|
|
Muamu ...
Date: 27 Jul 2002
- Havisemeki, vituko vya muamu
Sasa halitaki, langu la muhimu
Anitia dhiki, na yangu kaumu
- Nilipowafiki, tuchanganye damu
Na yangu batiki, nikaikesemu
Nikampa rafiki, wangu muadhamu
- Pesa kwa lukuki, katoa sehemu
Idhibiti benki, hilo sio gumu
Nitunzie hati, zenye tarakimu
- Wamimine nyuki, washike hatamu
Uwape bunduki, wachunge binamu
Walinde kasiki, na vilivyo humu
- Wavalishe kaki, walinzi wa zamu
Wapitishe reki, penye ndumu ndumu
Wasostahiki, wasilete sumu
- Siwezi mikiki, we wangu mramu
Ya nje ya miliki, chukua jukumu
Na yaliyobaki, hayo tarasimu
- Akawa hachoki, mapenzi matamu
Yakaniashiki, kapata wazimu
Kujatahamaki, kashanihujumu
- Huwezi sadiki, orodha timamu
Kuhusu itifaki, tuliyoazimu
Sitaki dhihaki, kumi hayetimu
- Ametarazaki, akanidhulumu
Madini samaki, elimu na simu
Mgao hautoki, kwa kimaalumu
- Kachochea chuki, nikawahasimu
Wangu marafiki, na yangu isimu
Nikawataliki, wote kwa awamu
- Sasa sidiriki, hata skirimu
Wanangu wa Piki, hawana kalamu
Na walio wengi, wakosa stimu
- Nikidai haki, ananishutumu
Papatu sitaki, lakini fahamu
Talenga mikuki, ikinilazimu
- Zile shoki shoki,zanitia hamu
Ewe mzanaki, siwe chakaramu
Nipe yangu keki, nami binadamu
Maa salaam.
Kassim
Muamu!
Date: 28 Jul 2002
- Hayo siyashiki, Aah Ya Kasimu
Wala siyataki, Ulonena humu
Usinidhihaki, Amu nkutamu
- Ulomuashiki, Akakudhulumu
Si kindakindaki, Mwenyewe wa Amu
Hakustahiki, Usijilaumu
- Kuipiga ndiki, Kwataka nidhamu
Panapo kisiki, Uwe ni timamu
Ndipo humchoki, Na hakwishi hamu
- Yanini malaki, Hayo si muhimu
Bora jimiliki, Na miko idumu
Hukuvuwa dhiki, Ukatabasamu
- Hutaki fataki, Na washika zamu
Wala mahandaki, Na wala mizimu
Ilindayo haki, Ni yako maqamu
- Hebu nisadiki, Nnayafahamu
Mie sishikiki, Na wangu Muamu
Ni wangu rafiki, Rihi ya nasimu
Ahsanteni
Saleh
|