|
Wanaukumbi Aslaam Aleykum;
Nisameheni kwa kushindwa
kuwatilia waraka wa wiki iliyopita. mahangaiko yalinitinga. kwa
hisani zenu, naomba muupokee. hii ni faida kubwa kwa wale walio
mbali na Tanzania linakofika gazeti la Rai zinamochapishwa makala
za uchambuzi ikiwemo ya Waraka kutoka Unguja. bakhti mbaya Habari
Corporation haijatia magazeti yake kwenye mtandao. Inshallah
Jumamosi nitawatilia wa wiki hii.
Ahsanteni.
Jabir
Idrissa+
Headline: Baraza la Wawakilishi ni Taasisi ya Umma
(3)
Baraza la Wawakilishi linatumiwa vibaya,
wakati linatarajiwa kuipeleka Zanzibar kwenye utandawazi ule wa
kuchagua yanayotufaa na kuyatengeneza kwa mazingira yaliopo kwetu.
Wapi?
Tulilonalo ni baraza la viongozi wenye
uwajibikaji mdogo kwa umma. Wananchi wanaumia kwa ufukara mijini
na vijijini, unaotokana na kipato kisichotosheleza mahitaji yao,
wengi hawana maji ya uhakika, safi na salama na fedha za kununulia
dawa nje ya Hospitali Kuu ya Mnazimmoja. Lakini wawakilishi
wanapiga siasa barazani. Kila wapinzani wakiuliza inakuwa nongwa,
majibu ni vijembe.
Maswali hayajibiwi
ipasavyo na mawaziri. Hayajibiwi ipasavyo kwasababu utasemaje
unaposikia waziri anajibu “nitamjibu kwa maandishi”,
“nitampatia maelezo ya kutosha tukionana baada ya hapa”,
“namuomba mheshimiwa mwakilishi tushirikiane kutatua tatizo
hili”, “namuomba anistahamilie kwa sababu takwimu sahihi
sinazo hapa”.
Namkumbuka Waziri wa Ujenzi
wa Dar es Salaam, John Magufuli. Namuita kamusi kwa sababu hana
asichokijua katika eneo lake, na si kwa hisia, kwa uhakika hasa wa
kilivyo. Anayajua madaraja makubwa na madogo yanayopita kwenye
barabara kuu mijini na vijijini, anayajua si kwamba yapo tu, bali
hata vipimo vyake vyote anavijua. Anajua habari ya nyumba za
serikali, wapi zilipo, lini zilijengwa, marekebisho gani
zinahitaji. Waziri Magufuli ni dictionaray bwana katika
eneo lake. Sijamuona waziri namna hii barazani kwetu.
Uhodari
wa waziri unahitaji mwenyewe kujishughulisha kwa mambo yanayohusu
wizara anayoiongoza, lakini pia ana nafasi kubwa ya kujua mengi
akitumia wasaidizi wake; wakurugenzi wa idara, makamishna wa
kamisheni, wakuu wa taasisi na kadhalika. Akiwabana hawa, hakuna
kitakachomshinda. Hawezi tena kusimama pale barazani akaueleza
umma unaomsikiliza kwamba “sina takwimu hapa.” Wewe ni waziri
unao wasaidizi wako, unao wataalamu wako lazima wajue kila kitu na
wakujulishe wewe ili ujiweke makini ukiulizwa. Unajua katika
orodha lipo swali kwanini usikusanye faili zima la eneo hilo
ukaingia nalo barazani. Au unadhani wawakilishi wote ni kama wewe,
hawafanyi kazi zao za nyumbani vizuri kabla ya kuja barazani. Wapo
wenye uwezo mkubwa na ndio hao wakiuliza hawapati majibu ila
kuonekana wambeya. Kwa hivyo mwakilishi bora aingie na kusinzia tu
halafu asaini posho ya kutwa.
Yote haya
yanatokea barazani ikionyesha kuna tatizo kubwa la uwezo wa baadhi
ya mawaziri katika kufahamu shughuli za wizara zao. Kwa sababu
hawajali majukumu yao, na makatibu wakuu wao, wakurugenzi na
makamishna wao, wanawaacha vivyo wakome. Tatizo la uvivu wa
kufikiri, na uwezo mdogo wa kutenda, kama asemavyo Rais Benjamin
Mkapa. Wazungu wanasema true colour
inajionyesha!
Hakuna kingine isipokuwa
Zanzibar inahitaji mabadiliko ya kila namna na kila sekta ya
maisha ndipo itajitoa katika umasikini wa kujitakia. Ilionao ni
umasikini wa kujitakia kwa sababu inazo raslimali nyingi
zilizosaidia nchi kama Mauritius kujikwamua hata leo kuwa ya mfano
kwa Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mauritius ina kipato cha
dola 5,000 kwa mwaka kwa raia wake wakati sisi hatujafikia dola
300 kwa mtu.
