Paukwa Pakawa!
Date: 04 April 2001
(m) Mwenye nadhari, huwaza, musingie ujingani
Havamii kutangaza, hupekura kwa makini
Mtama wautandaza, almasi uwanjani
Kuku hapo atacheza, mate yako mdomoni
Darumini yaangaza, nikipi akithamini.
(n) Nalikwenda matembezi, mji waitwa nakama
Nikakumbana na wezi, washindana kumkama
Ndama nuru kama mwezi, nikabaki kutizama
Nikajifanya kurunzi, kiwele anacho mama
Nyinyi kweli ni machizi, wakabaki kulalama.
(u) Usiku kwao mchana, sifa nyengine hawana
Ndoa zao kuachana, nanishani kuvikana
Kuteleza uungwana, mipango yao ya jana
Kila kitu wanakana, pembeni wasengenyana
Mambumbubu wamaana, kazi yao kugombana.
Hashil