|
Wanaukumbi wenzangu;
Ufuatao ni waraka uliochapishwa na
Rai toleo la Juni 30. Wale walio mbali na Tanzania na hasa
wasiobahatika kuyaona magazeti ya Tanzania na kwa kuwa yale ya
Habari Corporation hayajatiwa kwenye mtandao, basi kwa faida yenu
nawatilia netini humu.
Ahsateni.
Headline:
Baraza la Wawakilishi nalo ni Taasisi ya Umma
na jabir
idrissa
Nilisema hivi wiki iliyopita: Wazanzibari
wangependa ofisi zao zipewe watu wenye ujuzi na utulivu katika
kutoa huduma. Watu wanaoangalia athari za maamuzi yao kabla ya
kuyatoa. Katika uanasheria, kuna haja ya Hakimu anapotaka kutoa
hukumu, kupaswa kujiuliza mara kadhaa umma utaichukuliaje hukumu
atakayoitoa? Basi kila ofisa wa ofisi ya umma (ya serikali) naye
anawajibika kufikiri kwanza kabla ya kuamua. Ndio hapa tunasikia
kuna mahitaji ya viongozi bora siyo bora viongozi. Katika utendaji
kazi, tusiwe kama pweza kuvutia maslahi upande wetu. Tafakuri
jambo jema.
Maneno haya nimeona ni vizuri
kuyarudia leo hapa. Yana umuhimu mkubwa kurudiwa kwa sababu mada
yangu safari hii inajikita ndani kabisa ya Baraza la Wawakilishi,
chombo adhimu cha kuwasilisha masuala ya maslahi na wananchi.
Katika chombo hiki hakutakiwi ubinafsi wa kiasi chochote kile.
Kumbe wapo viongozi wanajisahau wamepelekwa mle ndani kwa sababu
zipi.
Wapo viongozi katika chombo hiki
hawatambui wajibu wao wakiwa katika chombo hiki na kwa sababu
hiyo, kwao, kupiga vijembe wenzao ndio mchango mkubwa na wa pekee
kila wakiruhusiwa kusema. Na hali hii iliyokuwepo hata baada ya
kuanza kwa baraza la kwanza lenye wawakilishi mchanganyiko mara
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, imenikumbusha nyuma
kidogo.
Wapiga kura wa jimbo la Mkunazini
(wakati ule) walipiga kura ya kutokuwa na imani na mbunge wao
baada ya kuona hawakilishi mawazo yao ndani ya Bunge bali akitumia
muda mwingi kueleza yasiyosaidia maendeleo na maslahi ya jimbo
lake. Watu wanaweza kusema hatua ya wapiga kura wale haikuwa na
nguvu yoyote kwa sababu haikufanikisha mbunge yule kuachia kiti,
lakini kidemokrasia, wapiga kura walionyesha kutoridhika kwao na
utendaji wa mbunge wao. Sema tu hatujawa katika jamii iliyoshiba
utamaduni wa mtu kuachia nafasi akiona amekanwa na watu
wake.
Na ndipo yalipokuja mawazo ya kutaka
iwepo sheria inayoruhusu wapiga kura kuweza kumkataa mwakilishi
wao katika vyombo hivi wakitosheka kuwa hafai tena kuwakilisha
mawazo yao kwa mujibu wa yalivyo maslahi yao. Tatizo kubwa hapa ni
kutokuwepo misingi madhubuti ya kuendeshwa nchi kidemokrasia.
Tuliingia kwanza katika mfumo ndipo tutafute misingi ya kufanya
shughuli zetu kwa kuzingatia misingi.
Tumetafuta
soji kabla ya farasi. Matokeo yake soji limekuwa haliendani na
farasi tuliyempata na ni vigumu kutafuta farasi mpya anayelingana
na soji tuliyokwishagharimika kuinunua. Balaa tupu na tupo kwenye
kona tunahitaji msaada mkubwa na muafaka madhubuti. Kwa hakika,
njia bado ndefu na ina miiba. Labda hatimaye tutavuka mkondo na
kufika salama safari yetu ya kupata kuishi kwenye nchi ya maziwa
na mito iliyonona na ikiwa haijachafuliwa mazingira yake.
Amin.
Pengine tungali na watu wasiofahamu
maana hasa ya chombo cha kutunga sheria: Baraza la Wawakilishi
hapa kwetu. Jamani hiki ni chombo adhimu. Chombo kinachotarajiwa
kunufaisha wananchi bila ya kuwabagua kwa aina yoyote ile ya
ubaguzi. Chombo adhimu kinachostahiki kila sifa ya kuwa ni chachu
ya kuendeleza watu wa nchi yetu Zanzibar. Chombo adhimu chenye
jukumu zito la kuendeleza uhusiano wa Zanzibar na Tanzania,
Zanzibar na nchi jirani, Zanzibar na Afrika, Zanzibar na Asia,
Zanzibar na Australia, Zanzibar na Uropa, Zanzibar na Marekani.
Uhusiano mzuri wa Zanzibar na dunia bwana.
Hiki
si chombo cha mzaha hata kidogo. Ndani ya ukumbi pale, si mahali
pa mtu, mwakilishi mtu mzima, kujinasibu eti kafanya hivi na vile
jimboni kwake, eti chama chake kimefanya hivi na vile, eti
mapinduzi daima, eti kupinga kila kitu kwa kuwa tu kimesemwa na
mpinzani wako. Sivyo na haitakiwi kuwa hivyo hata kidogo. Baraza
la Wawakilishi ni chombo kinachotakiwa kuwa njia ya kutatulia
matatizo ya umasikini mkali unaowakumba wana wa Unguja na Pemba.
Si chombo cha kutolea moshi wa chama fulani cha siasa.
Kila
mtu aliye ndani ya chombo hiki anapaswa kutambua kwamba akipewa
nafasi ya kuzungumza basi anatakiwa achunge atakayo kuyasema.
Afikiri mara mbili kabla ya kuomba nafasi ya kuzungumza. Afikiri
anayotaka kuyasema yatasaidia nini azma ya kuondoa (siyo
kupunguza) umasikini unaozidi kuwatambalia wananchi akianzia na
wapiga kura wa jimbo atokalo.
Mazungumzo ya
ndani ya chombo hiki yasiwe ya kuonyesha ubabe wa chama kwa sababu
kama chama kila mtu ana chake, na kwa kweli wapo wasiokuwa na
vyama na wanataraji wasemewe kwa yale yenye maslahi nao. Wa
kuyasema haya ni yule aliye ndani, mwakilishi aliyeingia kupitia
tiketi ya chama. Ndivyo itakavyo sheria uingie kupitia chama,
lakini tambua ya kuwa ukishaingia unawakilisha kila mtu wa jimboni
kwako siyo tu wa chama chako.
Kwanza hufahamu
kwa uhakika kama wote wa chama chako walikupigia au wote wasiokuwa
na vyama hawakukutilia voti. Ni uhuni tu unaofanyika petu lakini
haitakiwi kuwepo namna ya mpiga kura kutambulika amempigia mgombea
gani. Niisemayo ndiyo demokrasia iliyopea ambayo mizengwe na
takrima si njia ya kuingilia kwenye chombo hiki.
Hiyo
ni kwa waliopigiwa kura kuwakilisha wananchi ndani ya Baraza la
Wawakilishi. Wajibu wao hauna tofauti na wajibu wa kiongozi wa
Baraza, Spika anayeongoza vikao. Naye ana wajibu wa kuongoza
chombo hiki kwa uadilifu wa kuonekana hasa si wa kuhisiwa. Spika
anapokuwa muadilifu, atachunga heshima ya Baraza na asipokuwa
atavunja heshima ya Baraza hili. Uadilifu unatakiwa kwa kutoruhusu
wawakilishi kukashifiana kwa namna yoyote ile.
Uadilifu
unatakiwa udhihirike kwa kutoruhusu mwakilishi kusema
asiyoyafahamu au kusema ya kubuni kama zisemavyo kanuni. Lakini ni
namna nyingine ya kuchunga uadilifu pale Spika anapotenda haki kwa
wawakilishi wote bila ya kuzingatia fulani ni wa chama gani. Kwa
sababu Spika anatokana na chama cha siasa, haitarajiwi kwa namna
yoyote adhihirishe ukereketwa wa chama chake akiwa kwenye kiti
kile cha enzi. Kutenda kwa usawa na haki ndio iwe msingi
mkuu.
Baraza la Wawakilishi liongozwe kwa
kanuni na sheria si utashi wa Spika. Inakirihisha kuona kiongozi
wa chombo hiki anapalilia ukereketwa ndani ya Baraza hata kwa
kuzitenga kanuni. Ikitokea mwakilishi anatoa maelezo yaliyo
kinyume na kanuni za Baraza, ni kumsimamisha haraka. Mkiukaji
kanuni hapaswi kuonewa huruma. Kuna kitu kimenishangaza
kukishuhudia. Mwakilishi anahoji uthabiti wa maelezo ya mwenzake
lakini ikabainika ni kinyume na kanuni. Ni uadilifu kuchunga ile
kanuni kuliko kuachia ile hoja iendelee.
Tumeshuhudia
mara nyingi majaji wanapozikataa rufaa kwa sababu katika
kuwasilishwa kwake, utaratibu wa kisheria haukufuatwa. Jaji
hapaswi na kwa kweli wengi walio waadilifu wanakwepa kujiingiza
katika mtego wa kulazimisha rufaa hiyo isikilizwe eti kwa sababu
ni nzuri na ina umuhimu. Kufuata utaratibu wa kuiwasilisha hiyo
rufaa ni moja ya msingi mkuu wa utendaji haki katika mahakama, na
kwa hivyo katika chombo chochote kinachotakiwa kutenda kwa
haki.
Kiongozi wa Baraza anaporuhusu
mwakilishi aliyekiuka utaratibu katika kuwasilisha hoja barazani,
anapalilia kiburi kwa huyo mwakilishi aliyeruhusiwa na papo hapo
anamtia katika unyonge yule anayekusudiwa kuathirika na hoja hiyo
ikitolewa. Hapa inaonyesha wazi haki haikuzingatiwa badala yake
utashi wa mtu. Hii ni hatari kwa vyombo vyenye majukumu mazito
kinchi kama Baraza la Wawakilishi.
Lazima
iingie katika akili ya kila mmoja wetu imani kwamba Baraza la
Wawakilishi ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya uongozi wa nchi,
ikijumuishwa na Utawala (Serikali) na Mahakama. Kama mhimili huu
utakuwa unayumba katika utendaji wake itakuwa si vingine bali
kuashiria kwamba bado tuna safari ndefu ya kuondoa umasikini.
Umasikini wa kwanza tulionao wengi wetu ni wa kifikra, nao wapasa
kuondoshwa mawazoni mwetu.
Hata katika dini
tunaambiwa mtendee mwenzio unayopenda kutendewa wewe. Maana yake
mtendee mazuri kwa sababu nawe unapenda mazuri. Kauli hii
imekusudiwa kujenga uadilifu si kitu kingine. Uadilifu unatakiwa
katika kukaribisha mijadala inayojenga jamii siyo inayochochea
uhasama. Kwa kuwa Baraza la Wawakilishi nalo ni taasisi ya umma
kwa maslahi ya umma, basi ingekuwa jambo jema, uendeshaji wake
ukawa unaozingatia tu kanuni si jambo jingine.
Mada
hii nitaiendeleza wiki ijayo kwa kubainisha mifano inayoonyesha
udhaifu na umakini katika mijadala barazani.
Ends.
|