|
|
Kisa cha Sahibu Yangu!
Date: 22 Sep 2002
-
Nnasahibu mpenzi, umri wake makamo
Amejitia kitanzi, moyoni ndimo kiwamo
Kampata mwanagenzi, mwari na chake kisomo
Utadhani mbaa'mwezi, mashaalla ana kimo
-
Alikuja nishauri, kuwa anakwenda posa
Nikamwambia subiri, ndoa inataka pesa
Na kanzu ilonzuri, na naali za kisasa
Hakupinga akakiri, kingoja yangu ruhusa
-
Nyuma akanizunguka, akenda kwa baba'ake
Asimkute katoka, mama yupo peke yake
Maneno yalomtoka, kuwa anataka mke
Mama roho meshituka, akamwambia atoke
-
Machozi yanamtoka, kaja kwangu analia
Huku akinung'unika, hajui lakunambia
Mambo yameshamfika, asiyo yatarajia
Kahisi keshamtoka, hakuna nyengine njia
-
Tukaifunga safari, kumtafuta babaye
Ilikuwa laasiri, tulipo onana naye
Tukampa yetu siri, twamtaka bintiye
Ni muungwana jasiri, kajibu tukaribiye
-
Baba katoa shuruti, kwa mwanawe kumtowa
Anazitaka yakuti, kilo bila kupunguwa
Apewa nyumba binti, na khati kuandikiwa
Ndipo atapodhibiti, bintiye kuolewa
-
Tukapewa wiki mbili, tulete yetu jawabu
Katuvuruga akili, tukabakia mabubu
Kuzipata hizo mali, yataka nyingi sulubu
Hata miaka miwili, sirahisi kwa sahibu
-
Nikamwambia mwenzangu, kila jambo linakheri
Limeandikwa na Mungu, Kukuepusha na shari
Hili sio lako fungu, jikaze onesha ari
Najuwa unauchungu, sahau nakushauri
-
Tukakifunga kitabu, kwa nyuzi kukishonea
Yalo sibu yamesibu, kule hatukurejea
Ikawa ndio jawabu, baba kumpelekea
Tulihisi ni aibu, kwake tena kumwendea
Maher
|