.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Kisa Kilichonifika

 

Related links

 

Kisa kilichonifika (shairi)


Date: 10 Aug 2002
  1. Ilikuwa saa nane, nimetoroka kazini
    Siku ya jumaa nne, mchana jua kichwani
    Sina hata pesa nane, kapanda gari njiani
    Mbio nenda nimuone, mpenzi alo nyumbani
    Nahamu naye ayuni
  2. Nkawasili nyumbani, wambele wangu muango
    Mekuta kitasa ndani, kimefungiwa na gongo
    Nikenda wa ubavuni, meshindikwa kimipango
    Meusukuma kwa chini, mgumu kama mpingo
    Lipo jambo si uongo
  3. Nikabaki mlangoni, nusu bega ukutani
    Sijui nifanye nini, huyu bibi simuoni
    Silewi kenda kwa nani, hayangii akilini
    Hajibwaga zangu chini, moyo wanipiga ndani
    Kwa uchungu siutani
  4. Nikarukia ukuta, nikachupa hadi ndani
    Mambo niliyoyakuta, chungu chapwaga jikoni
    Mchuzi unatokota, unakauka chunguni
    Na moto unafukuta, unazimaliza kuni
    Meuepuwa motoni
  5. Kubwa lilonishangaza, njia aliyotokea
    Milango ameiweza, yote ameikomea
    Hakuna alobakiza, hata tundu kupenyea
    Chanipasuka kuwaza, kichwa nikifikiria
    Khabithi amekimbia
  6. Masaa kwenda pitani, dalili kuja sioni
    Sasa niende kwa nani, najiuliza moyoni
    Nianze kwa majirani, au ni kwao nyumbani
    Ikanijia kichwani, bora nibaki makani
    Mepiga konde moyoni
  7. Ilipongia jioni, nusu jua limajini
    Bibie yuko njiani, arudi miguu chini
    Yeye hajanibaini, kuwa niko dirishani
    Kakazana macho chini, kama mtu hayawani
    Kajuwa yu mashakani
  8. Sikumgoja kufika, nikatoka kwa haraka
    Ghadhabu zimenishika, moyo ukiungulika
    Nani sikushughulika, kujuwa anakotoka
    Mempa yake talaka, aende anakotaka
    Yaniepuke mashaka

Maher

Date: 10 Aug 2002

Umeifanya haraka, Kake Mahiri sikia
Kwa kuitoa talaka, Sisubiri kusikia
Kile kilichomfika, Bibie akakwambia
Ngesubiri kwanza kaka, Mwenzio kaelezea

Hujui kilomfika, Huko alikotokea
Hweupata uhakika, Haraka mmevamia
Alikutwa na mashaka, Sababu angekwambia
Ukaitoa talaka, Siweze kujitetea

Hata kama sehusika, Naona memuonea
Na awe mbaya fika, Hakiye kujitetea
Hapo ingefahamika, Mbichi na mbivuye pia
Lakini membandika, Talaka bila kujua

Kwa hapa nilipofika, Leo sitaendelea
Nakuomba wangu kaka, Jambo hili fikiria
Kwa kuitoa talaka, Bila nafasi kutoa
Bora ngepata hakika, Hatua ukachukua

Myonge wa Nyali

Mbarouk
N.York

Date: 11 Aug 2002

Hatua ulochukua, japokua si murua
Haki kwako kuchukua, kwa aliyokufanyia
Kutoka bila kujijua, kukuacha hofuu pia
Haya mambo wayatambua, hongera nakupa pia.

Salim.

Date: 11 Aug 2002

Kwa ndugu na majirani, tungo zenu kisikiya
Huburudika moyoni, sikio kafurahiya
Mwanikumbusha zamani, lugha wakiichezeya
Malenga wa kusifiya, adimu hatuwaoni

Chunga vina na mizani, ukitaka wafikiya
Mfano havilingani, vina vya owa na iya
Kitahadhari mwendani, haya ninayokwambiya
Mashaha tawafikiya, bila tatizo yakini

Ibrahim

Date: 12 Aug 2002

Ulilofanya si kosa, bali hukutumia hekima.
Hamaki zako hasa, sheitani amesimama.
Hujajua yalosaza, jahazi walizamisha?

Chama.

Date: 12 Aug 2002

Hatua uliyochukua, japo hukufikiria
Haki kwako kuchukua, kwa aliyokufanyia
Hutoka bila kujijua, kukuacha hofu pia
Haya mambo wayatambua, hongera nakupa pia.

Salim.

 

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet