.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Kifo Chake Zanzibari

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Kifo chake Zanzibari

23 may 1999

Nakualika hitima kifo chake zanzibari
Barua nayotuma ikufike jemadari
Ujule yanahima kufika uwe tayari

Tokea ulipo hama miaka ya dahari
Twalizidi kuzama maradhi makiriri
Daima kanaumwa kipenzi zanjewiri

Dawa zimekoma nyingi zenye kheri
Kensa imezama mauti yamejiri
Kaondoka daima mama zanzibari

Tulijaribu mapema kutibu kwa siri
Tukafanya hima labda tunusuri
Imetufika lawama kwanini tusisubiri

Mauti yake mama lilobaki nikaburi
Nalo walisakama wamo wamevinjari
Kulichimba hekima eti lina hatari

Upenuni wamezama wamo wanakariri
Mpango wametima tena upo tayari
Pengine utajinyima hitima wakihairi

Njoo tenda hima japo sema kwaheri
Usisahau ugema ndugu yangu jemadari
Kifo chake zenjibari kudumisha jamuhuri

Naomba kisha soma nijuze si tahayuri
Najuza kwa taaluma na wingi wako habari
Rais kuwa daima katiba twaisubiri

Namaliza nazizima nuru ya taa bahari
Kila nachosema ujue kiko tayari
Kaeni mkiyapima wazenji mtafakari

Mchache wa elimu

Baja

Kifo chake Zanzibari

24 may 1999

Wingu latanduka

Msiba huu na ule - zinjibari natamka
Mwanangu bado sifile - usinizike haraka
Jua lachomoza lile - wingu lile latanduka
Mwangaza ni ule pale - warudia kumurika

Kupatwa na masaibu - ni hikima za rabuka
Mitihani ya ajabu - wanangu kuweweseka
Hata mengine aibu - wanangu kubabaika
Ile mwanangu jawabu - ile pale ishafika

Subiri hebu ningoje - nitizame nainuka
Na hata nijikongoje - nipo kama mwanitaka
Wanangu nataka muje - moyo utafarajika
Ni machungu yalioje - wanangu kuatilika

Ni kama nyota angani - zinjibari namurika
Ninusuru ya manani - amina na muafaka

Saleh

Uhai wake Zanzibari

24 may 1999

Imenifika hilaki na mzigo wa lawama
Nje hakutokeki ndani kunanisakama
Jua sisameheki kwa maneno nilosema
Laiti ningehakiki katu singe nayasema

Kuona mahatuti ndipo pale katetema
Kadhani kuskuti nikutokwa na huruma
Mengi yamezatiti taabani wetu mama
Nikaona ya laiti tujiandae kwa hitima

Dawa iliyo smati mtini mlipo chuma
Nahizo zilonyeti zanafuu yake mama
Mnajuaje kizati afya yake ya daima
Kuwa hayamfiki mauti wetu mama

Muafaka sishariti wakulinda uzima
Wala simadhubuti kumponesha mama
Naona ndio tamati pemba weshasema
Marufuku kuketi wale walosimama

Ugonvi na tashtiti waendelea daima
Atasaini najati karandasi mlotuma
Lakini sikusaliti kasema mama salama
Nyumbani mikakati wapanga maziko mema

Katu sijamsaliti moyoni mapenzi ya mama
Nampenda marati mama awe mzima
Khofu imenizatiti akilini yanichoma
Naomba masahamati kama mama yumzima

Mchache wa elimu

Baja

Kifo chake Zanzibari

24 may 1999

Salaam

Nakushukuru mama kukiri kuwa uhai
Ya kuwa bado mzima ingawa ulizirai
Nzima yako kalima wanywa halua kwa chai
Na tena umesimama ya nyuma tena hujui

Kusema ku muangaza mwanao nimefurahi
Kusafika kwa giza kabla staftahi
Na vishindo kuchagiza jioni na asubuhi
Afyiayo kuchapuza mambo yetu kuyawahi

Uwambie ndugu zetu wasizue umekufa
Warudi nyumbani kwetu waje ziziba nyufa
Zinavuja nyoyo zetu kalafati kujazifa
Wasikimbie msitu zapungua zao sifa.

Mama useme sana kuwa dawa wahitaji
Wazilete kwa shehena waufanye ni mtaji
Waache mbuzi kuchuna unazama wetu mji
Yarabi ya subuhana tujazie mahitaji

Iwapo dawa tafika mama yetu hakikisha
Maishayo taokoka maradhiyo kusafisha
Donge nako tutafika hata kule kwetu wesha
Mama tamka hakika kwa kuwa muda waisha

Ally saleh

Barua ya muafaka

25 may 1999

Barua uloandika katika mwezi wapili
Umetuma menifika siku jumapili
Kukujibu ninataka kuanza kuinakili

Maneno mepangika mistari ya jamali
Nakshi zakushuka mezipanga kweli kweli
Lakini nina shaka mawazo kuyakubali

Umesifu muafaka eti njema dalili
Tena warukaruka wausifu kula hali
Wazipuuza shaka kwa pupa yakukubali

Maoni nakupa shika japo mimi nikombali
Daima kuaminika watu hao ni muhali
Chunga weka shaka muafaka mushkeli

Khofu moyo menifika madhubuti kwa dalili
Miaka iloyoondoka ulishinda kila hali
Kiti chako kakutoka kwa maguvu ukatili

Basi nakupa shika busara hii kalili
Muafaka tarajika uwe kitu cha halali
Lakini ukivunjika takulaumu dalali

Machozi tanimwaika nachelea udhalili
Kuchukua uloweka sikama kutupa mbali
Kama huo uhakika cheo chako ufahali

Kalamu yangu naweka kwa karatasi yapili
Majibu yako nataka japo maneno mawili
Uyatume kunifika yanitulize akili

Mchache wa elimu

Baja

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet