.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Kitendawili Natowa

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Kitendawili Natowa, Mwenye Bongo Kuchambuwa

Date:  01 July 2000

(a) Natowa kitandawili, mwenye jawabu kutowa
Wako watu sura mbili, majaraha yasopowa
Kuchupa kwao kuwili, nyoyo zao zaunguwa
Watakayo ni muhali, milele hayatokuwa.

(b) Akili zao ni ghali, kutu zinawasumbuwa
Wapigana na makali, mwenye fani hupekuwa
Warejea ya awali, hawavuki zao puwa
Wala hawana muhali, wamegeuka viluwa.

(c) Wanapeta pili pili, ungó wao chandaruwa
Upungufu wa akili, ukweli kuutambuwa
Wasemavyo waawali, wengine wajisumbuwa
Hatari yawakabili, kuviwasha vilopowa.

(d) Mkahawa sihoteli, kushindana kutambuwa
Dibeti zisoukweli, mtuno wakitumbuwa
Kisu kutiwa makali, mwerevu anang´amuwa
Ukweli muukubali, mwiko mwenziwe upawa.

 

wakatabahu

Hashil S. Hashil

 

Kitendawili (Jibu...)

01 July 2000

 

1. Watu wenye sura mbili, unao wasimulia
Si watu ni makubeli, wako tayari kuua
Tukae nao kwa mbali, roho wasije zitoa
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.

2. Wasifu wao tumbili, kila mti wachupia
Vipando vyetu halali, haweshi kuvivamia
Tena wafanya kejeli, majumbani waingia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.

3. Hawajali hawabali, wendekeza ya dunia
Nyoyo zao za jabali, imani 'mewapotea
Wanajikumbizia mali, nundu zao za ngamia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.

4. Asiyemcha Jalali, Muumba wetu Jalia
Hafai hastahili, kuwaongoza raia

Isiwe mara ya pili, fursa kumuachia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.

5. Beti tano ni kamili, kuongeza sina nia
Kwa chako kitendawili, jibu nimekutolea,
Nambie ewe Hashili, kama nimekipatia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.

Wassalaam,

Hassan,

Ottawa.

 

Kitendawili (Jibu...)

02 July 2000

Bwana Nidhamu nikweli Maneno uloyanena
Kweli umeona mbali Sina haja ya kusema
Ni lazima nikubali Nchi ilivyoinama
Watu hawa hawajali Na kuamini kiama

Na wewe bwana hashili Ni kweli kwamba waona
Umefunguwa kufuli Ya shaba si ya kubana
Manenoyo msumali Yaliyo jaa heikima
Watu hawa hawajali Na kuamini kiama

Hujafanya utapeli Mengine kuyamung'unya
Watu hawa hajali Raia wanavyoguna
Wagawana kila hili Bila kisisi kuona
Watu hawa hawajali Na kuamini kiama

Mali ya nci kwa meli Zakimbizwa kwa mapana
Ikiwa si ujangili Tuna lipi la kusema
Wanatucheza akili Kuamini wanonena
Watu hawa hawajali Na kuamini kiama

Hulaumu wafadhili Na wainzani bayana
Kelele za kweli kweli Eti wamewanyang'anya
Misaada ya gendeli Walotaka kugawana
Watu hawa hawajali Na kuamini kiama

Wahisani ni kivuli Wenyewe wanafichana
Kazi yao ni ushali Huku wakineemeshana
Na tena ni makatili Chembe imani hawana
Hawa watu hawajali Na kuamini kiama

Wajilimbikizia mali Kutuletea nakama
Bila ya kuona mbali Japo wesimama wima
Wajifanya madalali Nchi yaenda mrama
Watu hawa hawajali Na kuamini kiama

Wenzangu msinijali Mimi si tunzi mwema
Nawaacha mafahali wenye ujuzi na hima
Natokomelea mbali Wasije wakinilima
Hawa watu hawajali Na kuamini kiama

Peku

 

Kitendawili (Jibu...)

03 July 2000

(1) Kuzama kwenu hatari, fumbo mumelifumbua
Msemayo kama nari, jiji laweza ungua
Viongozi wenye mori, vizuri kuwapekua
Mwaka huu watapowa, kiburi kitapungua.

(2) Vijana wanavinjari, kuzikata zao pua
Hakuna tena Mapuri, wala kucheza kilua
Ikiwa shari nzuri, machozi yatapungua
Mwaka huu watapowa, kiburi kitapungua.

(3) Mw. Hassani hodari, uchambuzi wamurua
Watu hawa ni washari, nikweli wawezaua
Ubani wao hirizi, ukiwashwa waungua
Mwaka huu watapowa, kiburi kitapungua.

(4) Mw. Peku uchakari, kwa fani ulotungua
Maneneyo yanasiri, yai hapa laangua
Pia hawa majangiri, wananchi kuwajua
Mwaka huu watapowa, kiburi kitapungua.

(5) Kadi tama ninakiri, foleni naimegua
Mchango wenu hariri, hakuna kilopungua
Hazina zenu shairi, kofia tunazivua
Mwaka huu watapowa, kiburi kitapungua.

Ndugu yenu

Hashil S. Hashil

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet