Malipo Yakidhihiri!
Date: 3 Feb 2001
- Malipo yakidhihiri - Hayamjali hodari
Huwafika majabari - Wenye nguvu wajeuri
Hubana wasofikri - Waharibifu washari
Piya wasio dhamiri - Madhalimu mashuhuri
- Malipo yakidhihiri - Hayataki ushauri
Huvunja wenye viburi - Wapendao ufakhari
Huwasibu matajiri - Wa inadi na ghururi
Piya wasengenyi siri - Hata laghai waghuri
- Malipo yakidhihiri - Hutesa yakaathiri
Hukumba yakaadhiri - Mafatani watiriri
Huliza walovinjari - Kwa vitimbi vya dhahiri
Piya wapenda khabari - Waso na niya tahuri
- Mlipaji ni Qadiri - Alotuumba Qahari
Jirudi mja ukiri - Mabaya hayana kheri
Tubu usifanye ari - Tubu kwa Mola Ghafuri
Mabaya ayaghairi - Ulipwe mema mazuri
Saleh Barkey
Limetungwa 20th August, 1992