Ajabu ya Mtawala
Date: 26 Mar 1999
Kuongopa hadharani, huwa ni kubwa khatia
Tena ni kukosa soni, pia ila kujitia
Hasa mshika sukani, mbele alotangulia
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli
Ni dhamana kuikhini,na kukejeli sheria
Kuwafanya punguwani, watu walokuchagua
Mwenzetu wajiamini, hujali kitofatia
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli
Yalosomwa ukumbini, risala ukasikia
Kisha kusema mageni, eti ndiyo wayajua
Wachekesha Bin-yamini, mche mwenye kuumbua
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli
Kwamba ile tafrani, wewe hukuisikia
Amri ya Parokoni, msiba ilotutia
Kumbe mtawala gani, huyajui ya raia
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli
Hatuna matumaini, kuwa utafatilia
Ni mbinu kutuzaini, ili tupate tulia
Asokujueni nani, ghiliba na zenu ria
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli
Tulikwisha wabaini, matendo na zenu nia
Mliyaanza zamani, wewe unayarukia
Nyerere na wakoloni, walipita hiyo njia
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli
Tumeshakula yamini, nyuma mwiko kurudia
Wala haya hatuoni, yetu kuyapigania
Mnayokula sahani, sote tutaichangia
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli
Saif Issa Al-Meskiri
Date: 27 Mar 1999
Shairi limetulia, Mtunzi kaelekeza
Ujumbe metufikia, Mambo yote kamaliza
Nikilisoma nalia, Mchozi napukutiza
Mola atatujalia, Subira nyoyo kujaza
Wasiwasi nilonao, Muwafaka kupuuza
Tutajitwika vilio, Njia njema kuibeza
Kwa uchaguzi ujao, Hasama twakiribiza
Naomba neno la leo, Hakiba naiwekeza
Moyo unanitetema, Uchaguzi nikiwaza
Sipoondoka hasama, Vipi tutazungumza
Utabaki vipi wema, Kwa shari isipovizwa
Twakaribisha nakama, Muwafaka kuubeza
Mashahidi nawataka, Neno kuakibiza
Mwakani mtakumbuka, Damu ikitunukiza
Nia ni kulisindika, Na sio kuliombeza
Ila Mkapa hetaka, Salmin kamaliza.
Kurudisha Barazani, Muwafaka kumaliza
Ni dane dane yakini, Kabumbu kukokoteza
Goli kuwa kimiani, Ushindi kudanganyiza
Ila ukweli yakini, Kesho yetu twaiviza
Ally Saleh