.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Ya Rabbi Mola

 

Related links

 

Ya Rabbi Mola

Date: 16 June, 2001

  1. Ya Rabbi Mola Faridi, nakujia ni dhalili
    Ya Rabbi Mola Wahidi, nimejaa ujahili
    Ya Rabbi Mola Wadudi, wanitesa ubakhili
    Kwa nini sikudhukuri, mimi ni mali ya nani?
  2. Ya Rabbi Mola Jalali, unitoe ujingani
    Ya Rabbi Mola Kamali, nimeshindwa mtihani
    Ya Rabbi Mola Zamili, nimepotea jangwani
    Hutanitupa njiani, kwani mimi ni wa nani?
  3. Ya Rabbi Mola Karimu, sili sinywi cha haramu
    Ya Rabbi Mola Rahimu , kamwe siishi dawamu
    Ya Rabbi Mola Adhimu, sina kitu mahamumu
    Nileje kitu si changu, nami ni mja wa Mungu?
  4.  

    Ahmed Rashid

     

    Ya Rabbi Mola

    Date: 16 June, 2001

      Ya Rabbi ya Rahmani nirehemu mja wako
      Ya Rabbi mola Manani ninaomba toba yako
      Ya Rabbi mola Amini ghufrani sifa zako.
      Kwa nini sikudhukuri ewe wangu Mwenye enzi.

     

    Amour Nasser

    Ya Rabbi Mola

    Date: 16 June, 2001

    1. Ya Rabbi Mola Alimu, sitiri madhambi yangu
      Ya Rabbi Mola Qayyumu, unilinde na machungu
      Ya Rabbi Mola Hakimu, nayaogopa marungu
      Nitatendaje ithimu, na siku kiko qiyamu?
    2. Ya Rabbi Mola Razzaki, nipe mja nitosheke
      Ya Rabbi Mola Maliki, Kwako peke nijiweke
      Ya Rabbi Mola Khaliki, shetani nipige teke
      Nitakuwaje kiburi, sina lile sina hili?
    3. Ya Rabbi Mola Ghafuru, naasi wanisamehe
      Ya Rabbi Mola Qadiru, nilinde nisiwe penhe
      Ya Rabbi Mola Nadhiru, mja mimi hohe hahe
      Yawaje sikudhukuri, Rabbana ya Rahmani?
    4. Ya Rabbi Mola Raufu, mja nimejaa hofu
      Ya Rabbi Mola Latifu, ninashindwa na siafu
      Ya Rabbi Mola Atifu, naja Kwako uniafu
      Ni vipi sikudhukuri, Nawe u pamoja nami?
    5. Ya Rabbi Mola Majidu, ni Zako zote heshima
      Ya Rabbi Mola Mujidu, nakuabudu kwa hima
      Ya Rabbi Mola Muridu, kuwa nami kwa daima
      Nitachezaje na zama, kumbe kesho ni qiyama?

    Ahmed Rashid

     

     

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet