|
|
Mapenzi!
Date: 12 November 1999
- Mapenzi kitu ajabu, ni shani yake Manani
Hayahitaji sababu, sababu ilo makini
Hujimwaga bubububu, bububu maji ya pwani
Watu wakataajabu, kilichokupata nini!
- Hayahitaji dhahabu, mapambo mingi mwilini
Au wingi wa adabu, adabu za kizamani
Jamani mapenzi tabu, tabu yake huioni!
Mpaka uwe karibu, karibu yake mwendani!
- Mapenzi yakikusibu, yakasibu mtimani
Wageuka kuwa zubu, kwa wingi wa hamkani!
Wataraba kama dubu, dubu lisilo makani
Bila wako mahabubu, hakika umashakani.
- Mapenzi kama zabibu, zabibu mbivu mtini
Hata yawe ughaibu, utayafata kwa kani
Humsemesha na bubu, mapenzi akibaini
Wala hayana ubabu, ujana wa kizamani!
- Mapenzi si madhehebu, ya fikira au dini
Mapenzi si ustarabu, si haiba wala fani
Mapenzi si ukatibu, cheo hakina thamani
Mapenzi yanaghilibu, ajabu hii jamani!
- Hayana utaratibu, mapenzi ni maluuni!
Mapenzi kisebusebu, na kiroho mkononi!
Mapenzi ni merikebu, isiyo nahodha ndani!
Au punda mwenye nabu, hatari iso kifani.
- Mapenzi hayana jibu, mapenzi si mtihani!
Mapenzi sio kitabu, cha kusoma darasani
Mapenzi si aghalabu, kuwa sawa duniani
Imechoka yangu nibu, kalamu naweka chini.
Hassan Ali,
Ottawa.
|