Wao wana vifo 14 kwa watoto
wachanga katika kila 1,000 dhidi ya 102 tulionao Zanzibar. Maana
yake nini? Serikali ya Mauritius ina mtandao mzuri wa kujenga
uchumi wake na matokeo yake matunda ya mafanikio yanarudi kwa raia
zake. Wajawazito wanahudumiwa vizuri, wanalindwa dhidi ya magonjwa
kama malaria yanayoua wajawazito na wazaliwa wengi
Zanzibar.
Tofauti yetu nini na wao katika
raslimali? Wanayo ardhi nasi tunayo, wanayo bahari inawazunguka,
nasi tunayo ya kutosha, kwa hivyo wanategemea pia utalii, nasi
tunayo hazina ya kustawisha utalii. Wanao wataalamu, nasi tunao.
Nini sasa? Zile kelele zipigwazo na wahisani wakiwemo mataifa
tajiri zaidi duniani yaitwayo G8: tunapalilia rushwa, tunaviza
demokrasia, tunadharau utawala wa sheria, tunapuuza utawala bora
na tunakiuka haki za binadamu.
Serikali na
taasisi zake wanapodharau amri na maamuzi ya mahakama kama
inavyofanyika kuhusu suala la Abdalla Shariff wa Shakani
aliyehalalishiwa na Mahakama zote umiliki wa ardhi iliyovamiwa au
suala la Nasser Rashid Nasser (Cholo) aliyetakiwa asiondoke nchini
lakini ametoroshewa Dar es Salaam, maana yake nini? Wanajenga au
wanabomoa? Mambo matatu yanapaliliwa hapa: dharau ya mahakama,
uvunjaji haki za binadamu na ukosefu wa heshima kwa utawala
bora.
Serikali inapompa mtu kazi bila ya
kutangaza zabuni ilhali sheria ya zabuni ipo, inaporuhusu mtu
kuiuzia tofali kwa sh 600 badala ya sh 250 mpaka 300,
inapostawisha ukiritimba katika biashara ya mafuta huku ikidai
imeacha biashara huria, inapojenga kituo cha afya msituni kama
Founi Uwandani, na isipeleke daktari wala muuguzi, ni ukosefu wa
heshima kwa watu wake, ni uvunjaji wa misingi ya utawala bora. Ni
kuimarisha uozo na ndipo hapo wahisani wanapiga
kelele.
Itatuchukua karne nzima kuifikia
Mauritius kimaendeleo kwa mtindo huu. Wao wana uchumi mzuri kwa
sababu wametumia vizuri raslimali na si kuzifuja. Wanaopewa kazi
ya kuongoza wenzao hawatumii ubaguzi na uzandiki. Watapiga hatua
nyingi mbele sisi kutambaa itaendelea kuwa ndoto. Ndipo tunaposema
tunahitaji mabadiliko ili tujikwamue.
Awe mtu
ana uwezo wa kazi ndio ateuliwe kuongoza tangu chini mpaka juu.
Maendeleo yanaanzia kwenye nyumba. Tufike wakati mteuzi atafute
mtu kwanza na kumteua Sheha, badala ya kumteua Sheha na kumpa
kazi. Umetizama uwezo wake na uadilifu wake? Si kila mtu anafaa
kuongoza jamani. Vigezo muhimu!
Niliahidi
kuliendeleza suala la mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe,
Mwinyi Sadallah aliyepo Zanzibar, kutakiwa aombe radhi serikali
kwa kile alichokiripoti kutoka ndani ya Baraza la Wawakilishi
akimnukuu mjumbe wa baraza hilo. Wakubwa wanasema kilichoripotiwa
ni matokeo ya tafsiri potofu ya mwandishi wa habari. Eti alifanya
tafsiri potofu tu, si kwamba alimkariri msemaji sivyo.
Kuna
namna mbili katika maelezo yanayohusu suala hili yaliyotolewa na
Ikulu ya Zanzibar: kwanza Serikali inajenga picha ikitaka watu
waamini ya kuwa aliyenukuliwa na mwandishi hakutenda kosa. Pili ni
ile kwamba kosa limetendeka kwa mwandishi kutokana na kufanya
tafisiri ambayo kwao, Ofisi ya Rais, tafsiri inayodaiwa kufanywa
haikuwa sahihi.
Kwanza suala limefikia hatua
nyingine. Mwandishi anayejengewa hoja ya kufanya tafsiri potofu
hana haja ya kuomba radhi bali ni wajibu wa Mhariri wake. Barua
iliyotumwa kwa Mhariri ambayo imeambatanishwa na nakala ya
kumbukumbu (kitaalamu inaitwa hansard) ya Baraza, inamtaka
kufikia Julai 11 (Jumatatu) awe ameandika taarifa ya kuliomba
radhi Baraza kwa “kulisingizia.” Afanye hivyo katika ukurasa
wa mbele na kwa nafasi kama iliyotumika kutolea taarifa ya awali.
Akishindwa kutekeleza hayo, “hatua za kisheria zitafuata
mkondo.”
