.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Machozi Yalinitoka

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Machozi yalinitoka


Date: 15 Dec 2002

 

  1. Safari ilinijia, sikupanga sikubuni
    Rafiki yangu kangia, mchana niko kitini
    Kaja kanizawadia, bahasha tiketi ndani
    Kwa furaha kunambia, safiri nenda nyumbani

  2. Mbio memkumbatia, nikamvuta pembeni
    Asije mtu sikia, tunazungumza nini
    Wakijuwa alojia, taingia mashakani
    Yeye akaniridhia, akifahamu kwanini

  3. Bila hata kuchelewa, haraka memuuliza
    Kikubwa kilichokuwa, tiketi kujanitunza
    Kanijibu nimepewa, na yule wako Aziza
    Ufanye litalokuwa, wende ameniagiza

  4. Begi nikalipachua, lilojuu kabatini
    Nguo nikazitundua, zilizokuwa hengani
    Baadhi nikachukua, zilizomo sandukuni
    Nikapanga kipangua, zote ziingie ndani

  5. Nikawaaga nyumbani, nakwenda zangu safari
    Salaama usalimini, wakanambia kwaheri
    Nikaenda uwanjani, ndege tayari tayari
    Tukaruka tuhewani, hali ya hewa shuwari

  6. Tukikaribu kutua, nje wingu limetanda
    Kuteremka mvua, kushuka ikatushinda
    Tukangoja kupungua, kwisha'jengoni tukenda
    Muda haukuchukua, gari nikenda kupanda

  7. Mvua bado kinyesha, nami nikiwa garini
    Si yanguvu rasha rasha, miaka kiitamani
    Mengi imenikumbusha, wakati wa utotoni
    Njia nikainyoosha, moja kwa moja kwa eni

  8. Pole pole meingia, akiwa usingizini
    Wake meushikilia, mkono umkononi
    Taratibu kimwambia, kinong'ona sikioni
    Ewe mpenzi sikia, am'ka nakutamani

  9. Sauti kuisikia, karuka hakuamini
    Kuniona alilia, akanivaa mwilini
    Neno alilonambia, ni wewe au ni nani
    Huku kanishikilia, kama alivyo nguoni

  10. Nami sikujizuia, yalinitoka machozi
    Kwa kwikwi anavyolia, na kuzishusha pumzi
    Ana mengi kunambia, kwa haliyake hawezi
    Kila kimuangalia, yalinizidi majonzi

  11. Nikamlaza shingoni, mkono kimpapasa
    Mwengine uko begani, kiugonga kimuasa
    Nikimpoza mwandani, ayasahau makosa
    yakuishi ugenini, na mahaba kututesa

  12. Tukazifanya dhihaka, kama watoto wawili
    kwa furaha tukicheka, tukikumbuka awali
    na nyoyo zikafunguka, mioyo ikakubali
    nikawa nimeshafika, nikaapa sendi mbali

 

Maher Fundi.

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet