Mbiu ya mgambo!
Date: 18 Oct 2002
Hii yangu ya mgambo, mbiu nakupigieni
Ukumbi umezuka mambo, kumeingia mgeni
Anakimwaga kimombo, tusimjuwe ni nani
Kujisifu kwake nyimbo, alichonacho sioni
Ajuwae hajisifu, kwa yale anayojuwa
Husikizana harufu, hungoji ukaambiwa
Huwa yeye maarufu, watu wakamtambuwa
Vinginevyo huwa khofu, ni duni anoelewa
Mifano haimalizi, mibaya akiijuwa
Lakini huibarizi, wengine tukaelewa
Haitaki kubwa kazi, kirefu kufafanuwa
Kwani yote huwa wazi, mwerevu akatambuwa
Lilokubwa laajabu, lugha anayotumia
Ni ile aloharibu, kifungoni kuingia
Na sasa anajaribu, ya mwanzo kuyarudia
Nasi tumekuwa bubu, hakuna anomwambia
Kirefu chake kifungo, si cha mwezi kurudia
Hajatimu hata 'ngo, jela ameikimbia
Kam'pa mlinzi hongo, mlango kamfungulia
Karudi kwenye ulingo, bila khofu kaingia
Maher