Duru za ufuatiliaji suala hilo
zimesema kwa makusudi ‘ngoma’ imetupwa kwa Mhariri wa gazeti
ingawa barua ya Katibu wa Baraza wa Wawakilishi ninayejua anafanya
kazi asiyoipendelea kwa suala hili, inamsema hivi mwandishi: “juu
ya tabia yake ya mara kwa mara ya kupotosha taarifa za vikao vya
Baraza.” Hapa Zanzibar aachwe mwandishi anayependa kupotosha
taarifa za Baraza, tangu lini? Mwandishi hajatenda kosa anaandamwa
atende, tena mara kwa mara, aachiwe? Jaguju. Ukweli ni kwamba
wakubwa wanajua fika mwandishi alifanya kazi yake vizuri lakini
yaliyosemwa ni machungu kuyameza.
Waandishi
wa habari Zanzibar tunajua mengi kuliko wakubwa wanavyofikiria.
Kwani hatujui kwamba kuna mtu anaitwa Salum Abubakar alipewa kazi
ya ujenzi sehemu, alilipwa na nani? Kuna mtu alitoa fedha mfukoni
kumlipa basi hili lisemwe hadharani?
Naam,
alikuwa mwakilishi Said Ali Mbarouk wa jimbo la Gando, Wilaya ya
Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba aliyetoa malalamiko kuhusu kitendo
cha Rais kukaa katika nyumba binafsi wakati Serikali inazo nyumba
tatu mjini Zanzibar kwa ajili ya makazi yake. Akatoa mfano wa kwa
hivyo rais akitoka Makunduchi serikali ijenge nyumba Makunduchi na
akitoka Tumbatu ijengwe nyumba Tumbatu. Kwenye nakala ya hansard
iliyoambatanishwa na barua aliyotumiwa Mhariri wa Nipashe,
maneno hayo hayaonekani. Sasa yamekwenda wapi?
Isitoshe
kwa kutaka aeleweke zaidi hoja yake, mwakilishi wa Gando alifanya
kutoa mfano kwa kumtaja mwakilishi wa Rahaleo, Hafidh Ali Tahir,
kuwa hivi naye akipata kuchaguliwa kuwa Rais basi naye aseme “nina
nyumba yangu Maungani nakwenda kukaa kule, hili ni tatizo, utakuwa
huu ni mchezo ambao hauwezekani, lazima tutamtaka tumuone hapa.
Ile sehemu ya serikali tutamtengenezea hapa kama ni rangi, kama ni
carpet, kama ni samani tutanunua kuhakikisha kwamba anakaa
katika nyumba ambayo ni standard kwa wakati huo itakuwa
lazima aishi. Hatutopenda kutoa pesa zetu kwenda kumtengenezea
nyumba yake ile ya ghorofa pale Maungani. Mhe. Spika, hili
nashauri kwa nia njema kwamba tulishughulikie.”
Inaeleweka
wazi kwamba kulikuwa na jitihada nyingi za kutaka mwandishi
abadilishe alichokiripoti lakini alisema wazi hana ila
alichokiandika. Alitoa kauli hii mbele ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyeita baadhi ya
waandishi ofisini kwake kuzungumzia suala hilo. Kwa kuona
mwandishi amesimama kidete na kwamba upo ushahidi wa alichokisema,
amekwepwa na kutupiwa mzigo Mhariri wake.
Kitu
kizuri katika suala hili ni kwamba wakati baadhi ya viongozi wa
juu walipohusishwa, kama ni mbinu chafu ya kutaka kuwaingiza,
walitoa indhari ya kuwa wanaweza kuja kukwama mbele kwa sababu
kila kitu kinajulikana. Hapa ni Zanzibar, sema na wenzako wanne
hata watano asubuhi, adhuhuri wanayajua wengine sokoni na
magharibi yamefika majumbani. Sisi wamoja tu ziwepo jitihada
nyingi vipi za kujaribu kututenganisha. Na hii itaendelea kadiri
tusivyokuwa na utawala mzuri nchini. Kwa Mwinyi mimi nasema heko
umeonyesha msimamo unaotakiwa na Mhariri hujaomba radhi nikiamini
huombi. Acha suala hili lifike mahakamani ambako mwandishi na
gazeti watapewa fursa ya kujieleza. Kitu kizuri na ukweli
utajulikana.
Baraza litumiwe vizuri kwa
maslahi ya umma badala ya kutafuta watu uchawi, kutungiana
majungu. Hiki ni chombo adhimu na muhimu kwa maendeleo ya watu,
kwa kubadilisha sura ya nchi. Nchi yenye chombo cha kutunga
sheria kilicho madhubuti, ina nafasi ya kupiga hatua ya kupata
uchumi mzuri, utawala bora, utawala wa sheria na heshima kwa haki
za binadamu, nyenzo muhimu za kubadilisha nchi kimaisha.
Mabadiliko ya maana yatakayolinda misingi ya uhuru wa kila chombo
kati ya vile vilivyo mihimili katika uendeshaji wa nchi, ndiyo
yanayotakiwa na umma.
Ends.
|