

Sasa kama Muafaka wa CCM na CUF unazungumzia kwamba daftari la kudumu la wapiga kura ni hatua makini ya kuleta uchaguzi huru na wa haki na wa amani, halafu tushuhudie uchafuzi wa daftari hili huku kukiwa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa dhidi ya wachafuzi, tuamini kwamba watawala wangali na shida na Muafaka? Si kweli hata kidogo. Muafaka ni kuleta uadilifu katika siasa.

 

Rais Benjamin Mkapa anapomtaka Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula leo aitishe haraka kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu wa vyama hivi kuzungumzia Muafaka siku chache baada ya Rais Amani Abeid Karume akikiri hadharani daftari kukumbwa na matatizo ya kiutawala, si kitu cha bahati mbaya. Kuna matatizo ya kwelikweli yanayohitaji kushughulikiwa sasa si halafu.

 

Lakini matatizo haya yamekuwepo kwa muda mrefu na baadhi yake yamekuwa yakipaliliwa kwa nguvu kupitia harakati za vyombo vya dola baada ya viongozi wa dola wenyewe kutamka. Rais Mkapa mwenyewe amekwishatamka ya kuwa atatumia hata ikibidi nguvu za dola kukipatia chama chake ushindi, sasa nani anayeshangaa yanayotokea kuhusu Muafaka? Si tunajua, Rais akisema tu jambo, wa chini yake wanahangaika kuyatekeleza.

 

Katika rekodi, tunaambiwa viongozi wa CUF wamemwandikia Rais Mkapa mara tano kumtaka achukue hatua za kukwamua hali mbaya ya maendeleo ya Muafaka lakini ametingwa na kazi za Ikulu. Huku Zanzibar, Rais Karume hajakutana kwa miezi saba hivi na Tume ya Muafaka aliyoiunda kuratibu utekelezaji wa Muafaka. Utaratibu unahitaji kila mwezi angalau mara moja akutane na makamishna wa tume hii lakini labda naye hana nafasi. Mwenyekiti Mwenza wa Tume hii, Abubakar Khamis Bakary, amelalamika hivi karibuni kwamba mara kadhaa vikao vya Tume vimeshindikana kwa sababu wajumbe wa CCM hawafiki. Nini kimebaki kuamini CCM inaheshimu Muafaka?

 

Kwa sababu ya yote hayo, hata wakati huu kwa mtazamo wangu wa mambo, naona CCM ilishauvunja Muafaka na kinachofanyika ni jitihada tu za kujaribu kuvutia wafadhili waendelee kukubali kwamba serikali zimetimiza wajibu wake katika kuhakikisha unafanikiwa. Muafaka ungetekelezwa kisawasawa, utandu ulioigubika hali ya mambo Zanzibar usingekuwepo, wala wafadhili wasingeendelea kupata wasiwasi juu ya hatima ya Zanzibar katika uchaguzi ulio mbele yetu. Nawasihi wafadhili kwa kuwa wanatutakia mema, wasichoke kutia shime uchaguzi ufanyike kwa uhuru, amani na kwa uwazi. Tunasubiri kuona heshima ya Tanzania itakuwaje.

Ends.