Salmini hasalimiki!
1 March 2000
Mwendani sinishitaki, likupatalo nyamaza
Mimi sitokushiriki, wala sitakuuliza.
Kula mtupa tariki, hawachi kujipoteza
Asiyetaka kufunzwa, hasalimiki na jambo.
Nalikwambia kitambo, mwendani wangu sikiza
Sicheze na mawi mambo, ukanambiya 'tateza.
Leo mwapigana kumbo, kula wendapo husoza
Asietaka kufunzwa, hasalimiki na jambo.
Ulijifanya mwerevu, kulla jambo waliweza
Kwa kutamaniya nguvu, akili ukapoteza
Leo yamekua wavu, tatizi mekutatiza
Asietaka kufunzwa, hasalimiki na jambo.
Nalikwambia latisha, ukapinga tangu mbele
Na leo limekutwesha, vumilia vilevile
Mwiba wa kujitonesha, mtu haambiwi pole
Aso-onyeka milele, hasalimiki na jambo.
A. Cali