.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Kibati

 

Related links

 

Kibati!


Date: 27 Jul 2002
  1. Kibati ngoma ya inda, sijaona mfanowe
    Ina vijana makinda, wanaopiga mayowe
    Na malenga anadunda, kwa kuchokoza wenziwe
    Avumilia wee, kumbe chamtafuna kidonda.
  2. Wababe kimewashinda, walipotaka wajuwe
    Malenga aliwaponda, ikabadi wazomewe
    Wakafungua mikanda, wapate yatupa mawe
    Avumilia wee, kumbe chamtafuna kidonda.
  3. Warembo wanaodanda, wajionavyo wenyewe
    Sauti kama kinanda, watafuta mfanowe
    Ziligeuzwa magunda, mithili yake nguruwe
    Avumilia wee, kumbe chamtafuna kidonda.
  4. Wee mpiga kayanda, nina maneno na wewe
    Usijifanye kamanda, ujuwe yana mwishowe
    Ngazi hiyo ulopanda, haikugeuzi mwewe
    Avumilia wee, kumbe chamtafuna kidonda.
  5. Mwisho wa kuranda randa, nguvu Mola azitowe
    Takupachuwa kwa panda, tukukeshee msewe
    Tukutie kwenye sanda, uwe chakula cha chowe
    Avumilia wee, kumbe chamtafuna kidonda.
  6. Haneni mtakaunda, kibati na malengawe
    Wakifunguwa mafunda, Muhidini na Jumbewe
    Mapengo kama mabanda, meno hana mdomowe
    Avumilia wee, kumbe chamtafuna kidonda.
  7. Ingawa ninakipenda, ngoja wasia nitowe
    Chataka kisu cha landa, kufuata mdundowe
    Hashili usijekwenda, kheri wewe upumuwe.
    Avumilia wee, kumbe chamtafuna kidonda.

Maa salaam.

Kassim

Kibati!


27 Jul 2002

  1. Kumbe mwenzetu mkali, wajificha vichakani
    Ushairi wako ghali, wenye macho hawaoni
    Na pia waona mbali, mbizi zako ni za shani.

Nduguyo
Hashil

Kibati!


Date: 27 Jul 2002

  1. Ama nionavyo kweli, bado sijawa wa sifa
    Nikitunga tungo mbili, ya tatu sina umafa
    Hivi huitwi mkali, bali mtunzi kifafa
    Nawaomba maarifa, malenga wa kiswahili.
  2. Nawaita madalali, mlo juu ya ghorofa
    Tokeni niwasaili, msinigeuze lofa
    Mbaruku na Hashili, Salehe wacha dafafa
    Nawaomba maarifa, malenga wa kiswahili.
  3. Nawe Mahiri humbali, zilete zako sahifa
    Mwite na Hassani Ali, tuzizibe hizi nyufa
    Ngongele wa manazili, singoje hadi arafa
    Nawaomba maarifa, malenga wa kiswahili.
  4. Njooni nisijefeli, nikapatwa na maafa
    Tatengeza maakuli, niwaandalie dhifa
    Kwa mkeka wa ukili, sio juu ya masofa
    Nawaomba maarifa, malenga wa kiswahili.
  5. Nimeishiwa kauli, na nina njaa ya kufa
    Ngoja nitafute buli, nina mkate wa mofa
    Nigange yangu akili, nangoja zenu taarifa
    Nawaomba maarifa, malenga wa kiswahili.

Maa salaam.

Kassim


Kibati!


Date: 28 Jul 2002

  1. Salamu zimenifika, ndu'yangu Kassim Ali
    Nimeitika labeika, wito mikono miwili
    Tajitahidi kwandika, lau sahafia mbili
    Kila zinapo punguka, kazi zangu na shughuli
  2. Natamani nikufate, lakini uliko mbali
    Hukaribu nikupate, uliyo bahari kali
    Tajaribu kwenda tete, kwa hatua mbili mbili
    Kusudi nisikuwate, nikiwa ntahimili
  3. Mungu kakupa kipaji, pasi mwenyewe kujuwa
    Khibra kakufariji, ukawa mwingi kwelewa
    Huna unachohitaji, maarifa ushapewa
    Huhitaji mkongoji, unakwenda sawa sawa

 

Maher

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet