|
|
Mlolala Amkeni!
Date: 26 Aug 2002
- Ndugu zangu amkeni, nje kushapambazuka
Haraka natutokeni, jogoo limeshawika
Tusisimame twendeni, tena tufanye haraka
Zanzibar imipangoni, wabara kujaiteka
Tuwe macho sidhihaka
- Mbinu zinajibaini, kila kukicha ningeni
Nasi tumo hatarini, kama hatuko makini
Hawa sio majununi, wanayofanya yakini
Nia ni kutuhaini, watuzamishe majini
Wenzangu tahadharini
- Tulikuwa tuna vyetu, tajiri wa kila hali
Mahasidi hawa watu, wevi wa zetu mali
Hawakubakisha kitu, ila kimoja viwili
Mikubwa hii michatu, watumeza kweli kweli
Tuweke yetu akili
- Bado wamo mawindoni, kutaka kutumaliza
Waliyo madarakani, wambele kushindikiza
Wajifanya hamkwani, wamo kutuangamiza
Inatilisha huzuni, wenzetu wanatuuza
Haya siyakupuuza
- Tusimameni kidete, tuzivunje nguvu zao
Kwa umoja tuwe sote, tuwatowe wende kwao
Mungu katuumba wote, dola kila watu lao
Kutembea ni popote, sio kuchukuwa chao
Bora kutengana nao
Maher Fundi.
|