From: Zanzinet Admin
Subject: waraka kutoka unguja (fwd)




Mwaka 2005 uwe wa kuijengea Z'bar hatima

Waraka kutoka Unguja

Na jabir idrissa

Mwaka 2005 umeingia na umetuingilia huku tukikumbuka maafa ya kijinga yaliyotokea wakati wa uandikishaji wa watu katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Yale yalikuwa maafa ya kijinga kwa sababu kulikuwa na sababu nyingi za kuyaepuka.

 

Kama hujafahamu nini tunazungumzia kuhusu suala hili, hebu jiulize ni kwanini kuna utulivu mkubwa wakati huu uandikishaji unapoendelea katika Mkoa wa Kaskazini Pemba. Ukiwa ulisoma waraka uliopita umepata jibu. Nimeondoka Pemba lakini ripoti mbalimbali zinazonijia zinathibitisha kuna utulivu wa hali ya juu vituoni.

 

Kwa sababu hiyo basi, nachukua fursa hii kuwaunga mkono wote, iwe kwa makundi ya kibinafsi, mtu binafsi yake au makundi ya kitaasisi, waliochangia kustawi kwa utulivu kwenye vituo vya uandikishaji. Kutoka ndani ya moyo wangu, nawajuvya kuwa wanayotenda hata kuchangia utulivu huu, ndio uzalendo wa kweli.

 

"Uzalendo wa kweli" itakuwa ndio mkazo wangu mkubwa katika mwaka huu muhimu mno kwa Zanzibar kwa kuwa inaingia katika mtihani mwingine utakaoijengea hatima. Itakuwa ni hatma mbaya au nzuri. Kwanini?

 

Mara mbili, tangu kuingia tena kwa mfumo wa vyama vingi (Zanzibar ilikuwa na vyama vingi kabla ya Januari 12, 1964), wenye siasa za ushindani, Zanzibar imeshindwa kujenga jamii ya kistaarabu inayong'arisha demokrasia ya kweli, siasa za utengamano na mustakbali mzuri wa nchi. Hatujafanya uchaguzi mzuri hata mara moja, ingawa huwa tunaanza vizuri lakini tamati inakuwa ya mashaka matupu. Mashaka haya ndiyo yanakuwa chanzo kikuu cha matatizo yanayofuatia uchaguzi huo.

 

Hatukuwa na muafaka tulipoingia uchaguzini 1995 lakini baada ya matokeo kuwa ya mashaka matupu, na kwa kuwa mashaka hayo yalisababisha nchi kukwama kimaendeleo, na kwa kuwa watawala hawakuwa tayari kutumia nguvu ya utawala kutandika mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi wa 2000, tuliingia tu huku mashaka yakiendelea.

 

Muafaka wa 1999 uliosimamiwa na Jumuiya ya Madola, ukaonekana upuuzi mtupu. Hakuna wa kulaumiwa bali CCM ambao viongozi wao walisema mapema kuwa muafaka huo hauna mashiko. Kauli za kukebehi muafaka huu zilikuwa dhahir shahir upande huu. Kuteuliwa mjumbe wa kawaida wa Baraza la Wawakilishi kuusaini kwa niaba yao, waliona haitoshi kuonyesha dharau juu ya wananchi, wakazidisha kebehi kwa kauli nzitonzito ikiwemo ndani ya Baraza tukufu. Ikathibitika utayari kwa chama hiki ulivyokuwa bado.

 

Wa chama tawala wanaweza kuguna hapa, lakini ndiyo ukweli kwamba mapendekezo yaliyokuwa katika muswada wa sheria wa Mabadiliko ya Katiba ulioandaliwa (ilitakiwa uzingatie yaliyoafikiwa ndani ya Muafaka) na Serikali iliyotokana na Mapinduzi matukufu, ili upitishwe kabla ya uchaguzi ule wa pili, hayakuwa ya maslahi ya kweli ya wananchi wa Zanzibar, zaidi ya kuwa ya watawala. Huu ndio ukweli.

 

Muswada ungekuwa umetoa mapendekezo ya kuwezesha kuwepo mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi ulio huru hasa, wa haki kabisa, na ulio wazi kikwelikweli, mambo yangekuwa mengine. Na hili ndio tatizo letu la msingi; kutengeneza kitu kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar.

 

Mara zote hapa kwetu, kwa kuwa kuna viongozi wanaendekeza uhafidhina wa kutupwa, kinatengenezwa kitu kwa ajili ya kulinda maslahi ya wachache wenye nacho dhidi ya wengi wasio nacho. Hawa wasio nacho, kwa kuwa ni wengi kwa kila namna, wakionyesha kukataa kutumiliwa, ndipo mashaka yanapokuja.

 

Na inafaa tukubaliane ya kuwa kupinga kutumiliwa ni jambo la ukombozi wa nafsi na kwa maana tunayokusudia, kwa nchi kwa ujumla wake. Hivyo lazma watu wapinge kutumiwa kwa sababu wasipopinga wataingia katika dhima ya kuwa njia ya wengine kupanda ngazi. Ni hapa hapa hupenda nisisitize kuwa Zanzibar, kama keki, ni yetu sote na tuile kwa ushirika.

 

Hivyo kwa kuwa mashaka yaliendelea baada ya uchaguzi wa 2000, na kwa kuwa wasio nacho wengi walipinga kutumiwa kupandisha wachache ngazi ya kufaidi peke yao keki tulohulukiwa sote na muumba, vyama vikuu vinavyotugawa Unguja na Pemba, CCM na CUF, viliamua na viliketi.

 

Masikini! Vyama vyenye watu wa kufaa kuheshimiwa vilivutwa mpaka kwenye kona, vikawa havina pa kushika, isipokuwa kukaa pamoja, huku kila kimoja kikijua fika kwamba ni kazi ngumu kukutana meza moja. Lakini angalau wa CCM waliona wana dhamana ya ulinzi wa wananchi, lazma wakubali kukaa na watu ambao kwa bahati mbaya, wanaowaona si lolote si chochote.

 

Wakubwa hawa walipomaliza kutafakari makosa yaliyotendeka walitoa tamko mapema la haja ya kuendeshwa siasa madhubuti zinazozingatia maslahi ya nchi na watu wake. Tamko hili la Machi, lilihitimisha na Muafaka II uliosainiwa Oktoba 9, 2001 viwanja vya Ikulu. Laiti kama si dharau ya muafaka wa 1999, kusingekuwa na Muafaka II asilan abadan.

 

Upinzani unaposema hakutakuwa na Muafaka III si kwamba unatishia watawala, bali unawatanabahisha kutekeleza wajibu wao kwa nchi na watu wake kuweka mambo sawa ili uwanja wa ushindani uwe mwanana usiochoma. Kila chama kinapotia mguu kiwanjani, kusiwe tena na kupigana madaluga. Si tunajua kupigana madaluga ni dhambi mpirani!

 

Yaliyotokea Mkoa wa Kusini Pemba katika uandikishaji wapiga kura ni ishara kuwa bado tuna tatizo kubwa la wakubwa kutotaka mabadiliko. Huwa wanaamini kuwa wanachokisema wao kupitia vyombo vya habari vinavyowatumikia badala ya kutumikia umma, kitaungwa mkono na kila mtu tena kwa wakati wote, maana wao ndio walioshika hatamu za uongozi wa nchi. Ni wao peke yao hakuna wengine. Hatuna kingine ila kupata kiwanja mwanana cha kupambana kisiasa.

 

Wengi tunaamini mchawi wa Zanzibar angalipo. Naona hasa tungali naye karibu na anatafuta tu cha kufanya ili azidi kudhihirisha ubaya wake kwa nchi yetu. Huyu ni mchawi asiyetaka watu wa visiwa hivi watembee kifua wazi wakitamba kwa maendeleo ya kweli si ya hadithi. Kwao, wacha, waione Zanzibar inapiga hatua mwiko!

 

Wajua ikipiga hatua, nakusudia tukiwa na utawala mzuri, sheria zikisimamiwa kwa haki si kwa kelele za majukwaani huku watawala wakizipuuza amri za mahakama, huduma za jamii zikiwa imara kikwelikweli, njia zikiwa zinawaka lami kisawasawa si kwa kuhabatisha, na bandari ya Malindi ikiwa inasheheni meli kubwa na ndogo za bidhaa za kuingia na kutoka, hakutakuwa na mivutano ya kijinga, na isipokuwepo, wengi wa watu wanaoamini keki ni yao peke yao, watakuwa wameanguka puu ja ndege aliyehujumiwa.

 

Ndio unajua kwao siasa ni ajira, wasipokamata madaraka wameadhirika njiani. Si tumekuwa tukiwaona baadhi yao wanavyokufa haraka mara wanapotoka. Tunawaona hawa leo wanakodi milango ya maduka sawa na walalahoi, wanapanda gari za umma nasi, wanaomba nafuu ya bei ya vitu marikiti (sokoni), wanarudi kwenye baraza zetu walizokuwa wameziasi kwa sababu ya ukubwa. Wafanyeje? Ni kwa sababu walichokipata kimekwisha haraka wasivyotarajia kwa sababu kimetokana na dhulma tupu.

 

Kutetea mauaji ni aina ya dhulma na kwa sababu muumba aliapa anayeitoa roho ya kiumbe wake pasina kusimamia sheria aliyoiweka atamuadhibu naye, ndio tunaona wanaadhirika mitaani wakitoka ukubwani. Mauaji ya kijinga yanayotokea kutokana na mazingira ya ovyo yanayojengwa na watawala, hayakubaliki. Damu ya mwananchi wa Shumba mjini mwaka 1992, ya wenzetu wengine wa 2001, na hii ya Juma Omar Juma na Meja Ayoub Mohamed Suleiman itarudishwa.

 

Ukisema hivi watawala wanakasirika na kuishia kuandaa kesi. Wanaogopa kwamba watu wangali wanakumbuka maovu yaliyotendwa nao. Na woga zaidi ni kwamba wanajua kelele hizi zikiendelea, itatokea siku kweli itadhihiri. Na si uongo, ukweli utadhihiri siku moja kama tunavyoshuhudia kwa Mzee Pinochet. Yu kikongwe, lakini wapi Mahakama imempa nafasi ya haki yake ya kuhilikika kwa maovu aliyoyafanya, hata kama si kwa mkono wake lakini alikuwa kiongozi yakitendeka. Itakuwa hivyo hivyo.

 

Kwa hivyo mwaka 2005 ni wa uchaguzi. Kila chama kinatengeneza karata zake ili wakati utakapofika wazitupe kwa makini na kutegemea matunda makini. CCM na CUF tunavitarajia ndivyo vitakavyoendelea kushikana koo hapa kwetu Zanzibar. Vitaendelea kugombania kura labda 400,000 na kidogo za Wazanzibari. Wanatafuta nini vyama hivi kutoka kwa umma? Ulwa tukiamini ni kwa ajili ya kutumikia watu ambao takwimu zinaonyesha zaidi ya nusu yao wanaishi chini ya kiwango cha umaskini kinachotakiwa na mataifa.

 

Wengi wetu tunaishi bila ya kula milo mitatu kwa siku. Maana yake hatuna siha ya kupambana na raia wa mataifa mengine katika ulimwengu uliojaa ustadi katika kila nyanja, hata ya ujambazi, kwa sababu ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Hakuna biashara, hakuna soko, hivyo hakuna uchumi unaoweza kutuhudumia hivi tukiendelea kuzaliana kwa sababu kwingi hakuna umeme watu ikiingia magharibi wafanyeje kama si kulala.

 

Tunajigamba mijini tu huku wenzetu kule Kiuyu Mbuyuni, Maziwang'ombe, Shumba Viamboni, Makangale, Msuka (Wilaya ya Micheweni), Gando, Mgogoni, Kinyasini, Fundo Kisiwani, Ole dodo (Wete) wanalala gizani kila siku. Tuko katika mpumbao mkubwa mijini kwa sababu wenye hatamu hawawajibiki kuhudumia walio masikini vijijini. Akinamama wanatembea masafa wakitafuta maji, vinginevyo waendelee kutegemea maji ya kisima.

 

Mkulima wa Micheweni lazma aende mjini Wete kuuza viazi na ndizi zake kidogo maana hakuna soko karibu naye. Mvuvi alazimike kusafiri kwa miezi mitatu nje ya anapoishi akihangaika kutafuta soko nchini Kenya. Kipindi hicho mama na watoto wake sita saba anamtegemea nani? Dunia ilivyoharibika jamaa mara anaoa kule hata bila ya kupima virusi, analeta nini nyumbani? Ukimwi.

 

Ndivyo anavyoteseka mwanamke wa Kizanzibari wa kijijini. Anaachiwa familia kubwa huku waume wametoka kwenda kuchuma mbali kwa sababu karibu nao mazingira ya biashara, ya kilimo, ya uvuvi, ya viwanda, yamevurugwa kwa sababu ya utawala mbovu.

 

Lahaula, hali ya Micheweni imenisitikisha na wenzangu tukiwa katika semina ya kutathmini vipi sisi waandishi wa habari tunaweza kufanya kusaidia kuondolewa umasikini. Unakuta mtoto wa miaka kumi hana shule, eti katumwa mjini kuja kununua vidonge vya Panadol lakini amepewa sh 20. Ataipata wapi? Unamuuliza umetumwa kweli dawa, anakujibu "ni kweli amenituma mama maana ndugu yangu anaumwa homa." Umepata kusikia kinachoitwa malaria kupona kwa kidonge hiki? Hiki si ni kidonge cha kupozea tu nguvu za malariaquine au zile zinazoitwa za kisasa zinazosumbua waumwaji kwa kuwamaliza nguvu? Ndio lakini afanyeje mtoto huyu na ametumwa?

 

Unamuona alivyo mchafu si wa nguo tu bali yaonyesha hajakoga kwa siku mbili tatu, lakini usiulize kama amekula asubuhi. "Sijala kaka." Ikiwa ni wewe utafanyaje? Unazo za kumpa kutosha kupata vidonge? Unafikiria vidonge vitamezeka kwa mtoto ambaye hajala kitu na maziwa kufuani kwa mama yanatoka kwa shida kwa sababu ya njaa pia. Utoe tu japo kidogo kumsaidia. Huyo unampa angalau sh mia tatu. "Unasikia hii mia kanunue dawa lakini hizi nunua unga pale ukampe mama mwambie hii zawadi kutoka mjini tupike uji tunywe." Eti ndio tunaondoa umasikini hivi. Na siku inayofuata?

 

Basi haya ndiyo maisha ya watu wengi wa vijijini Unguja na Pemba. Hawawezi kupata milo mitatu, hawana umeme, hawana maji safi na salama, wakiumwa hawana dawa maana hawana uchumi nyumbani, ingawa wamezungukwa na mikarafuu, bahari kubwa inayotambaa kwa masafa na fukwe murua za kuchochea watalii kutesa kabla ya tsunami kuhamia. Pembeni mwao kuna ardhi ya rutba kwa kilimo, kuna ardhi haina rutba lakini ikitengenezwa itazalisha kama si mazao ya kilimo, basi viwanda vidogo vya usindikaji samaki, mbogamboga na matunda mtawalia tuliyonayo.

 

Leo Pemba inafikia wiki haina umeme kwa sababu hakuna mafuta ya kuendeshea vinu vya umeme vya Wesha. Na hapa inasingiziwa tsunami imeleta fadhaa baharini kwa hivyo eti meli haijafika kutoka Mombasa? Meli ya mafuta ilitumwa lini wakati gharika ikija tayari inajulikana mafuta ya IDO yatakwisha? Mambo ya wakubwa wakipata zulia wanaficha uzembe wao. Ndivyo tunavyokwenda karne ya 21. Tubadilikeni maana inawezekana. Au kwanini haiwi? 

 

Ni kwa sababu hatuna wataalamu wazalendo, hatuna nyenzo kweli kama tunavyoendelea kuambiwa tungali katika nchi changa na demokrasia haiwezekani kwa sababu tungali na njaa matumboni? Si kweli. Vyote tunavyo, tunao wataalamu maana wapo Wazanzibari kwa mamia nje ni wataalamu walisomeshwa na serikali yetu lakini walibezwa wakatimkia huko. Wana hamu ya kurudi lakini waje kufanya kazi na nani?

 

Tukubali hatuna ukweli, hatu wazalendo wa nafsi zetu wala nchi. Tunajidai tu kuipenda huku moyoni tunajipenda wenyewe tu. Ofisa wa serikali anajua kumhamisha mtumishi atapaswa apatiwe mafao kwanza, analazimishwa ahame kwanza, asipohama anafukuzwa. Walifukuzwa kwa mamia baada ya uchaguzi 1995, leo wanarudishwa kwa shingo upande. Barua zao hazijawafikia kwa miezi miwili eti hawajulikani walipo? Walifukuziwa wapi mwituni? Kinachotafutwa washindwe kuripoti mapema wafukuzwe tena.

 

Basi ni kufukuzana tu kazini, na ukiwa si CCM ndio utajuta kuzaliwa au kuhamia Zanzibar. Siku hizi hakuna kazi, nafasi ya kusoma nje, wala nini kama hakuna uhakika u mwana CCM kidhati. Wakubwa wameweka mtandao wa kutafuta mizizi ya muombaji kazi, baba yake, babu yake, na waliowatangulia. Kisa? Unatafuta kazi. Usiondoke ukaenda nje unakotakiwa. Mamia wako nje kwa namna hii.

 

Tunataka uongozi utakaowaona hawa ni hazina, warudi hata kwa ahadi ndogondogo za kuwapatia nyumba hizi mpya zinazosubiri huruma kugaiwa. Wawekwe pale, wapatiwe gari mpya mpya zinazoshindana kwa honi mpaka vichochoroni nyakati za usiku. Wapatiwe wafanye kazi ya umma badala ya kuziachia zikipakia vimada na watoto wa kimayai. Nyingine (hasa za wazi) hupakiwa miche ya migomba, makaa na vifaa vya ujenzi siku za Jumamosi na Jumapili, safari za wapi? Sehemu ambako wakubwa wanajenga mahekalu.

 

Tuwe wakweli tukitambua kuwa kuna kundi la wenzetu hawana chakula cha siku na hawana pa kutegemea ila hapa nchini kwao. Tuonyeshe utu kwa kuwasaidia kwa kila mtumishi na alipo. Nafasi aliyonayo ajue yaweza kushikwa na mtu kama yeye hivyo asiwe mungu mtu; atumikie watu. Tuondokane na ubwana na utwana ambao kwa bahati mbaya umerudi maofisini kwa sura mpya baada ya kusokomezwa kupitia mapinduzi. Mapinduzi yenyewe ni ya miaka 40 lakini nchi inarudishwa nyuma kwa zaidi ya miaka 100. Ajabu na kweli. Itaendelea kwa hapa "Heri ya mwaka mpya 2005."

Ends. 


_______________________________________________
Zanzinet mailing list
Zanzinet@zanzinet.org
http://www.zanzinet.org/mailman/listinfo.cgi/zanzinet


Visit ZANZINET Web Site