.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

When One of Us!

 

 

 

 

 

 

Related links

 

When one of us!

28 Dec 2001

 

When one of us, amekosea akateleza
We need not fuss, baina ya wetu wenza
'Cause it's not righteous, kumhukumiza
Farka ikihanikiza, can break all of us.

Let's not pass, hukumu za kumliza
Lest we miss, baraka zake Muweza
'Cause in this mass, wajibu kujituliza
Farka ikihanikiza, can break all of us.

Mails with virus, zitakapojitokeza
Might not be intentious, huko zilikoanza
'Cause what's not obvious, ni kama usiku wa kiza
Farka ikihanikiza, can break all of us.

Better be judicious, na uanze kuuliza
Be then gracious, wajibu wako timiza
'Cause its fatuous, machafu ukijibiza
Farka ikihanikiza, can break all of us.

This forum is famous, kwa kutoa muangaza
This is not circus, si vyema kujitangaza
'Cause each one of us, wajibu kumliwaza
Farka ikihanikiza, can break all of us.

 

Kassim

When one of us!

29 Dec 2001

 

Kasimu si sawa vile - Kaa hili ulijuwe
Ninasema kwa kelele - Tena napiga mayowe
Wauharibu mchele - Kuutiya changarawe

Mshairi mraibu - Kasimu kama si wewe
Wanagenzi si sababu - Lilo silo liridhiwe
Watusemesha mabubu - Tugombe lako lisiwe

Ulinuwiya muruwa - Virusi wadhibitiwe
Ila hukudunda sawa - Mserego si msewe
Tungo bwana kama dawa - Miko musiipinduwe

Samahani

Saleh

 

When one of us!

30 Dec 2001

Salamu natanguliza, wastahiki malenga
Msije nipatiliza, mimi mwezenu mchanga
Yale yaliyonikinza, yasije yakanifunga
Limewaudhi malenga, shairi la kingereza

Yale niliyoyaanza, ya ugeni wa kutunga
Naona yameniponza, hapa ndani ya kiunga
Mmeanza kupaaza, na huku mkinizonga
Limewaudhi malenga, shairi la kingereza.

Lipi lililochukiza, kati ya niliyoronga
Nyoyo lisiloliwaza, wala lisilozikonga
Dosari lililokoza, kuwashinda manyakanga
Limewaudhi malenga, shairi la kingereza.

Bado ninawauliza, nini mnachokipinga
Na kama nimeteleza, lugha mbili kuziunga
Wajibu kuniongoza, na sio kunisimanga
Limewaudhi malenga, shairi la kingereza.

Mimi bado najifunza, vina vyangu kuvipanga
Ili nipate suuza, sirudie kukuunga
Nitunge tungo aziza, sio zile za kulenga
Limewaudhi malenga, shairi la kingereza.

 

Maa salaam.

Kassim

 

When one of us!

30 Dec 2001

Kasimu wewe si kinda - Matunzi wayajuliya
Kwanza wejifanya nunda - Tupate kukaripiya
La sasa nimelipenda - Shairi limetimiya
Pete huvishiwa chanda - Siyo kidole cha gumba

Tungo ni raha na pambo - Fasaha Sawahiliya
Ukingonjera Kimombo - Nani atakusikiya
Bwana usizuwe mambo - Kakeyo nakuusiya
Pete huvishiwa chanda - Siyo kidole cha gumba

Kila chombo na wimbile - Tega sikiyo sikiya
La umombo likimbile - Virusi watuvamiya
Kiswahili kisifile - Hebu bwana zingatiya
Pete huvishiwa chanda - Siyo kidole cha gumba

 

Saleh

 

When one of us!

30 Dec 2001

hakuna alokereka, ewe kasimu sikia
binafsi kwa hakika, tungoyo meshangiria
namna livyopangika, kwa hesabu za murua
lile tulilolitaka, ni jina kulipatia

kila liloteremka, kutoka kwake Jalia
na haya yalofanyika, na viumbe wa dunia
tangu zama na miaka, jina asilia
lile tulilotaka, ni jina kulipatia

mtoto napozalika, jinale hutangulia
huo ndio muhalaka,tunaozungumzia
hatupingi kwa hakika, tungozo kutuletea
lile tulilolitaka, ni jina kulipatia

wali uliopikika, na choroko kuutia
kwa kwetu sie msuka, mseto huitwa pia
japo ni wali hakika, na sie twautambua
lile tulilolitaka, ni jina kulipatia

ukingoni nimefika, siwezi tena tembea
uzee umetushika, miaka yatukimbia
mkongojo nautaka, ili nipate hatua
lile tulilotaka, ni jina kulipatia

 

Mbarouk

N.York

 

When one of us!...Hulalaje?

31 Dec 2001

1. Nawakhubiri malenga - Mulotanda kiungani
Ni vipi jama mwaringa - Waila hamuyaoni
Murikeni zenu panga - Tungo zenda Uzunguni
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

2. Mwenetu hodi kabisha - Kwa tungo ya walakini
Miye henibabaisha - Ati muhali wa nini
Papo nikamkatisha - Arudi ajimakini
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

3, Sisemi kadhamiriya - Hamdhulumu mwandani
Bali kakoseya njiya - Kama sivyo nikanyeni
Kizungu kikiingiya - Tungo zetu buriyani
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

4. Ninaowakusudiya - Wahenga ZANZINETINI
Ikiwa mumesikiya - Ilimu musitukhini
Na kama yawaridhiya - Pia hayo twambieni
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

5. Simsimangi mwenetu - Alonasa mtegoni
Bali kuna hao watu - Haya wanayatamani
Waifuje lugha yetu - Watuvuruge zizini
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

6. Uwapi mwenye maqamu - Nikupendae moyoni
Profesa Burahimu - Nuru Sharifu huneni
Tuwaidhi mahashumu - Naungulika rohoni
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

7, Uwapi bwana nidhamu - Wa Ali bwana Hasani
Mwenye tungo tamu tamu - Lughayo pekee fani
Njoo nawe muadhamu - Usisite ukingoni
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

8. Mbaruku wa Sharifu - Vipi wangu muhisani
Uliyonena khafifu - Hebu lenga mbeleni
Ugunduwe udhaifu - Mwewe kalenga uwani
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

9. Inukeni wamahiri - Nyote mulio wavuni
Najuwa muko kathiri - Muliyonayo semeni
Kizungu hakiwakeri - Kuingizwa matungoni
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

10. Tama nasitiya hapa - Nawaomba samahani
Musinidhani narapa - Ninakatika maini
Kazi sasa nishawapa - Ibukeni ajizini
Hulalaje na maiti - Hata chozi usitoke

 

Saleh

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet